Sunday, May 17, 2026

UMOJA WA WANAUME MKOMBOZI (UWWM) KUNUNUA MABASI MAWILI

UMOJA wa Wanaume Mkombozi (UWWM) wanatarajia kununua mabasi madogo mawili ya abiria ili kukabiliana na changamoto ya usafiri kutoka na kuingia kwenye Mtaa wa Mkombozi uliyopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Hayo yalisemwa na Katibu wa (UWWM) Mwinjilisti Williama Wami wakati wa uzinduzi wa umoja huo na Mfuko wa umoja ambapo changamoto ya usafiri ni kubwa kwani kuna basi moja tu linalofanya safari zake kati ya Mkombozi na Mbezi Jijini Dar es Salaam.

Wami alisema Mtaa huo umepakana na Wilaya ya Ubungo ambapo wanapata mahitaji yao eneo la Kibamba Njia Panda Shule kutokana na ukaribu tofauti na Kibaha ambako ni mbali.

"Wakazi huku ni wengi sana lakini tatizo kubwa ni usafiri ambapo kutokana na ubovu wa barabara magari mengi hayawezi kufika kwani kuna basi moja tu ambalo linatoa huduma lakini sisi malengo yetu ni kununua mabasi madogo mawili ili kurahisisha usafiri,"alisema Wami 

Alisema kuwa kwa sasa wanatumia usafiri wa pikipiki ili kufika majumbani au kutoka kwenda kwenye shughuli zao za kila siku kujiletea kipato lakini usafiri huo ni gharama kubwa sana.

"Kupitia umoja wetu tulihamadisha kupatikana kwa basi hilo lakini bado halikidhi mahitaji kwani uhitaji ni mkubwa sana kwani uwezo wa baadhi ya watu kupanda pikipiki kwao ni mzigo mkubwa lakini kupitia daladala gharama inakuwa nafuu,"alisema Wami.

Aidha alisema kuwa malengo yao mengine ni kujenga ukumbi mkubwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano na sherehe utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 500 ambapo kwa sasa huwabidi kufanya shughuli hizo nje ya mtaa huo pia kuanzisha Chama Akiba na Mikopo ili kukopeshana kwa riba nafuu.

"Vitu tulivyofanya ni kuvuta maji na kujenga vyoo vya kisasa kwenye soko jipya na tunatarajia hapo kuwa na stendi tunaishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kutuanzishia soko tunaomba watupe kibali ili watu waanze kufanya biashara,"alisema Wami.

Aliongeza kuwa miradi hiyo mbali ya kutoa huduma itakuwa ni vyanzo vya mapato ya umoja kwani lengo ni kuleta maendeleo ya Mtaa na kwa mwananchi mmoja mmoja pia ni kusaidiana katika shida na raha na kauli mbiu ni Baba kichwa cha Familia.

Umoja huo ulianzishwa mwaka jana na una wanachama 265 huku wanachama hai ni 205 hadi sasa wana kiasi cha shilingi milioni 10 benki ambapo kila mwezi mwanachama huchanga shilingi 5,000.

Thursday, May 14, 2026

UMOJA WA WANAUME MKOMBOZI WASAIDIA KUPATIKANA DAMU CHUPA 13



UMOJA wa Wanaume Mkombozi (UWWM) umefanikisha kupatikana kwa damu kiasi cha chupa 13 kwa ajili ya Kituo cha Afya Kata ya Pangani Wilayani Kibaha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa umoja  kilichopo Mtaa wa Mkombozi Wilayani Kibaha Katibu wa UWWM Mwinjilisti William Wami alisema kuwa lengo ni kuisaidia wagonjwa kwenye kituo hicho.

Wami alisema kuwa umoja huo ulianzishwa kwa ajili ya kuisaidia jamii katika masuala mbalimbali ili kuleta maendeleo kwenye Mtaa huo na Wilaya nzima ya Kibaha.

"Mbali ya kuchangia damu pia tumepanda miti kwenye eneo itakapojengwa Zahanati kwenye Kituo cha Afya cha Kata ya Pangani na Shule ya Msingi Mkombozi lengo likiwa ni kutunza mazingira kwenye maeneo hayo,"alisema Wami.

Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Diwani wa Kata ya Pangani John Katele ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha alisema kuwa umoja huo umeonyesha moyo wa kibinadamu wa kujitolea ili kunusuru maisha ya wengine.

Katele alisema kuwa damu ni muhimu sana hasa kwa wanawake ambao wanajifungua kwani huhitaji damu nyingi au wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kwenye kituo hicho. 

Katele alisema kuwa jamii inapaswa kujitolea ili kukabiliana na changamoto ya damu kwenye kituo hicho hivyo kupunguza changamoto hiyo kwani damu huhitajika wakati wote.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Alex Ditopile alisema kuwa anawashukuru wananchi waliojitolea damu kwani tayari wameshaanza kuzalisha mama wajawazito na matumizi ya damu ni makubwa kwani kwa mwezi wanatumia chupa 10.

Ditopile alisema kuwa kwa sasa wana chupa tano na inapotokea wameishiwa damu huchukua Kituo cha Afya cha Lulanzi na kwa sasa wanapokea wagonjwa wengi tangu kituo hicho kilipofunguliwa Desemba 2025.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkombozi Jackson Msaki alisema kuwa kikundi hicho ni kwa ajili ya wanaume wote kwenye Mtaa huo na haubagui mtu yoyote.

Msaki alisema kuwa umoja huo umeweza kuhamasisha kupatika kwa usafiri wa daladala kutokea Mtaa huo hadi Mbezi kujenga choo na kuvuta maji kwenye soko jipya.

Umoja huo ulianzishwa mwaka 2025 kikiwa na wanachama 105 huku kwa sasa kikiwa na wanachama 265 hai wakiwa 205 kikiwa na kauli mbiu ya "Mwanaume Kichwa cha Familia".


Thursday, May 7, 2026

RAIS SAMIA ANAENDELEA KUPELEKA FURAHA NA NEEMA KWA WATUMISHI WA UMMA TANZANIA.-KIKWETE


Nimezungumza na maafisa tawala na RasilimaliWatu , katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa AICC, Arusha na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao na kuleta furaha kwa watumishi wa umma ili kwa upande mwengine nao wapeleke furaha na neema kwa Watanzania . 

Nimeyaeleza hayo kufuatia maamuzi mbalimbali yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha maslahi ya Watumishi wa umma nchini yanaboreka. 

Uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali kupandisha madaraja watumishi 219,042 ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha utumishi wa umma nchini Tanzania. 

Hatua hii ambayo imepata ridhaa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma (2025): +35.1% , Ongezeko la kima cha chini sekta binafsi (2025/26): +33.4% 

Aidha Sekta mbalimbali zinakwenda athiriwa na maboresho haya ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, baharini, madini ,utamaduni n.k 


Matokeo haya kitakwimu zinaonyesha kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo inaonyesha uongozi wa kimkakati unaoweka mbele ustawi wa watumishi na ufanisi wa taasisi za umma.

Tuesday, May 5, 2026

VIJANA WATAKA MFUMO UKOPAJI UBORESHWE KUVUTIA VIJANA

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kibaha Mjini umeishauri Wizara ya Maendeleo ya Vijana kuangalia upya mfumo wanamna ya kuwapata vijana kukopa ili wengi waweze kunufaika.

Akizungumza ofisini kwake Katibu wa (UVCCM) Kata ya Tangini Lazaro Benjamin alisema kuwa Wizara inapaswa kuweka mfumo rafiki na kuweka masharti nafuu.

Benjamin alisema kuwa kuweka masharti magumu kunakwamisha vijana wengi kupata fursa ya kufikia mikopo hiyo inayowalenga vijana.

"Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa wanapokosa mitaji wanakosa fursa ya kujiajiri na matokeo yake ni kuongezeka kwa ukosefu wa ajira umasikini na hata kukata tamaa,"alisema Benjamin.

Alisema kuwa kuna umuhimu sasa wa kuongeza bajeti ya mikopo ya vijana ili iwafikie wengi zaidi pia kutoa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili mikopo itumike kwa ufanisi.

"Lengo liwe ni kuwafikia vijana wengi zaidi iwezekanavyo kwani maendeleo ya Taifa letu yanategemea uwezeshaji wa vijana wake na wafanye maboresho ili kuhakikisha uwiano unazingatiwa,"alisema Benjamin.

Aidha alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kwani hiyo ni hatua kubwa na ya kupongezwa na inaonesha dhamira ya kweli ya serikali katika kuinua vijana wa Taifa la Tanzania.

"Wizara ifanye utafiti kwani takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya vijana 30,384 waliomba mikopo hii lakini vijana waliokidhi vigezo vya kukopeshwa ni 1,961tu,"alisema Benjamin.

Aliongeza kuwa idadi kubwa sana ya vijana zaidi ya asilimia 90 hawakupata fursa hiyo utafiti ufanyike ili kujua ni kwa nini idadi hiyo kutokidhi vigezo na kama bajeti ni ndogo basi iongezwe ili asilimia ya vijana wanaoomba mikopo waweze kuongezeka na kupanua wigo wa ajira kwani wakipata watajiajiri.