Friday, March 10, 2023

CHAMA CHA MADEREVA WANAWAKE TANZANIA CHAJA NA MIKAKATI MIKUBWA

CHAMA Cha Madereva Wanawake Tanzania (CWMT) kinatarajia kuanzisha kampuni ya usafirishaji ili kujiongezea kipato na kutoa ajira kwa wanachama wake.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa chama hicho Naetwe Ihema alisema kuwa lengo ni kumkwamua mwanamke ili ajitegemee na asiwe tegemezi.

Ihema alisema kuwa madereva wanawake kwa sasa ni wengi ambao wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Taasisi za serikali na binafsi lakini walikuwa hawana Umoja wao.

"Tumeanzisha chama hichi ambacho mwanzo ilikuwa ni kikundi tukaona tujiongeza na kuwa chama ambacho kimesajiliwa na moja ya malengo yetu ni kuwa na kampuni ya usafirishaji kwa mabasi ya kwenda mikoani na daladala ambapo wanachama wetu watakuwa ndiyo madereva,"alisema Ihema.

Alisema kuwa wanatarajia kuongea na watu wenye kampuni za mabasi kwa kuanzia mabasi madogo (daladala) ili waingie makubaliano kama ni kuwakopesha au njia yoyote ili waweze kupata mabasi ili waanze kufanya hiyo kazi.

"Tutaanzisha hiyo kampuni ya usafirishaji kwani ajira kwa madereva wanawake ni changamoto ambapo waajiri wanakuwa hawawaamini wanawake lakini ni madereva wazuri na uwezo wao ni mkubwa,"alisema Ihema.

Aidha alisema kuwa madereva wanawake hawasababishi ajali kutokana na kuwa makini na hofu ya kuogopa kupoteza uhai wa watu ndiyo sababu udereva wao ni wa kujihami na siyo kujiamini.

"Mafanikio tuliyoyapata kwa mtu mmoja mmoja ni kuweza kuhudumia familia ambapo kwa wale walioolewa wanauwezo wa kushirikiana na waume zao katika kuendesha maisha na ambao hawajaolewa wanasomesha, wamejenga na wanafanya maendeleo makubwa,"alisema Ihema.

Aliongeza kuwa sifa ya mwanachama awe anaendesha chombo chochote cha moto ambapo baadhi ya wanachama wao ni marubani wa ndege, manahodha wa meli, madereva wa mitambo ya ujenzi, magari ya mizigo, mabasi makubwa, madereva wa treni, madereva wa uba, madereva wa mwendokasi na magari ya watu binafsi. Chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 na kina wanachama 120.




WEJISA WASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI



WANAWAKE WA WEJISA WAJUMUIKA KUSHEHEREKEA SIKU YA WANAWAKE DAR

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Weka Jiji Safi (WEJISA Company Ltd) kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake Bi.Nuru Hassan amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwemo wafanyakazi wanawake jambo ambalo limeongeza uchapakazi kwa jinsia hiyo.

Nuru amesema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo inafanyika Machi 8 ya Kila mwaka.

"Rais wetu Samia tunamuunga mkono kwa sababu nafasi aliyonayo amesaidia kuongeza mwamko kwa wanawake kufanya kazi na wale ambao walikuwa hawana kazi na kutafuta shughuli zozote ili waweze kujiondoa kwenye utegemezi," alisema Nuru.

Amesema kuwa kampuni ya WEJISA itaendelea kushirikiana na Serikali bega kwa bega na ndiyo maana leo tumekuja hapa kusheherekea pamoja na kujifunza mengi kwa wafanyakazi wetu wanawake,"alisema Nuru Hassan

Aidha amesema kuwa amepata faraja kujumuika na Wanawake hao kwani wamekuwa chachu ya Maendeleo ya Kampuni hiyo.

Wanawake hao wa WEJISA wanatoka vitengo mbalimbali ikiwemo wanaosafisha maeneo ya Jiji, ikiwemo ufagiaji, ukusanyaji wa taka na usafi wa mazingira.

Lengo la tukio hilo ni kupeana moyo kama Wanawake katika kuamua mambo na kufanikisha utendaji bora wa kazi.

Kwa upande wake Patricia Kimelemeta Mwandishi Kinara wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alitoa mada ya malezi na makuzi kwa watoto katika tukio hilo la kusheherekea siku ya Wanawake, ambapo alitoa rai Kwa wazazi kuendelea kutoa elimu kwa watoto wao ikiwemo kujenga ukaribu wa kuwachunguza ilikujua changamoto wanazokutana nazo.

Kwa upande wao baadhi ya Wanawake wafanyakazi wa WEJISA waliishukuru kampuni hiyo kwani imekuwa mkombozi kwao na wamekuwa wakifanya kazi moyo.

"Mimi nina familia, nikitoka nyumbani naandaa kabisa chakula kwa wanangu.

Aidha, amewataka Wanawake kuzingatia sheria za Usalama barabarani kwani wamekuwa wakishuhudia matukio mengi, ikiwemo wao kugongwa.' Alisema Bi. Asha Salum.

Kwa upande wake. Bi. Sharifa Magombeka amesema kuwa, anafanya kazi ya kuzoa taka ilikupata kipato chake halali,

"Mwanamke ni kujitambua, nafanya kazi yangu ya kuzoa taka hii kupata kipato kihalali, tunamshukuru Mhe Rais kuendelea kuweka mazingira ya ufanyaji kazi na tumejumuika hapa tumepata elimu, lakini pia tumefurahia pamoja" alisema Sharifa.


Thursday, March 9, 2023

JWTZ WATANGAZA NAFASI KUJIUNGA NA JESHI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa miaka miwili wa mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kurudishwa majumbani.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiao wa (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Ilonda wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu nafasi za kujiunga na Jeshi hilo.

Ilonda amesema kuwa nafasi hizo zinawahusu vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.

Amesema kuwa nafasi hizo haziwahusu vijana ambao bado wapo katika kambi mbalimbali za JKT kwa sasa bali zinawahusu wale ambao tayari wamemaliza mikataba yao ya mafunzo ya miaka miwili na kurudishwa majumbani na wenye vigezo vilivyotajwa vya kuomba nafasi hizo.

"Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya Jeshi hilo Dodoma kwanzia leo tarehe 9 Machi hadi tarehe 20 Machi 2023 yakiwa na viambatanisho kama vile nakala ya kitambulisho cha Taifa au namba ya Nida, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya muombaji,"amesema Ilonda.

Aidha amewataka wananchi kuwa makini na matapeli kwani kumekuwa na tabia ya kuibuka matapeli pindi matangazo hayo ya nafasi ya kujiunga na Jeshi hilo zinapotangazwa. 

KIKWETE AOMBA USHIRIKIANO KUTIMIZA LENGO LA RAIS KUWA NA MUUNDO WA UTUMISHI KWA USTAWI WA TAIFA

MHE. RIDHIWANI KIKWETE AOMBA USHIRIKIANO KUTIMIZA LENGO LA MHE. RAIS LA KUWA NA SERA ZA KIUTUMISHI NA MIUNDO YENYE TIJA KWA USTAWI WA TAIFA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na Idara ya Uendelezaji Taasisi kumpa ushirikiano wa kutosha kwenye eneo la kusimamia uendelezaji wa sera katika Utumishi wa Umma na miundo ya Taasisi za Umma.

Mhe. Kikwete ametoa rai hiyo Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na Idara ya Usimamizi wa Taasisi kwa nyakati tofauti kilicholenga kufahamu majukumu yanayotekelezwa na Idara hizo pamoja na kuhimiza uwajibikaji.

 Amesema kuwa ili aweze kumsaidia vema Waziri mwenye dhamana kufikia lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwa na sera za utumishi wa umma zenye tija na miundo inayotekelezeka kiutendaji kwa ustawi wa taifa.

Mhe. Kikwete amesema ameteuliwa na Mhe. Rais kumsaidia Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utumishi wa umma na utawala bora, hivyo hana budi kufahamu kwa kina majukumu yanayotekelezwa na idara hizo ili aweze kuyazungumzia pale yanapohitaji ufafanuzi na uelewa kwa umma.

“Malengo ya kukutana nanyi leo ni kufahamiana na kujua majukumu yenu kwa kina kwa kuwa mimi nina jukumu la kumsaidia Mhe. Waziri kujibu maswali ya kiutumishi na utawala bora yanayoulizwa Bungeni,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

Ameongeza kuwa, anatamani kujua kila kitu kinachofanyika katika idara hizo pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo kiutendaji kwani kwa kufanya hivyo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza kwa ufanisi lengo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha Kikwete ameitaka Idara ya Undelezaji Sera kuhuisha sera za kiutumishi ili ziendane na wakati na ziweke mazingira rafiki ya kuzihusisha sekta binafsi kutoa mchango katika kuboresha utumishi wa umma kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza.

Wednesday, March 8, 2023

KIKWETE ATAKA USHIRIKIANO KUTIMIZA LENGO LA RAIS DK SAMOA SULUHU HASSAN KUWA NA SERA KWA USTAWI WA TAIFA

MHE. RIDHIWANI KIKWETE AOMBA USHIRIKIANO KUTIMIZA LENGO LA MHE. RAIS LA KUWA NA SERA ZA KIUTUMISHI NA MIUNDO YENYE TIJA KWA USTAWI WA TAIFA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na Idara ya Uendelezaji Taasisi kumpa ushirikiano wa kutosha kwenye eneo la kusimamia uendelezaji wa sera katika Utumishi wa Umma na miundo ya Taasisi za Umma.

Mhe. Kikwete ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na Idara ya Usimamizi wa Taasisi kwa nyakati tofauti kilicholenga kufahamu majukumu yanayotekelezwa na Idara hizo pamoja na kuhimiza uwajibikaji.

 Amesema kuwa ili aweze kumsaidia vema Waziri mwenye dhamana kufikia lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwa na sera za utumishi wa umma zenye tija na miundo inayotekelezeka kiutendaji kwa ustawi wa taifa.

Mhe. Kikwete amesema ameteuliwa na Mhe. Rais kumsaidia Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utumishi wa umma na utawala bora, hivyo hana budi kufahamu kwa kina majukumu yanayotekelezwa na idara hizo ili aweze kuyazungumzia pale yanapohitaji ufafanuzi na uelewa kwa umma.

“Malengo ya kukutana nanyi leo ni kufahamiana na kujua majukumu yenu kwa kina kwa kuwa mimi nina jukumu la kumsaidia Mhe. Waziri kujibu maswali ya kiutumishi na utawala bora yanayoulizwa Bungeni,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

Ameongeza kuwa, anatamani kujua kila kitu kinachofanyika katika idara hizo pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo kiutendaji kwani kwa kufanya hivyo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza kwa ufanisi lengo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Kikwete ameitaka Idara ya Undelezaji Sera kuhuisha sera za kiutumishi ili ziendane na wakati na ziweke mazingira rafiki ya kuzihusisha sekta binafsi kutoa mchango katika kuboresha utumishi wa umma kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza.

TASAC YATOA FURSA SEKTA USAFIRISHAJI MAJINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

SHIRIKA la Wakala wa  Meli Tanzania (TASAC) linatoa fursa katika sekta ya usafiri majini kwa kuazisha utaratibu kwa kusajili meli kwa masharti nafuu ukarabati wa ujenzi wa meli na kuazisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa Pwani, viwanda vya utengenezaji wa maligafi za ujenzi wa boti za plastiki pamoja na kujenga bandari rasmi za uvuvi.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kaim Abdi Mkeyenge wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika. 

Mkeyenge amesema shirika hilo limefanikiwa kuboresha ufanisi wa bandari kwa kupunguza uwezo wa shehena inayoruhusiwa kukaa bandarini kwa wakati mmoja kutoka asilimia 65 hadi asilimia 50 kwa kuweka amri ya Tozo ya Bandari Kavu ambapo wamefungua ofisi 11 za Shirika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma karibu na wananchi Shirika lina ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Rukwa, Ukerewe pamoja na Geita.

Amesema TASAC imefanikiwa kukagua meli za kigeni 36 kwa kipindi kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 na kuanzia Januari 2023 wamekagua meli za kigeni 37 ambapo shirika linategemea kukagua meli 61 hadi kufikia Juni 2023.

TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018. 

Kuundwa kwa TASAC ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususan kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Pia kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji na hii ni kwa sababu Tanzania ina ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi wenye urefu takriban Kilomita 1,424, Maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa

Tuesday, March 7, 2023

OSHA YAPATA MAFANIKIO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953.

Aidha ongezeko hilo ni sawa na asimilia 276 na  idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA  Khadija Mwenda akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mwenda amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320 upimaji wa afya kutoka wafanyakazi 363,820 hadi kufikia wafanyakazi milioni 1.1 waliopimwa katika kipindi hicho cha miaka miwili kutotokana na kupunguzwa kwa ada mbalimbali.

Amesema kuwa kuboreshwa mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika ongezeko hilo ni tafsiri kwamba hali ya usalama na afya  katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika.

Ameongeza kuwa ongezeko la asilimia 175 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia wafanyakazi 43,318. 

"Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine 105 yalitozwa faini,"amesema Mwenda. 

Amebainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kuchunguza ajali mbali mbali zinazotokea katika sehemu za kazi kwa lengo la kubaini vyanzo vya ajali hizo ili kushauri namna bora ya kuzuia ajali kutokea tena.

Dhima kuu ya  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni kuelimisha na kuhamasisha masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuweka mifumo thabiti itakayo zuia ajali, magonjwa na vifo pamoja na uharibifu wa mali ili kupunguza gharama za uendeshaji na kukuza uchumi wa Taifa.