Na John Gagarini,
Kibaha
UKARABATI wa
miundombinu ya Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani
unatarajia kukamilika ifikapo Machi 20 mwaka huu na utapunguza kukatika umeme
mara kwa mara.
Kazi hiyo ya ukarabati
ilianza mwishoni mwa mwaka jana ulikuwa ukamilike Februari mwaka huu ulishindwa
kukamilika kwa kipindi hicho kutokana na ukubwa kazi hiyo ya kubadili
miundombinu ambayo imechakaa.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Meneja wa TANESCO mkoa huo Sana
Idindili alisema kuwa kutokana na zoezi hilo kumesababisha baadhi ya maeneo
kupata mgao wa umeme.
Idindili alisema kuwa ukarabati
huo ambao uko kwenye mradi umeongeza siku kutokana na kazi hiyo kuwa na ugumu
tofauti na mtazamo wa mwanzo.
“Ni kweli kumekuwa na
tatizo la umeme kukatika pamoja na mgao lakini hii inatokana na ukakarabati
unaoendelea lakini hadi ifikapo Machi 20 tutakuwa tumekamilisha na huduma ya
umeme itaendelea kama kawaida,” alisema Idindili.
Aidha alisema kuwa
siku hizo ziliongezeka kutokana na kipindi cha mwisho wa mwaka kulikuwa na
sikukuu ambazo ilibidi shughuli zisifanyike ndiyo sababu ya kuongeza siku zaidi
za kukamilisha zoezi hilo ambalo lilikuwa la miezi mitatu.
“Katika wiki kuna siku
tatu za kukata umeme kwa ajili ya kazi lakini nawatoa hofu wananchi kuwa mara
baada ya ukarabati huo watapata huduma nzuri na watafanya shughuli zao kama
kawaida,” alisema Idindili.
Alibainisha kuwa
katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za ukatikaji wa umeme wamekuwa
wakitoa matangazo kwa kutangaza na kwa wale wenye matumizi makubwa ya umeme
wamekuwa wakiwaandikia barua juu ya hali hiyo.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
WAKULIMA wa Matunda na
Mbogamboga nchini wametakiwa kuachana na matumizi ya dawa za kuulia wadudu
badala yake watumie wadudu wanaokabiliana na wadudu waharibifu ili kunusuru
afya za walaji na soko la nje ya nchi.
Aidha mbinu hii ya
Kibaiolojia hutumia wadudu marafiki kama vile Nyigu ambao hudhibiti inzi au
wadudu waharibifu ambao hutaga mayai yao ndani ya tunda au kwenye mmea na
kuharibiwa na nyigu huyo.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Visumbufu vya Mimea
na Mazao kwa Njia ya Baiolojia (NBCP), Elibariki Msami alipoongea na mwandishi
wa habari hizi ofisini kwake.
Msami alisema kuwa njia
rahisi ni kuwatumia wadudu hao ambao wameonyesha kuwadhibiti wadudu hao
waharibifu kwa kiwango kikubwa hivyo kuepusha matumizi ya madawa.
“Tumekuwa tukifanya
utafiti kwa muda sasa ambapo tumeweza kuwazalisha nyigu hao ili wapambane na
wadudu waharibifu kwenye matunda kama vile embe, machungwa na mapera pamoja na
matunda mengine,” alisema Msami.
Alisema kuwa
teknolojia hiyo ya wadudu ilifanywa hasa kwenye maembe ambayo yalikuwa yakioza
kutokana na inzi wa embe kuyashambulia kwa kiasi kikubwa ambapo uharibifu umefikia
kati ya asilimia 50 hadi 80 ya uharibifu.
“Kuna aina mbalimbali
za wadudu wanaopambana na wadudu waharibifu ambao tunawazalisha na wameonyesha
uwezo mkubwa wa kukabiliana na wadudu hao waharibifu,” alisema Msami.
Alibainisha kuwa
upuliziaji wa dawa husababisha athari kwa wadudu marafiki ambao hupambana na
wadudu waharibifu, wakulima, mimea, wanyama na mazingira huathirika na madawa
hayo.
“Kwa upande wa
mbogamboga baadhi ya wakulima wamekuwa wakitumia madawa na kuwafanya wadudu hao
kuwa sugu pia dawa hizo wamekuwa wakizitumia muda mfupi kabla ya kuvuna jambo
ambalo si zuri kiafya,” alisema Msami.
Ofisa huyo mwandamizi
wa kituo hicho alisema changamoto kubwa inayowakabili katika kuwaeneza wadudu
hao ni ukosefu wa fedha unachokikabili kituo hicho na kuimba serikali kukisadia
ili kiweze kuzalisha wadudu hao kwa wingi.
Alisisistiza kuwa
wadudu wapya wanaoletwa toka nje ya nchi kwa njia ya mbegu zinazoingiza hapa
nchini ndiyo wamekuwa changamoto kubwa na wakulima wawe na imani na teknolojia
hiyo isiyo na athari zozote.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
KUFUATIA bei ya Mafuta
kushuka wananchi wameiomba serikali kupitia mamlaka zake kushusha bei za nauli
ambazo hazijashuka licha ya hali hiyo kujitokeza.
Walibainisha kuwa
kipindi cha nyuma wamiliki wa vyombo vya usafiri walikuwa wakipandisha bei mara
mafuta yanapopanda bei.
Akizungumza na gazeti
hili mkazi wa Maili Moja wilayani Kibaha Said Ng’ombe alisema kuwa bei ya nauli
inatokana na umbali na bei ya mafuta ambayo imeshuka kwa kiasi kikubwa.
“Tunaipongeza Serikali
kwa kuhakikisha bei imeshuka na kuwadhibiti wauzaji wa bidhaa hiyo kuuza kwa
bei iliyopo sokoni lakini pia wangepanga bei mpya za nauli kutokana na unafuu
wa mafuta ili maisha yaweze kuwa mazuri,” alisema Ng’ombe.
Ng’ombe alisema kuwa
mamlaka zinazohusika zinatakiwa kuliangalia hilo kwa undani kwani nauli bado
ziko palepale na hazijashuka.
“Tunaomba kuwe na
uwiano kama mafuta yameshuka bei na nauli nazo zishuke kwani walikuwa
wakilalamika kuwa bei ya mafuta ni kubwa ndisyo kisa cha nauli kuongezeka sasa
washushe na nauli,” alisema Ng’ombe.
Kwa upande wake Kibena
Mtoro alisema kuwa endapo nauli itashuka itasaidia kuwapunguzia mzigo wananchi
hivyo kufanya hali ngumu ya maisha kushuka na kuwa na hali nzuri.
Mtoro alisema kuwa nauli
imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi hivyo ushukaji wa wamafuta uambatane na
ushukaji wa nauli pamoja na vitu vyote vinavyotegemea mafuta.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment