Wednesday, July 19, 2023

TCRA KUENDELEA KUSIMAMIA SEKTA YA MAWASILIANO

MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema inaendelea kusimamia Sekta ya Mawasiliano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha Sekta ya Mawasiliano inatoa mchango katika maendeleo ya nchi na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu.

Hayo ameyasema Mkurugezi Mtendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini dodoma kuhusu taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TCRA 2022/23 na Mpango kazi 2023/24.

Dkt,Jabiri amesema Takwimu zinaonesha kuwa wastani wa bei ya dakika ndani ya Mitandao bila kifurushi zinaendelea kushuka na  Mwenendo wa gharama za upigaji wa simu nje ya kifurushi zimeendelea kushuka hivyo kwa gharama za mwingiliano kumepelekea kuwa na tofauti ndogo sana ya gharama za kupiga simu ndani na nje ya mtandao.

Aidha, Dkt Jabiri ametoa rai kwa Vyombo vya utangazaji kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na weledi katika kutoa maudhui, vilevile kwa wananchi kutosambaza maudhui ambayo yanakiuka misingi ya sheria, mila na desturi za Taifa la Tanzania. 

TCRA ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Namba 12 ya mwaka 2003 baada ya kuunganishwa kwa iliyokuwa Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC) na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC). TCRA ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 1 Novemba 2003.

WAZALISHAJI CHUMVI WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI





WAZIRI wa Madini Dk Dotto Biteko amewatakaka wazalishaji wa chumvi nchini kuongeza uzalishaji chumvi ili kukidhi soko la ndani na la nje kutoka tani 273,000 kwa mwaka hadi tani 303,000.

Aliyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja kutembelea kuona uzalishaji wa chumvi kwenye kampuni za Sea Salt na Stanley and Sons Ltd zilizopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.

Dk Biteko alisema kuwa uzalishaji wa chumvi utakapo ongezeka utasaidia kuongeza mapato na kutoa ajira kwa wananchi ambapo asilimia 15 ya chumvi ndiyo inayopelekwa soko la nje.

"Chumvi hiyo inatumika kwa ajili ya chakula, viwandani na kuuzwa soko la nje ambapo chumvi kutoka nje ya nchi inauzwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na inayozalishwa ndani kutokana na gharama za uendeshaji,"alisema Dk Biteko.

Alisema kuwa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama mamlaka za serikali za mitaa zinapaswa kufanya marejeo ya sheria zake ndogo ili zilingane ambapo kwa sasa kila Halmashauri inatoza gharama zake.

"Serikali baada ya kuona malalamiko ya wazalishaji walifuta kodi 17 na mrabaha kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji ili bei iwe ndogo,"alisema Dk Biteko.

Aidha alisema kuwa makampuni hayo pia yawasaidie wazalishaji wadogo kwa kununua chumvi yao ili kuongeza uzalishaji na kuwataka wazalushaji hao kutokuwa watu wa kulalamika sana juu ya tozo na kodi kwani fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kutoa huduma za maendeleo.

"Tanzania ina Pwani kubwa lakini uzalishaji wa chumvi ni mdogo licha ya kuzuia chumvi za nje ili kukuza soko la chumvi inayozalishwa hapa nchini lakini pia wazalishaji wazingatie ubora,"alisema Dk Biteko.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Pwani Mhandisi Ally Maganga alisema kuwa Wilaya ya Bagamoyo inazalisha chumvi tani 90,000 hadi 100,000 kwa mwaka na kuingiza kati ya shilingi milioni 300 hadi miluoni 350.

Maganga alisema kuwa kuna leseni 48 za uchimbaji chumvi huku ndogo zikiwa 46 ambapo ni 15 tu ndizo zinafanya kazi huku nyingine zikiwa hazifanyi kazi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji, soko na mazingira.

Awali Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge pia kupunguzwa gharama kwa magari yanayochukua chumvi kutozwa fedha nyingi na Hifadhi za Taifa (Tanapa) ambapo makampuni hayo kutumia barabara za hifadhi ya Saadani.

Mkenge alisema kuwa endapo baadhi ya changamoto zikiondolewa Bagamoyo inaweza kulisha chumvi nchi nzima kwani wanauwezo huo wa uzalishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya H J Stanley and Sons Richard Stanley alisema kuwa baadhi ya changamoto ni kukosekana kwa umeme, maji na ubovu wa barabara.

Stanley alisema kuwa changamoto nyingine ni uingizwaji wa chumvi toka nchi nyingine ambapo miundombinu ikiwa mizuri gharama za chumvi zitapungua na bei itashuka.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Shauri Selenda alisema kuwa kilio cha wawekezaji hao kinafanyiwa kazi kwa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa maji na umeme na barabara.

Selenda alisema tayari miundombinu hiyo imewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha ili kuwaondolea kero wawekezaji hao.

Mwisho.

Monday, July 17, 2023

MAMLAKA YA UDHIBITI MBOLEA NCHINI TFRA YAHIMIZA UWEKEZAJI VIWANDA VYA MBOLEA NCHINI

MAMLAKA ya udhibiti wa mbole nchini (TFRA) inaendelea kudhibiti ubora wa mbolea kuhamasisha uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea na kuimarisha utoaji huduma bora kwa wakulima.

Aidha itahakikisha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbolea kwa nchi za afrika mashariki na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
 
Hayo  ameyasema Leo july 17, 2023  Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania(TFRA) Dkt. Stephan Ngailo wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/24 

Dkt Ngailo amesema  Kilimo ni biashara ambapo amebainisha kuwa Mamlaka hiyo itahakikisha ajenda na maono hayo yanafikiwa kwa kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa mbolea bora kwa wakati na kwa bei himilivu.

Alisema lengo la sera ni kuendeleza sekta ya kilimo yenye ufanisi, ushindani na faida Hivyo kuboresha maisha ya Watanzania na kufikia ukuaji mpana wa uchumi na kupunguza
umaskini

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Sheria ya Mbolea Namba 9 ya Mwaka 2009 (Fertilizer Act, 2009) na kanuni zake za Mwaka 2011,TFRA ilianza kutekeleza majukumu yake mnamo Agosti 2012.

PPRA YAWATAKA WADAU WAKE KUZINGATIA MAADILI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewataka wanaojihusisha na Ununuzi wa Umma ikiwemo watumishi wa Umma na wazabuni kuzingatia maadili katika utendaji wao.

Aidha Mamlaka haitasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria wale wote watakaokiuka taratibu au watakajihusisha na kuisababi utakaoisababishia hasara serikali.

Hayo ameyasema Leo July 17 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Eliakim Maswi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini dodoma kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya PPRA na mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa fedha 2023/24.
      
Maswi amesema Ununuzi wa Umma unakabiliwa na hatari kubwa ya rushwa ambapo watendaji na maafisa serikalini wamekuwa wakilalamikiwa na kuhisiwa kuwa wanajihusishwa na vitendo vya rushwa kwa kutoa mikataba na kuwapa faida zisizo halali wazabuni wasiyo na sifa.

Amesema serikali inaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mifumo ya kielektroniki Ili kuleta tija na ufanisi unaostahili katika utekelezaji wa bajeti husika.         

Katika Mwaka wa fedha 2023/24 Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma  imetenga shillingi billion 40.4 kwa ajili ya utekelezaji wa Majukumu yake ambapo kiasi cha shilling billion 20 ni kwa ajili ya uendeshaji na ukaguzi wa taasisi  nunuzi pamoja na ujengwaji wa uwezo wa watumishi.

Sunday, July 16, 2023

MWENYEKITI WA UWT TAIFA CHATANDA AIELEKEZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUTATUA CHANGAMOTO ZA NDOVU LINDI

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa CC Mary Chatanda ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inashughulikia changamoto za ndovu waliovamia makazi ya watu Mkoani Lindi. 

Ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Naipingo Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi. 

Amefafanua kuwa ndovu hao wamevamia makazi ya watu kutokana na wananchi kuingia katika maeneo ya Hifadhi.

"Wizara ya Maliasili Utalii shirikianeni na Wizara ya Mifugo muwatoe wafugaji walioingia kwenye maeneo ambayo ndovu wanakaa" Chatanda amesisitiza 

Ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe kuwatoa wananchi katika hifadhi ili kunusuru mazao ya wananchi yanayoliwa na ndovu pamoja na vifo vya wananchi. 

Kufuatia hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii  Mhe. Mary Masanja ameahidi  Wizara ya Maliasili na Utalii kupeleka helikopta ya kufukuza ndovu ambayo  itaweka kambi katika maeneo husika.

"Tutahakikisha tunaleta helikopta ambayo itakaa kuondoa ndovu hawa  ili wananchi waishi bila taharuki" Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inajua Changamoto zinazowakabili wananchi hivyo imepanga  kuongeza idadi ya askari na kujenga vituo vya askari ili kuondokana na tatizo la ndovu.

Kuhusu malipo ya kifuta jasho/machozi, Mhe. Masanja amesema Serikali imetenga fedha  kiasi cha shilingi milioni 612 kwa Wilaya ya Nachingwea mwaka ili kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan ndovu.

Pia amesema Serikali itachukua vijana kwenye maeneo yenye changamoto za ndovu na kuwapatia mafunzo ya kukabiliana na wanyamapori hao.

Thursday, July 13, 2023

TASAF YABADILISHA MAISHA YA AKINAMAMA WAJENGA NYUMBA ZA KISASA



MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeleta mabadiliko makubwa kwa walengwa wake ambapo Zubeda Juma miaka (70) mkazi wa Kijiji cha Kisanga kata ya Masaki Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani amefanikiwa kujenga nyumba ya tofali kutoka nyumba ya udongo aliyokuwa anaishi awali.


Aidha Halima Salehe naye amefanikiwa kujenga nyumba ya tofali kutokana na fedha za mfuko huo ambao umekuwa mkombozi kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini.

Juma akitoa ushuhuda mbele ya Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete alipotembelea Kijiji hicho kuzungumza na walengwa na wananchi.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete alimchangia na wadau wengine walimchangia huku Halmashauri ya Kisarawe ikiahidi kuhakikisha inakamilisha sehemu itakayobakia.

Alisema kuwa nyumba yake ambayo ni ya kisasa imekamilika ambapo anaishi ila amebakiza kuweka milango na madirisha ambayo ameyaziba kwa kutumia mabati.

Naye Salehe alisema kuwa nyumba yake imefikia hatua ya boma ili kukamilika na kumshukuru Rais Dk Samii Suluhu Hassan kwa kuendeleza mpango huo kutoka kwa mtangulizi wake na kuwafanikisha kubadilisha maisha yao.

Naibu Waziri Ridhiwani alisema mpango huo una lengo la kuwaondoa wananchi kwenye lindi la umasikini ambapo watu milioni 1.3 wananufaika na mpango huo wa kunusuru kaya maskini na kuondoka kwenye umaskini na utegemezi.

Wednesday, July 12, 2023

WATUMISHI WAFANYE KAZI KIMKAKATI

WATUMISHI wa Umma wametakiwa kufanya kazi kimkakati kwa kuwatumikia wananchi na kwa kuwa na wivu wa maendeleo sehemu wanazozifanyia kazi kwa kuacha alama.

Hayo yalisemwa na NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwenye ofisi za Halmashauri hiyo zilizopo Mlandizi.

Alisema kuwa serikali inafanya shughuli zake kimkakati hivyo lazima nao wafanye kazi kwa kuzingatia mikakati hiyo ya serikali ili mipango ya maendeleo kwa wananchi ifikiwe.

"Serikali ina mikakati yake hivyo lazima kila mtumishi wa umma ahakikishe anazingatia mikakati iliyopo ili kufanikisha malengo ya maendeleo kwa wananchi ambapo wanawategemea watumishi kuwaonyesha njia,"alisema Kikwete.

Alisema asingependa kuona watumishi hawawajibiki kwenye maeneo yao ya kazi na kusababisha malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi yasifanikiwe hivyo wasije wakajikuta wanaondolewa au kufukuzwa kazi.

"Kutokana na changamoto zilizopo hapa ofisa utumishi Edward Mahona nakutaka ushughulikie chanfamoto za watumishi siyo lazima kuleta kwetu kwani baadhi ya mambo mnaweza kuyatatua wenyewe hivyo tatua mara moja,"alisema Riziwani.

Aidha alisema kuwa ofisa huyo anatakiwa kukaa na watumishi na kuongea nao kujua changamoto zao kwani malalamiko yaliyotolewa yanapaswa kufanyiwa kazi ili wafanye kazi kwa moyo kwani shida zao zinatatuliwa.

Moja ya watumishi Winifrida Toegale ambaye ni ofisa mtendaji wa kijiji alisema kuwa wanatumia fedha zao binafsi kwani hakuna fedha wanazopewa kwa ajili ya kuendeshea ofisi.

Toegale alisema kuwa licha ya kutumia fedha zao za mishahara lakini kwa upande wao walioajiriwa mwaka 2012 hawakupandishwa vyeo hadi mwaka 2020 jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa na inawavunja moyo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Butamo Ndalahwa alisema kuwa wanakabiliwa na uhaba wa watumishi 441 ambapo waliopo ni 1,571 na mahitaji ni 2,012 na wameweka bajeti ya kuajiri watumishi 211 kwenye kada mbalimbali.

Ndalahwa alisema kuwa madai ya watumishi 342 ni milioni 756 ambapo madai yaliyolipwa ni 251 ya shilingi milioni 455 bado madai 91 yenye thamani ya shilingi milioni 329 kwa upande wa watumishi 70 waliogushi vyeti 56 walijaza fomu huku 12 bado taratibu zinaendelea.