Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Riadha Tanzania (RT) kimetakiwa kiandae mkutano
mkuu wa chama ili kupitia rasimu ya katiba baada ya mkutano kama huo
kuahirishwa Juni na kutakiwa kufanyika Novemba mwaka jana lakini hadi sasa
hakuna taarifa ya kufanyika mkutano kama huo .
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwenyekiti wa
chama cha riadha mkoa wa Pwani (CRAA) Joseph Luhende alisema kuwa baada ya
kushindikana kufanyika kwa mkutano kwa ajili ya kupitisha rasimu hiyo huko
mkoani Morogoro iliamuliwa kuwa mkutano kama huo ufanyike lakini hadi sasa
imekuwa kimya.
Luhende alisema kuwa upitishaji wa rasimu ya chama
ilishindikana kutokan na kuchelewa hivyo kupangwa Novemba mwaka jana na hadi
sasa hakuna taarifa yoyote ya kufanyika mkutano kwa ajili ya kukamilisha zoezi
hilo.
“Mbali ya kushindikana kupitishwa kwa rasimu ya katiba hiyo
pia vyama vilitakiwa visitumie katiba ya zamani na tulivyouliza tuliambiwa kuwa
tusubiri na sasa inakaribia kufika mwaka lakini hakuna lolote linaloendelea
hali ambayo inakatisha tamaa,” alisema Luhende.
Alisema mchezo wa riadha unakumbwa na changamoto nyingi hivyo
rasimu hiyo ingepitishwa ingesaidia kuboresha riadha lakini utekelezaji umekuwa
mgumu na rasimu ndiyo inayopelekea kupata katiba ambayo ni kila kitu sawa na
dira ya mwelekeo wa mchezo huo.
“Utendaji kazi unakuwa mgumu kutokana na kutakiwa tusitumie
katiba ya zamani hivyo ni vema rasimu hiyo ikapitishwa ili tuweze kupata katiba
mpya ambayo itatuongoza,” alisema Luhende.
Aidha alisema kuwa kutokana na mipango ya RT kutokuwa mizuri
kumechangia nchi kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa mfano ile ya
Olimpiki ambapo Tanzania iliambulia patupu kwenye mchezo huo na kuwataka
viongozi wa shirikisho hilo kuwa makini katika kutekeleza majukumua yao.
Akijibu kuhusiana na suala hilo kwa njia ya simu katibu mkuu
wa RT Suleiman Nyambui alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa fedha
ndiyo inapelekea wao kushindwa kuandaa mkutano mkuu wa kupitisha rasimu hiyo ya
katiba ili kupata katiba mpya.
“Tunaendelea kuwasiliana na wafadhili mbalimbali ili tuweze
kupata fedha kwa ajili ya kuandaa mkutano huo wa kupata katiba ambayo itaongoza
chama baada ya mkutano wa awali kushindwa kuendelea baada ya viongozi wa mikoa
ambao walisema hawajaisoma vizuri hivyo ikashindika kuijadili rasimu hiyo,”
alisema Nyambui.
Nyambui alisema walipeleka katiba mikoani kwa ajili ya wao
kutoa mapendekezo lakini hawakuweza kuyapeleka ambapo ni mikoa mitatu tu ndiyo
iliyotoa mapendekezo yake ambayo ni Dar
es Salaam, Arusha na Dodoma huku mingine ikiwa bado.
“Tunatarajia kuitisha mkutano mkuu kabla ya mwaka haujaisha
ili kukamilisha zoezi la kupata katiba baada ya marekebisho kufanyika kwenye
mkutano na kikwazo kikuu ni ukosefu wa fedha,” alisema Nyambui.
Mwisho.