Saturday, April 4, 2026

MKIMBIZA MWENGE KITAIFA AIPONGEZA STAMICO KWA KUIBEBA AGENDA YA KITAIFA YA NISHATI SAFI


*STAMICO YASHIRIKI UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU KITAIFA PEMBA.* 

▪️Mkimbiza Mwenge Kitaifa aipongeza STAMICO kwa kuibeba ajenda ya kitaifa ya Nishati Safi.

▪️Atoa msisitizo kwa Taasisi na Shule Mkoani Kusini Pemba kutumia Nishati ya Rafiki Briquettes 

▪️Nishati Safi ya Rafiki Briquettes  kuanza kuuzwa Kisiwani Pemba

▪️Dkt. Mwasse: STAMICO kuwawezesha kontena wanawake na Samia Mkoa wa Kusini Pemba 

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeshiriki katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge ambazo umefanyika katika viwanja vya Gombani Kisiwani Pemba.

Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huo alikuwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Tukio hilo pia lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

STAMICO imewakilishwa na Dkt Venance Mwasse, Mkurugenzi  Mtendaji ambaye aliambatana na baadhi ya maafisa kutoka kitengo cha Masoko na Mahusiano.

Katika mbio za mwaka huu za Mwenge wa Uhuru, kauli mbiu ni: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Maendeleo.” Kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa Watanzania katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Mbio hizi zinatarajiwa kuendelea katika mikoa mbalimbali ya nchi, Tanzania Bara na Visiwani.

Sambamba na uzinduzi huo, pia kumefanyika maonesho ya Taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi yaliyolenga kutoa elimu na kuonesha huduma mbalimbali kwa wananchi.

 Katika maonesho hayo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) nalo limeshiriki kwa kuonesha bidhaa na huduma zake kwa Wananchi.

Awali, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake na Samia Mkoani Kusini Pemba Bi Sabra Masoud Ally alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO  kwa ulezi na ushirikiano unaotolewa na STAMICO katika kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na usambazaji wa nishati safi ya Rafiki briquettes.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mwasse aliahidi kuendelea kusaidia kikundi hicho kwa kuwapatia kontena  mwezi huu wa nne, ili yaweze kutumika kama vituo vya kuuzia nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes. Aidha, alisisitiza kuwa STAMICO itaendelea kufanya uhamasishaji mkubwa wa matumizi ya nishati hii safi katika mikoa ya Kaskazini na Kusini  Pemba, kwa lengo la kulinda mazingira na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida.

Akitembelea banda la STAMICO,Mkimbiza Mwenge kitaifa,Ndugu Wazo Mwangonda aliipongeza STAMICO kwa kubeba kikamilifu ajenda ya Kitaifa ya nishati safi na Kusisitiza taasisi na Shule za Mkoa wa Kusini Pemba kutumia Nishati ya Rafiki Briquettes.

STAMICO  inaendelea na azma yake ya kuwa kinara katika kuhamasisha matumizi  ya Nishati Safi kwa kutekeleza kwa vitendo ajenda muhimu za Serikali.

No comments:

Post a Comment