Tuesday, July 5, 2016

CHAURU YAWATAKA WAFUGAJI KUONDOA NGOMBE KWENYE SHAMBA LAO

Na John Gagarini, Bagamoyo

UONGOZI Chama Cha Ushirika wa Wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) wamewataka wafugaji walioko kwenye shamba hilo kuhamisha mifugo yao ambayo imekuwa ikifanya uharibifu wa mazao pamoja na miundombinu ya umwagiliaji.

Akizungumza kwenye kikao cha wakulima na wafugaji waliopo kwenye shamba hilo ambalo liko kwenye kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani Bagamoyo mwenyekiti wa chama hicho Sadala Chacha amesema kuwa uharibifu uliofanywa ni mkubwa sana.

Chacha amesema kuwa kutokana na baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye shamba hilo la umwagiliaji la mpunga kumewasababishia hasara kubwa wanachama wake na uharibifu wa miundombinu.

Amesema kuwa serikali ilishawatengea eneo lao liitwalo Mnyanama lakini hawataki kwenda wakidai kuwa hakuna huduma za kijamii jambo ambalo limewafanya waendelee kukaa hapo na huku mifugo hiyo hasa ngombe wakiendelea kufanya uharibu wa miundombinu na kula mazao ya wakulima.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakikaa vikao vya mara kwa mara ili kujaribu kuangalia utaratibu wa namna ya kufuga na wao kulima lakini wao wamekuwa wakilishia mifugo kwenye mashamba hayo ya wakulima na kusababisha ugomvi mara kwa mara.

Ameongeza kuwa wamechoshwa na vitendo hivyo vya wafugaji vya kuingiza ngombe kwenye shamba hilo huku sheria aikikataza mifugo kuingia kwenye eneo hilo lakini utekelezaji wa suala hilo umekuwa mgumu kwani mifugo bado inaingizwa shambani hapo.

Kwa upande wake mmoja wa wafugaji Lupina Kirayo amesema kuwa tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.

Lupina amesema kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo kuwaondoa hapo.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura amekiri kutokea changamoto ya ngombe kuingizwa kwenye shamba hilo na kusema kuwa ili kuondoa tatizo hilo ni wafugaji hao kuondoa mifugo hiyo na kuipeleka kule walikopangiwa.

Mbura amesema kuwa wafugaji hao hawataki kwenda huko kwa madai kuwa hakuna huduma za kijamii kama zahanati, shule na malambo ya maji kwa ajili ya mifugo yao hali ambayo imefanya ugomvi kwenye shamba hilo kutokwisha kwa muda mrefu sasa.

Shamba hilo la umwagiliaji mpunga lilianzishwa miaka ya 60 na lina wanachama wapatao 894 na lina ukubwa wa hekta 3,209 huku za makazi zikiwa hekta 720 ambapo baada ya mavuno ya mpunga wanachama hulima mazao mengine kama vile mahindi,ufuta na mtama pamoja na kilimo cha mbogamboga.

Mwisho.


WATENDAJI WATAKAOSHINDWA KUKAMILISHA ZOEZI LA UPATIKANAJI MADAWATI KUJIFUKUZISHA KAZI

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU mpya wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama ametoa siku 24 kwa watendaji wa kata na maofisa tarafa kuhakikisha wanakamilisha zoezi la upatikanaji wa madawati na atakayeshindwa kukamilisha zoezi hilo kwenye sehemu yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Mshama ametoa agizo hilo mjini Kibaha kwenye mkutano alioundaa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na watendaji hao na baadhi ya wakuu wa Idara za Elimu, Ardhi na Mazingira na kusema kuwa watendaji hao wanapaswa kukamilisha zoezi hilo ifikapo Julai 29 mwaka huu.

Amesema kuwa agizo la Rais Dk John Magufuli ilikuwa ni Juni 30 mwaka huu hivyo hakuna sababu ya watedaji hao kushindwa kutekeleza agizo hilo kwani muda uliotolewa ulishapita.

Aidha amesema kuwa Baadhi ya watendaji wamefanikiwa kukamilisha zoezi nawapongeza lakini wengine wameshindwa kukamilisha hivyo anatoa muda hadi Julai 29 wawe wamekamilisha na atakayeshindwa atakuwa kajifukuzisha kazi mwenyewe kwa kushindwa kuwajibika.

Akielezea juu ya uwezekano wa kukamilisha hilo amesema kuwa yeye kule alikotoka wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe alipambana na kufanikiwa kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa ambapo madawati yalipatikana na kuwa na ziada ya madawati 2,000 hivyo hata Kibaha hakuna sababu ya kushindwa kufanya hivyo kwani hakuna jambo ambalo linashindikana.

Amesisitiza kuwa Maagizo waliyopewa wao wakuu wa wilaya na Rais ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini kwani haiwezekani nyumbani watoto wakae kwenye makochi au sofa lakini wakifika shule wanakaa chini lazima watendaji hao wahamasishe wananchi kuchangia miundombinu ya elimu.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha amesema kuwa watendaji hao wanapaswa kuwahamasisha wananchi kuchangia unpatikanaji wa madawati hakuna haja ya kusema kuwa eti watu wagumu kuchangia.

Amesisitiza kuwa Kama mtendaji ameshindwa kukamilisha zoei hilo ni kwamba ameshindwa kazi kwani sheria zipo na wanapaswa kuzitumia ili kufanikisha zoezi hilo la upatikaaji wa madawati.

Naye mtendaji wa kata ya Kongowe Said Kayangu alikiri kuwa baadhi ya maeneo zoezi hilo limeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.

Kayangu amesema kuwa watahakikisha muda uliosalia wanakamilisha zoezi hilo na kusema kuwa watajipanga vizuri ili kufanikisha zoezi hilo ili kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli ili kila mtoto aweze kukaa kwenye dawati.

mwisho.



Saturday, July 2, 2016

johngagariniblog: WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI

johngagariniblog: WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI: Na John Gagarini, Kibaha   MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wapya wa wilaya wlioteuliwa na Rais Dk John...

Friday, July 1, 2016

WAKUU WA WILAYA WAPYA WAAPISHWA PWANI


Na John Gagarini, Kibaha

 

MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wapya wa wilaya wlioteuliwa na Rais Dk John Magufuli mkoani humo kuinua pato la wananchi wa mkoa huo kutoka milioni 1.2 kwa mwaka hadi milioni 3 kwa mwaka.

 

Aliyasema hayo jana mjini Kibaha wakati akiwaapisha wakuu hao wa wilaya wapya na kusema kuwa pato la mwananchi wa mkoa wa Pwani liko chini sana licha ya kuwa na fursa mbalimbali za kipato.

 

Ndikilo alisema kuwa kutoakana na pato hilo la wananchi kuwa dogo kiasi hicho hata mchango wa mkoa kwa Pato la Taifa ni dogo sana la asilimia 1.8 jambo ambalo linapaswa kuwekewa mkakati wa kupandisha pato hilo ili liwe na mchango mkubwa kwa mwananchi na Taifa kwa ujumla.

 

“Nawapongezeni kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hizi na mkoa tayari umeandaa mpango kazi wake kwa ajili ya kuinua pato la mwananchi hivyo mnapaswa kuweka vipaumbele ambavyo vitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya unayoongoza,” alisema Ndikilo.

 

Alisema kuwa hakuna sababu ya mkoa kuendelea kuwa na pato dogo huku kukiwa na vyanzo vingi vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali mbalimbali kama vile uvuvi, kilimo, korosho, maliasili ikiwa ni pamoja na mbuga za wanyama na madini mbalimbali.

 

“Mfano ni majumba mengi yanayojengwa Dar es Salaam kokoto na mawe yanatoka mkoa wa Pwani hivyo hakuna sababu ya kuwa maskini tuna zao la korosho ambapo kwa msimu uliopita wakulima waliuza korosho zenye tahamani ya shilingi bilioni 18,” alisema Ndikilo.

 

Aliwataka wahakikisha wanawajibika na kutowalea watumishi ambao ni kikwazo na wenye urasimu wa kuwahudumia wananchi ambao hufika ngazi ya mkoa kulalamika ili hali ngazi za chini kuna watendaji ambao wangeweza kutatua matatizo hayo.

 

“Changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi na usalama, wahamiaji haramu, matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi nisingependa mambo haya yatokee tena hakikisheni mnatimiza wajibu wenu na kuwaondolea kero wananchi,” alisema Ndikilo.

 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa moja ya changamoto ambazo atakabiliana nazo ni pamoja na wahamiaji haramu kw akudhibiti bandari 19 ambazo zimekuwa ni njia ya wahamiaji hao haramu.

 

Naye Asumpter Mshama alisema kuwa moja ya mambo atayapaa kipaumbele ni kuhakikisha fedha kwa makundi ya vijana na akinamama asilimia 10 zinatoka ili wananchi waweze kujenga uchumi wao na ule wa Taifa.

 

Wakuu wapya walioapishwa jana ni pamoja na Shaibu Nunduma wilaya ya Mafia, Filberto Sanga Mkuranga, Gulamu Kifu wilaya ya Kibiti, Asumpter Mshama wilaya ya Kibaha, Juma Njwayo wilaya ya Rufiji na Majid Mwanga wilaya ya Bagamoyo huku Happyness William hakuweza kuapishwa kutokana na dharura.

 

Mwisho.


 MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto akimkabidhi zana za kufanyia kazi mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulamu Kifu, baada ya kumwapisha kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu huyo wa mkoa

Mkuu mpya wa wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto wakati wa hafla iliyofanyika mjini Kibaha ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo ambao waliteuliwa hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli

Mkuu mpya wa wilaya Rufiji Juma Njwayo kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wakiapishwa wakuu wa wilaya za mkoa huo kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa huo. 



Saturday, June 25, 2016

WAKANUSHA KUPAKA KINYESI NA KUVUNJA OFISI YA KATA

Na John Gagarini, Kibaha

WAKAZI wa Mtaa wa Machinjioni Loliondoa au Sagulasagula waliobomolewa nyumba zao na Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kwa tuhuma za kujenga nyumba kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko wamekanusha kuapaka kinyesi na kuvunja vioo vya ofisi ya kata ya Maili Moja.

Akizungumza na waandishi wa habari moja ya wahanga wa tukio la bomoa bomoa hiyo iliyofanyika Juni 16 na 17 mwaka huu ambapo watu hao walifanya uharibifu huu siku moja baada ya bomobomoa hiyo huku jumla ya nyumba 18 zilibomolewa, Said Tekelo amesema kuwa wao hawahusiki na tukio hilo na wamesikitishwa na kitendo hicho.

Tekelo amesema kuwa kitendo hicho kimefanywa na watu ambao walikuwa na malengo yao na hawaungi mkono watu waliofanya uharibifu huo kwani ni tukio ambalo ni kinyume cha sheria na hakistahili kuunga mkono.

Amesema kuwa wao kama wahanga wa bomobomoa hiyo hawawezi kufanya hivyo kwa sababu bado wako katika kutafuta haki yao waliyoipoteza baada ya nyumba zao kubomolewa pasipo kupewa fidia yoyote hivyo wasingeweza kufanya uharibifu.

Aidha amesema kuwa vi vema vyombo vya kisheria vikafanya yake ili kubaini wale waliofanya hivyo na kuwachukulia hatua kazi za kisheria kwani hao ni wahalifu kama wahalifu wengine na hawahusiani na waliobomolewa nyumba zao.

Amebainisha kuwa suala lao liko mahakamani tangu zoezi la kubomolewa nyumba zao lilipofanyika na hawaungi mkono watu waliofanya hivyo na wanawalaani vikali watu hao ambao wamejificha kwenye mwamvuli wa uhalifu.


MWISHO

ZEGERENI KUJENGA SHULE YA MSINGI

Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Zegereni wilayani Kibaha umefayatua matufali 2,500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule ya Msingi katika mtaa huo ambao unategemea mtaa wa Visiga kuwapeleka watoto wao umbali wa kilometa nane.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati wa zoezi la kuwapa zawadi wanafunzi wa darasa la saba ambao wamefanya vizuri na kuwa kwenye 10 bora mwenyekiti wa mtaa huo Rashid Likunja amesema kuwa wanatarajia kuanza ujenzi wa shule hiyo kuanzia Julai Mwaka huu ili ifikapo mwakani watoto wao waanze kusoma kwenye shule hiyo.

Likunja amesema kuwa fedha za kununulia kiwanja chenye ukubwa wa hekari sita zimetokana na mchango wa shilingi 5,000 kila kaya ambapo hatua ya ujenzi itaanza kwa kutumia tofaali hizo huku wakiwa na mifuko 12 ya simenti wakianza na madarasa mawili, ofisi na matundu manne ya vyoo.

Amesema kuwa kwa sasa wako kwenye harakati za kupata kibali cha ujenzi pamoja na ramani toka Halmashauri ya Mji ili waweze kuanza ujenzi huo na utawapunguzia watoto wao kwenda kusoma mbali pia huwabidi kuvuka barabara ya Morogoro ambapo ni hatari kwao kwani wengine ni wadogo sana.

Aidha amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia ili waweze kutekeleza azma yao ya ujenzi wa shule hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa watoto wanaotoka mtaa huo ambao wanafikia zaidi ya 200 wanaosoma madarasa mbalimbali kutoka mtaa huo ambao wanasoma shule jirani ya Visiga.


Mwisho.   

Thursday, June 23, 2016

MILIKINI MAENEO KIHALALI KUEPUKA MIGOGORO YA ARDHI-RC

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakazi wa mkoa huo kufuta taratibu na sheria za kumiliki ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi ambayo kwa sasa imeshamiri na inaweza kuhatarisha amani.

Aidha amesema kuwa mkoa hautasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu ambao wanavamia maeneo ya watu na kuyauza kama wanavyofanya baadhi ya watu kwani ni kinyume cha sheria na watachukuliwa hatua kali ili waachane na tabia hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na baadhi wananchi kutoka wilaya ya Mkuranga Ndikilo alisema kuwa kumekuwa na migogoro mingi ambayo imesababisha wananchi kutokuelewana wao kwa wao.

“Moja ya mfano ni Kijiji cha Kazole Kitongoji cha Magodani Kata ya Vikindu wilaya ya Mkuranga kuna baadhi ya watu wanajifanya kamati ya ardhi ya Kijiji hicho kulivamia shamba la kampuni ya Soap Allied Industry ambalo lina ukubwa wa hekari 1,750 likiwa na hati ya umiliki 271 ambayo iliipata tangu mwaka 1988 ambalo lilitengwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji,”alisema Ndikilo.

Ndikilo alisema kuwa kamati hiyo ambayo imekuwa ikiuza viwanja kwenye eneo hilo inafanya makosa kwa kuwauzia watu kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria kwani eneo hilo lina mmiliki halali ambaye anamiliki kisheria.

“Kama haitoshi watu hao walikwenda kwenye vyombo vya sheria lakini walishindwa na kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mtu hivyo hawapaswi kuingie kwenye eneo hilo lakini wanakamati hao bado wanaendelea kuwauzia watu na kujipatia mamilioni ambayo yote yanaingia mifukoni mwao na wamejinufaisha kupitia shamba hilo lakini wanawaibia watu kwani mmiliki mwenyewe yupo,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa suala la shamba hilo linachukuliwa kisiasa lakini mwisho wa siku linaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwani watu waliotoa fedha zao watakapoambiwa waondoke watadai fedha zao na hakuna mtu wa kuwarejeshea hivyo kuleta migogoro ambayo haitakiwi.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa ni vema watu wakafuata sheria bila ya shuruti kwani eneo hilo limeshatolewa maamuzi baada ya watu waliouziwa kwenda mahakamani na kuonekana kuwa kampuni hiyo ndiyo yenye uhalali wa kumiliki eneo hilo hivyo watu kuingia humo ni kuvunja sheria na wanaweza kukamatwa na polisi

Mushongi alisema kuwa watu hawapaswi kuingia kwenye eneo hilo ambapo hivi karibuni zaidi ya watu 20 waliingia kwenye shamba na kukamatwa na kwa kuwa hati ya umiliki bado haijatenguliwa watu wasiingie na kama wanaona wana haki ni vema wakaenda mahakama za juu kudai haki yao lakini si kulivamia.


Mwisho.