Thursday, April 28, 2016

REA KUNUFAISHA VIJIJI KWA MRADI WA MABILIONI


Na John Gagarini, Kisarawe

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) unatarajia kusambaza umeme kwa wananchi 11,000 wenye thamani ya shilingi bilioni 30 kwenye vijiji 109 vya mkoa huo .

Kwa mujibu wa Mhandisi mkuu wa Mradi huo wa REA mkoa wa Pwani Leo Mwakatobe alisema mradi huo wa awamu ya pili utakamilika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.

Mwakatobe alisema kuwa lengo kubwa kwa sasa ni kutekeleza agizo lililotolewa na serikali la kuhakikisha miradi hiyo ya umemem vijijini inawafiki wananchi wengi na kwa wakati uliopangwa.
“Tumeshaanza katika kutekeleza miradi hiyo katika maeneo ya Chalinze, Kisarawe na tutaendelea katika sehemu mbali mbali za Mkoa wetu wa Pwani na tunatarajia kufikia vijiji vipatavyo 109 vilivyopo katika Mkoa wetu,” alisema Madulu.   
Alisema kuwa kuwa mbali ya kuendelea kukutekeleza miradi hiyo hata hivyo wanakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa  wakati wanapotaka kupitisha miundomibu katika makazi ya watu.

“Baadhi ya watu wamekuwa hawataki kuridhia umeme kupita kwenye maeneo yao au kutaka fidia kubwa hali ambayo inasababisha kuwa na changamoto za hapa na pale lakini hata hivyo tunajitahidi kuwaelewe umuhimu wa miradi hiyo na kupata nishati hiyo ya umeme,” alisema Mwakatobe.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani  Martin Madulu alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza  agizo lililotolewa na serikali kuhakikisha wanawafikia wateja wao wote hususani wale wa vijijini  kwa lengo kuweza kuwaunganishia umeme kwa bei nafuu.

Madulu alisema kuwa watahakikisha wanafanya jitihada ili kuwafikia wateja wao ili waweze kuwa na nishati ya umeme katika maeneo mbai mbali hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Wakati huo huo wakazi zaidi wa 100 katika  kijiji cha  Nyeburu  Wilayani Kisarawe waliokuwa na tatizo  la upatikanaji wa nishati ya umeme na kuishi  katika giza  kwa kipindi cha muda mrefu kwa sasa wamenufaika baada ya  kuunganishiwa umeme kutokana na  kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu wa pili.

Baadhi ya wakazi hao walisema kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuleta chachu kubwa ya kimaendeleo katika kijiji hicho kwani mwanzoni   walikuwa wanashindwa tutimiza malengo yao waliyojiwekea kutokana na kutokuwa na nishati hiyo ya umeme.

Mwisho.

Tuesday, April 26, 2016

BODI YA MIKOPO TCU YASHAURIWA KUKOPESHA WANAFUNZI VYUO VYA KATI

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI na Bodi ya Mikopo Nchini (TCU) imeshauriwa kuviingiza kwenye mpango wa mikopo wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Kati kama ilivyo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu wakati mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu wa (CCM).
Sharifu alisema kuwa wanafunzi hao ni sawa na wale wa vyuo vikuu na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu na wanahitaji mikopo ili waweze kupata elimu ya juu.
“Hali ya sasa ni ngumu na wazazi ni wale wale wanahitaji kupunguziwa mzigo wa kulipa ada ambazo ni kubwa hivyo tunaona kuwa kuna haja ya serikali kuviingiza na vyuo vya kati kwenye mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa kwa kuwa nchi imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora hadi kufikia elimu ya juu ambayo ndiyo inaweza kumsaidia mtoto.
“Kwa sasa elimu ya juu ndiyo inayotakiwa tofauti na elimu ya kawaida ambayo si ya juu ambayo kwa sasa haina nafasi ya muhitimu kupata ajira hivyo kulazimisha watu wapate elimu ya juu,” alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa shirikisho hilo ni mboni ya chama na linafanya kazi kubwa ya kukijenga chama kwani hapo ni tanuru la kuandaa viongozi wa baadaye wa kukiongoza chama pamoja na nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Maulid Bundala  ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa Mkoa Mwinshehe Mlao alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alisema kuwa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM linafanya kazi kubwa ya kukitetea chama.
Bundala alisema kuwa CCM imeleta ukombozi ndani ya nchi na ni chama kikongwe hivyo kwa wanavyuo waliojiunga na shirikisho hilo wako sehemu salama kwani mawazo yao yataleta manufaa kwa nchi.
Aidha alisema kuwa nchi kwa sasa ina hitaji kuongozwa na wasomi hivyo wasomi hawa wataleta mabadiliko na chama kiko tayari kubadilika na wao wananafasi ya kumshauri Rais na wao ndiyo watakaoliinua taifa.
Naye naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Siraji Madebe alisema kuwa shirikisho lao linakabilia na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wancahama wake wale wa vyuo vya kati kutotambuliwa na Bodi ya Mikopo hivyo kutopata mikopo.
Madebe alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali lakini watahakikisha wanaendeleza umoja wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa shirikisho hilo ambayo ni kuwaunganisha wasomi walio vyuo kuwa na umoja wao ili kukipigania chama.

Mwisho.

Friday, April 22, 2016

SUMATRA POLISI KUWABURUTA MAHAKAMANI MADEREVA WA DALADALA WANAOKATISHA RUTI

Na John Gagarini, Kibaha
MADEREVA wa mabasi ya abiria yanayotoa huduma wilayani Kibaha yanayotokea Mbezi na Ubungo Jijini Dar es Salaam watakaokatisha ruti watafikishwa mahakamani badala ya kupigwa faini.
Akizungumza na gazeti hili Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) mkoani Pwani Nashon Iroga alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya madereva hao kudharau faini hizo na kulipa kwa urahisi.
Iroga alisema kuwa wamiliki wa mabasi hayo maarufu kama Daladala wamekuwa wakilipa faini na kuendelea kukatisha ruti hivyo kuwapa usumbufu abiria wanokwenda maeneo mbalimbali.
“Madereva hawa wamekuwa kama sugu licha ya kupigwa faini lakini wanalipa kwani wanaona kama ni afadhili kulipa faini na kukatisha ruti kuliko kuwafikisha abiria kule waendako,” alisema Iroga.
Alisema kuwa abiria wengi wanaokwenda maeneo ya Chalinze, Mkata, Msata na Mlandizi wamekuwa wakilalamika kuwa madereva hao hukatisha ruti na kugeuzia Kongowe kwa madai kuwa abirai wanaobaki ni wacheche hivyo wanapta hasara kuwapeleka maeneo hayo.
“Utakuta basi limetokea Ubungo au Mbezi na leseni yake inaonyesha linakwenda mfano Chalinze, Mkata, Msata  na Mlandizi akianza safari anakuwa na abiria wa kutosha lakini njiani abiria wanashuka hivyo wakifika Kongowe wanageuza wakidai kuwa abiria ni wachache hivyo hawapatia faida ndiyo wanakatisha ruti,” alisema Iroga.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Pwani (RTO) Abdi Isango alisema kuwa hadi juzi madereva sita walipandishwa kizimbani kutokana na kukatisha ruti hizo.
Isango alisema kuwa wao waliomba leseni kufika hayo maeneo ambayo yametajwa na yameandikwa kabisa lakini hawawafikishi abiria kule walikosema na wamekuwa wakiwafaulisha kwenye mabasi mengine.
“Tumeona ili kukomesha tabia hiyo ya kukatisha ruti ni kuwapeleka mahakamani madereva wao wenyewe kwani faini wanaidharau na kulipa lakini kwa sasa ni kuwafikisha mahakamani tumeona njia hii itasaidia kwani faini ya shilingi 30,000 au ile ya 250,000 ya SUMATRA zimekuwa zikilipwa na wamiliki wao,” alisema Isango.
Alisema kuwa madereva 25 wanatafutwa baada ya kutenda kosa hilo na kukimbia huku wawili wakiyaacha magari na kukimbia lakini bado wanatafutwa na mara watakapokamatwa watafikishwa mahakani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mwisho. 

SOKO LA MLANDIZI WALILIA USAFI

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA kwenye soko la Mlandizi Wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuwajengea mitaro kwenye soko hilo ili kuruhusu maji kupita wakati wa mvua kwani soko hilo liko kwenye hali mbaya.
Akizungumza na waandishi wa habari Sauda Said alisema kuwa mvua inaponyesha maji yanajaa na kuwa kero kwa wateja wanaofika kununua bidhaa.
Said alisema kuwa mbali ya kutokuwa na mitaro pia soko hilo lina uchafu mwingi kutokana na kutotolewa kwa kipindi kirefu na kusababisha uchafu huo kutoa harufu kali.
“Changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa vya kufanyia usafi kwani mbali ya kutoa kiasi cha shilingi 200 kila siku kama ushuru usafi haufanyiki ipasavyo hivyo kufanya mazingira ya soko kuwa machafu,” alisema Said.
Alisema kuwa soko hili kwa sasa linazalisha uchafu mwingi sana lakini tatizo ni halmashauri kushindwa kuondoa uchafu kwa wakati na kufanya mlundikano wa uchafu kuwa mkubwa hali ambayo ina hatarisha afya za watumiaji.
Naye mwenyekiti wa soko hilo Thobias Michael alisema kuwa soko hilo ni kubwa kuliko masoko yote mkoani Pwani na linahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe lakini mazingira yake si rafiki kwa watumiaji kutokana na uchafu kukithiri.
Michael alisema kuwa waliahidiwa kuwa watajengewa soko la kisasa ili kuondokana na changamoto wa soko hilo kwa sasa kuwa dogo kutokana na kuwa na wafanyabiashara wengi.
“Kwa sasa idadi ya wafanyabiashara ni 450 ni kubwa sana na uzalishaji wa uchafu ni mkubwa sana lakini uzoaji taka unakwenda taratibu sana na vifaa vya kufanyia usafi hakuna kwani hata gari la kuzolea taka hakuna inawabidi Halmashauri kukodisha,” alisema Michael.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha Dk Mariamu Maliwa alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa gari la Halmashauri kwa ajili ya kuzolea uchafu lakini wanakodisha gari kwa ajili ya kuzoa uchafu huo.

Mwisho.

KIBAHA WADHIBITI KIPINDUPINDU

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu eneo la Mlandizi ambao uliolipuka Machi mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake mjini Kibaha Dk Mariamu Maliwa alisema kuwa walifanikiwa kuudhibiti kwa kufungia biashara za vyakula ambazo hazikutimiza masharti ya afya.
Dk Maliwa alisema kuwa mgonjwa wa mwisho aliyekuwa amelazwa kwenye kituo cha afya Mlandizi aliruhusiwa Aprili 21na kufanya kutokuwa na mgonjwa Kipindupindu hata mmoja kutoka wagonjwa 115 waliogundulika kuwa na ugonjwa huo kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
“Kwa zaidi ya kipindi cha wiki moja tulizuia biashara zote za vyakula pamoja na matunda kwani tuliona kuwa sehemu hizo zilikuwa chanzo cha ugonjwa huo na tulipozifungia wagonjwa walipungua lakini kabla ya kuzifungia kulikuwa kunapatikana wagonjwa hadi nane kwa siku moja hali amabayo ilikuwa ni mbaya sana,” alisema Dk Maliwa.
Alisema kuwa mbali ya kuzuia biashara zote za vyakula pia walikuwa wakitoa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa kuhamasisha usafi kwenye maeneo ya biashara, majumbani na sehemu zinazozalisha uchafu kwa wingi, uzoaji taka na kuhamasisha matumizi ya vyoo na kwa wale wasio na vyoo wachimbe vyoo.
“Walikaidi kujenga vyoo tumewapeleka mahakamani kwani wanaonekana kukaidi maagizo hayo kwani kujisaidia holela nako kuna changngia kuenea kwa ugonjwa huu,” alisema Dk Maliwa.
Aidha alisema kuwa wagonjwa hao walitoka kwenye maeneo mbalimbali ya Kibaha na nje ya Kibaha ambapo Ruvu walikuja wagonjwa 63, Mlandizi 27, Visiga na Kongowe 13, Dutumi wanane, Vingunguti na Mbezi wawili, Mzenga mmoja na wale waliokufa mmoja alifia hospitali huku wawili wakifia majumbani.
Alisema kuwa wataruhusu wauzaji wa vyakula mara watakapoona kuna mabadiliko ya ufuataji wa kanuni za afya mara baada ya maofisa wa afya kupita na kujiridhisha kuwa vyanzo vyote vya ugonjwa huo vimedhibitiwa na kuzingatiwa kwa kanuni za usafi na kuwataka wananchi kuweka mazingira yao kwenye hali ya usafi.
Mwisho.

KEC SACCOS YAKOPESHA WANACHAMA WAKE MABILIONI YA FEDHA

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Ushirika wa Mikopo cha Shirika la Elimu Kibaha (KEC SACCOS LTD) kimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 kwa wanachama wake kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa Ushirika huo Kachingwe Kaselenge alisema kuwa mtaji wao kwa sasa umefikia zaidi ya Bilioni 2.
Kaselenge alisema kuwa kwa sasa akiba ndani ya chama imefikia bilioni 1.7 hisa zikiwa ni shilingi milioni 213.9 na mkopo ni bilioni 2.2 ambapo kwa kila mwezi wanatoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 190.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa chama kinaendelea vizuri kwani marejesho ni asilimia 98 hadi 99 ni wanachama wachache tu ambao wanarejesha kwa matatizo nah ii inatokana na kuwa na mikopo sehemu nyingine kwani sheria inasema mtumishi anapokopa lazima ibaki asilimia 1/3 ya mshahara wake,” alisema Kaselenge.
Alisema kuwa wanachama wao ni watumishi wa Shirika hilo lakini kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wameongeza wanachama ambao ni wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (KDC) na wale wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha (KTC) pamoja na wafanyakazi waofisi ya mkuu wa mkoa.
“Chama chetu ni moja ya vyama vikongwe hapa nchini kwani kwa mwaka huu kinatimiza miaka 50 tangu kunzishwa kwake na tunajivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata tangu kuanzishwa kwake kwani wanachama wameweza kunufaika na mikopo inayotolewa kwani zaidi ya watu 5,040 wananufaika kwa siku na mikopo hii kwani wanachama wana miradi mbalimbali kama ya mabasi, shule, ufugaji bodaboda na shughuli nyingine za kimaendeleo,” alisema Kaselenge.
Aidha alisema kuwa mtaji walio nao ni wa ndani kwani hawakopi kwenye mabenki kama baadhi ya vyama vinavyofanya hivyo hawana deni lolote wale mkopo kwenye taasisi za kifedha ambapo hubidi kuweka riba kubwa ili kufidia mikopo kwani kutokana na kuwa na mtaji wa ndani riba yao ni asilimia 1.6.
“Kuna mikopo ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Dharura kama vile misiba na majanga mbalimbali, Maendeleo ikiwa ni pamoja na ujuenzi wa nyumba usafiri na ufugaji, Elimu kusoma na kusomesha na mwanachama anapofariki familia inalipwa 300,000 na kama ni mwenza wake analipwa 200,000 kwani asilimia moja ni bima ya mkopo na endapo anafariki deni linakufa na fedha zake watalipwa ndugu bila ya kukatwa chochote kwani bima itakuwa inalinda mkopo huo,” alisema Kaselenge.
Alibainisha kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwa na ushindani mkubwa toka kwenye taasisi za kifedha ambazo zinawashawishi wanachama wao kujiunga nao kwa kuwalipia madeni wanayodaiwa kwenye chama, sheria kutaka vyama hivyo kutolipa kodi lakini wanaaambiwa walipe kodi na mwanachama anauwezo wa kukopa mara tatu ya akiba yake aliyojiwekea kati ya shilingi milioni moja hadi milioni zaidi ya 20.
Ushirika huo ulianzishwa mwaka 1966 ukiwa na wanachama ukiwa na wanachama 66 lakini kwa sasa una wanachama 840 na kilianzishwa kwa ajili ya  kusaidiana na kusaidia jamii inayowazunguka kwa kujitolea misaada sehemu mbalimbali kama hospitali na maeneo yenye uhitaji.
Mwisho.

Monday, April 18, 2016

SEKRETARIETI PWANI KUCHUNGUZA FEDHA ZILIZORUDISHWA HAZINA NA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amesema kuwa ataituma sekretarieti ya mkoa wa Pwani kufuatialia kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za mkoa huo kuchunguza juu ya fedha kiasi cha shilingi milioni 249, 452,390 kuwa zimerudishwa Hazina ikiwa ni sehemu ya fedha kiasi cha shilingi milioni 641,361,239 ambazo ni hasara zilizolipwa kwa watumishi hewa 25.
Mbali ya kuituma sekretarieti kufuatilia suala la fedha hizo pia amewataka wakuu wa wilaya kutumia vyombo vya dola kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia watu waliohusika kuchukua fedha hizo.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Kibaha Ndikilo alisema kuwa serikali haijaridhishwa na majibu ya wakurugenzi hao kuwa fedha hizo wamezirejesha Hazina huku kukiwa hakuna viambatanisho vyovyote ambavyo vinaonyesha kuwa fedha hizo zilipelekwa hazina.
“Serikali inataka kujua ni nani aliyehusika kuchukua fedha hizo kinyume cha taratibu za kazi kwani watumishi hao ni hewa lakini cha ajabu walikuwa wakilipwa mishahara kwa kila mwezi na kuitia serikali hasara kiasi hicho,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa kati ya hao watumishi hewa ni wale ambao wamefariki dunia, wasio kuwepo kazini kuacha kazi na wastaafu lakini walikuwa wanalipwa kama vile wako kazini jambo ambalo ni kinyume cha sheria na wanastahili kuchukuliwa hatua kali mara watakapo kutwa na tuhuma hizo.
“Zoezi hili litaendelea kufanyika ili kubaini ni njia gani walizokuwa wakizitumia hadi kufikia kulipwa fedha hizo ili hali hawako kazini na kuisababishia serikali hasara kubwa kiasi hicho hali ambayo imefanya zoezi hilo kufanywa kwa watumishi wa serikali ili kuwabaini,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema alisema kuwa kama kuna watu walikuwa wakifoji na kujipatia fedha hizo endapo watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha wizi huo wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuiibia serikali.
Alisisitiza kuwa suala la watumishi hewa lilikuwa ni kama kansa ambayo inaitafuna nchi lakini baada ya Rais Dk John Magufulia kubaini na kuagiza kutafutwa watumishi hewa ni dhahiri hatua zitakazochukuliwa zitakomesha watumishi hewa waliokuwa wanaiibia serikali.
Mwisho.