WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imezitaka Shule za Kimataifa nchini kujisajili kwenye mifumo na miongozo ya elimu na kiserikal ili kukidhi matakwa ya kisheria.
Hayo yalisemwa na Dk Maulid Maulid aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara Caroline Nombo wakati wa kufunga mafunzo ya siku nne kwa wamiliki wa shule hizo juu ya namna ya uendeshaji wa shule hizo mafunzo yaliyofanyika kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha.
Maulid alisema kuwa ili elimu inayotolewa na shule hizo za kimataifa lazima zihakikishe zinafanya usajili wao kupitia mifumo iliyowekwa ili kuendana na mfumo wa elimu wa nchi.
"Wamiliki wa shule hizi wanapaswa kufanya usajili kwenye mifumo ya elimu ili elimu inayotolewa itambulike na iwe na ubora unaotambulika na ushindani kimataifa kwa kuzingatia mitaala ya nchi yetu,"alisema Maulid.
Alisema kuwa shule hizo zinapaswa kujisajili kwenye mamlaka mbalimbali za taasisi za elimu ili ziweze kuendana na mifumo iliyopo ikiwemo kwenye Baraza la Mitihani NACTE na mamlaka za serikali.
"Lazima wafuate mifumo yote ya kiithibati na ubora bila kusahau kuzingatia sera ya elimu ambayo ndiyo inayotoa mwongozo wa elimu kwa taasisi za kielimu,"alisema Maulid.
Aidha alisema kuwa pia mitaala yao iendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo ili wanafunzi wawe na uelewa wa juu ya Dira hiyo ambapo kwa sasa ni ya 2050.
"Mitaala yao iendane na Dira ya Maendeleo kwani inazingatia utoaji elimu bora ambayo inaangalia viaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo kwa wananchi,,'alisema Maulid.
Kwa upande wake moja ya washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mhasibu wa shule ya kimataifa ya Renie Joshua John alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa shule yake kwani amepata elimu ya namna ya kuweka vizuri masuala ya fedha.
John alisema kuwa wamepata uelewa mzuri wa namna ya kuendesha shule zao na kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya kisheria ambayo wanapaswa kuifuata.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Tanzania School Leadership Institute (TSLI) na kusimamiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia waliwahusisha wamiliki, walimu wakuu, wahasibu na viongozi wa shule za kimataifa hapa nchini

No comments:
Post a Comment