Wednesday, August 16, 2023

WATAKIWA KUTUNZA MISITU KWA VIZAZI VIJAVYO

 

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS ) imesema kuwa uhifadhi wa rasilimali za Misitu ni manufaa ya kizazi cha Sasa na vizazi vya baadae hivyo jamii inapaswa kujiepusha kuchoma moto Misitu pamoja na uvunaji haramu.

Hayo yamesemwa Leo Agosti 16,2023 na  Kamishna wa uhifadhi wakala wa huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Silayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hifadhi hiyo ndani ya Miaka ya miwili ya serikali ya awamu ya sita .

Amesema kuwa sekta ya Misitu na nyiki nchini ni muhimu kutokana na mchango wake Katika ukuaji wa sekta ya Utalii, Maji , kilimo, mifugo, nishati pamoja na viwanda hivyo kutokana  na umuhimu huo Wadau wote wanapaswa kulinda rasilimali za Misitu.

Aidha amesema kuwa wakala umeendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi za Misitu na jamii inayoizunguka ambapo jumla ya hekta 296,881 za maeneo  zimetolewa kwa wananchi kwa ajili ya makazi , kilimo na ufugaji.

Pia wakala unaendea kutoa Elimu ya uhifadhi na usimamizi wa Misitu kwa jamii sambamba na kuimarisha mipaka kwa kuisafisha , kuweka vigingi na mabango Ili kuzuia uvamizi Katika maeneo ya hifadhi.

*MADEREVA WAVUNJA SHERIA KUDHIBITIWA CHALINZE*


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo amewataka askari wa Polisi Chalinze kutokuwa na muhali kwa madereva wanaokiuka Sheria za usalama barabarani.

Kauli hiyo imetolewa Leo Agosti 16 akiwa katika siku ya pili ya ziara ya ukaguzi katika Wilaya zilizopo Mkoa wa Pwani ambapo alizungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali akiwataka  kutokuacha jukumu la ukamataji wa madereva wanaovunja Sheria kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani pekee,badala yake nao wachukue hatua ili kuweza kutokomeza ajali za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kibinadamu kama vile kuyapita magari mengine bila tahadhari, mwendo kasi, matumizi ya vileo na kutokuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.

Hivi karibu watu wa nne wa familia moja walipoteza maisha katika ajali ya barabarani eneo la Mapatano, Kata ya Mbwembwe tukio ambalo lilivuta hisia kwa watu wengi kutokana na ajali hiyo ya barabarani.

Kamanda Lutumo amesema " Askari wote wana jukumu la kutoa taarifa kwa wenzao waliopo barabarani pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kuvunja Sheria za usalama barabarani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa".

Aidha, amewakumbusha umuhimu wa utoaji huduma bora pindi wanapowakamata madereva wanaovunja Sheria kwa kuwaeleza makosa yao kabla ya kutoa adhabu ili wajue makosa yaliyopelekea kupewa adhabu husika.

*POLISI BAGAMOYO WATAKIWA KUBADILIKA KIUTENDAJI*



Askari Polisi Wilaya ya Bagamoyo wametakiwa Kubadilika kifikra na kufanya kazi kwa weledi na kuachana na utendaji kazi wa mazoea.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo  wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa kuangalia utendaji wa kazi Wilayani hapo  wakati akizungumza na Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ambapo amewataka kuzingatia ufanyaji kazi kwa mujibu wa Sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kupeleka utendaji usioridhisha.

Pia, Kamanda Lutumo amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi kwa kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili vitakavyolichafua Jeshi ambavyo huweza kusababisha kufukuzwa kazi.

Kadhalika, amewataka askari kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya utendaji bora kwa kutenda haki kwa tunao wahudumia vituoni " Wananchi hawapendi kuja kwenye vituo vyetu ila wanafika kwa kuwa wanashida zinazohitaji kusaidiwa nasi hivyo ni jukumu letu kuwapa huduma bora wanapofika kwenye vituo vyetu vya Polisi”, Alisema.

Aidha, amewakumbusha askari umuhimu wa kutunza vizuri vielelezo na kutokuwa na tamaa au kushawishika katika kuiba vielelezo hivyo viwapo kituoni. "Ni jukumu letu kulinda vielelezo vilivyopo kituoni na kuhakikisha vinatunzwa vizuri na siyo kuwa sehemu ya upotevu wa vielelezo hivyo ambavyo vitatumika kama ushahidi Mahakamani.

Polisi (M) Pwan

TAKUKURU PWANI YABAINI MIRADI KAMATI HEWA MIRADI YA HALMASHAURI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini uwepo wa kamati hewa kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Takukuru Mkoa huo Christopher Myava alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Myava alisema kuwa kutokana na kamati hewa kunasababisha mianya ya rushwa katika malipo yanayofanyika.

"Pia tumebaini kuwa jamii kutokuwa na umiliki wa miradi hiyo kutokana na kutoshirikishwa katika utekelezaji wake mfano ujenzi wa kituo cha afya Kisiju ambapo jamii haikushirikishwa kabisa,"alisema Myava.

Alisema kuwa mradi mwingine ambao ulibainika kuwa na changamoto ni mzabuni aliyechaguliwa kupeleka vifaa vya ujenzi shule ya sekondari ya kata ya Shungubweni hakuomba kazi hiyo kwenye mfumo wa serikali wa TANEPS.

"Mzabuni huyo alipewa zabuni kinyume cha utaratibu na tukafanya kikao na Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha waombaji wa zabuni wanashindanishwa ili kuondoa dhana ya utoaji zabuni kwa upendeleo,"alisema Myava.

Alibainisha mradi mwingine ni kwenye soko la Mnarani Halmashauri ya Mji Kibaha wakusanyaji wa ushuru kutotoa risiti za mashine EFD baada ya wafanyabiashara kufanya malipo kwa kisingizio cha ubovu wa mashine.

"Sababu nyingine wanasema kuwa eti mashine haina chaji hali ambayo imesababisha wakusanyaji kutumia fedha hizo kwa matumizi yao binafsi,"alisema Myava.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo kunakosekana kumbukumbu za wafanyabiashara waliofanya malipo hivyo kusababisha upotevu wa mapato.

"Maegesho ya magari nako kuna upotevu wa mapato unaosababishwa na utendaji mdogo wa kukusanya mapato ambapo baadhi ya wakusanyaji hutoza viwango tofauti vya ushuru kwa malori yanayoegeshwa sokoni tofauti na vilivyowekwa kwenye sheria ndogo,"alisema Myava.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Pwani alisema kuwa baada ya kubaini hayo walifanya kikao na wadau wa soko na kuweka maazimio ikiwa ni pamoja na kudai risiti, kutoa taarifa za ubovu wa mashine na kuweka vibao vinavyoonyesha tozo.

MKUU WA MKOA WA PWANI ABUBAKAR KUNENGE AZINDUA MPANGO WA UKUSANYAJI MAPATO


MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ili wapatiwe mafunzo ya Mpango Mkakati wa Kuongeza  Mapato ambayo ndiyo dira ya Rais na TAMISEMI.

Kunenge aliyasema hayo Mlandizi wakati akizungumza na wataalamu mbalimbali na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha alipokuwa akifungua mafunzo ya namna ya kuongeza mapato kwenye Halmashauri kupitia mpango wa miaka mitano wa Mpango Mkakati wa Kuongeza Mapato kwa kipindi cha miaka mitano ijayo mafunzo yaliyoandaliwa GIZ.

Alisema kuwa upatikanaji wa mapato mengi kutasaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo na kupunguza kero kwa wananchi na hiyo itamsaidia Rais.

"Ifikie hatua Halmashauri zetu zitoe gawio kwa serikali kama ilivyo kwa mashirika ya umma ili kuisaidia ili iweze kuhudumia Watanzania hivyo wote kwenye miradi mikubwa ya nchi ikiwemo ile ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo yetu,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa Halmashauri zishirikiane na GIZ ili kupata mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza mapato pia watumie teknolojia ili kukusanya mapato ambapo mapato yakiongezeka itasaidia kuipa uwezo serikali kuhudumia wananchi wake.

"Tubuni vyanzo vipya vya mapato na tusitegemee kuuza ardhi tu peke yake kwani inakwisha tubuni vyanzo ambavyo ni endelevu hususani kwenye sekta ya uwekezaji ambayo ina nafasi kubwa ya kutuinua kiuchumi ili tuweze kuongeza mchango wetu kwenye uchumi,"alisema Kunenge.

Alibainisha kuwa Halmashauri ziangilie namna ya tozo ili zisiwe kero na kusababisha kuua au kukwamisha uwekezaji ambapo mapato ni takwimu kwa kujua wanaostahili kulipa ili mkusanye kwa mujibu wa sheria. 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa George Nsajigwa Mpango Mkakati huo wa Kuongeza Mapato kwa Halmashauri hapa nchini uko kwenye mikoa ya Arusha, Tanga, Pwani ambapo ndo mkoa wa kwanza kufanya mafunzo hayo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana ambapo malengo yao kwa Halmashauri ya Kibaha Mji ni kufikia makusanyo ya shilingi bilioni 30 na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kukusanya bilioni 20 katika kipindi cha miaka mitano.

John alisema kuwa ili kufikia malengo hayo wameamua kuwa na mafunzo ili kuwa na mipango ya kisayansi katika ukusanyaji wa mapato pia kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ambavyo wanaamini vitawafikisha huko.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Butamo Ndalahwa alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kupata mbinu mpya za ukusanyaji wa mapato ambapo kwa mwaka jana Halmashauri hiyo iliongoza kwa ukusanyaji mapato.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Peter Laizer mshauri wa mradi wa utawala bora wa fedha kutoka shirika hilo alisema kuwa mafunzo hayo yatawahusisha wataalamu wa masuala ya fedha kwenye Halmashauri kushirikiana na vitengo vingine.

WAKULIMA WATAKIWA KUTUMIA MBEGU ZILIZOTHIBITISHWA NA WAKALA WA MBEGU (TOSCI)

Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewataka wakulima na jamii kwa ujumla watumie Mbegu zilizothibitishwa ili kuongeza mavuno tija na kipato.

Hayo amesemwa Mkurugezi mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania Patrick Ngwediagi  Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mwaka wa fedha 2022/2023 na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 ya taasisi hiyo.

Amesema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 12 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuendelea na uboreshaji wa shughuli za uthibiti na usimamizi wa ubora wa mbegu pamoja na utekelezaji mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi ( AFDP) kwa kujenga Maabara ya Mbegu.

Aidha amesema kuwa jukumu kubwa la Taasisi hiyo ni kusimamia shughuli za uzalishaji wa Mbegu na biashara ya Mbegu Ili kuhakikisha wakulima na Wadau wengine kuwa Mbegu wanazouziwa zenye Lebo ya TOSCI  ni sahihi kwa matumizi.                                    

Pia amesema kuwa matumizi ya Lebo za ubora za TOSCI kumesababisha kupungua kwa tatizo la uwepo wa Mbegu feki na zilizo na ubora hafifu hapa nchini.

Monday, August 14, 2023

DAWASA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA MIRADI SABA

Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi  Saba ya kimkakati  ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji na mradi wa maji Kwala. 

Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Mkuu was DAWASA Kiula Kingu  Leo Agosti 11,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.

 Kingu amesema Miradi  iliyotekelezwa imegharimu shilingi bilioni 425.9 inalenga  kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa  ya pembezoni.

Aidha Kingu ameeleza pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi, DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo. Hii ni kwa sababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira.

Hata hivyo Mradi mwingine ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.

DAWASA pia imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku. Miradi hii itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30 ambavyo vitasaidia kuboresha usafi wa mazingira. 

Ameeleza kwamba miradi hii itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu pia Wakandarasi  wanaendelea na ujenzi na gharama za miradi  ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.

Alimalizia kwa kusema Miradi hii ni ya kisasa na  mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.