Friday, April 3, 2015
HABARI MPYA ZA PWANI
Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo amewataka wadau wa
mchezo wa bao kuwafundisha vijana ili kuendeleza mchezo huo ambao ulipendwa na
wapigania uhuru wa nchi akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Alitoa rai hiyo mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na
viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini wakati wa juma la jumuiya hiyo
lililoadhimishwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mchezo wa bao uliodhaminiwa na
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ili kumuenzi Baba wa Taifa
aliyekuwa akiupenda mchezo huo.
Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mchezo huo unachezwa zaidi na
wazee kuliko vijana hivyo kuna umuhimu wa kuwafundisha vijana ili waupende
mchezo huo na kuuendeleza.
“Tunampongeza mbunge kudhamini mashindano ya bao ambayo yalishirikisha
timu kutoka mitaa yote ya kata 11 za Kibaha Mjini na kuwashirikisha wazee huku
vijana wakiwa ni wachache,”alisema Ndikilo.
Alisema kuwa ili kumujenzi Baba wa Taifa wadau mbalimbali wa
mchezo huo wanapaswa kuwaweke mazingira mazuri ya kushiriki mchezo huo ambao ni
maarufu kwa wakazi wa mikoa ya Pwani.
Kwa upande wake Koka alisema kuwa lengo la kudhamini
mashindano ni kuuhamasisha mchezo huo ili usipotee na kuwafanya wazee nao
wapate kushiriki michezo.
Koka alisema kuwa ataendelea kuhamasisha mchezo huo hasa kwa
vijana ili uweze kupendwa na kuwavutia wengi kuliko kungangania baadhi ya
michezo kwani hata huo una nafasi yake.
Katika mashindano hayo timu ya Kata ya maili Moja ilifanikiwa
kuwa bingwa na kujinyakulia kiasi cha shilingi 300,000 huku kata ya Kibaha
wakijinyakulia 200,000 na kata za Mkuza, Mbwawa, Misugusugu, Tumbi, Visiga,
Pangani, Kongowe na Picha ya Ndege zilijinyakulia 100,000 kila moja kwa
ushiriki wao.
Aidha mashindano ya kukuna nazi wanawake Zuhura Rashid
alijinyakulia 70,000, akifuatiwa na Sara Alfred aliyejipatia 50,000 huku Zuhura
Ally akipata 30,000 huku washiriki wengine wakijinyakulia 20,000 kila mmoja kwa
ushiriki wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani amemwomba mkuu
wa mkoa wa Pwani kuzihimiza Halmashauri kuwawezesha wajasiriamali wanawake na
vijana kupata asilimia 10 ya mikopo kwa ajili yao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha mbele ya mkuu wa mkoa huo Evarist
Ndikilo alipokuwa akiongea na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Mji wa Kibaha
wakati wa maadhimisho ya juma la Wazazi.
Koka alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo toka halmashauri
ni changamoto kwa makundi hayo hali inayowafanya walalamike kutopatiwa fedha
hizo ambazo zimetengwa kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali.
“Mkuu wa mkoa naomba usaidie uwaandikie barua wakurugenzi wa
Halmashauri za wilaya za mkoa huu kuhakikisha zinawapatia fedha hizo makundi ya
akinamama na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuendeleza shughuli zao
za ujasirimali,” alisema Koka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Dk Athuman
Mokiwa alisema kuwa moja ya changamoto ianyowakabili ni ukosefu wa fedha kwa
ajili ya kupima kiwanja chao kilichopo Simbani.
Dk Mokiwa alisema wanaomba Halmashauri iwapimie kiwanja chao
ili waweze kuwa hati ya umiliki na kuweza kuweka wawekezaji ili Jumuiya iweze
kujiongezea kipato.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alisema kuwa
maombi yote yaliyotolewa na Jumuiya ya Wazazi yapelekwe kwa maandishi ofisini
kwake ili aweze kuwafikishia ujumbe wahusika.
Ndikilo aliipongeza Jumuiya hiyo na kusema ndiyo Jumuiya
kiongozi kwani imeyabeba makundi yote ya chama wakiwemo vijana, akinamama na
wazee hivyo lazima iwe mfano wa kuwa muhimili wa chama.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa Masjala za Ardhi kutasaidia kukabiliana
na migogoro na kupandisha thamani ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye vijiji
mkoani Pwani.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chakenge wilayani
Kisarawe wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alipotembelea
Masjala ya Kijiji hicho, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Cheyo
Nkelege alisema kuwa uanzishwaji wa Masjala hizo huwafanya wanakijiji kuwa na
hati za umiliki za kimila.
Nkelege alisema kuwa Masjala hizo zina faida kubwa hususani
kwa wananchi wa vijijini kwani wanaweza kuwa na hati miliki za mashamba yao
ambazo zinaweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo dhamana na rehani.
“Faida za kuanzishwa Masjala hizi kwanza inasaidia kupata
hati za umiliki za kimila, kurasimisha ardhi kwa wawekezaji, kuongeza thamani
ya ardhi, kuhifadhi nyaraka za ardhi na kupunguza migogoro ya mipaka ambayo
imesababisha hadi vifo,” alisema Nkelege.
Alisema kuwa faida nyingine ni kuwa na mipaka inayoeleweka na
kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekithiri baina ya wananchi na Vijiji kwa
Vijiji hivyo ni mpango mzuri unaopaswa kuigwa sehemu mbalimbali nchini.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa Masjala
hiyo ni kichocheo cha maendeleo kwani itatunza kumbukumbu mbalimbali za ardhi
na itawaondolea umaskini.
Ndikilo alisema kuwa jambo jema kwani hati miliki hizo
zitatambulika kisheria na zitaweza kutumika kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuweka dhamana kwa ajili ya kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za
maendeleo.
Akisoma risala juu ya ujenzi huo Belina Denisa alisema kuwa
ujenzi huo umekamilika ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 40 bila ya
samani za ndani ambayo ni fidia iliyotolewa na kampuni ya Sun Bio Fuel kwa
kijiji hicho baada ya kuchukua shamba kijijini hapo. Kutokana na ubora wa
Masjala hiyo mkuu wa mkoa huyo aliahidi kuwapatia 500,000 na 500,000 zitatolewa
na mbunge wa Jimbo la Kisarawe Hussein Jaffo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametumia kiasi
cha zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali waliojiunga
kwenye vikundi 150.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kongamano la
wajasiriamali wa Jimbo hilo na kusema kuwa lengo ni kuwafikia wajasiriamali
woete kwenye mitaa na kata hasa wale waliojiunga kwenye vikundi.
Koka alisema kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na shughuli
mbalimbali za ujasairiamali ikiwemo biashara pamoja na uzalishaji wa bidhaa
mbalimbali ambazo huziuza kwenye masoko mkoani humo na nje ya mkoa.
“Tumedhamiria kuwawawezesha wajasiriamali kiuchumi kwa
kuwapatia fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi za kuweza
kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa familia,” alisema Koka.
Alisema kuwa wajasiriamali wana uwezo wa kuinua kipato cha
jamii kwani ndiyo shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwawezesha kumudu maisha
kuliko ajira za kuajiriwa ambazo ni chache.
“Kama mnavyojua ujasiriamali umechukua nafasi kubwa ya
kiuchumi na umewasaidia watu wengi kujiajiri hususani vijana na akinamama hivyo
kuacha kuwa tegemezi,” alisema Koka.
Kwa upande wa mke wa Mbunge huyo Selina Koka ambaye ni mlezi
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Kibaha Mjini amekuwa akiwapatia mafunzo
ya ujasiriamali alisema kuwa kwa sasa wanawake wengi wameamka na kuendesha
familia kupitia shughuli hizo.
Selina alisema kuwa wajasirimali wanachotakiwa ni kuhakikisha
wanajiunga kwenye vikundi ili waweze kupata misaada ya fedha kwa ajili ya
kuendeshea shughuli zao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
HOSPITALI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imekamilisha
ujenzi wa chumba kipya cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya wilaya hiyo
ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya kuwa na chumba kidogo hali
iliyokuwa ikiwafanya kupeleka kuhifadhi maiti hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akisoma risala mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo
aliyetembelea hospitali hiyo ya wilaya, mganga mkuu wa wilaya Dk Happiness
Ndosi alisema kuwa hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa.
Dk Ndosi alisema kuwa ndugu wa marehemu walikuwa wakipata
taabu kuhifadhi maiti na kuzipeleka Jijini Dar es Salaam hivyo kutumia gharama
kubwa hadi wakati wa mazishi.
“Chumba cha maiti cha zamani kilikuwa na uwezo wa kuhifadhi
maiti wawili tu na kilijengwa miaka ya 1950 hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya
kuhifadhi miili ya marehemu ambapo huwabidi kuipeleka Muhimbili,” alisema Dk
Ndosi.
Alisema kuwa chumba hicho cha sasa hivi kitakuwa na uwezo wa
kuhifadhi miili 36 kwa wakati mmoja endapo itatumika vizuri hivyo kuondoa
changamoto hiyo.
“Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi milioni 102 ambazo
zimetoka serikali kuu ikiwa ni maombi maalumu ambapo umekamilika kwa asilimia
99 na kwa sasa imebaki kuingiza umeme pekee na utaingia muda wowote kuanzia
sasa na mafundi wanaendelea na kazi,” alisema Dk Ndosi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Subira Mgalu
alisema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa chumba hicho kwani
imewaondolea mzigo wa kuhifadhi maiti.
“Ilikuwa ni shida mtu akifa apelekwe Muhimbili halafua
arudishwe gharama zilikuwa ni kubwa sana hivyo imesaidia kupunguza usumbufu
hivyo watu wataweza kujipanga kuandaa shughuli za mazishi kwa nafasi,” alisema
Mgalu.
Mgalu alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo ambao umefanywa
na serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na kwa gharama nafuu
kwani sasa hawatapata usumbufu tena wa kuhifadhi maiti.
Naye mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa utu wa binadamu
utalindwa kwani kipindi cha nyuma mwili ulikuwa unazikwa harakahara kwani
ukikaa muda hata siku mbili una haribika hivyo kutoitendea haki maiti na
utawapunguzia gharama.
Ndikilo alisema watapata muda mzuri wa kuweza kuandaa mipango
ya mazishi kwa ajili ya kuwahifadhi wapendwa wao ambapo nyuma walikuwa wakikosa
muda wa kuweka mipango mizuri.
Mwisho.
Wednesday, April 1, 2015
HABARI LEO
Na John Gagarini,
Kibaha
KITUO cha Afya cha
Mkoani wilayani Kibaha mkoani Pwani kinakabiliwa changamoto ukosefu wa
vitanda 40 kwenye wodi ya wajawazito
hali inayosababisha kitanda kimoja kulaliwa na akinamama wanne.
Hayo yalibainika
wakati wa ziara ya Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini na kwenye kituo hicho
kilichopo mjini Kibaha kwenye maadhimisho ya wiki ya Jumuiya hiyo.
Ziara hiyo ya
kutembelea kituo hicho iliongozwa na mlezi wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ambayo huambatana na shughuli mbalimbali za
Kijamaii.
Ofisa Muuguzi wa Kituo
hicho Prisca Nyambo alisema kuwa changamoto hiyo ni kubwa sana kwani vitanda
vilivyopo ni nane.
“Kama mnavyoona
vitanda viko nane tu kwa ajili ya mama wajawazito lakini idadi ya wajawazito
wanaokuja kwa mwezi ni 250 hadi 300 ambapo idadi hiyo ni kubwa sana kwa kituo
chetu,” alisema Nyambo.
Nyambo alisema kuwa
idadi ya wajawazito waliojifungua mwezi Januari walikuwa 342 na Februari
walikuwa 344 ambapo hadi Machi 31 mama wajawazito 300 walikuwa tayari
wameshajifungua.
“Idadi ya mama
wajawazito wanaohudumiwa hapa ni wengi sana na tunaomba wadau mbalimbali
wajitokeze kuchangia vitanda na magodoro yake ili tukabiliane na changamoto
hii,” alisema Nyambo.
Aidha alisema kuwa
vifo vya watoto kwa mwezi Januari ilikuwa ni tisa na mwezi Februari vilikuwa
vifo saba ambavyo vinatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na akinamama
hao kwenda wakiwa katika hatua za mwisho kabisa pamoja na matumizi ya dawa za
kienyeji za kuongeza uchungu.
Kwa upande wake mlezi
huyo wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka alisema kuwa anaguswa na hali hiyo ambapo
alitoa vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya kujifungulia zikiwemo dawa, pamba na
vifaa vy kukatia vitovu.
Selina alisema kuwa
changamoto zingine atazifanyia kazi kwa kushirikiana na mbunge wa Jimbo hilo
Silvestry Koka ili kuwaondoa adha wanayoipata akianamama wajawazito wanaokwenda
kujifungua kituoni hapo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
MTOTO Joel Roman (3)
wa mtaa wa Ungindoni wilayani Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia baada ya
kutumbukia kwenye kisima cha maji alipokuwa akicheza.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Geofrid Nombo
alisema kuwa mtoto huyo aliondoka nyumbani na kuelekea kisimani akiwa peke
yake.
Nombo alisema kuw atukio
hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi baada ya mtoto huyo
kuondoka bila ya mama yake Marry Ngowi kujua.
“Alipoondoka mama yake
alimtafuta bila ya mafanikio ndipo alipowaambia majirani wenzake kisha kuanza
kumtafuta na ndipo walipokuta ndala zake zikiwa nje ya kisima huku yeye akiwa
amedumbukia kwenye kisiama hicho,” alisema Nombo.
Aidha alisema kuwa
mtoto huyo alikuwa akienda na mama yake kisimani hapo hivyo akawa amekariri
eneo hilo ambalo si mbali na nyumba waliyokuwa wakiishi.
“Kisima hicho cha maji
ni kirefu unaokaribia kufika futi tano na hutumiwa na watu wa eneo hilo kwa
ajili ya matumizi ya kufulia na kuogea wakati wa kiangazi lakini kwa bahati
mbaya kilikuwa wazi na hakikuzibwa juu,” alisema Nombo.
Aliongeza kuwa
kutokana na tukio hilo alimwamuru mmiliki wa kisima hicho ambaye alimtaja kwa
jina moja la Frank akifunike au akifukie ili kuepusha matukio kama hayo
yasiweze kutokea. Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Chalinze
KIJIJI cha Wafugaji
cha Mindutulieni kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo kinapoteza ngombe zaidi ya
600 wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Ndigana unaosababisha hasara ya shilingi
milioni 200 kila mwaka.
Akisoma risala ya
wanakijiji hao ofisa mtendaji Meisi Sokoroti kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze
Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara yake alisema kuwa ugonjwa huo umekuwa
unawatia hasara kubwa.
Sokoroti alisema kuwa
vifo vingi vinatokana na baadhi ya magonjwa ukiwemo huo ambao unawaletea ngombe
homa kali na kusababisha vifo .
“Hata hivyo baadhi ya
dawa zimekuwa na gharama kubwa ambapo dawa kama Butalex inauzwa kwa bei ya
shilingi 50,000 hali ambayo inawasababisha baadhi ya wafugaji kushindwa kumudu
gharama hiyo,” alisema Sokoroti.
Alisema kuwa tatizo
hilo la ngombe kufa kwa wingi lmedumu kwa kipindi cha miaka minne sasa ambapo
dawa mbalimbali za mifugo zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa sana.
“Ili kukabiliana na
changamoto hii tunaomba serikali ituletee dawa za mifugo zenye ruzuku ya
serikali ili kupunguza hasara hiyo,” alisema Sokoroti.
Aidha alisema kuwa ni
vyema serikali ikavitumia vyama vya wafugaji katika kuwapatia ruzuku ya dawa
kwani kwa sasa wauzaji wa dawa hizo wanawauzia kwa gharama kubwa mno.
Kwa upande wake
alisema kuwa kutokuwa na madawa ya ruzuku kumetokana na ufinyu wa bajeti toka
halmashauri lakini mara bajeti itakapokuwa nzuri wataweka ruzuku kwenye dawa
hizo.
Ridhiwani alisema kuwa
changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha ndiyo unachangia changamoto hiyo na kuwa
serikali inafanyia kazi suala hilo.
Mwisho.
IMEELEZWA kuwa mabaraza ya
wafanyakazi katika sehemu za kazi ni vyombo muhimu katika kuongeza ufanisi wa
kazi ikiwa ni pamoja kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu maslahi ya
wafanyakazi taasisi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki
mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akifungua
mkutano wa Baraza la Wafanyakzi wa Ofisi ya Rais Tume ya Mipango.
Ndikilo alisema kuwa wajibu wa
mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri
na watumishi wanatambua wajibu wao na haki zao na wanazingatia maadili ya
utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi wenye tija, staha na
upendo.
“Hata kama kutakuwa na sera, sheria
na kanuni nzuri za kazi kama hakuna malenbgo ya pamoja na ushirikiano baina ya
mwajiri na mwajiriwa ni vigumu taasisi hiyo kuwa na tija hivyo mabaraza yana
wajibu wa kumshauri mwajiri ili kuleta tija na mashikamano wa pamoja,” alisema
Ndikilo.
Alisema kuwa si vizuri kwa watumishi
kutumia muda mwingi katika kudai maslahi mazuri zaidi kuliko kupima kiwango cha
utekelezaji wa wajibu wao wa kazi hivyo viongozi wa mabaraza wana wajibu
wa kuwahimiza wafanyakazi kutimiza wajibu wao ili kufikia malengo.
“Nyie mmepewa majukumu makubwa
kitaifa kama vile kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Taifa
na kufanya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano
kuandaa mwongozo wa usimamizi wa utekelezaji wa umma na kukamilisha tafiti
mbalimbali zinazoharakisha maendeleo ya uchumi wan chi yetu na mahitaji ya
kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo mwaka 2015,” alisema Ndikilo.
Kw upande wake mwenyekiti wa baraza
hilo Florence Mwanri alisema kuwa tume imeendelea kukabiliana na changamoto ya
upatikanaji wa fedha katika kutekeleza majukumu yake pamoja na kupata wataalamu
wenye weledi.
Mwanri ambaye pia ni Naibu Katibu
Mtendaji anayesimamia klasta ya huduma za jamii na idadi ya watu alisema kuwa
katika kuhakikisha watumishi wanafanya kazi iapasavyo wamekuwa wakiwajengea
uwezo kupitia mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ili
kuwaongezea ufanisi katika utendaji kazi wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha
Mjini Selina Koka anatarajia kuanzisha mfuko wa kutoa mikopo isiyokuwa na riba
kwa wajasiriamali wa jimbo hilo utakaojulikana kama Chap Chap wa kuwasaidia
waweze kuinua uchumi wao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa
mkutano na wajasiriamali wanawake ambao wamewezeshwa mafunzo ya utengenezaji wa
bidhaa mbalimbali.
Selina alisema kuwa ameamua kufanya
hivyo kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wajasiriamali kwani taasisinyingi za
kifedha zinaweka riba kubwa kwenye mikopo.
“Wajasiriamali wengi wanashindwa
kuendeleza shughuli zao kutokana na riba kubwa wanazotozwa ambazo haziwezi
kuwakomboa kiuchumi lakini mfuko huu utakuwa hauwatozi riba yoyote,” alisema
Selina.
Alisema kuwa mkopo huo utaanzia kiasi
cha shilingi 50 hadi 200,000 lakini lengo ni kwa wale wenye biashara ndogo
kabisa.
“Tunatarajia kuwakopesha watu mmoja
mmoja na vikundi kwa kupitia kwa mabalozi, wenyeviti wa mitaa na madiwani
kwenye kata zote 11 za Kibaha Mjini bila ya kujali itikadi ya chama lengo ni
kuwainua wajasiriamali,” alisema Selina.
Aidha alisema hadi sasa tayari hadi
sasa wamevifikia vikundi 150 na kutumia gharama ya kiasi cha shilingi milioni
150.
Alibainisha kuwa mfuko huo unatrajia
kuanza kukopesha kabla ya mwishoni mwa mwaka huu na kusema kwa sasa wako kwenye
taratibu za kuandaa namna ya kutoa mikopo hiyo kisheria na kuwataka wale
watakaokopeshwa wawe waaminifu katika kurejesha.
Kwa upande wake Mbunge huyo alisema
kuwa anampongeza mkewe kwa kuweza kumsaidiaa katika kuwawezesha wajasiriamali
hususani wanawake.
Koka alisema kuwa yeye kwa
kushirikiana na mke wake watahakikisha malengo ya kuanzishwa mfuko huo
yanafikiwa ili kuwakwamua wanakibaha.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI wa dini wametakiwa kuacha
kujiingiza kwenye siasa badala yake wawahudumie waumini wao katika masuala ya
kiroho.
Hayo yalisemwa na Mwangalizi mkuu wa
Kituo cha Maandiko cha (PMC) kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Mchungaji Gervase
Masanja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mch Masanja alisema kuwa viongozi wa
dini kazi yao kubwa ni kuwaelekeza mambo muhimu ya kumjua Mungu pamoja na
kuishi kwa amani baina ya mtu na mtu na taifa kwa taifa.
“Viongozi wa dini tuna kazi kubwa
kwani waumini wanahitaji huduma kubwa za kiroho hivyo haipendezi kujiingiza
kwenye siasa na tudumishe amani iliyopo hapa nchini,” alisema Mch Masanja.
Alisema kuwa kazi ya siasa ni vema
ikaendeshwa na wanasiasa wenyewe huku viongozi wa dini wakiwa ni wapatanishi na
walinda amani ya nchi.
“Pia tusisahau kushiriki kwenye
masuala makubwa yaliyopo mbele yetu yakiwemo kujiandikisha kwenye Daftari la
wapiga kura, kura za maoni ya katiba inayopendekezwa na kushiriki kwenye
uchaguzi mkuu mwezi Oktoba,” alisema Mch Masanja.
Aidha alisema anawaomba wakristo na
wananchi kujitokeza kwa wingi katika upigaji wa kura ya maoni ya katiba
inayopendekezwa na si kususia.
“Kuipigia kura katiba inayopendekezwa
ni haki yako ya msingi hivyo mwananchi hupaswi kuisusia na kura utakayopiga ni
siri yako lakini si vema kutopiga kura hiyo kwa mustakbali wan chi yetu,”
alisema Mch Masanja.
Mwisho.
Wednesday, March 25, 2015
ABAKA WANAE KWA MIAKA MIWILI MFULULIZO
Na Mwandishi
Wetu, Kibaha
MKAZI wa
Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani Said Kundum (52) anatuhumiwa kuwabaka
watoto wake wawili wa kike kwa kipindi cha miaka miwili na kuwasababishia
maumivu makali.
Akizungumza
na waandishi wa habari mtoto mkubwa wa mtuhumiwa ambaye anasoma darasa la saba
katika Shule ya Msingi ya Miembe Saba jina limehifadhiwa (15) alisema kuwa baba
yake alikuwa akimbaka yeye na mdogo wake kwa nyakati tofauti.
Alisema kuwa
baba yake alianza kumbaka tangu mwaka 2013 ambapo kwa kipindi chote hicho
alipokuwa akiwafanyia vitendo hivyo aliwatishia kuwa atawaua endapo watasema
kwa mtu yoyote.
“Baba
alikuwa akitubaka kwa nyakati tofauti wakati mama akiwa anaenda sokoni Kariakoo
kuuza mboga huku akituacha na baba nyumbani na kutufanyia vietendo hivyo mimi
na mdogo wangu ambaye anasoma darasa la tatu shule ya Msingi Tandau akiwa na
miaka (12),” alisema Mwanafunzi huyo.
Aidha alisema
kuwa wakati wakifanyiwa vitendo hivyo walikuwa wakisikia maumivu makali lakini
aliwaambia kuwa wajikaze kwani baadaye watazoea na hawata sikia tena maumivu.
“Tulivumilia
kwa kipindi choete hicho lakini Jumamosi Machi 21 ilibidi ni mwambie mama na
kusema potelea mbali liwalo na liwe kama ataniua basi lakini hatuwezi kuvumilia
vitendo hivyo,” alisema mwanafunzi huyo.
Alibainisha
baada ya kumwambia mama yao ilibidi atoe taarifa kwa viongozi wa serikali ya
mtaa wa Miembe Saba ambao nao waliwataarifu polisi ambao walimkamata baba yake.
Naye mama
mzazi wa watoto hao Rahima Mshamu
alisema kuwa yeye hakujua kinachoendelea kati ya mume wake na watoto wake kwani
alikuwa akimuacha na watoto na hakutegemea kama angeweza kuwafanyia watoto wake
vitendo hivyo vya ukatili.
Mshamu alisema
tangu alipoona na mume wake amekuwa akifanya biashara ya kuuza mboga za majani
ambazo huzikusanya nyakati za jioni hadi usiku kisha kuzipeleka sokoni Kariakoo
Jijini Dar es Salaam.
“Mume
wangu nilikuwa nikimuamini kama baba na sikutegemea kama angeweza kufanya hivyo
na huwa nakusanya mboga kwenye maeneo mbalimbali huko mashambani majira ya saa
12 jioni baada ya hapo tunazisafirisha usiku kwenda Kariakoo ambapo kule huwa
tunazifikisha usiku wa manane na ifikapo saa 11 alfajiri tunakuwa tumemaliza na
tunaanza safari ya kurudi nyumbani,” alisema Mshamu.
Alisema kuwa
hayo ndiyo maisha waliyokuwa wakiishi tangu walipohamia kutokea Kibamba mwaka
2012 ambapo kwa kiasi kikubwa yeye amekuwa akiiendesha familia hiyo kwani mume
wake hana kazi maalumu.
“Roho
inaniuma sana kwani nimekuwa nikihangaika kuhakikisha kuwa familia yangu
haipati shida watoto wanakwenda shule na ana mtoto wake ambaye sijazaa naye
yuko sekondari namlipia ada na michango mingine na mahitaji yote lakini mume
wangu yeye haangaiki kwa chochote tukio hili limeniuma sana nashindwa hata
kujizuia,” alisema huku akilia kwa uchungu.
Aidha alisema
kuwa kutokana na kumpenda mume wake alimnunulia pikipiki kwa ajili ya kuongeza
kipato cha familia lakini aliuza pikipiki hiyo jambo ambalo lilimfanya ashindwe
kumwelewa kuwa ana tatizo gani lakini alishangazwa na afya za watoto wake
kuumwa magonjwa UTI kila mara.
“Mimi na
yeye hatukuwa na ugomvi wowote ambapo hivi karibuni alijaribu kuuza sehemu ya
eneo letu na nilipomuuliza alikataa hadi yule mnunuzi alipokuja na kutaka
kumalizia fedha zilizobaki ndipo niligundua kuwa aliuza eneo hilo kwa nguvu
bila ridhaa yangu na kusema kuwa aliwabaka watoto kuwa tuna ugomvi wa eneo hilo
si kweli kwani suala la eneo ni la mwezi Machi huku yeye akiwabaka watoto miaka
miwili iliyopita,” alisema Mshamu.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa mtaa huo Hamis Shomary alisema kuwa baada ya kumhoji
mtuhumiwa alikiri kufanya matukio hayo na kusema kuwa aliamua kufanya hivyo
kutokana na ugomvi aliokuwa nao na mke wake na kuwa alikuwa akimnyima unyumba.
Shomary alisema
kuwa mtuhumiwa alifikishwa polisi kwenye kituo cha Kongowe ambako anashikiliwa
kwa hatua zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kusubiri kupelekwa mahakamani.
Mwalimu mkuu
wa shule ya Miembe Saba anayosoma mwanafunzi huyo Rajab Chalamila alisema kuwa
mwanafunzi huyo alikuwa anaonekana mnyonge na mawazo mengi.
Chalamila
alisema kuwa kutokana na hali ya mwanafunzi huyo alimwita baba mzazi zaidi ya
mara mbili na kumwambia kuwa ampeleke hospitali mwanae na alisema alimpeleka na
kukutwa na malaria lakini hali bado ilikuwa inajirudia na kuonekana kuwa
ameathirika kisaikolojia. Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio
hilo.
Mwisho.
Wednesday, March 18, 2015
RIDHIWANI AENDELEA NA ZIARA JIMBONI CHALINZE
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani akiweka udongo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Kijiji cha Mkange wakati wa ziara yake kutembelea jimbo hilo kuona shughuli za maendeleo. |
Mzee Halfana Mgobanya wa kijiji cha Gongo akichota maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kijiji hicho ni moja ya vijiji vya jimbo hilo vinavyokabiliwa na tatizo la uhaba wa maji. |
Baadhi ya akinamama wa kijiji cha Mkange wakiwa wanachota maji huku kukiwa na foleni kubwa ya madumu ya maji eneo hilo nalo linakabilia na tatizo la maji ambayo yamekuwa yakitoka mara chache. |
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akifyetua tofali wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za maendeleo kwenye jimbo hilo |
Friday, March 6, 2015
CHAMA CHA WAIGIZAJI PWANI CHATOA MISAADA KWA WAGONJWA HOSPITALI YA TUMBI
Na John Gagarini,
Kibaha
CHAMA cha Waigizaji Tanzania
(TFDAA) mkoa wa Pwani kimetoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha.
Misaada hiyo kwa ajili
ya wagonjwa ilitolewa na baadhi ya wasanii kwa lengo la kuwafariji ambapo
baadhi hawana ndugu wa kuwafariji.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kutoa misaada hiyo katibu wa chama hicho
mkoani Pwani Kadnas Nassir alisema kuwa misaada hiyo ni moja ya shughuli
zinazofanywa na kundi hilo.
“Wagonjwa ni wenzetu
na mtu yoyote anaweza kuumwa kwa hiyo tumeona umuhimu wa kuwasaidia misaada kama
sehemu ya kuwajibika kwetu na kuwafariji ili waone kuwa kuwa jamii ya sanaa
nayo iko nao katika hali walizonazo,” alisema Nassir.
Nassir alisema kuwa
misaada hiyo licha ya kwamba siyo mikubwa sana lakini ni faraja kwa wagonjwa
ambao waliwapatia sabuni, dawa za meno nguo za watoto pamoja na mafagio ya
usafi kwa hospitali hiyo pia walifanya usafi.
“Sisi mbali ya kutoa
burudani pia tunajukumu la kuisadia jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kwenye matatizo na furaha,” alisema Nassir.
Naye moja ya wagonjwa
waliopatiwa msaada huo Beatrice Shirima alisema chama hicho kimeonyesha
ubinaadamu kwani baadhi ya watu wana uwezo lakini hawonyeshi kujali watu wenye
matatizo.
Kwa upande wake
muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo ya Tumbi Felisia Mungulele misaada hiyo
imeleta faraja kubwa kwa wagonjwa na wameona kuwa jamii inawajali na watu
wengine wajitokeze kusaidia kama hivyo.
Mwisho.
HABARI ZA PWANI
Na John Gagarini,
Kibaha
UKARABATI wa
miundombinu ya Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani
unatarajia kukamilika ifikapo Machi 20 mwaka huu na utapunguza kukatika umeme
mara kwa mara.
Kazi hiyo ya ukarabati
ilianza mwishoni mwa mwaka jana ulikuwa ukamilike Februari mwaka huu ulishindwa
kukamilika kwa kipindi hicho kutokana na ukubwa kazi hiyo ya kubadili
miundombinu ambayo imechakaa.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Meneja wa TANESCO mkoa huo Sana
Idindili alisema kuwa kutokana na zoezi hilo kumesababisha baadhi ya maeneo
kupata mgao wa umeme.
Idindili alisema kuwa ukarabati
huo ambao uko kwenye mradi umeongeza siku kutokana na kazi hiyo kuwa na ugumu
tofauti na mtazamo wa mwanzo.
“Ni kweli kumekuwa na
tatizo la umeme kukatika pamoja na mgao lakini hii inatokana na ukakarabati
unaoendelea lakini hadi ifikapo Machi 20 tutakuwa tumekamilisha na huduma ya
umeme itaendelea kama kawaida,” alisema Idindili.
Aidha alisema kuwa
siku hizo ziliongezeka kutokana na kipindi cha mwisho wa mwaka kulikuwa na
sikukuu ambazo ilibidi shughuli zisifanyike ndiyo sababu ya kuongeza siku zaidi
za kukamilisha zoezi hilo ambalo lilikuwa la miezi mitatu.
“Katika wiki kuna siku
tatu za kukata umeme kwa ajili ya kazi lakini nawatoa hofu wananchi kuwa mara
baada ya ukarabati huo watapata huduma nzuri na watafanya shughuli zao kama
kawaida,” alisema Idindili.
Alibainisha kuwa
katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za ukatikaji wa umeme wamekuwa
wakitoa matangazo kwa kutangaza na kwa wale wenye matumizi makubwa ya umeme
wamekuwa wakiwaandikia barua juu ya hali hiyo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
WAKULIMA wa Matunda na
Mbogamboga nchini wametakiwa kuachana na matumizi ya dawa za kuulia wadudu
badala yake watumie wadudu wanaokabiliana na wadudu waharibifu ili kunusuru
afya za walaji na soko la nje ya nchi.
Aidha mbinu hii ya
Kibaiolojia hutumia wadudu marafiki kama vile Nyigu ambao hudhibiti inzi au
wadudu waharibifu ambao hutaga mayai yao ndani ya tunda au kwenye mmea na
kuharibiwa na nyigu huyo.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Visumbufu vya Mimea
na Mazao kwa Njia ya Baiolojia (NBCP), Elibariki Msami alipoongea na mwandishi
wa habari hizi ofisini kwake.
Msami alisema kuwa njia
rahisi ni kuwatumia wadudu hao ambao wameonyesha kuwadhibiti wadudu hao
waharibifu kwa kiwango kikubwa hivyo kuepusha matumizi ya madawa.
“Tumekuwa tukifanya
utafiti kwa muda sasa ambapo tumeweza kuwazalisha nyigu hao ili wapambane na
wadudu waharibifu kwenye matunda kama vile embe, machungwa na mapera pamoja na
matunda mengine,” alisema Msami.
Alisema kuwa
teknolojia hiyo ya wadudu ilifanywa hasa kwenye maembe ambayo yalikuwa yakioza
kutokana na inzi wa embe kuyashambulia kwa kiasi kikubwa ambapo uharibifu umefikia
kati ya asilimia 50 hadi 80 ya uharibifu.
“Kuna aina mbalimbali
za wadudu wanaopambana na wadudu waharibifu ambao tunawazalisha na wameonyesha
uwezo mkubwa wa kukabiliana na wadudu hao waharibifu,” alisema Msami.
Alibainisha kuwa
upuliziaji wa dawa husababisha athari kwa wadudu marafiki ambao hupambana na
wadudu waharibifu, wakulima, mimea, wanyama na mazingira huathirika na madawa
hayo.
“Kwa upande wa
mbogamboga baadhi ya wakulima wamekuwa wakitumia madawa na kuwafanya wadudu hao
kuwa sugu pia dawa hizo wamekuwa wakizitumia muda mfupi kabla ya kuvuna jambo
ambalo si zuri kiafya,” alisema Msami.
Ofisa huyo mwandamizi
wa kituo hicho alisema changamoto kubwa inayowakabili katika kuwaeneza wadudu
hao ni ukosefu wa fedha unachokikabili kituo hicho na kuimba serikali kukisadia
ili kiweze kuzalisha wadudu hao kwa wingi.
Alisisistiza kuwa
wadudu wapya wanaoletwa toka nje ya nchi kwa njia ya mbegu zinazoingiza hapa
nchini ndiyo wamekuwa changamoto kubwa na wakulima wawe na imani na teknolojia
hiyo isiyo na athari zozote.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
KUFUATIA bei ya Mafuta
kushuka wananchi wameiomba serikali kupitia mamlaka zake kushusha bei za nauli
ambazo hazijashuka licha ya hali hiyo kujitokeza.
Walibainisha kuwa
kipindi cha nyuma wamiliki wa vyombo vya usafiri walikuwa wakipandisha bei mara
mafuta yanapopanda bei.
Akizungumza na gazeti
hili mkazi wa Maili Moja wilayani Kibaha Said Ng’ombe alisema kuwa bei ya nauli
inatokana na umbali na bei ya mafuta ambayo imeshuka kwa kiasi kikubwa.
“Tunaipongeza Serikali
kwa kuhakikisha bei imeshuka na kuwadhibiti wauzaji wa bidhaa hiyo kuuza kwa
bei iliyopo sokoni lakini pia wangepanga bei mpya za nauli kutokana na unafuu
wa mafuta ili maisha yaweze kuwa mazuri,” alisema Ng’ombe.
Ng’ombe alisema kuwa
mamlaka zinazohusika zinatakiwa kuliangalia hilo kwa undani kwani nauli bado
ziko palepale na hazijashuka.
“Tunaomba kuwe na
uwiano kama mafuta yameshuka bei na nauli nazo zishuke kwani walikuwa
wakilalamika kuwa bei ya mafuta ni kubwa ndisyo kisa cha nauli kuongezeka sasa
washushe na nauli,” alisema Ng’ombe.
Kwa upande wake Kibena
Mtoro alisema kuwa endapo nauli itashuka itasaidia kuwapunguzia mzigo wananchi
hivyo kufanya hali ngumu ya maisha kushuka na kuwa na hali nzuri.
Mtoro alisema kuwa nauli
imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi hivyo ushukaji wa wamafuta uambatane na
ushukaji wa nauli pamoja na vitu vyote vinavyotegemea mafuta.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)