Wednesday, March 8, 2023

TASAC YATOA FURSA SEKTA USAFIRISHAJI MAJINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

SHIRIKA la Wakala wa  Meli Tanzania (TASAC) linatoa fursa katika sekta ya usafiri majini kwa kuazisha utaratibu kwa kusajili meli kwa masharti nafuu ukarabati wa ujenzi wa meli na kuazisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa Pwani, viwanda vya utengenezaji wa maligafi za ujenzi wa boti za plastiki pamoja na kujenga bandari rasmi za uvuvi.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kaim Abdi Mkeyenge wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika. 

Mkeyenge amesema shirika hilo limefanikiwa kuboresha ufanisi wa bandari kwa kupunguza uwezo wa shehena inayoruhusiwa kukaa bandarini kwa wakati mmoja kutoka asilimia 65 hadi asilimia 50 kwa kuweka amri ya Tozo ya Bandari Kavu ambapo wamefungua ofisi 11 za Shirika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma karibu na wananchi Shirika lina ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Rukwa, Ukerewe pamoja na Geita.

Amesema TASAC imefanikiwa kukagua meli za kigeni 36 kwa kipindi kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 na kuanzia Januari 2023 wamekagua meli za kigeni 37 ambapo shirika linategemea kukagua meli 61 hadi kufikia Juni 2023.

TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018. 

Kuundwa kwa TASAC ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususan kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Pia kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji na hii ni kwa sababu Tanzania ina ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi wenye urefu takriban Kilomita 1,424, Maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa

Tuesday, March 7, 2023

OSHA YAPATA MAFANIKIO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953.

Aidha ongezeko hilo ni sawa na asimilia 276 na  idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA  Khadija Mwenda akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mwenda amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320 upimaji wa afya kutoka wafanyakazi 363,820 hadi kufikia wafanyakazi milioni 1.1 waliopimwa katika kipindi hicho cha miaka miwili kutotokana na kupunguzwa kwa ada mbalimbali.

Amesema kuwa kuboreshwa mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika ongezeko hilo ni tafsiri kwamba hali ya usalama na afya  katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika.

Ameongeza kuwa ongezeko la asilimia 175 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia wafanyakazi 43,318. 

"Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine 105 yalitozwa faini,"amesema Mwenda. 

Amebainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kuchunguza ajali mbali mbali zinazotokea katika sehemu za kazi kwa lengo la kubaini vyanzo vya ajali hizo ili kushauri namna bora ya kuzuia ajali kutokea tena.

Dhima kuu ya  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni kuelimisha na kuhamasisha masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuweka mifumo thabiti itakayo zuia ajali, magonjwa na vifo pamoja na uharibifu wa mali ili kupunguza gharama za uendeshaji na kukuza uchumi wa Taifa.


Monday, March 6, 2023

WANAWAKE WATUMIE MITANDAO KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA

Na Mwandishi Wetu Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Doroth Gwajima  amewataka wanawake wahakikishe wanatumia huduma za mitandao ili kufikia usawa wa kijinsia kwenye maendeleo kwa kupata taarifa mbalimbali za kijamii kama Afya, Elimu, Kilimo, biashara na zinginezo.

Gwajima ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yatakayofanyika March 8 mwaka huu.

Amesema kuwa  pengo la wanawake kumiliki simu na kutumia Mtandao linaongezeka zaidi kwa wanawake wenye umri  mkubwa ( wazee) , wanawake wanaoishi vijinini, pamoja na wanawake wenye ulemavu Mwaka 2022 takwimu zinaonesha asilimia 63 ya wanawake duniani walitumia Mtandao ukilinganisha na asilimia 69 ya wanaume.

Aidha amesema kuwa kwa kushirikiana na jamii yenyewe serikali itaendelea kuelimisha na kufanyia kazi kuondoka vikwazo vyote vinavyozuia mwanamke kutumia Teknolojia ya kidigitali.

Pia ametoa wito kwa wanawake na jamii kwa ujumla kujitokeza kuadhimisha sikukuu ya wanawake duniani chini ya uongozi wa waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na ameimiza wanawake kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi yaliyo ngazi zote Hadi vijinini Ili kunufaika na uwezeshaji wa serikali na wadau wake.

Sunday, March 5, 2023

WATATU WAFA AJALINI WAMO ASKARI POLISI WAWILI

WATU watatu wakiwemo askari wawili wa Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walifariki papo hapo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Machi 5 mwaka huu majira ya saa 11:45 alfajiri huko maeneo ya Mavi ya Ng'ombe Kijiji cha Mboga Kata ya Msoga Tarafa ya Chalinze katika Barabara ya Chalinze/Segera.

"Gari lenye namba za usajili T 323 BAL aina ya Toyota Cresta likiendeshwa na mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) askari wa kituo cha Polisi Chalinze akitokea Chalinze kuelekea Lugoba liliacha njia kutoka upande wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugonga kalavati kisha kupinduka na kusababisha vifo vya watu watatu na mmoja kujeruhiwa,"alisema Lutumo.

Aliwataja askari waliokufa kuwa ni Mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) aliyekuwa dereva wa gari hilo, Konstebo  Emmiliana Charles (26) wote askari wa kituo cha Polisi Chalinze na Karimu Simba (27) ambaye ni karani wa Mahakama ya Wilaya Lugoba.

"Majeruhi huyo ambaye naye  ni askari wa Kituo cha Polisi Chalinze Konstebo Mwanaidi Shabani (25) ameumia maeneo mbalimbali ya mwili wake na amepelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi,"alisema Lutumo.

Aidha alisema kuwa uchunguzi wa awali umeweza kubaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka.

"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Lugoba kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi,"alisema Lutumo.

Thursday, March 2, 2023

WATAKA KUHARAKISHWA UJENZI NYUMBA YA MKURUGENZI NA WAKUU WA IDARA

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wametaka kuharakishwa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara kwani imepita muda mrefu ujenzi huo bado haujaanza.

Wakizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo walisema kuwa kwa kuwa tayari azimio la ujenzi huo limeshapitishwa hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi.

Diwani wa Kata ya Mtambani Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa kama hakuna changamoto yoyote ni vema kuanza ujenzi ili watumishi hao wawe na makazi ndani ya Halmashauri.

Mwafulilwa alisema kuwa kama eneo hilo halina mgogoro wowote kwanini ujenzi hauanzi ambapo eneo hilo ni jirani na ilipojengwa hospitali ya Wilaya.

"Tunataka kikao kijacho tupate majibu kuwa ujenzi unaanza lini ili tuweze kuufanya kwa wakati kwani hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi,"alisema Mwafulilwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema kuwa baadhi ya Madiwani walikuwa na hofu kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro.

Makala alisema kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro baadhi ya watu waliibuka na kusema ni lao hivyo kama lina changamoto ni vema wakaelezea ili waweze kujua.

Naye Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Brown Nziku alisema kuwa eneo hilo zamani lilikuwa likimilikiwa na Taasisi ya Mkonge na kupewa kampuni ya UFC lakini ilifutiwa hati na Rais ambapo watu walilivamia.

Nziku alisema kuwa baada ya kurudishwa serikalini ilikabidhiwa Halmashauri ambapo walipewa hekari 9.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara.

Alisema kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya manunuzi na baada ya hapo ujenzi utaanza mara moja.


NANE WAJERUHIWA AJALI YA BASI LA HAPPY NATION

WATU nane wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria la kampuni ya Happy Nation kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa basi hilo lilipinduka baada ya kujaribu kulipita gari lililokuwa limesimama.

Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Februari 2 mwaka huu majira ya 8:30 usiku kwenye Kijiji cha Ruvu Kata ya Vigwaza Wilaya ya Kipolisi Chalinze Bagamoyo.

"Basi hilo lenye namba za usajili T 526 DVJ lilikuwa likiendeshwa na Vincent Mbasha (39) mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam na chanzo lilikuwa likilikwepa gari la mizigo aina ya Scania lenye namba T 299 BYF na tela namba T 308 BYF lilikuwa limepata hitilafu na kutoweka alama yoyote kuashiria kuwa kuna gari ndipo dereva huyo wa basi akalikwepa na kupinduka,"alisema Lutumo.

Alisema kuwa basi hilo lilikuwa na abiri 47 ambapo majeruhi wako hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo hali zao zinaendelea vizuri. 

Aidha aliwataja majeruhi hao kuwa ni Nuru Mohamed (38), Selimanda Abdala (63), Amina Jumanne (48), Faudhia Ismail (23), Fredina Omary (15) Abtatus Jovin (18), Idat Reman (27) na Aida Suleiman (24).

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambaye aliwatembelea majeruhi hao alisema kuwa madereva wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Kunenge alisema kuwa alipata taarifa kuwa dereva huyo alitaka kulipita gari hilo upande wa kulia badala ya kushoto ambapo ni uzembe hivyo ni vema wakazingatia sheria.

Naye Mganga mfawidhi wa Tumbi Amani Malima alisema kuwa waliwapokea majeruhi hao ambapo wameumia maeneo mbalimbali ya miili yao na wanaendelea vizuri na matibabu.

Malima alisema kuwa wagonjwa hao wanaendelea na vipimo mbalimbali vikubwa ilikugundua majeruhi hao wameumia kiasi gani.


Wednesday, March 1, 2023

MAOFISA ELIMU KATA,WALIMU WAJENGEWA UWEZO

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imeendesha semina ya kuwajengea uwezo maofisa Elimu kata,walimu walimu wa shule za msingi na sekondari juu ya masuala ya VVU/UKIMWI mahala pa kazi kwa lengo la kuondoa unyanyapaa na ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya Mji Kibaha Siwema Cheru amesema semina hiyo ni mwendelezo wa Mafunzo mengine ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wadau mbalimbali ili kuondoa vitendo vya unyanyasaji sehemu za kazi na kwamba sasa wamefikiwa waratibu wa Elimu kata na walimu ambao ni wadau wakubwa kwenye jamii na wanakaa na wanafunzi muda mrefu ambao pia ni wahanga


Dr.Mariam Ngaja ameeleza kuwa walimu wakipata uelewa wa semina hiyo wanawajibu wa kuwafundisha wanafunzi wao kuhusu afya ya uzazi kwa Vijana na maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya ngono na Elimu ya madawa ya kulevya.


Ngaja ameongeza kuwa semina hiyo ambayo ni utekezaji wa Kawaida wa Idara ni utekelezaji wa mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Tanzania hasa kwa wasichana balehe na wanawake Vijana .


Mwalimu Augustine Seso aliyeshiriki semina hiyo ameishukuru Halmashauri kwa kuigharamia na kwamba imewafikia muda muafaka na Sasa wanakwenda kwenye jamii kutimiza lengo la kutoe Elimu ili kuondosha unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwenye jamii.