Wednesday, December 6, 2023

TPFNET CHALINZE WATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO DOLPHINE.

 

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoa wa Pwani, Disemba 05, 2023 wametoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika kituo cha Dolphine kilichopo Kijiji cha Kipera, Kitongoji cha Mwanabele Wilayani humo.

Akizungumza akiwa kituoni hapo,  Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lyidenge alisema jukumu la ulezi wa watoto wenye uhitaji na kuwatunza ni la jamii nzima hivyo wao wakiwa ni sehemu ya wazazi wameguswa katika siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa Kijinsia kufikia kwa watoto hao wenye uhitaji na kuweza kutoa msaada wa vitu mbalimbali. 

"Jamii inapaswa kutambua malezi ya watoto na kuwatunza na kuwatembelea mara kwa mara kujua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi watoto wenye uhitaji kwenye vituo vya malezi ni la watu wote na kufanya hivyo ni kuwapa faraja watoto walio kwenye vituo hivyo kuona jamii ina wajali na kuwathamini".Alisema Lyidenge.

Lyidenge amewapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa malezi ya watoto hao akiweka wazi kuwa jambo wanalolifanya la kuwalea watoto kwenye maadili mema ni kubwa sana mbele ya Mungu na la kupongezwa. 

Amesema kuwa watoto hao endapo wangeachwa bila ulezi kwenye kituo hiki wangeweza kuwa katika makuzi mabaya hivyo kutumbukia kwenye makundi ya kihalifu na hivyo kupeleka Jamii kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili.

Aidha, Lyidenge amewaasa watoto hao kuwa wasikivu kwa walezi wao na kutambua kuwa wao ni taifa la kesho akiwasisitiza kusoma kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za changamoto walizonazo kwa walezi wao bila woga ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii  Bi. Linna Jackson Mlay ameahidi kuendeleza ushirikiano na walezi wa kituo hicho katika kutatua changamoto mbalimbali walizonazo.

Nae msimamizi wa kituo hicho Anna Munisi amelishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze kwa msaada waliowapatia na kuomba wananchi wengine kuendelea kusaidia kituo hiko kwani uhitaji ni mkubwa katika maelezi ya watoto waliopo kituoni hapo.

Msaada uliotolewa na Jeshi la Polisi kituoni hapo ni unga wa sembe, mchele, sabuni,  madaftari, kalamu na taulo za watoto.

Monday, December 4, 2023

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI YAWATAKA WANAWAKE KUMUENZI BIBI TITI MOHAMED KWA KULETA MAENDELEO

WANAWAKE nchini wametakiwa kupambana kuiletea nchi maendeleo kama alivyofanya Bibi Titi Mohamed ambaye aliasidiana na Mwasisi wa Taifa Julius Kambarage Nyerere kuleta uhuru wa Tanzania.

Aidha amewataka kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo. 

Hayo yamesemwa Mlandizi Wilayani Kibaha na Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Punzi wakati wa mafunzo kwa wanawake ya Ijue Kesho yako.

Punzi amesema kuwa katika kupigania nchi kupata uhuru alishirikiana na Bibi Titi Mohamed hadi Uhuru ukapatikana hivyo wanawake nao wawe mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya nchi.

"Nyerere alijenga misingi ya maendeleo na aliona umuhimu wa mwanamke na ndiyo sababu alishirikiana na Bibi Titi katika mapambano ya Uhuru hivyo nanyi msikae nyuma lazima mpambane kuleta maendeleo ya nchi,"amesema Punzi.

TASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI YAWAPONGEZA WAANDAJI WA MAFUNZO YA IJUE KESHO YAKO KWA WANAWAKE MLANDIZI KIBAHA

 


Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ndugu Omary Punzi wakati wa mafunzo ya Ijue Kesho yako kwa wanawake wa mkoa wa Pwani yaliyofanyika Mlandizi Wilayani Kibaha.

Punzi alipata nafasi ya kuwashukuru na kuwaambia wanawake kuwa Mwalimu Nyerere alijenga misingi ya Uzalendo, kujituma na kujitoa kwa hali na mali katika nchi na misingi ambapo misingi hiyo ilitokana na nguvu ya Mwanamke katika kuleta maendeleo.

Alisema Mwalimu Nyerere katika Uongozi wake alijitahidi sana kuwainua wanawake mfano mzuri ni Bibi TITI MOHAMMED ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu katika kupigania Uhuru wa Taifa  na hakuna Taifa lolote linaloendelea ikiwa Mwanamke atawekwa nyuma.

"Ushauri wangu serikali inatakiwa kuwekeza nguvu kubwa ya kuhakikisha mwanamke anapatiwa mahitaji yote ya msingi endelevu ya kumwezesha katika kumuinua kiuchumi,"alisema Punzi.

Kwa upande wake mgeni rasmi Mkali Kanusu mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini ambaye alimwakilisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM NEC Hamoud Jumaa, aliwapongeza waandaji na wawezeshaji kwa mada zilizokuwa zinatolewa ni nzuri na mahiri kwa wakati tulionao kwa Serikali ya Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kanusu alishauri matukio kama hayo yafanyike mara mbili kwsa mwaka kwani itasaidia kuwakumbusha watu maadili ya Watanzania na kama chama wamelipokea na kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za maendeleo kwa wanawake wa Kibaha na Tanzania kwa ujumla.

Naye Mwakilishi wa Taasisi ya IJUE KESHO YAKO Ndugu Martha Kyoka alisema lengo kuu la Taasisi hiyo ni kuhakikisha wanamjengea uwezo mwanamke kujitambua na kutekeleza malengo katika maisha na jamii kwa ujumla ambapo takribani wanawake 100 walipatiwa mafunzo hayo.

Masomo waliyofundishwa ni pamoja na Afya ya Akili, malezi ya mume na mtoto nyumbani, nafasi ya kujitambua, Uwekezaji, Maono na Mikopo na Ujasiriamali.

Sunday, November 26, 2023

*KATENI UMEME KWA WADAIWA - DKT. BITEKO AIAGIZA TANESCO*

*📌Akemea vikali wahujumu wa miundombinu ya umeme, Asema Serikali iko kazini, Itawashughulikia*

*📌Ataka TANESCO  kusikiliza na kujibu Wateja kwa haraka*

*📌Asisitiza utunzaji wa Mazingira*

Arusha

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia umeme ambapo Shirika hilo linadai jumla ya Shilingi Bilioni 224 kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Binafsi na waliohama na madeni kutoka mita za zamani za umeme kwenda za kisasa hali inayopelekea changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Amesema hayo tarehe 26 Novemba 2023, wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru mkoani Arusha ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi  wa ujenzi  wa njia  kuu ya umeme  ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya ( Kenya- Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP).

“Hapa Arusha tu, TANESCO anadai wateja wake shilingi bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wanachi wadogowadogo bali Taasisi za Serikali na Wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira,  wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira; TANESCO anahitahi fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko pia ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi na ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za umeme nchini kwa aina mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwepo wa Julius Nyerere (MW 2115), ambao umefikia asilimia 94 ambapo amesema kuwa, Mkandarasi ameshafunga mashine mbili tayari kwa kuanza majaribio ya kuzalisha umeme.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekemea vikali watu wote wanaohujumu miundombinu ya umeme akitolea mfano wizi wa shaba na mafuta ambapo kati ya tarehe 25 Novemba, 2023 na 26 Novemba, 2024 kuna matukio 14 katika Ukanda wa Pwani ya kuharibu au kuhujumu miundombinu ya umeme, ambapo ameeleza kuwa, Serikali itawashughulikia kwa kuendesha msako na watakapopatikana sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye Shirika hilo ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe, “huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi.” 

Dkt. Biteko ametaka Watanzania  kulinda vyanzo vya maji ambavyo vinazalisha umeme, amesema vyanzo hivyo visipolindwa vitapelekea athari mbalimbali zikiwemo kwenye uzalishaji umeme, na pia ameitaka TANESCO kutokukaa nyuma  katika masuala ya utunzaji wa mazingira bali washirikiane na Wizara inayoshughulika na suala la mazingira na NEMC ili wote kwa pamoja washirikiane kusimamia mazingira.

Kuhusu utekelezaji wa kituo hicho cha umeme cha Lemuguru kilichopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Dkt. Biteko amesema kuwa mradi huo ni mkubwa na unagharimu Dola za Marekani milioni 258.8 na kina faida mbalimbali ikiwemo kupelekea wananchi umeme usiokatika mara kwa mara na kituo kitaimarisha hali ya umeme mkoani Kilimanjaro na Arusha.

Dkt. Biteko vilevile ameipongeza TANESCO kwa hatua mbalimbali inazochukua ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuongeza kiwango cha Gesi Asilia kinachozalisha umeme.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa njia Kuu ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga kuelekea Kenya, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Peter Kigadye, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoani na migodi ya uchimbaji madini na hivyo kuwezesha kufikia uwezo wa juu wa megawati 2000 katika kusafirisha umeme.

Amesema, utekelezaji wa mradi unahusisha vipengele Sita  ikiwemo ujenzi wa njia 8 za laini ya kV 400/33 kutoka Kituo kipya cha kupoza umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha yenye urefu wa kilomita 414.3, Babati -Arusha kilomita 150, Arusha –Namanga, Kilomita 114.3 ambao umefikia asilimia 96.

Ameeleza mradi huo pia unahusisha, upanuzi wa vituo vya kupoza umeme ambao umefikia asilimia 98.72, mradi wa usambazaji umeme kwa vijiji vilivyopitiwa na mradi vijiji na ujenzi wa vituo vyq kupoza umeme vya Dodoma, Singida, ambavyo vimekamilika.

*DKT. BITEKO ATUNUKU VYETI KWA WAHITIMU 439 CHUO CHA MWEKA*

 

*📌Awataka kuchukia rushwa na kulinda Maliasili kwa Wivu Mkubwa*

*📌Apongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi wa Sekta*

*Kilimanjaro* 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametunuku vyeti vya ngazi mbalimbali kwa wahitimu 439 wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka, mkoani Kilimanjaro ambapo amewaasa kuwa chochote watakachofanya kuchukia rushwa, kutojitajirisha katikati ya hali ngumu za wananchi na walinde maliasili za nchi kwa wivu mkubwa na kuwa walinzi wa wenzao.

Amesema hayo tarehe 25 Novemba, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mahafali ya 59 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, mkoani Kilimanjaro ambapo Mahafali hayo yameenda sambamba na Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo hicho.

“Chuo hiki ni kiungo muhimu katika Sekta ya Maliasili na Utalii, kuanzishwa kwake kulitokana na  tamko la Baba wa Taifa, Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Kongamano la Uhifadhi wam Wanyama Pori mwaka 1961, na kupitia tamko hilo alionesha dhamira na utayari wake wa kuifanya Afrika kuwalinda wanyama na mazingira yao kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo, hivyo nyinyi ndio mnaoendeleza kazi lengo hilo la Baba wa Taifa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Chuo hicho pia ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani kwani Chuo hicho kinapata wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema kuwa, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa Chuo hicho katika ukuaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini na hivyo ameahidi kuwa kama kuna changamoto zozote Serikali itazichukua na kuzifanyia kazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia vyema sekta ya Maliasili na Utalii ambayo amesema kuwa ni kiungo kikubwa kwenye uchumi wa nchi kwani bila Sekta hiyo mapato na fedha zinazohitajika kuendeleza miradi mbalimbali zinaweza kuwa na changamoto ya upatikanaji.

Amesema, Utalii unachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, na asilimia 25 ya fedha za kigeni, pia ni chanzo kikubwa cha ajira nchini kwani unachangia ajira milioni 1.5 na zaidi ya asilimia 11 ya ajira zote hapa nchini.

Dkt. Biteko aliongeza kuwa, asilimia 80 ya Utalii nchini unatokana na Wanyama pori, ambao wametokana na mazingira yetu tuliyoyahifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, misitu pamoja na hifadhi za wanyama.

Katika Mahafali hayo wahitimu 439 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Utalii, Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, Stashahada ya Juu ya Utalii wa Wanyamapori, Astashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori na Cheti cha Msingi cha Usimamizi wa Wanyamapori.  

Mahafali hayo yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Ricardo Mtumbuida.

Thursday, November 23, 2023

MAOFISA KILIMO PWANI WAPEWA VISHKWAMBI KUBORESHA UTENDAJI KAZI

MKOA wa Pwani umewakabidhi Vishkwambi 345 kwa Maofisa Kilimo wa Wilaya za mkoa huo ili kuleta tija na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge wakati akikabidhi vifaa hivyo ambavyo vimetolewa na Serikali.

Kunenge amesema kuwa matumizi mengine ni kusajili wakulima ambao bado hawajaingizwa kwenye mfumo na kuboresha taarifa za wale waliosajiliwa ili wahudumiwe kwa idadi na kujua mahitaji yao ya pembejeo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala wa mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amesema wanaishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwapatia vifaa hivyo.

Naye Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Joseph Njau amesema kuwa vifaa hivyo vitawawezesha kutekeleza majukumu yao na kuongeza uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima kwenye maeneo yao.

Wednesday, November 22, 2023

JAMII MKOANI PWANI YATAKIWA KUWALINDA WATOTO

JAMII Mkoani Pwani imetakiwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kumuondolea vikwazo na kutoa taarifa kwa wanaofanya vitendo vya ukatili ili mtoto aweze kutimiza ndoto zake.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta alipokuwa akizindua mradi wa Usalama wa Watoto (UWAWA) awamu ya pili unaosimamiwa na Christian Social Services Commission (CSSC).  

Mchatta amesema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi ambapo jamii inatakiwa kuwalinda kwani nao wana ndoto zao za kuwa nani katika jamii mara wamalizapo masomo yao.

"Mradi wa uwawa una lengo la kuimarisha usalama wa watoto utasaidia kuanzishwa dawati la kushughulikia changamoto za watoto kukabiliana na ukatili kwa watoto shuleni na sehemu yoyote wawapo watoto,"amesema Mchatta. 

Naye Ofisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto wakati mwingine vinatokana na utandawazi na baadhi wanafanyiwa na wazazi wa kuwazaa kama kuwanyima chakula na watoto hujikuta wakifanya vibarua ili wapate fedha.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki wa (CSSC) Makoye Wangeleja amesema kuwa wanaushukuru mkoa kwa kutoa ushirikiano kwani vita hiyo siyo lelemama kwani watu wanaowafanyia vitendo hivyo ni watu ambao huwezi kuwafikiri na inabidi kujipanga ili kukabili vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto na watafuata taratibu ili kuweka misingi mizuri ya kuwalinda watoto.