Friday, March 6, 2015

CHAMA CHA WAIGIZAJI PWANI CHATOA MISAADA KWA WAGONJWA HOSPITALI YA TUMBI

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Waigizaji Tanzania (TFDAA) mkoa wa Pwani kimetoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha.
Misaada hiyo kwa ajili ya wagonjwa ilitolewa na baadhi ya wasanii kwa lengo la kuwafariji ambapo baadhi hawana ndugu wa kuwafariji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa misaada hiyo katibu wa chama hicho mkoani Pwani Kadnas Nassir alisema kuwa misaada hiyo ni moja ya shughuli zinazofanywa na kundi hilo.
“Wagonjwa ni wenzetu na mtu yoyote anaweza kuumwa kwa hiyo tumeona umuhimu wa kuwasaidia misaada kama sehemu ya kuwajibika kwetu na kuwafariji ili waone kuwa kuwa jamii ya sanaa nayo iko nao katika hali walizonazo,” alisema Nassir.
Nassir alisema kuwa misaada hiyo licha ya kwamba siyo mikubwa sana lakini ni faraja kwa wagonjwa ambao waliwapatia sabuni, dawa za meno nguo za watoto pamoja na mafagio ya usafi kwa hospitali hiyo pia walifanya usafi.
“Sisi mbali ya kutoa burudani pia tunajukumu la kuisadia jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye matatizo na furaha,” alisema Nassir.
Naye moja ya wagonjwa waliopatiwa msaada huo Beatrice Shirima alisema chama hicho kimeonyesha ubinaadamu kwani baadhi ya watu wana uwezo lakini hawonyeshi kujali watu wenye matatizo.
Kwa upande wake muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo ya Tumbi Felisia Mungulele misaada hiyo imeleta faraja kubwa kwa wagonjwa na wameona kuwa jamii inawajali na watu wengine wajitokeze kusaidia kama hivyo.

Mwisho.   

No comments:

Post a Comment