Wednesday, April 1, 2015

HABARI LEO

Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mkoani wilayani Kibaha mkoani Pwani kinakabiliwa changamoto ukosefu wa vitanda  40 kwenye wodi ya wajawazito hali inayosababisha kitanda kimoja kulaliwa na akinamama wanne.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini na kwenye kituo hicho kilichopo mjini Kibaha kwenye maadhimisho ya wiki ya Jumuiya hiyo.
Ziara hiyo ya kutembelea kituo hicho iliongozwa na mlezi wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ambayo huambatana na shughuli mbalimbali za Kijamaii.
Ofisa Muuguzi wa Kituo hicho Prisca Nyambo alisema kuwa changamoto hiyo ni kubwa sana kwani vitanda vilivyopo ni nane.
“Kama mnavyoona vitanda viko nane tu kwa ajili ya mama wajawazito lakini idadi ya wajawazito wanaokuja kwa mwezi ni 250 hadi 300 ambapo idadi hiyo ni kubwa sana kwa kituo chetu,” alisema Nyambo.
Nyambo alisema kuwa idadi ya wajawazito waliojifungua mwezi Januari walikuwa 342 na Februari walikuwa 344 ambapo hadi Machi 31 mama wajawazito 300 walikuwa tayari wameshajifungua.
“Idadi ya mama wajawazito wanaohudumiwa hapa ni wengi sana na tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kuchangia vitanda na magodoro yake ili tukabiliane na changamoto hii,” alisema Nyambo.
Aidha alisema kuwa vifo vya watoto kwa mwezi Januari ilikuwa ni tisa na mwezi Februari vilikuwa vifo saba ambavyo vinatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na akinamama hao kwenda wakiwa katika hatua za mwisho kabisa pamoja na matumizi ya dawa za kienyeji za kuongeza uchungu.
Kwa upande wake mlezi huyo wa Jumuiya ya Wazazi Selina Koka alisema kuwa anaguswa na hali hiyo ambapo alitoa vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya kujifungulia zikiwemo dawa, pamba na vifaa vy kukatia vitovu.
Selina alisema kuwa changamoto zingine atazifanyia kazi kwa kushirikiana na mbunge wa Jimbo hilo Silvestry Koka ili kuwaondoa adha wanayoipata akianamama wajawazito wanaokwenda kujifungua kituoni hapo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MTOTO Joel Roman (3) wa mtaa wa Ungindoni wilayani Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji alipokuwa akicheza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Geofrid Nombo alisema kuwa mtoto huyo aliondoka nyumbani na kuelekea kisimani akiwa peke yake.
Nombo alisema kuw atukio hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi baada ya mtoto huyo kuondoka bila ya mama yake Marry Ngowi kujua.
“Alipoondoka mama yake alimtafuta bila ya mafanikio ndipo alipowaambia majirani wenzake kisha kuanza kumtafuta na ndipo walipokuta ndala zake zikiwa nje ya kisima huku yeye akiwa amedumbukia kwenye kisiama hicho,” alisema Nombo.
Aidha alisema kuwa mtoto huyo alikuwa akienda na mama yake kisimani hapo hivyo akawa amekariri eneo hilo ambalo si mbali na nyumba waliyokuwa wakiishi.
“Kisima hicho cha maji ni kirefu unaokaribia kufika futi tano na hutumiwa na watu wa eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya kufulia na kuogea wakati wa kiangazi lakini kwa bahati mbaya kilikuwa wazi na hakikuzibwa juu,” alisema Nombo.
Aliongeza kuwa kutokana na tukio hilo alimwamuru mmiliki wa kisima hicho ambaye alimtaja kwa jina moja la Frank akifunike au akifukie ili kuepusha matukio kama hayo yasiweze kutokea. Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo. 
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
KIJIJI cha Wafugaji cha Mindutulieni kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo kinapoteza ngombe zaidi ya 600 wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Ndigana unaosababisha hasara ya shilingi milioni 200 kila mwaka.
Akisoma risala ya wanakijiji hao ofisa mtendaji Meisi Sokoroti kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara yake alisema kuwa ugonjwa huo umekuwa unawatia hasara kubwa.
Sokoroti alisema kuwa vifo vingi vinatokana na baadhi ya magonjwa ukiwemo huo ambao unawaletea ngombe homa kali na kusababisha vifo .
“Hata hivyo baadhi ya dawa zimekuwa na gharama kubwa ambapo dawa kama Butalex inauzwa kwa bei ya shilingi 50,000 hali ambayo inawasababisha baadhi ya wafugaji kushindwa kumudu gharama hiyo,” alisema Sokoroti.
Alisema kuwa tatizo hilo la ngombe kufa kwa wingi lmedumu kwa kipindi cha miaka minne sasa ambapo dawa mbalimbali za mifugo zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa sana.
“Ili kukabiliana na changamoto hii tunaomba serikali ituletee dawa za mifugo zenye ruzuku ya serikali ili kupunguza hasara hiyo,” alisema Sokoroti.
Aidha alisema kuwa ni vyema serikali ikavitumia vyama vya wafugaji katika kuwapatia ruzuku ya dawa kwani kwa sasa wauzaji wa dawa hizo wanawauzia kwa gharama kubwa mno.
Kwa upande wake alisema kuwa kutokuwa na madawa ya ruzuku kumetokana na ufinyu wa bajeti toka halmashauri lakini mara bajeti itakapokuwa nzuri wataweka ruzuku kwenye dawa hizo.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha ndiyo unachangia changamoto hiyo na kuwa serikali inafanyia kazi suala hilo.
Mwisho.  

 Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa mabaraza ya wafanyakazi katika sehemu za kazi ni vyombo muhimu katika kuongeza ufanisi wa kazi ikiwa ni pamoja kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu maslahi ya wafanyakazi taasisi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakzi wa Ofisi ya Rais Tume ya Mipango.
Ndikilo alisema kuwa wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu wao na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi wenye tija, staha na upendo.
“Hata kama kutakuwa na sera, sheria na kanuni nzuri za kazi kama hakuna malenbgo ya pamoja na ushirikiano baina ya mwajiri na mwajiriwa ni vigumu taasisi hiyo kuwa na tija hivyo mabaraza yana wajibu wa kumshauri mwajiri ili kuleta tija na mashikamano wa pamoja,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa si vizuri kwa watumishi kutumia muda mwingi katika kudai maslahi mazuri zaidi kuliko kupima kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao wa kazi hivyo viongozi  wa mabaraza wana wajibu wa kuwahimiza wafanyakazi kutimiza wajibu wao ili kufikia malengo.
“Nyie mmepewa majukumu makubwa kitaifa kama vile kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Taifa  na kufanya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano kuandaa mwongozo wa usimamizi wa utekelezaji wa umma na kukamilisha tafiti mbalimbali zinazoharakisha maendeleo ya uchumi wan chi yetu na mahitaji ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo mwaka 2015,” alisema Ndikilo.
Kw upande wake mwenyekiti wa baraza hilo Florence Mwanri alisema kuwa tume imeendelea kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa fedha katika kutekeleza majukumu yake pamoja na kupata wataalamu wenye weledi.
Mwanri ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia klasta ya huduma za jamii na idadi ya watu alisema kuwa katika kuhakikisha watumishi wanafanya kazi iapasavyo wamekuwa wakiwajengea uwezo kupitia mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ili kuwaongezea ufanisi katika utendaji kazi wao.
Mwisho.     

Na John Gagarini, Kibaha
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka anatarajia kuanzisha mfuko wa kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa wajasiriamali wa jimbo hilo utakaojulikana kama Chap Chap wa kuwasaidia waweze kuinua uchumi wao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa mkutano na wajasiriamali wanawake ambao wamewezeshwa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.
Selina alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wajasiriamali kwani taasisinyingi za kifedha zinaweka riba kubwa kwenye mikopo.
“Wajasiriamali wengi wanashindwa kuendeleza shughuli zao kutokana na riba kubwa wanazotozwa ambazo haziwezi kuwakomboa kiuchumi lakini mfuko huu utakuwa hauwatozi riba yoyote,” alisema Selina.
Alisema kuwa mkopo huo utaanzia kiasi cha shilingi 50 hadi 200,000 lakini lengo ni kwa wale wenye biashara ndogo kabisa.
“Tunatarajia kuwakopesha watu mmoja mmoja na vikundi kwa kupitia kwa mabalozi, wenyeviti wa mitaa na madiwani kwenye kata zote 11 za Kibaha Mjini bila ya kujali itikadi ya chama lengo ni kuwainua wajasiriamali,” alisema Selina.
Aidha alisema hadi sasa tayari hadi sasa wamevifikia vikundi 150 na kutumia gharama ya kiasi cha shilingi milioni 150.
Alibainisha kuwa mfuko huo unatrajia kuanza kukopesha kabla ya mwishoni mwa mwaka huu na kusema kwa sasa wako kwenye taratibu za kuandaa namna ya kutoa mikopo hiyo kisheria na kuwataka wale watakaokopeshwa wawe waaminifu katika kurejesha.
Kwa upande wake Mbunge huyo alisema kuwa anampongeza mkewe kwa kuweza kumsaidiaa katika kuwawezesha wajasiriamali hususani wanawake.
Koka alisema kuwa yeye kwa kushirikiana na mke wake watahakikisha malengo ya kuanzishwa mfuko huo yanafikiwa ili kuwakwamua wanakibaha.
Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI wa dini wametakiwa kuacha kujiingiza kwenye siasa badala yake wawahudumie waumini wao katika masuala ya kiroho.
Hayo yalisemwa na Mwangalizi mkuu wa Kituo cha Maandiko cha (PMC) kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Mchungaji Gervase Masanja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mch Masanja alisema kuwa viongozi wa dini kazi yao kubwa ni kuwaelekeza mambo muhimu ya kumjua Mungu pamoja na kuishi kwa amani baina ya mtu na mtu na taifa kwa taifa.
“Viongozi wa dini tuna kazi kubwa kwani waumini wanahitaji huduma kubwa za kiroho hivyo haipendezi kujiingiza kwenye siasa na tudumishe amani iliyopo hapa nchini,” alisema Mch Masanja.
Alisema kuwa kazi ya siasa ni vema ikaendeshwa na wanasiasa wenyewe huku viongozi wa dini wakiwa ni wapatanishi na walinda amani ya nchi.
“Pia tusisahau kushiriki kwenye masuala makubwa yaliyopo mbele yetu yakiwemo kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura, kura za maoni ya katiba inayopendekezwa na kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba,” alisema Mch Masanja.
Aidha alisema anawaomba wakristo na wananchi kujitokeza kwa wingi katika upigaji wa kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na si kususia.
“Kuipigia kura katiba inayopendekezwa ni haki yako ya msingi hivyo mwananchi hupaswi kuisusia na kura utakayopiga ni siri yako lakini si vema kutopiga kura hiyo kwa mustakbali wan chi yetu,” alisema Mch Masanja.
Mwisho.
    














No comments:

Post a Comment