Na John Gagarini,
Kibaha
KAMATI za Maadili kwenye klabu za waandishi wa habari nchini
zimetakiwa kutumia busara katika kuwapatanisha waandishi na wadau mara
kunapotokea migongano baina yao ili kumaliza pasipo kwenda mahakamani kuepusha
vyombo vya habari kutozwa faini kubwa.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na ofisa kutoka baraza la habari
Tanzania (MCT) Asterius Banzi wakati wa mafunzo ya siku moja kwa kamati ya
maadili ya Chama Cha Waandishi wa habari mkoani Pwani (CRPC) yaliyofanyika
kwenye ofisi za chama hicho.
Banzi alisema kuwa ni vema kamati hizo zikatumia uungwana
kutatua migogoro kwani endapo malalamiko hayo yatapelekwa mahakamani athari
zake ni kubwa hasa kwa upande wa vyombo vya habari kupigwa faini kubwa ambazo
zitasababisha vyombo hivyo kufungwa.
“Baadhi ya walalamikaji wamedai fidia kubwa kwa vyombo vya
habari na kupeleka vyombo hivyo kufungwa au kuyumba na kushindwa kuhudumia
wananchi kupata taarifa ikiwa ni moja ya haki zao za msingi za kikatiba,”
alisema Banzi.
Aidha alisema kuwa ni vema mambo hayo yakatatuliwa kirafiki
kwani endapo yakifikishwa mahakamani athari zake ni kubwa kuliko yangemalizwa
kwenye kamati hizo.
Pia alivitaka baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinakutana
na matatizo ya kuwachafua wadau wao ndani ya jamii kukubali kukaa meza moja na
walalamikaji ili kufikia muafaka kwa kujenga mahusiano mazuri.Banzi alisema
kuwa vyombo vya habari na wananchi ni marafiki hivyo lazima kuwe na mahusiano
mazuri kwa pande zote ili kuepuka migogoro isiyo na lazima.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imemchagua wakili wa
kujitegemea Saiwelo Kumwenda kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ambayo imetuliwa na
chama hicho.
Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikwenda kwa Elizabeth Ngai huku
katibu wa kamati hiyo akiwa ni Athuman Mtasha.
Kamati hizo kwenye klabu za waandishi wa habari ziliundwa kwa
lengo la kusuluhisha migogoro baina ya wanahabari na wadau ili kuzingatia
maadili ya kazi za waandishi wa habari.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka
amewataka waandishi wa habari mkoani humo kujiunga na mafunzo ya Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) kwenye kambi ya Ruvu uiliyopo Mlandizi wilayani Kibaha
yanayotarajiwa kuanza wakati wowote ili kujiimarisha kikakamavu na kujenga
uzalendo wa nchi yao.
Aliyasema hayo hivi karibuni aliopoongea na waandishi wa
habari mjini Kibaha na kusema kuwa mafunzo ya JKT ni muhimu hasa ikizingatiwa
yanamfanya mshiriki kujua uzalendo wa nchi yake kama wanavyotarajia kwenda
baadhi ya wabunge mafunzo hayo yatakapoanza.
Koka alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watu wa aina
yote na si kwa baadhi ya watu kwani waandishi wataweza kuielezea vizuri nchi
yao pale watakapokuwa wakiandika habari zao.
“Kazi ya uandishi ni sawa na ya jeshi hivyo endapo watapata
mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku ambapo wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa,” alisema Koka.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi hichi waandishi wamekuwa
wakishambuliwa hivyo endapo watapata mafunzo hayo yatawasaidia kujilinda na
baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwateka waandishi na kuwadhuru.
“Zamani watu wengi walipitia mafunzo hayo kwa mujibu wa
sheria hivyo kwa sasa kwa kuwa serikali imerejesha mafunzo hayo na waandishi
nao wajitokeze ili waweze kupata mafunzo ambayo ni mazuri katika kuuweka mwili
vizuri pia kuweza kujilinda,” alisema Koka.
Alibainisha kuwa waandishi kama baadhi ya wabunge
waliojitokeza kushiriki mafunzo hayo nao wajitokeze, hivi karibuni serikali
ilirudisha utaratibu wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kuanzia mwaka huu.
Katika hatua nyingine alilaani baadhi ya watu ambao wamekuwa
wakiwashambulia waandishi na kusema kuwa kufanya hivyo ni kunyanganya uhuru wa
vyombo vya habari katika kufanya kazi zao.
Alisema inashangaza kuona waandishi wanashambuliwa pasipokuwa
na sababu za msingi na kuwasababisha kufanya kazi zao kwa woga kuhofiwa
kupigwa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM)
kutoka wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Rugemalila Rutatina amewataka vijana
kwenye wilaya hiyo kukitumia chuo cha ufundi Stadi (VETA) kilichopo wilayani
humo ili kujiongezea ujuzi kuliko kuwaachia vijana kutoka mikoa mingine kusoma
kwenye chuo hicho.
Aliyasema hayo hivi karibuni mjini Kibaha alipokutana na
baadhi ya vijana kutoka kata mbalimbali kwenye wilaya ya Kibaha, kuzungumzia
masuala ya kuboresha mazingira katika wilaya hiyo na kusema kuwa vijana wengi
hawakitumii chuo hicho ambacho kimejengwa eneo la Kongowe.
Rutatina alisema kuwa inashangaza kuona vijana kwenye wilaya
na mkoa wa Pwani kutokitumia chuo hicho licha ya wao kuwa jirani na chuo hicho
huku vijana wengi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa wanakitumia ipasavyo
chuo hicho.
“Changamoto kubwa inaonekana ni vijana wengi kutokukitambua
chuo hicho kutokana na kukosa taarifa za uwepo wake jambo ambalo linawafanya
washindwe kujiunga nacho hivyo vijana wanapaswa kutafuta taarifa na si kusubiri
vijana toka nje ya mkoa wajae na kuanza kulalamika,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa hiyo ni fursa ambayo vijana wa Kibaha na mkoa
wanapaswa kuitumia kwani hata kama hawajafanikiwa kusoma masomo ya sekondari
wana nafasi ya kujiunga na chuo hicho ambacho kinawapatia stadi za ufundi
mbalimbali.
“Kama tujuavyo ufundi ni muhimu kwani kila kitu kinauhusiano
na ufundi hivyo taaluma ya ufundi haiwezi kuepukika kwa maendeleo ya jambo
lolote na hiyo ndiyo itakayowasaidia vijana katika mkoa wa Pwani kujikwamua na
hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kwamba hata masuala ya biashara na ujasiriamali
yanafundishwa ambapo vijana wengi kwa sasa wamejiajiri na endapo watapata
mafunzo ya chuo hicho wataweza kupata ujuzi na kuboresha shughuli zao.
“Maisha mazuri hayawezi kuja bila ya kujishughulisha kwani
wakijiunga na mafunzo ya VETA wataweza kujiajiri na kukabiliana na tatizo la
ajira kwa vijana kwani wataweza kujiajiri kupitia elimu watakayokuwa wameipata
kwenye chuo hicho,” alisema Rutatina. Chuo hicho kilizinduliwa mwaka jana na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mwisho.
Na John
Gagarini, Kibaha
WAKAZI zaidi
ya 1,500 wa Mtaa wa Zogowale, Kibaha Mjini mkoani Pwani, wanatarajia kunufaika
na mradi wa maji ambao una uwezo wa kutoa maji lita 6,000 kwa saa.
Akizungumzia
mradi huo wakati wa uzinduzi wa mradi huo ,mhandisi wa maji katika halmashauri
ya mji wa Kibaha Grace Lyimo alisema idadi hiyo ya watakaonufaika ni sawa na
asilimia 1.4 ya wananchi wa Kibaha Mjini hivyo kufanya jumla ya wanaopata maji
kuwa ni asilimia 64.
Lyimo alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya mradi ulianza rasmi Mei
2012 na kukamilika mwaka huu kwa gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 192
ambapo mkandarasi ameshakabidhiwa zaidi ya milioni 156 hadi sasa.
“Mradi wa maji Zogowale uliibuliwa na jamii yenyewe
na
wananchi walipaswa kuchangia zaidi ya milioni Nne ikiwa ni asilimia
2.5 ya gharama ya ujenzi ambapo waliweza kuchangia milioni moja na
laki saba na arobaini na tano, miasaba sabini na tano,” alisema Lyimo.
Aidha alisema
kwa sasa mkandarasi anaendelea na umaliziaji wa kazi
ndogondogo zinazojitokeza na mfumo wa maji upo kwenye uangalizi kwa miezi sita.
Aliwataka wananchi
kulinda miundombinu hiyo ya maji ili huduma hiyo iwe ya uhakika kwa lengo la
kuondokana na kero ya maji katika mtaa huo.
Mwisho