Wednesday, January 20, 2016

MAMA NA WATOTO WAKE WAWILI WAFA KWA RADI WATATU WAJERUHIWA

Na John Gagarini, Pwani
MVUA zinazoendelea kunyesha hapa nchini zimeendelea kuleta madhara baada ya Mama na watoto wake wawili kufa huku watu wengine watatu wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu ofisa mtendaji wa kata ya Mchukwi wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Ami Lipundundu alisema kuwa familia hiyo ilikuwa ikiota moto baada ya kuchota maji ya mvua.
Lipundundu alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 18 mwaka huu majira ya saa 11 jioni kwenye Kijiji cha Mchukwi B walipokuwa wanaota moto baada ya mvua kunyesha.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Decilia Simba (42) watoto wake Debora Simba (4) na Amani Matimbwa 1 na nusu huku waliojeruhiwa wakiwa ni Maua Ngwande (13) anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Mchukwi, Suzana Daudi (12) na mdogo wa marahemu aitwaye Mama Tariq.
“Marehemu alitoka kwenye kikundi cha kuweka na kukopa cha Jitegemee ambapo yeye ni mwanachama alipofika nyumbani mvua ikaanza kunyesha akawa anakinga maji ya mvua yeye na watoto wa ndugu yake,” alisema Lipundundu.
Alisema kuwa baada ya hapo waliwasha moto kwenye jiko lao ambalo liko jirani na mti wa Mfenesi na kuota kwani walikuwa wameloa ndipo radi ilipopiga ikakwepa mti ikawapiga wao.
“Marehemu na wanawe walifia njiani wakati wakipelekwa Hospitali ya Mchukwi kwa ajili ya matibabu ambapo majeruhi bado wamelaazwa hopsitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Lipundundu.
Aidha alisema kuwa wiki iliyopita mtu mmoja naye alifariki kwa kupigwa na radi na mwishoni mwa mwaka jana huko Ikwiriri mtu mmoja pia alifariki dunia. Polisi mkoa wa Pwani walithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha.
Mwisho.

Monday, January 18, 2016

NDC YAPEWA MIEZI MITATU

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imelipa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) miezi mitatu kuhakikisha linapata kiasi cha dola za Kimarekani Milioni 2.1 kwa ajili ya kiwanda cha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mmbu wanaoeneza Ugonjwa wa Malaria Tanzania Biotech Product Ltd kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Aidha alishangazwa na shirika hilo kwa kuajiri wafanyakazi 143 Julai mwaka 2015 ambao wanalipwa mishahara pasipo kuzalisha kitu chochote kwani wanapokea mishahara ya bure jambo ambalo alisema kuwa halipendezi.
Agizo hilo limetolewa jana mjini Kibaha na katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dk Adelhelm Meru alipotembelea kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa Julai 2015 na Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Ethiopia.
Dk Meru alitoa agizo hilo kutokana na kutoridhishwa na maombi ya NDC kuomba kiasi hicho serikalini kutoka kwa Godwill Wanga Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika hilo kwa lengo la kufanya majaribio pamoja na kuanza uzalishaji.
“Serikali haiwezi kutoa kiasi hicho cha fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya huduma za jamii hivyo fanyeni kila njia kwa kukopa kwa kufanya nini ombeni hata benki ya uwekezaji nchini TIB ili mhakikishe mnapata fedha hizo na majaribio yanaanza ili uzalishaji uanze tumechelewa kwa kipindi cha miaka minne,” alisema Dk Meru.
Alisema kuwa inatosha kwani serikali ililipa gharama zote za ujenzi wa kiwanda hicho dola milioni 22 na kilitakiwa kianze kazi tangu mwaka 2012 ikasogezwa hadi Julai 2015 lakini hadi sasa ni miezi sita imepita lakini uzalishaji bado.
“hatuwezi kuwa kioja tafuteni fedha hizo dola milioni 1 kwa ajili ya majaribio na dola milioni 1.2 kwa ajili ya mtaji kwani malengo ya serikali ilikuwa na lengo kiwanda kianze kazi kwa muda uliopangwa ili kiweze kukabiliana na ugonjwa wa Malaria na ziada ya dawa kuuzwa nje ya nchi hivyo kuweza kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Dk Meru.
“Nataka ifikapo Mei Mosi mwaka huu mimi nije na Waziri wangu ili tuone uzalishaji unaanza mara moja kwani moja ya sera za nchi hasa katika awamu hii ya tano ni kujenga uchumi kupitia viwanda na kuwa nchi yenye uchumi wa kati ili kuleta maendeleo ya wananchi pia iko kwenye dira ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano,” alisema Dk Meru.
Awali akielezea juu ya maendeleo ya kiwanda hicho Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NDC Wanga alisema kuwa baadhi ya vifaa kwenye mashine ziliathiriwa na umeme kutokana na na kukatika katika hali ambayo ilisababisha uzalishaji ushindwe kuanza.
Wanga alisema kuwa kutokana na ucheleweshaji huo wa kuanza kufanya kazi ilibidi wataalamu kutoka nchi ya Cuba inakotoka teknolojia hiyo Labio Farm kudai gharama zaidi za ujenzi hivyo kudai fidia.
“Kiwanda hichi kinahitaji msaada hata kwa mkopo kiasi cha dola milioni 2.1 ili kuweza kukamilisha hatua zilizobakia kwani wataalamu wetu wameishiwa mtaji baada ya muda kuongezeka na kutokana na matatizo ya kuharibika vifaa vya mashine za kiwanda hichi,” alisema Wanga.
Alisema kuwa teknolojia hiyo ni mpya na mara uzalishaji utakapoanza itasaidia kukabiliana na ugonjwa wa Malaria kwani dawa hiyo ina uwezo wa kuua mazalia ya mbu na baadaye kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingine ikiwa ni pamoja na mbolea na madawa mbalimbali.
Mwisho.

Thursday, January 14, 2016

PANGANI YAPIGA MARUFUKU MUZIKI WA VIGODORO

Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA vijana wawili kuchomwa moto na mmoja kujeruhiwa mwishoni mwanzoni mwa wiki hii kwenye mtaa wa Vikawe kata ya Pangani wilayani Kibaha mkoani Pwani kamati ya ulinzi na usalama ya kata imepiga marufuku muziki wa vigodoro ili kuepusha mauaji kama hayo.
Marufuku hiyo inakuja baada ya tukio la kufa vijana hao ambao ni Alex Kapungu (18), Godfrey Ernest huku Omary Mohamed akijeruhiwa kwenye tukio lililotokea januari 10 mwaka huu majira ya saa 2:50 usiku kwenye mtaa huo, baada ya vijana hao kutuhumiwa kuwa ni wezi baada ya kuibuka kwa vurugu zilizosababisha baadhi ya vijana waliokuwa kwenye mziko huo kufanya uporaji kwenye maduka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana diwani wa kata ya Pangani Agustino Mdachi alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama ilifikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa muziki huo umekuwa chanzo cha vurugu ambazo zimesababisha vifo pamoja na wizi kwenye maeneo unakopigwa muziki huo.   
Mdachi alisema kuwa hilo ni tukio la pili la mauaji ambayo yametokeo kwenye muzikio huo ambao unatumiwa sana na waendesha pikipiki ambapo imebainika kuwa waendesha bodaboda hao hasa wale wanaofanya biashara nyakati za usiku maarufu kama Mapopo wengi wao ni wezi na hujificha kwenye mgongo wa kazi hiyo.
“Uchunguzi umebaini kuwa wengi wa wa mapopo hao hujihusisha na vitendo vya wizi kwani wakati muziki unaendelea huanzisha vurugu na na kuwaibia watu ambapo wengi wao huwa na mapanga wanapokwenda kwenye muziki huo ambao unatamba kwa sasa,” alisema Mdachi.
Alisema kuwa kutokana na kubaini kuwa muziki huo umekuwa ukichangia vitendo vya uhalifu katika kata ya Pangani waliamua kwa pamoja kuzuia upigwaji wa muziki huo kwa kipindi kisichojulikana ili kuepukana na vitendo hivyo vya uhalifu pamoja na mauaji.
“Kwa ujumla Kigodoro mara nyingi hakiishi salama kwani mara nyingi vurugu zimekuwa zikitokea na vijana wanauana kutokana na muziki huu hivyo tumeamua kusitisha muziki huu ili kupunguza wimbi hili la uhalifu na mauaji,” alisema Mdachi.
Aidha alisema kuwa kwa sasa wameamua kufanya doria kwa muda wote kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kukabiliana na matukio hayo ya kihalifu ambayo mengi yanafanywa na waendesha pikipiki.
Mwisho.

ARDHI KUPIMWA KWA NJIA YA KILETRONIKI KWA MAJARIBIO MIKOA MITATU HATI KUPATIKANA KWA SIKU MOJA

Na John Gagarini, Kibaha

WIZARA ya Ardhi na Makazi iko kwenye mpango wa kupima maeneo yote hapa nchi kupitia mpango wa majaribio wa kutoa hati za kumiliki ardhi kwa njia ya Kieletroniki ndani ya siku moja ili kila mwananchi aweze kumiliki ardhi kisheria.
Hayo yalisemwa  hivi karibuni mjini Kibaha na Waziri wa Ardhi na Makazi Wiliam Lukuvi wakati alipofanya zaiara ya siku moja wilayani Kibaha kuangalia changamoto zinazoikabili idara ya ardhi kwenye mkoa huo.
Lukuvi alisema kuwa utoaji hati za kumiliki ardhi kwa haraka itasaidia kupunguza migogoro ambayo imejitokeza kutokana na kuchelewa kutolewa kwa hati hizo ambapo watu wamekuwa wakivamia maeneo yaliyowazi.
“Upatikanaji wa hati unasaidia kuepusha migogoro pia uvamizi kwani kutokana na uchelewaji wa kupatikana hati kunasababisha mtu kushindwa kumiliki kihalali eneo lake hivyo tunataka tuondokane na ucheleweshaji huo,” alisema Lukuvi.
Alisema kuwa majaribio hayo yataanza kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro kupitia mfumo wa Kieletroniki ambapo mfumo huo endapo utafanikiwa utasamabazwa nchi nzima na kuweza kufikia malengo ya kupima ardhi ya nchi nzima.
“Utashangaa mfumo huu wa sasa kuna baadhi ya watu wamekuwa kwenye mchakato wa kupatiwa hati kwa muda mrefu tangu mwaka 2013 lakini wamekuwa wakitumia ofa pekee jambo ambalo hatulitaki tena,” alisema Lukuvi.
Aidha alisema ametoa hadi mwisho wa mwezi huu Halmashauri kuhakikisha unawapatia hati watu wote walioomba hati kwani ofa hazitatambuliwa tena hivyo wanatakiwa kufanikisha zoezi hilo ili kuondoa kero kwa wananchi.
“Tunataka tuondokane na kero ya kucheleweshwa kupatikana kwa hati kwani mbali ya maeneo kuvamiwa na changamoto nyingine pia watu wanaweza kuzitumia hati zao katika kukopa kwenye mabenki au taasisi za kifedha kwa  ajili ya shughuli zao za maenedeleo,” alisema Lukuvi.
Mwisho.    


OFISA ARDHI AWEKWA KITI MOTO LUKUVIA AMTAKA AWALIPE WANANCHI

Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mwanalugali wilayani Kibaha mkoani Pwani kulalamika mbele ya Waziri wa Ardhi na Makazi Wiliam Lukuvi juu ya kushindwa kulipwa fidia ya viwanja vyao vilivyochukuliwa na Halmashauri kwa zaidi ya miaka 18 iliyopita wakazi hao sasa watalipwa ifikapo Machi mwaka huu.
Ahadi hiyo ilitolewa na Halmashauri mbele ya Waziri Lukuvi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani hapa kujua kero mbalimbali zitokanazo na masuala ya ardhi na kusema kuwa ofisa ardhi wa Mji huo endapo atashindwa kutekeleza hilo basi atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Akitoa ahadi hiyo ofisa ardhi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Edward Mbala baada ya kubanwa na wananchi hao ambao walisema kuwa wamekuwa wakizungushwa kwa kipindi hicho huku wakiwa hawajui hatma yao.
Moja ya wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Merry Yohana alisema kuwa maeneo yao yalichukuliwa na Halmashauri kipindi hicho na kuahidiwa kuwa wangelipwa fidia na wengine wangepewa viwanja katika maeneo hayo lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika licha ya kuwa viwanja hivyo tayari walishaviuza kwa watu wengine.
“Tunapata shida sana kwani walichukua maeneo yote licha ya kuwa ni jambo zuri la maendeleo lakini kwa kipindi cha miaka 18 tumekuw atukifuatilia bila ya mafanikio kwani tunazungushwa tu na hakuna majibu ya uhakika kuwa  ni lini tutalipwa kwenye eneo la Kitalu E,” alisemaYohana.
Kufuatia malalamiko hayo Waziri Lukuvi alimwita ofisa ardhi ili atoe majibu ambapo alisema kuwa ni kweli watu hao wamekuwa wakidai kwa kipindi hicho lakini Hlamashauri iko kwenye utaratibu wa kuwalipa majibu ambayo hayakumridhisha waziri.
“Mkuu ni kweli kuna watu wanadai fidia na wengine wanadai viwanja na huu ulikuwa ni mradi lakini tuko kwenye utaratibu wa kuwalipa na tutawalipa wakati wowote mara taratibu zitakapokamilika kwani tunahangaika kuhakikisha madai yao yanapata majibu,” alisema Mbala.
Hata hivyo waziri alimwambia atoe ahadi kuwa ni lini watakuwa wamekamilisha zoezi hilo ambapo alisema kuwa baada ya miezi miwili kutoka sasa fedha hizo zitakuwa zimepatikana kiasi cha shilingi bilioni 1.4 pamoja na kuwapatia viwanja wengine.
Kwa upande wake Waziri Lukuvi alisema kuwa haipendezi wananchi kukaa muda mrefu bila ya kulipwa fidia ya maeneo yao ambayo yalichukuliwa na Halmashauri kwani kuchelewesha kulipa kunasababisha migogoro isiyo ya lazima.
“Wananchi ofisa ardhi ameahidi hapa mbele yangu na ninyi hivyo msiwe na wasiwasi Bw Ardhi kwa kuwa umeahidi mwenywe muda mtkaowalipa hawa wananchi endapo utashindwa utakuwa umejifukuzisha kazi mwenyewe,” alisema Lukuvi.
Lukuvi aliwataka wananchi hao kukubali muda huo wa miezi miwili kwani walishakaa muda wa miaka 18 hivyo atahakiki wanaodai fidia na wale wanaodai viwanja kwani muda umekuwa mrefu sana na watu wanataka wafanye maendeleo yao.
Mwisho.

Sunday, January 10, 2016

WAAZIMIA KUJENGA SHULE YA SEKONDARI KWA SASA WATOTO WAO WANASOMA UMBALI WA KILOMETA ZAIDI YA 8

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Mtaa wa Mbwate kata ya Mkuza wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwapatia greda kwa ajili ya kuchimba visiki kwenye eneo ambalo wamelifyeka kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.
Wametoa ombi hilo baada ya kuanza kusafisha eneo kwa ajili ya sekondari kutokana na watoto wanaokaa mtaa huo kusoma kwenye sekondari ya kata ya Nyumbu ambayo iko umbali wa kilometa zaidi ya 8 hali ambayo inawafaya wanafunzi wanaotoka kwenye mtaa huo na jirani kukumbuna na changamoto nyingi hivyo kushindwa kumaliza shule.
Akizungumza na waandishi wa habari mkazi wa mtaa huo Alex Mathias alisema kuwa wamefikia hatua hiyo ya kujenga sekondari ili kuwapunguzia adha watoto wao kusoma mbali hivyo kushindwa kusoma kwa ufanisi hivyo wakipatiwa greda litasaidia kusafisha eneo hilo.
“Kule ni mbali sana kama mzazi huna fedha za kumlipia pikpiki kila siku kiasi cha shilingi 2,000 kwenda na kurudi basi mwanafunzi anakutana na mitihani mingi ambapo wengine wanakuwa hawafiki shule na kufikia hatua ya kuacha shule huku kwa upande wa wale wa kike wamekuwa kijiingiza kwenye vishawishi na kudanganywa na waendesha pikipiki na kujikuta wakiambulia kupata mimba,” alisema Mathias.
Kwa upande wa Salama Rajab alisema kuwa wanafunzi wamekuwa wakipata taabu ya kufika na kurudi kutoka shule kwani umbali wanaposoma kunawapunguzia ari ya kusoma.
Rajab alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo itakuwa mkombozi kwa watoto wao hali ambayo itawafanya wafanye vizuri kwenye masomo yao kwani watakuwa na mazingira mazuri ya kusomea tofauti na ilivyo sasa.
Naye mwenyekiti wa mtaa huo Abdala Mtandio alisema kuwa kutokana na eneo hilo na maeneo jirani kukosa shule ya sekondari walifikia maamuzi ya kuanzisha wazo la kujenga shule ili kuwapunguzia watoto wao kero ya kusoma mbali.
Mtandio alisema kuwa wanalishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Nyumbu kwa kuwapatia eneo lenye ukubwa wa hekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa huduma za jamii ambapo ndo wamenza na maandalizi ya shule ya sekondari.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutusaidia kuweza kuanza ujenzi wa shule yetu ya sekondari kwani kwa sasa tunasafisha eneo letu ambapo kila Jumamosi tunalifyeka kwa ajili ya ujenzi huo,” alisema Mtandio.
Alisema kuwa wameazimia kuwa ifikapo 2017 wanafunzi waanze kusoma hapo ambapo watakuwa wamekamilisha angalau madarasa matatu kwa kuanzia ambapo kila kaya inajitolea kufyeka ambapo kuna kaya 554 zenye wakazi 2,863.

Mwisho.  

Friday, January 8, 2016

PWANI YAPATA ZAIDI YA MILIONI 500 KWA AJILI YA ELIMU BURE

Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani umepokea kiasi cha shilingi milioni 579.5 kwa ajili ya utekelezaji wa dhana ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Ndikilo alisema kuwa fedha hizo tayari zimetumwa kwenye akaunti za shule hizo ambapo kwa shule za Msingi zimepokea kiasi cha shilingi milioni 167,297,00 na sekondari wamepewa kiasi cha shilingi milioni 412,249,000.
“Fedha hizo ni kwa ajili ya maendeleo ya shule ikiwa ni pamoja na ada, chakula ,gharama za mitihani na gharama nyingine ambazo zimetolewa maelekezo kwa walimu wakuu,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa fedha hizo zitasimamiwa na mkoa ambapo mwalimu mkuu yoyote atakayetumia kinyume cha utaratibu kwa ubadhirifu atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Walimu wakuu, Wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa Wilaya wanatakiwa kukiri kwa maandishi mara watakapoziona fedha hizo kwenye akaunti zao,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa kutokana na kutolewa fedha hizo walimu wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyotea kama vile ulinzi, maji, umeme na michango mingine kwani fedha hizo zitatumika kwenye masuala yote.
“Michango yoyote kwa wadau kama watakuwa wamekubaliana lazima wapate kibali cha Waziri wa TAMISEMI kupitia mkuu wa mkoa ili kuchangisha michango kwa wananchi ambapo mkoa wetu una jumla ya shule za msingi 553 na sekondari 108,” alisema Ndikilo.

Mwisho.   

Tuesday, January 5, 2016

HALMASHAURI KUTOA HUDUMA KADRI YA UWEZO WAKE

Na John Gagarini, KibahaKATIKA kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji huduma kwa wananchi Halmashauri ya Mji wa Kibaha imesema kuwa itatatua kero hizo kadiri ya uwezo wa fedha za miradi ya maenedeleo zinavyopatikana.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Gladys Dyamvunye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa kuna changamoto za utoaji huduma kwani kila mwananchi anataka maendeleo.
Dyamvunye alisema kuwa changamoto ni nyingi kwani ili kuondoa kero lazima huduma ziboreke lakini kutokana na mahitaji ya huduma kuongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu kila wakati.
“Kadiri maendeleo yanavyokuja mahitaji ya huduma nayo yanaongezeka hivyo kuonekana kama huduma ni kidogo lakini tutaendelea kutoa huduma kadiri ya uwezo wetu ili kuwaondolea changamoto wananchi,” alisema Dyamvunye.
Alisema kuwa halmashuri itahakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinaboreshwa ili kuondoa malalamiko yasiyo ya msingi kwani lengo ni kuboresha utoaji huduma ambayo ndiyo kazi ya Halmashauri.
“Bajeti ya fedha inaweza kuwa ni tatizo hivyo baadhi ya huduma zinaonekana kama hazitolewi kiufasaha lakini si lengo la Halmashauri yetu kwani matazamio yetu ni huduma bora kwa wananchi ili waipende serikali yao,” alisema Dyamvunye.
Aliwataka wananchi kushirikiana na halmashauri yao ili iweze kutoa huduma ambazo zitakabili changamoto zilizopo kwa wananchi na kusema wataendelea kuhudumia wananchi kadiri ya uwezo wao.

Mwisho.      

HALMASHAURI YASAKA MILIONI 16 KUKARABATI TAA ZA STENDI AMBAZO HAZIWAKI MIEZI 10 ILIYOPITA

Na John Gagarini, KibahaHUKU watumiaji wa stendi kuu ya mabasi ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wakilalamika kukosekana kwa taa kwenye stendi hiyo kwa kipindi cha miezi 10 Halmashauri ya Mji wa Kibaha imesema kuwa iko katika harakati za kutafuta fedha kiasi cha shilingi milioni 16 kwa ajili ya kukarabati taa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Mhandisi wa Halmashauri ya Mji huo Dismas Marango alisema kuwa baadhi ya taa kwenye stendi hiyo zimeungua hali inayofanya stendi hiyo kuwa gizani kwa kipindi chote hicho.
Marango alisema kuwa mara baada ya baadhi ya taa hizo kuungua waliwasiliana na Temesa ambao ndiyo wanaohusika na ukarabati wa umeme na magari ya serikali walifuatilia juu ya tataizo hilo na kugundua kuungua kwa baadhi ya taa hizo ambazo ziko zaidi ya 10.
“Waligundua kuungua kwa taa hizo huku nyingine zikiwa hazina mwanga mkali ambapo gharama ya kukarabati ni shilingi milioni 16 ili huduma hiyo iweze kurejea katika hali yake ya kawaida na kuondoa adha ya watumiaji wa stendi hiyo kuwa gizani,” alisema Marango.
Alisema kuwa gharama hizo ni kubwa sana hali ambayo inawafanya washindwe kurejesha huduma ahiyo ya taa kwa muda sasa lakini hata hivyo wanaendelea na michakato ya kutafuta fedha hizo ili kurejesha huduma hiyo.
“Suala hili ni la ghafla hivyo hata bajeti yake haikuwepo lakini tunaendelea na michakato mbalimbali ili kupata fedha hizo ili kuhakikisha taa zinawaka na kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa stendi wakiwemo abiria na wale wanaofanyabiashara kwenye stendi yetu,” alisema Marango.
Aliwataka watumiaji wa stendi hiyo kuwa na uvumilivu wakati Halmashauri ikihangaika kupata fedha kwa ajili ya kurudisha huduma ya taa kwani hata wao wanachukizwa na hali hiyo lakini mipango inafanywa kurudisha hali ya kawaida.
Mwisho.

WALIOTELEKEZA VIWANJA VYA KITOVU CHA MJI WAPEWA MIEZI SITA KUVIENDELEZA

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha imetoa muda wa miezi sita kwa watu walionunua viwanja kwenye kitovu cha mji kujenga kama sheria za ujenzi vinavyoonyesha na kwa sasa hawatakuwa tena na majadiliano kwa watakaoshindwa kujenga watanyanganywa viuwanja hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ambazo watachukua kwa watu walioshndwa kuendeleza viwanja hivyo tangu walipovinunua mwaka 2010 ofisa ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Edward Mbala alisema kuwa watu hao walipew ahadi mwaka 2015 wawe wamejenga.
Mbala alisema kuwa licha ya kupewa muda wote huo lakini watu hao wameshindwa kujenga hadi sasa licha ya kuwa na maongezi ya mara kwa mara kati ya Halmashauri na wawekezaji hao mara kwa mara lakini hadi sasa wameshindwa kuyaendeleza maeneo hayo.
“Mara ya mwisho tuliwaita Aprili mwaka jana lakini walisema kuwa tatizo kubwa lililowafanya washindwe kuanza ujenzi kwenye viwanja hivyo ni hadi pale Halmashauri itakapokuwa imefanya ujenzi wa Stendi na Soko jambao ambalo tuliwaambia kuwa wao waendelee na ujenzi huku sisi tukitafuta wabia kwa ajili ya ujenzi wa vitu hivyo,” alisema Mbala.
Alisema tayari wameshapata benki ambayo itawakopesha kwa ajili ya ujenzi wa soko pamoja na stendi ambapo zaidi ya bilioni 20 zinatarajiwa kutumika kujenga miuondombinu hiyo hivyo wale walionunua viwanja waanze ujenzi.
“Tumesha waambia wayaendeleze maeneo hayo na tayari tumewapa miezi  sita kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo na endapo watashindwa kujenga sheria itachukua mkondo wake kwa kuwanyanganya na kuwapa wengine,” alisema Mbala.
Aidha alisema kuwa tayari wameshatoa matangazo sehemu mbalimbali na kwa wamiliki hao ili waendeleze maeneo yao ambayo ndiyo yanaonyesha sura ya mji  wa Kibaha lakini kwa sasa maeneo hayo bado ni vichaka.
Mwisho.

Sunday, January 3, 2016

KIBAHA KUJENGA STENDI NA SOKO

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja na Soko baada ya kupata mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 20 toka Benki ya Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea baina ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na benki hiyo.

Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado zinaendelea ikiwa ni pamoja na kupata kibali .

“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa ambayo thamani yake itakuwa ni shilingi bilioni 20 pamoja na soko litakalokuwa na thamani ya shilingi bilioni 9 hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo ni dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa wa Pwani hususani wale wa makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake huwalazimu kwenda kununua bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar es Salaam jambo ambalo linafanya bei za bidhaa kuwa juu.

“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa ni kama malango wa Jiji la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita hapa na kwenda huko kisha wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa hivyo kupandisha bei kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo litajengwa sambamba na stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na uwezo wa kuingia na kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na udogo wa soko lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.

Mwisho.
  

   


Saturday, January 2, 2016

MKULIMA AOKOTA BOMU LA KUTUPWA KWA MKONO

Na John Gagarini, Kibaha
MKULIMA wa Mtaa wa Sagare wilayani Kibaha mkoani Pwani Hassan Omary ameokota bomu la kutupwa kwa mkono  ambalo lilisahaulika wakati wa Operesheni Tokomeza iliyofanyika nchini Julai mwaka 2015.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonventura Mushongi alisema bomu hilo lilisahaulika wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo la kukamata wahalifu mbalimbali waliokuwa wakiiba Maliasili za nchi.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka 2015 majira ya saa 5 asubuhi wakati mke wa Omary alipokuwa akilima aligonga kitu kigumu cha chuma na alipokitoa aliona kitu kama bomu na kumwita mumewe aliye waita watu wakiwemo viongozi wa mtaa huo.
“Baada ya kuona hivyo Omary alitoa taarifa polisi na kusema kuwa wameona bomu ndipo polisi walipofika na kubaini kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono ambalo fuse yake ili haribika,” alisema Mushongi.
“Halikuweza kulipuka lakini endapo lingepata joto kali mfano joto la moto lingeweza kulipuka lakini hata hivyo tumeshukuru Mungu kuwa halikuweza kulipuka kwa muda wote huo kwnai endapo lingelipuka lingeweza kuleta madhara,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa baadaye ilibainika kuwa inawezekana bomu hilo la kutupwa kwa mkono liliachwa kwa bahati mbaya  wakati wa Operesheni Tokomeza iliyofanyika Julai mwaka jana.
“Kwa kushirikiana na jeshi letu tutalipelekwa kwa wataalamu wa mabomu ambao ni Jeshi la wananchi (JWTZ) kwa ajili ya kujua zaidi kuhusiana na bomu hilo ikiwa ni pamoja na kuliharibu ili lisiweze kuleta madhara,” alisema Mushongi.
Awali mwenyekiti wa mtaa wa Sagale Bernego alisema kuwa mama huyo alikuwa akisafisha shamba kwenye eneo la Omary ambalo limekuwa likichimbwa vitu vilivyoachwa zamani na watawala wa Kijerumani na Kiarabu maarufu kama Tunu.
Bernego alisema kuwa machimbo hayo ya Tunu yalikuwa yakifanywa na mmiliki huyo ambapo eneo hilo lilizua utata miaka michache iliyopita kwani kumekuwa na mambo ya miujiza yamekuwa yakitokea kwenye machimbo hayo.
Mwisho.        


DEREVA BODABODA ACHOMWA KISU AFA WALIKUWA WAKIGOMBEA MWANAMKE

Na John Gagarini, Kibaha
DEREVA Bodaboda Ally Kasimu (23) mkazi wa Kilimahewa wilayani Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia kwa kuchomwa kisu na waendesha pikipiki wenzake wakati wakigombea mwakanamke.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja kata ya Pangani, Ramadhan Mwaya alisema kuwa marehemu alikufa wakati wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpaya wa 2016 na kuaga mwaka 2015.
Mwaya alisema kuwa marehemu alikutwa na umauti huo akiwa amekaa pembeni na pikipiki yake huku wenzake wakimgombea mwanamke kisha kumchoma yeye kutokana na ugomvi wa wenzake waliokuwa wakigombana.
“Madereva hao pamoja na watu wengine walikuwa kwenye sherehe hizo ambazo ziliandaliwa na Halima Kitwana ambazo ziliambatana na muziki maarufu Kigodoro ulianza majira ya saa 2 usiku na baada ya muziki kwisha baada ya saa sita kamili waliondoka lakini baadaye walionekana kumgombea mwanamke ndipo walipomchoma mwenzao,” alisema Mwaya.
Alisema kuwa marehemu alichomwa kisu sehemu ya tumboni na kujeruhiwa vibaya ambapo walijaribu kumkimbiza hospitali ya Rufaa ya Mkoa  ya Tumbi kwa ajili ya matibabu lakini alifariki wakiwa njiani.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonventura Mushongi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu waliohusika na tukio hilo walikimbia na wanaendelea kutafutwa kujibu tuhuma za mauaji.
Mushongi aliwataka wananchi wa mkoa huo kuwa makini katika kipindi hichi cha sherehe za kusherehekea kuukaribisha mwaka mpya kwa kutotumia vilevi kupita kiasi ili kuepukana na matukio ya uvunjifu wa amani.

Mwisho.