Thursday, March 7, 2013

WAWILI WAFA


Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MLINZI wa kampuni ya ulinzi ya S&M ambaye alikuwa akilinda ofisi ya DAWSCO wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Juma Hassan (45) ameuwawa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi baada ya kuvamia ofisi hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa watu hao ambao idadi yao haikuweza kufahamika mara moja walimteka kasha kumtupa baada ya kumfunga kamba miguuni na mikononi pia walimziba na plasta mdomoni na puani.
Alisema kuwa baada ya kumteka waliingia kwenye ofisi hiyo na kuiba kompyuta nne ambazo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja kasha kutoweka.
“Tunaendelea na upeelelezi kujua ni watu gani waliofanya tukio hilo la kusikitisha na tunawaomba wananchi kutoa taarifa endapo watasikia juu ya watu walio husika na tukio hilo.
Alisema kwenye tukio linguine makazi wa Mkoani Kibaha Amani Aidan au Mgaya (24) amepoteza maisha baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kugongana na gari.
Kamanda Matei alisema tukio hilo lilitokea Machi 5 saa 1 usiku eneo la TAMCO barabara ya Dar es Salaam – Morogoro ambapo pikipiki hiyo ili gongana na gari namba T 787 AWC aina ya Toyota Coaster lililokuwa likiendeshwa na Thadei Makala (58).
Aidha alisema katika ajali hiyo mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Amina (22) mkazi wa Picha ya Ndege Kibaha alikimbizwa hospitali ya Tumbi kwa matibabu zaidi baada ya kupata majeruha sehemu za kichwani kulia.
Mwisho.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamtafuta Ramadhan Mfaume maarufu kama Ngosha kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya Short Gun na fuvu la mnayama aina ya Fungo na Ngiri.
Akizungmza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani hapo Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 4 mwaka huu.
 Kamanda Matei alisema kuwa vitu hivyo vilikamatwa nyumbani kwake kwenye eneo la Fitina haina Posho Kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilaya ya Bagamoyo.
 Aidha alisema kuwa mbali ya silaha hiyo ambayo namba zake hazikuweza kufahamika mara moja pia kulikutwa risasi 29.
Alisema mtuhumiwa huyo alitoroka na anatafutwa kuhusiana na tukio hilo na kuwataka wananchi kutomiliki silaha hizo bila ya kibali ili kuepukana na mkono wa sheria.
Mwisho. 


Tuesday, March 5, 2013

MADENI MAKUBWA SHIRIKA



WAAFANYAKAZI na Wazabuni mbalimbali wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) mkoani Pwani wanalidai shirika hilo kiasi cha zaidi ya shilingi biloni moja.
Hayo yalisemwa juzi na mkurugenzi wa shirika hilo Dkt Cyprian Mpemba, wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia.
Dkt Mpemba alisema kuwa madeni hayo ni ya wazabuni wanaodai kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 286, wafanyakazi wanaodai zaidi ya shilingi milioni 277 na makandarasi mshauri wa hospitali ya Tumbi anayedai kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 600.
“Madeni hayo ni changamoto kwetu kwani ruzuku inayotolewa na serikali haitoshelezi kabisa ambapo kwa bajeti ya mwaka 2010/2011 fedha zilizotolewa na serikali zilikuwa ni pungufu kwa asilimia 15 huku bajeti ya mwaka 2011/2012 ilikuwa pungufu kwa asilimia 48,” alisema Dkt Mpemba.
Alisema mbali ya madeni hayo pia shirika lina mahitaji makubwa ambapo wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kumalizia jengo la hospitali, zaidi ya bilioni moja, milioni 500 kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari bingwa na wasaidizi, uchakavu wa majengo kiasi cha shilingi milioni 300, matengenezo ya magari na majengo zaidi ya milioni 131, maji, umeme, bima, madawa na shajala shilingi zaidi ya milioni 143, chumba cha kuhifadhia maiti shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukarabati.
“Kutokana na changamoto ya fedha ripoti ya mkaguzi mkuu wa serikali ya mwaka huu imetahadharisha kuwa shirika lipo kwenye hatari ya kushindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani inaonekana mahesabu ya shirika yana mwelekeo mkubwa wa uhaba wa kumudu kulipa watoa huduma wastani wa bilioni moja,” alisema Dkt Mpemba
Aidha alisema wastani wa mapato ya ndani ya shirika hilo ni kati ya shilingi milioni 800 na bilioni moja kwa mwaka ambazo hazikidhi matumizi stahiki kwa idadi ya watumishi waliopo 985 hivyo kuiomba serikali kuongeza ruzuku ya mwaka kutoka bilioni 1.9 na kufikia bilioni 3.6.
Akijibu hoja hizo Waziri Ghasia alisema kuwa kuhusu madeni watalifanyia kazi suala hilo ili kuweza kupunguza chanagamoto ya ukosefu wa fedha kwenye shirika hilo la Umma ambalo limekuwa na mchango mkubwa ambayo ni kutoa huduma za kielimu, afya na kupambana na umaskini.
‘Pia  ifike wakati mwende kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kukopa kuliko kutegemea ruzuku ya serikali ambapo kwa bajeti iliyopita hali ya kifedha haikuwa nzuri, kwani mashirika ya umma yanatakiwa yajiendeshe yenyewe na si kuisubiri serikali pekee,” alisema Ghasia.
Alisema KEC ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo ufugaji kuku na ng’ombe endapo vitapatiwa fedha litaweza kujiendesha kwa kiasi fulani hivyo kumudu kufanya shughuli zake za kila siku, awali Waziri alitembelea mashamba ya kuku, kiwanda cha kutengenezea trei za mayai na hospitali ya Tumbi akiwa na uongozi wa shirika na bodi.
Mwisho.  

Friday, March 1, 2013

MTOTO AUNGUZWA NA MAJI YA MOTO




Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Mtaa wa Kwa Mfipa wilayani Kibaha Nuru Rashid amewashangaza wakazi wa mtaa huo kwa kushindwa kumpeleka hospitali mwanae mwenye umri wa miaka miwili na nusu baada ya kuungua na maji ya moto.
Akizungumza na baba mzazi Ally Said alisema mwanae ambaye ni wa jinsi ya kiume ameungua kifuani na kusababisha kidonda kikubwa hadi kwenye mkono wake wa kushoto hakumpatia matibabu yoyote hadi siku iliyofuata.
Said alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 27 mtaani hapo nyumbani kwa mama yake mazazi ambaye walitengana naye zaidi ya mwaka mmoja uliopita ambapo aliolewa na mume mwingine.
“Mimi baada ya kupata habari juu ya mwanangu kuunguzwa na maji siku iliyofuata nilikwenda nyumbani kwake kutaka kumchukua mwanangu ili nimpeleke hospitali lakini alikataa na kusema hadi baba yake wa kambo aje jambo ambalo alilikataa na kumchukua kwa nguvu,” alisema Said.
Alisema kuwa mkewe amekuwa akimficha juu ya matatizo hasa pale anapoumwa na mbaya ni pale alipomficha mwanae baada ya kuungua na kushangaa ni kwanini hataki kumpeleka hospitalini.
Jitihada za kumpata mama huyo yazikuweza kuzaa matunda licha ya mwandishi kufika nyumbani kwake na kuambiwa kaenda dukani na hata aliposubiriwa hakuweza kutokea.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Hai Hai alikiri kupata tukio hilo na kusema kuwa ukweli halisi alikuwa nao mama huyo ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na mtoto huyo ambaye alikuwa akilia kutokana na maumivu makali aliyoyapata.
Hai alisema kuwa hatua aliyoichukua ni kuandika barua ambayo ilibidi ipelekwe polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria na kupatiwa matibabu kwa mtoto huyo na kusema hicho ni kitendo cha unyanyasaji na kuwanyima haki watoto wadogo.
Mwisho.     
 Mtoto aliyeunguzwa na maji ya moto akiwa amepumzika huku nyumbani kwao huko Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani (Picha na John Gagarini)






MBUNGE ALIPA HASARA ILIYOSABABISHWA NA MGAMBO


Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka amelazimika kuwalipa fedha kiasi cha shilingi 275,000 wanawake watatu wanaouza samaki baada ya mgambo wa kata ya Maili Moja kumwaga samaki wao kwa madai ya kukiuka kanuni za afya.
Koka ilibidi alipe fedha hizo kwa wafanyabiashara hao baada ya kuangua kilio mbele ya mbunge huyo wakati wa mkutano na wananchi wa Kibaha.
Alisema hayo yalikuwa makosa ya kibinaadamu yaliyofanywa na mgambo hao wakati wakitekeleza zoezi la usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha.
“Suala la afya ni muhimu na mgambo hawa waliteleza na kujikuta wakiharibu mali za wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki zao huku wengine wakiwa wamekopa fedha kwa ajili ya kufanyia biashara hiyo,” alisema Koka.
Mbunge huyo alisema kuwa kuanzia sasa wafanyabiashara na mgambo hao kwa kushirikiana na ofisi ya afya ya kata kila upande kufuata kanuni na sheria ili kufanikisha suala la afya.
Kwa upande wao wakinamama hao mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Said alisema kuwa mgambo hao walifika kwenye biashara yake na kusema kuwa kwakuwa hakupima afya yake na kuwamwaga samaki wake wenye thamani ya shilingi 65,000.
Naye mfanyabiashara mwingine Nuru Msangi alisema kuwa mgambo hao walichukua samaki wake wenye thamani ya shilingi 75,000 na kuzimwaga kwa madai kuwa naye hakupima afya yake.
Alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanashindwa kupima afya zao kutokana na gharama kubwa ya kupima ya shilingi 5,000 na pia walisema wao kama wanshinikizwa kupima je kwa wateja wanaokwenda kununua mbona hawabanwi.
Mbunge huyo alizitaka pande mbili hizo kati ya idara ya afya ya kata hiyo na wafanyabiashara kuanza mahusiano mazuri upya ili kuondoa ugomvi unaojitokeza mara kwa mara pia halmashauri itoe elimu juu malipo hayo ya kupima afya ya shilingi 5,000.
Mwisho.    

Thursday, February 28, 2013

FRIENDS OF SIMBA WATAKIWA KUJITOKEZA KUTATUA MGOGORO



Na John Gagarini, Kibaha
MARAFIKI wa Simba (Friends of Simba) wametakiwa kuingilia kati tatizo lililopo kwenye klabu yao ili iweze kuwa na mwenendo mzuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki timu yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msemaji wa tawi la Simba wilayani Kibaha “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa hadi sasa timu hiyo bado haijapata tiba ya tatizo lililopo ndani ya klabu hiyo.
Lardhi alisema kuwa wakati huu wa matatizo wanachama na wadau wa Simba lazima wajitokeze kusaidia timu ili iweze kufanya vema kwani kwa sasa mwenendo wake ni mbaya.
“Marafiki wazuri huonekana wakati wa shida hivyo tunataka marafiki wetu wajitokeze kuinusuru timu kwani kwa sasa timu inaonekana kufanya vibaya kwenye michezo yake tofauti na matarajio ya wengi,” alisema Lardhi.
Alisema kuwa marafiki wa Simba mbali ya kusaidia fedha pia wanatakiwa kuisaidia timu hiyo kwa mchango wa mawazo ili kujua tatizo lililopo hadi timu kufanya vibaya kwenye michezo yake.
“Wanapaswa kuonyesha upendo wao kwa klabu kwani hadi sasa hatujaona jitihada zozote walizofanya kuinusuru timu na matokeo mabaya, tunawpongeza wanaposaidia timu katika mazingira yote pia waonyeshe upendo hata kama timu inafanya vibaya ili kuinusuru timu yetu ambayo inatetea ubingwa wake wa ligi kuu ya Tanzania Bara,” alisema Lardhi.
Msemaji huyo wa tawi la Simba wilayani Kibaha alisema kuwa Wanasimba wanatakiwa kuungana katika kipindi hichi kigumu kinachoikabili timu yao kwa kuwa na matokeo mabaya inayoyapata ili kujinusuru na kupata matokeo mazuri.
“Tunapaswa kuungana na kuonyesha mshikamano ili kuisaidia timu yetu kwani timu inapofanya vibaya tunaumia sana hivyo tuungane ili kuiletea maendeleo mazuri,” alisema Lardhi.
Ameipongeza kamati ya utendaji kwa kuandaa mkutano wa kujadili kiini cha timu kufanya vibaya katika michezo yake hali ambayo inaifanya timu hiyo kuwa kwenye mashaka ya kutetea ubingwa wake.
Mwisho.