Friday, April 3, 2015

HABARI MPYA ZA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo amewataka wadau wa mchezo wa bao kuwafundisha vijana ili kuendeleza mchezo huo ambao ulipendwa na wapigania uhuru wa nchi akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Alitoa rai hiyo mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Kibaha Mjini wakati wa juma la jumuiya hiyo lililoadhimishwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mchezo wa bao uliodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ili kumuenzi Baba wa Taifa aliyekuwa akiupenda mchezo huo.
Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mchezo huo unachezwa zaidi na wazee kuliko vijana hivyo kuna umuhimu wa kuwafundisha vijana ili waupende mchezo huo na kuuendeleza.
“Tunampongeza mbunge kudhamini mashindano ya bao ambayo yalishirikisha timu kutoka mitaa yote ya kata 11 za Kibaha Mjini na kuwashirikisha wazee huku vijana wakiwa ni wachache,”alisema Ndikilo.
Alisema kuwa ili kumujenzi Baba wa Taifa wadau mbalimbali wa mchezo huo wanapaswa kuwaweke mazingira mazuri ya kushiriki mchezo huo ambao ni maarufu kwa wakazi wa mikoa ya Pwani.
Kwa upande wake Koka alisema kuwa lengo la kudhamini mashindano ni kuuhamasisha mchezo huo ili usipotee na kuwafanya wazee nao wapate kushiriki michezo.
Koka alisema kuwa ataendelea kuhamasisha mchezo huo hasa kwa vijana ili uweze kupendwa na kuwavutia wengi kuliko kungangania baadhi ya michezo kwani hata huo una nafasi yake.
Katika mashindano hayo timu ya Kata ya maili Moja ilifanikiwa kuwa bingwa na kujinyakulia kiasi cha shilingi 300,000 huku kata ya Kibaha wakijinyakulia 200,000 na kata za Mkuza, Mbwawa, Misugusugu, Tumbi, Visiga, Pangani, Kongowe na Picha ya Ndege zilijinyakulia 100,000 kila moja kwa ushiriki wao.
Aidha mashindano ya kukuna nazi wanawake Zuhura Rashid alijinyakulia 70,000, akifuatiwa na Sara Alfred aliyejipatia 50,000 huku Zuhura Ally akipata 30,000 huku washiriki wengine wakijinyakulia 20,000 kila mmoja kwa ushiriki wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani amemwomba mkuu wa mkoa wa Pwani kuzihimiza Halmashauri kuwawezesha wajasiriamali wanawake na vijana kupata asilimia 10 ya mikopo kwa ajili yao.
Aliyasema hayo mjini Kibaha mbele ya mkuu wa mkoa huo Evarist Ndikilo alipokuwa akiongea na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Mji wa Kibaha wakati wa maadhimisho ya juma la Wazazi.
Koka alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo toka halmashauri ni changamoto kwa makundi hayo hali inayowafanya walalamike kutopatiwa fedha hizo ambazo zimetengwa kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali.
“Mkuu wa mkoa naomba usaidie uwaandikie barua wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya za mkoa huu kuhakikisha zinawapatia fedha hizo makundi ya akinamama na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuendeleza shughuli zao za ujasirimali,” alisema Koka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Dk Athuman Mokiwa alisema kuwa moja ya changamoto ianyowakabili ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kupima kiwanja chao kilichopo Simbani.
Dk Mokiwa alisema wanaomba Halmashauri iwapimie kiwanja chao ili waweze kuwa hati ya umiliki na kuweza kuweka wawekezaji ili Jumuiya iweze kujiongezea kipato.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alisema kuwa maombi yote yaliyotolewa na Jumuiya ya Wazazi yapelekwe kwa maandishi ofisini kwake ili aweze kuwafikishia ujumbe wahusika.
Ndikilo aliipongeza Jumuiya hiyo na kusema ndiyo Jumuiya kiongozi kwani imeyabeba makundi yote ya chama wakiwemo vijana, akinamama na wazee hivyo lazima iwe mfano wa kuwa muhimili wa chama.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa Masjala za Ardhi kutasaidia kukabiliana na migogoro na kupandisha thamani ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye vijiji mkoani Pwani.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chakenge wilayani Kisarawe wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo alipotembelea Masjala ya Kijiji hicho, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Cheyo Nkelege alisema kuwa uanzishwaji wa Masjala hizo huwafanya wanakijiji kuwa na hati za umiliki za kimila.
Nkelege alisema kuwa Masjala hizo zina faida kubwa hususani kwa wananchi wa vijijini kwani wanaweza kuwa na hati miliki za mashamba yao ambazo zinaweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo dhamana na rehani.
“Faida za kuanzishwa Masjala hizi kwanza inasaidia kupata hati za umiliki za kimila, kurasimisha ardhi kwa wawekezaji, kuongeza thamani ya ardhi, kuhifadhi nyaraka za ardhi na kupunguza migogoro ya mipaka ambayo imesababisha hadi vifo,” alisema Nkelege.
Alisema kuwa faida nyingine ni kuwa na mipaka inayoeleweka na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekithiri baina ya wananchi na Vijiji kwa Vijiji hivyo ni mpango mzuri unaopaswa kuigwa sehemu mbalimbali nchini.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa Masjala hiyo ni kichocheo cha maendeleo kwani itatunza kumbukumbu mbalimbali za ardhi na itawaondolea umaskini.
Ndikilo alisema kuwa jambo jema kwani hati miliki hizo zitatambulika kisheria na zitaweza kutumika kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka dhamana kwa ajili ya kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Akisoma risala juu ya ujenzi huo Belina Denisa alisema kuwa ujenzi huo umekamilika ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 40 bila ya samani za ndani ambayo ni fidia iliyotolewa na kampuni ya Sun Bio Fuel kwa kijiji hicho baada ya kuchukua shamba kijijini hapo. Kutokana na ubora wa Masjala hiyo mkuu wa mkoa huyo aliahidi kuwapatia 500,000 na 500,000 zitatolewa na mbunge wa Jimbo la Kisarawe Hussein Jaffo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametumia kiasi cha zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali waliojiunga kwenye vikundi 150.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kongamano la wajasiriamali wa Jimbo hilo na kusema kuwa lengo ni kuwafikia wajasiriamali woete kwenye mitaa na kata hasa wale waliojiunga kwenye vikundi.
Koka alisema kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasairiamali ikiwemo biashara pamoja na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ambazo huziuza kwenye masoko mkoani humo na nje ya mkoa.
“Tumedhamiria kuwawawezesha wajasiriamali kiuchumi kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi za kuweza kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa familia,” alisema Koka.
Alisema kuwa wajasiriamali wana uwezo wa kuinua kipato cha jamii kwani ndiyo shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwawezesha kumudu maisha kuliko ajira za kuajiriwa ambazo ni chache.
“Kama mnavyojua ujasiriamali umechukua nafasi kubwa ya kiuchumi na umewasaidia watu wengi kujiajiri hususani vijana na akinamama hivyo kuacha kuwa tegemezi,” alisema Koka.
Kwa upande wa mke wa Mbunge huyo Selina Koka ambaye ni mlezi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Kibaha Mjini amekuwa akiwapatia mafunzo ya ujasiriamali alisema kuwa kwa sasa wanawake wengi wameamka na kuendesha familia kupitia shughuli hizo.
Selina alisema kuwa wajasirimali wanachotakiwa ni kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi ili waweze kupata misaada ya fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe           
HOSPITALI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imekamilisha ujenzi wa chumba kipya cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya wilaya hiyo ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya kuwa na chumba kidogo hali iliyokuwa ikiwafanya kupeleka kuhifadhi maiti hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akisoma risala mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo aliyetembelea hospitali hiyo ya wilaya, mganga mkuu wa wilaya Dk Happiness Ndosi alisema kuwa hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa.
Dk Ndosi alisema kuwa ndugu wa marehemu walikuwa wakipata taabu kuhifadhi maiti na kuzipeleka Jijini Dar es Salaam hivyo kutumia gharama kubwa hadi wakati wa mazishi.
“Chumba cha maiti cha zamani kilikuwa na uwezo wa kuhifadhi maiti wawili tu na kilijengwa miaka ya 1950 hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya kuhifadhi miili ya marehemu ambapo huwabidi kuipeleka Muhimbili,” alisema Dk Ndosi.
Alisema kuwa chumba hicho cha sasa hivi kitakuwa na uwezo wa kuhifadhi miili 36 kwa wakati mmoja endapo itatumika vizuri hivyo kuondoa changamoto hiyo.
“Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi milioni 102 ambazo zimetoka serikali kuu ikiwa ni maombi maalumu ambapo umekamilika kwa asilimia 99 na kwa sasa imebaki kuingiza umeme pekee na utaingia muda wowote kuanzia sasa na mafundi wanaendelea na kazi,” alisema Dk Ndosi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Subira Mgalu alisema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa chumba hicho kwani imewaondolea mzigo wa kuhifadhi maiti.
“Ilikuwa ni shida mtu akifa apelekwe Muhimbili halafua arudishwe gharama zilikuwa ni kubwa sana hivyo imesaidia kupunguza usumbufu hivyo watu wataweza kujipanga kuandaa shughuli za mazishi kwa nafasi,” alisema Mgalu.
Mgalu alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo ambao umefanywa na serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na kwa gharama nafuu kwani sasa hawatapata usumbufu tena wa kuhifadhi maiti.
Naye mkuu wa mkoa Ndikilo alisema kuwa utu wa binadamu utalindwa kwani kipindi cha nyuma mwili ulikuwa unazikwa harakahara kwani ukikaa muda hata siku mbili una haribika hivyo kutoitendea haki maiti na utawapunguzia gharama.
Ndikilo alisema watapata muda mzuri wa kuweza kuandaa mipango ya mazishi kwa ajili ya kuwahifadhi wapendwa wao ambapo nyuma walikuwa wakikosa muda wa kuweka mipango mizuri.
Mwisho.
 

         

No comments:

Post a Comment