Monday, August 14, 2023

DAWASA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA MIRADI SABA

Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi  Saba ya kimkakati  ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji na mradi wa maji Kwala. 

Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Mkuu was DAWASA Kiula Kingu  Leo Agosti 11,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.

 Kingu amesema Miradi  iliyotekelezwa imegharimu shilingi bilioni 425.9 inalenga  kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa  ya pembezoni.

Aidha Kingu ameeleza pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi, DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo. Hii ni kwa sababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira.

Hata hivyo Mradi mwingine ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.

DAWASA pia imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku. Miradi hii itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30 ambavyo vitasaidia kuboresha usafi wa mazingira. 

Ameeleza kwamba miradi hii itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu pia Wakandarasi  wanaendelea na ujenzi na gharama za miradi  ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.

Alimalizia kwa kusema Miradi hii ni ya kisasa na  mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.

TUME YA MAENDELEO USHIRIKA TANZANIA YAONDOA BODI 55

Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania imeondoa bodi za vyama  vya Ushirika 55  ambazo hazikufuata kanuni na taratibu za Ushirika,na kupeleke masuala 30 polisi na masuala 47 Takukuru kwaajili ya kuyafanyia Kazi.

Hayo yameelezwa na Mrajisi wa vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt Benson Ndiege katika mkutano wake Jijini Dodoma akieleza utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Aidha Dkt Ndiege amesema katika kuhakikisha Maafisa Ushirika wanaweza kubaini na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili vyama wameamua kutoa mafunzo kwa Maafisa hawa.

Hata hivyo tume hiyo ufanya ukaguzi wa Mara kwa Mara katika vyama vya Ushirika ikiwa lengo ni kubaini uzingatiwaji wa matakwa ya Sheria kanuni na miongozo mbalimbali inayohusiana na utendaji wa vyama vya Ushirika.

TAASISI YA MWALIMU NYERERE YATOA MISAADA KWA JAMII.




TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Chuo cha Afya cha St David cha Jijini Dar es Salaam wametoa misaada ya kadi za bima ya afya ya jamii (CHF) vifaa vya shule na vyakula kwa wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha kwa ajili ya bima za afya kwa baadhi ya wagonjwa waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, vifaa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Muungano Wilayani Kibaha na vyakula kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Mkokozi Wilaya ya Mkuranga, katibu wa taasisi hiyo Omary Punzi alisema kuwa moja ya jukumu lao ni kuisaidia jamii.

Naye Josephine Kiondo muuguzi wa wodi ya watoto ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi alisema kuwa wanaishukuru taasisi hiyo kwa kuwasaidia familia hizo kupata kadi za bima zitawasaidia kukabiliana na gharama za matibabu na kuomba kuendelea kuwasaidia wanajamii.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Muungano Faith Tawe alisema kuwa wanashukuru kuwasaidia wanafunzi hao kwani itawapa ari ya kusoma ambapo baadhi ya wazazi wanalea watoto kwenye hali ngumu na kusababisha wanafunzi hao kukosa baadhi ya mahitaji ya shule hivyo kutofanya vizuri kwenye masomo yao.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mkokozi Richard Tiyara alisema kuwa wanashukuru kwa misaada ya vyakula kwani wana changamoto kubwa ya chakula na shule hiyo ina wanafunzi wenye ulemavu 79 ambapo wanaoishi bweni ni 23 ambapo bweni hilo ni kwa wasichana tu limejengwa kwa thamani ya shilingi milioni 140



Friday, August 11, 2023

HOSPITALI YA MUHIMBILI KUPANDIKIZA MIMBA

Katika kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hospital ya Taifa Muhimbili inampango wa kuanzisha huduma za kupandikiza mimba na upandikizaji Figo, uloto na vifaa vya usikivu ambapo  wakati wowote  kwa Wanawake ambao wana matatizo ya kutopata ujauzito watapata huduma hiyo.

Hayo amesemwa Agosti 10, 2023 Mkurugezi Mtendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa  shughuli mbalimbali na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/2024.

Amesema kuwa hospital ihiyo imeona iazishe huduma hizo ili kupunguza wingi wa watu wanaokwenda nje ya inchi kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Pia amesema kuwa hospitali hiyo imeanzisha utaratibu wa kulipia huduma ya maegesho ilii isaidie kupunguza msongamano wa magari ndani ya hospitali kutokana na watu kuegesha magari katika maeneo hayo 

Katika hatua nyingine amesema kuwa wanatarajia kubomoa Hospitali hiyo na kujenga kubwa zaidi kwaajili ya kuboresha utoaji wa huduma bora za Afya na kuendana na wakati.

Mbali na hayo Hospitali hiyo,katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 imeidhinishiwa na Serikali jumla ya Shilingi Bilioni170.6 ili kutekeleza vipaumbele vyake.


TEA KUTUMIA BILIONI 8 KUFADHILI MIRADI UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI

Mamlaka ya Elimu Tanzania ( TEA ) imepanga kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini ambapo fedha hizo zitatumika kufadhili miradi 82 katika shule 81 zikiwemo shule 48 za msingi na 33 za sekondari Katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi Mkuu wa mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye  wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa fedha ya Mwaka 2023/2024.

Geuzye amesema kuwa miradi hii itakapokamikika itanufaisha wanafunzi 39,484 na walimu 169 Katika shule za msingi na sekondari Ili kuhakikisha sekta ya Elimu inasonga mbele.

Amesema kuwa kwa mwaka 2023/2024 mfuko wa Elimu wa Taifa utatoa ufadhili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia Katika taasisi Moja ya elimu ya juu Tanzania - Zanzibar ambao mradi huu umepanga kutumia sh Million 300 katika utekelezaji wake.

Aidha amesema katika kuunga mkono azma ya serikali ya kuhamishia makao makuu ya Nchi jijini dodom TEA kupitia mfuko wa Elimu ilifadhili Miradi ya shule mpya ya msingi inayofundisha kwa lugha ya kiingereza ya Msangalalee kwa thamani ya sh Milioni 750.

Thursday, August 10, 2023

SERIKALI YAIDHINISHA BAJETI YA BILIONI 24 KUBORESHA HUDUMA HOSPITALI YA MKOA WA DODOMA GENERAL

Serikali imeidhinisha bajeti ya bilioni 24 kwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma General Hospital kwa mwaka wa fedha 2023/24  kuboresha huduma za afya na kufikisha asilimia 99 za utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Akizungumza leo jijini Dodoma, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ernest Ibenzi amesema watumishi wa hospitali hiyo wanaendelea kupata mafunzo sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Dkt. Ibenzi amesema mafunzo hayo yanawasaidia kujua teknolojia mpya ili kuendeleza juhudi za kuboresha huduma hospitalini hapo.

Amesema hospital hiyo imekua ikipokea wagonjwa wengi kwa siku wa kufikia na kuondoka takribani 1500 huku wanaolazwa wakiwa 250 hadi 350 akisema hospitali hiyo imekua ikipokea wagonjwa kwa asilimia kubwa na siyo watu wa kutembelea.

Amesema hospitali inajumla ya majengo 12 ya vyumba vya kufanyia upasuaji huku ikipokea wagonjwa70 kwa siku wanaofanyiwa upasuaji kwa lengo la Kuboresha  huduma za Afya ndani ya hospitali na kuondoa kero ya ucheleweshwaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Ibenzi ametoawito kwa Wanawake wajawazito waliofikia hatua za mwisho za kujifungua kuwahi katika vituo vya afya ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza na kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi.

Kuhusu changamoto ya msongamano wa wagonjwa kwenye wodi ya watoto ambapo watoto hulazwa wawiliwawili katika kila kitanda, Dkt. Ibenzi ameeleza kwamba tatizo hilo litakwisha ndani ya wiki mbili zijazo.

Aidha, Daktari huyo amearifu kwamba hospitali yao inaendelea kutatua changamoto mbalimbali ili wananchi wapate huduma bora.

Kwa miaka miwili iliyopita Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma ilikua ya kwanza kidunia kwa kutoa huduma Nzuri za upasuaji kwa wagonjwa na kupona haraka na kwa wakati.

Akitaja Vipaumbele Dkt. Ibenzi amesema kwa miaka miwili ijayo hospitali hiyo itajenga jengo lingine la gorofa 5 kwa lengo la kuimarisha huduma za Afya kuwa bora zaidi.

Hospitali hiyo inafikisha miaka 103 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1920 ikitekeleza kauli mbiu ya Wizara ya kwamba Huduma bora kipaumbele chetu karibu tukuhudumie

Wednesday, August 9, 2023

UJENZI WA HOSPITALI YA MBAGALA RANGI TATU, GHOROFA SITA ITAGHARIMU SH: BIL 10.8

UJENZI WA HOSPITALI YA MBAGALA RANGI TATU, GHOROFA SITA ITAGHARIMU SH: BIL 10.8

Na. WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo ametembelea Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu na kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo itakayo kuwa na Ghorofa Sita na itagharimu shilingi Bilioni 10.8.

Waziri Ummy amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa Bilioni Mbili katika ujenzi wa jengo la ghorofa Sita la Hospitali ya Mbagala Rangi tatu ambalo litagharimu Bilioni 10.8 ili kupunguza changamoto za msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hiyo iliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam.

“Nilifanya ziara hapa mwaka juzi 2020 na mwaka jana  2021 nikapokea kero ya msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hii na kuipeleka kwa Rais Dkt. Samia na ametoa Biloni Mbili ili kukamilisha ujenzi huu”, amesewa Waziri Ummy.

Amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo tayari kutoa fedha za huduma kwani idadi ya watu imekua ikiongezeka ndani ya Wilaya ya Temeke ambapo kwa sasa kila mwezi anatoa fedha za dawa. 

“Baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia kutoa Bilioni Mbili na Wizara ya Afya imetoa Bilioni Mbili pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wametenga Bilioni Mbili kwa hiyo tayari kuna Bilioni Sita, nimefanya kazi chini ya Rais Samia kwa karibu sana, fedha hizo zilizobakia ambayo ni Bilioni Nne ni ndogo chini ya uongozi wake”, amesema Waziri Ummy

Katika ziara hiyo Waziri Ummy  amepokea taarifa ya hali ya maendeleo katika Sekta ya Afya ndani ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.  Mobhare Matinyi.

Wakati akipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Waziri Ummy amewataka watendaji wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanatafuta maeneo ya kujenga majengo ya huduma za Afya ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya msongamano wa kupata huduma. 

Pia, Waziri Ummy amewaagiza watendaji hao kuhakikisha wanasimamia zoezi la kutoa chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 ili waweze kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam  wameweza kutoa chanjo hiyo kwa asilimia 106.

Mwisho, Waziri Ummy amesema Kwa sasa hali ya ujenzi wa jengo hilo ni asilimia Tano ambapo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, kwa fedha za Benki ya Dunia, Fedha za ndani ya Halmshauri na pamoja na fedha za Rais Samia.