Sunday, October 8, 2023

*WAZIRI KAIRUKI AIPONGEZA TAWA KWA USIMAMIZI BORA WA WANYAMAPORI NCHINI*

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa jitihada za dhati katika kuleta maendeleo ya uhifadhi nchini ikiwa ni pamoja na Usimamizi mzuri wa Wanyamapori 

Mhe. Kairuki ametoa pongezi hizo Oktoba 7, 2023 alipotembelea bustani ya Wanyamapori hai katika maonesho ya Saba ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo - SITE yanayofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam

".. niwashukuru wote lakini zaidi niwashukuru TAWA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya kwa ajili ya maendeleo ya uhifadhi pamoja na kuendelea kusimamia hifadhi zetu mbalimbali na kuhakikisha pia kunakuwa na Utalii ambap ni endelevu unaozingatia masuala mazima ya uhifadhi" alisema Mhe. Kairuki

Aidha Waziri Kairuki amesema Wizara yake kupitia TAWA imepeleka bustani ya Wanyamapori hai katika maonesho hayo ili kuendelea kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na kuvitumia na kuona rasilimali tulizonazo kama Taifa.

Maonesho haya  yanafikia tamati leo Oktoba 8, 2023.

JUMUIYA WAZAZI PWANI YATAKA MAMLAKA USIMAMIZI KUSHIRIKIANA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani amezitaka mamlaka za usimamizi kushirikiana katika utoaji wa vibali ili kuondoa muingiliano wa kimamlaka.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Wazazi mkoa wa Pwani Jackso Kituka wakati wa kikao cha Baraza la Wazazi Mkoa kilichoganyika Mjini Kibaha.

Kituka amesema kuwa baadhi ya mamlaka zimekuwa zikitofautiana kimaamuzi ambapo moja inaweza ikawa inakataa huku nyingine ikiruhusu kuhusu suala fulani.

"Mfano kama vile Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) linakataza upigaji wa muziki wenye kelele ambapo ni uchafuzi wa mazingira lakini ofisi ya utamaduni inaruhusu upigaji wa muziki kwenye kumbi za starehe,"amesema Kituka.

Naye ofisa mazingira kutoka NEMC Joseph Rugatiri akijibu baadhi ya maswali kuhusu mazingira amesema kuwa vibali vya uchimbaji mchanga hutolewa na halmashauri kama taratibu za uchimbaji mchanga zinakiukwa wananchi wanapaswa kutia malalamiko kwenye ofisi za mitaa na kama hakuna marekebisho taarifa zipelekwe kwao ili wachukue hatua na kuhusu kelele za muziki alisema kila eneo lina kiwango cha sauti.

Saturday, October 7, 2023

NSSF PWANI YAWA YA TATU KITAIFA UTOAJI HUDUMAFA

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Pwani, umeshika nafasi ya tatu kitaifa katika utoaji huduma kwa ufanisi kwa wateja wake.

Aidha mfuko huo umeahidi utendaji kazi unaoendana na kasi ya Nssf ya sasa ambayo inahitaji ujali kwa wateja na kutoa huduma bora.

Kaimu Meneja NSSF Pwani Rehema Mutungi akifunga maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kimkoa, alieleza utoaji huduma bora kwa wateja wao ni jadi yao na imeonyesha dhahiri nafasi waliyoipata kitaifa.

"Tunahitaji kufika namba moja ,huu ni utamaduni wetu kuhudumia wateja kwa ubora na kwa wakati ,tunaamini miaka ijayo tutafanya vizuri zaidi"alieleza Rehema.

Rehema anasisitiza ushirikiano,umoja kwa watumishi na watendaji wa NSSF ili kutoa huduma kwa ufanisi.

Vilevile Rehema alihimiza ,kila mmoja kujitathmini na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kudumisha imani kwa wanachama na wadau.

Katika kufunga maadhimisho hayo kimkoa wametoa vyeti na zawadi kwa wa

Friday, October 6, 2023

MKOA WA PWANI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

SERIKALI ya Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Serikali Kuu itahakikisha miundombinu muhimu inayotumika kwenye maeneo ya uwekezaji inajengwa ili kuwaondolea usumbufu wawekezaji.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipotembelea kiwanda cha King Lion Investment (King Lion Steel Mill) kinachojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za chuma kilichopo eneo la viwanda la Zegereni Wilayani Kibaha.

Kunenge amesema kuwa serikali inatekeleza miradi mbalimbali kwenye maeneo ya uwekezaji ikiwemo ya Barabara, Umeme, Maji na Gesi ili kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake meneja wa kampuni hiyo Arnold Lyimo amesema kuwa mradi huo unagharama ya zaidi ya shilingi bilioni 160 na kitakuwa kiwanda kikubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na utakamilika Juni 2024 na kuanza uzalishaji.

Lyimo amesema kuwa kitakapokamilika kitazalisha chuma tani 350,000 kwa mwaka ambapo malighafi za kuzalishia chuma na zitauzwa ndani na nje ya nchi zikiwemo Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na kitatoa ajira 400 za moja kwa moja 5,000 ajira za muda.

Thursday, October 5, 2023

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MKOA WA PWANI LATOA TAHADHARI MVUA ZA EL NINO

 

*TAARIFA YA KAMANDA WA ZIMAMOTO PWANI ALIPOKUWA MGENI RASMI MAHAFALI YA 16 SHULE YA SEKONDARI KWALA - KIBAHA*

KAMANDA wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani SSF Jenifa Shirima kuwakumbusha wananchi  kuzingatia tahadhari zinazoendelea kutolewa kuhusu uwezekano wa kunyesha mvua kubwa za Elninyo.

Shirima ameyasema hayo alikpokuwa mgeni rasmi Mahafali ya 16 ya Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari  Kwala iliyopo Kata ya Kwala Wilaya Kibaha na kuwataka watu wote wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka kabla ya mvua hizo kuanza kunyesha ili kuepuka madhara.

Aidha amewaahidi kwamba atahakikisha changamoto walizoainisha atazifikisha sehemu husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi ambapo alitoa mchango wake fedha taslimu, vifaa vya kuzima na kung’amua moto kwa uongozi wa shule hiyo.

Pia alitoa zawadi za vifaa vya ki taaluma kwa wanafunzi wahitimu na Wanafunzi Skauti ambapo alipata nafasi ya kugawa vyeti kwa wahitimu pamoja na walimu na wanafunzi waliofanya vizuri zaidi.

NSSF YAPIGA VITA VITENDO VYA RUSHWA

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Pwani, imetoa rai kwa Mtumishi ama Mtendaji yeyote anaejihusisha na vitendo vya rushwa kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vinachangia kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wateja.

Akifungua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kimkoa, Meneja wa NSSF Mkoani Pwani, Witness Patrick ,amesema wanashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU) kudhibiti mazingira ya vitendo vya rushwa kwenye maeneo ya kazi.

Amewaasa ,kila mmoja kujitathmini na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kudumisha imani kwa wanachama na wadau.

Witness ameeleza kuwa, mfuko hautamvumilia mtendaji yeyote atakaeshindwa kuendana na viwango na kasi ambayo mfuko unatarajia kuifikia.

Anasema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapinga rushwa kwa vitendo, na Nssf inaunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kukemea masuala yote ya rushwa.

Vilevile Witness amewahimiza ,watumishi na wananchi wema kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotendeka katika maeneo yao ya kazi kwani kutokutoa taarifa ni kushiriki rushwa.

Halikadhalika," anawasihi kutumia mfumo mpya wa NISS katika kuandikisha wanachama wengi zaidi wa mfumo wa kujichangia kwa hiari ili kuongeza wigo wa kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi.

Naye mwanachama wa Nssf Kibaha, Vicent Ndumbili ameipongeza Nssf kwa kujali wateja wake.

Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi kimataifa mwaka 1984 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja ambapo mwaka huu 2023 yanaanza octoba 2-octoba 6 kilele.


Mwisho

TCCIA INVESTMENT KUONGEZA MTAJI KUFIKIA BILIONI 47


KAMPUNI ya TCCIA Investment inatarajia kuongeza mtaji wake na kufikia bilioni 47 kutoka bilioni 37 ambazo zimewekezwa kwenye masoko mbalimbali ya hisa.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Peter Kifungomali wakati akizungumza na wanahisa wa mkoa wa Pwani juu ya hisa walizowekeza.

Kifungomali amesema kuwa ongezeko hilo ni hadi itakapofika mwaka ujao wa fedha ambapo thamani imeongezeka kwa asilimia 53 kwa mwaka 2022.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chemba ya wafanyabiashara ya TCCIA Mkoa wa Pwani sehemu ya biashara Fadhili Gonzi amesema kuwa baadhi ya wanahisa walikuwa na maswali mengi juu ya fedha zao.

Naye mmoja wa wanahisa Ayubu Mtawazo amesema kuwa hisa ni moja ya sehemu salama ya kuwekeza fedha ambapo watu wengi wamenufaika.

Clara Ibihya amesema kuwa manufaa ya hisa ni makubwa kwani ukishawekeza fedha zako hupati tena usumbufu kutakiwa marejesho bali unasubiri kupata fedha.