Sunday, April 26, 2015

HABARI MBALIMBALI ZA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Pwani kimechagua viongozi wake kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Uchaguzi huo ambao ulifanyika mjini Kibaha mwishoni mwa wiki hii ulimerejesha madarakani mwenyekiti wa zamani John Kirumbi ambaye alijinyakulia jumla ya kura 43 kati ya kura 85 za wajumbe wa uchaguzi huo na kuwashinda wenzake sita.
Kirumbi aliwashinda Hamis Kwangaya aliyejipatia kura 41 na Rajab Chalamila aliyepata kura moja huku wengine wakiambulia patupu huku Stella Kiyabo akipata nafasi ya kuwakilisha mkoa ngazi ya Taifa alijinyakulia kura 58.
Katika nafasi hiyo wagombea Hebert Mgimi aliyepata kura 15 na Mikidadi Mbelwa 12 huku nafasi ya mwaka hazina ikienda kwa Abubakary Alawi aliyepata kura 48, Honesta Mwilenga akipata kura 34 na Neema Wasato akipata kura mbili.
Kwa upande wa mwakilishi wa wanawake Martha Kanyawana alipata kura 55, Happy Mahava alipata kura 29 na Ajenta Mrema alipata kura moja upande wa nafasi ya mwakilishi wa watu wenye ulemavu Mohamed Ngomero alipata kura 48 akifuatiwa na Robert Bundala kura 37.
Nafasi ya uwakilishi wa vijana Judith Mangi alishinda kwa kura 42, David Phares alipata kura 27 na Charles Tesha kura 11, mwakilishi wa wenyeviti ni Mustapha Julius kura 80 huku za hapana zikiwa ni tano.
Kwa upande wa mjumbe kwenda baraza la Wafanyakazi TUCTA ni Rajab Mhambage aliyepata kura 71 kura nane za hapana na moja iliharibika huku wajumbe wawili kwenda TUCTA ni Grace Kalinga kura 54 na  Herbet Ngimi kura 28 huku kura mbili zikiharibika.
Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo katibu wa CWT Pwani Joseph Nehemia alisema kuwa uchaguzi huo ulikwenda vizuri licha ya changamoto ndogondogo za hapa na pale.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha ACT Wazalendo mkoani Pwani kimeanza kujiimarisha baada ya kuweza kujinyakulia wanachama 1,200 kutoka vyama mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini  Kibaha katibu wa ACT mkoa wa huo Mrisho Halfan alisema kuwa chama hicho kimeweza kupata wanachama wengi kwa muda mfupi kutokana na sera nzuri ilizonazo.
Halfan alisema kuwa sera za chama hicho ni zile alizokuwa akitekeleza Mwalimu Julius Nyerere za uzalendo wan chi yake na si manufaa ya mtu au watu wachache.
“Uzinduzi wa matawi nao umesaidia kuwavutia watu kujiunga na chama chetu ambacho ni chama cha wazalendo na kina mlengo tofauti na vyama vingine na kitaleta mageuzi ya kweli,” alisema Halfan.
Alisema kuwa ACT inakuja kivingine ili kufikia lengo la kuwasaidia wananchi kwani baadhi ya vyama havina sera nzuri zaidi ya kushambuliana majukwaani.
“ACT ni chama cha ukweli sisi hatutaki siasa za kukashifiana kama baadhi ya vyama vinavyofanya ambapo hutumia muda mwingi kushambulia upande fulani lakini vinashindwa kuwajibika kwa wananchi,” alisema Halfan
Aidha alisema kwa sasa watu wanataka maendeleo na si malumbano kwani yamewapotezea muda watu badala ya kutafakari kuleta maendeleo ambayo ndiyo kiu ya kila Mtanzania.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha wa wafanyakazi wa hifadhi ya mahoteli na majumbani na huduma za jamii (CHODAWU) kimewaomba waajiri kuchagua wafanyakazi bora na hodari wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa CHODAWU mkoani Pwani Paul Msilu alisema kuwa waajiri wafanye uchaguzi mzuri juu ya wafanyakazi bora.
Msilu alisema kuwa kwa mwaka huu chama chao ndiyo kinachoandaa sherehe za wafanyakazi kupitia shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwenye mkoa huo zitakazofanyika wilayani Mafia.
“Tunawaomba waajiri kuwachagua wafanyakazi bora ili iwe motisha na kuondoa manunguniko juu ya uteuzi wa wafanyakazi wenye sifa za kuwa bora,” alisema Msilu.
Aidha alisema anaomba waajiri kuwapatia zawadi zinazostahili ili kuwafanya wafanyakazi wajitume wawapo kazini kwani motisha ya zawadi nzuri ndizo zitaleta jitihada za uwajibikaji.
“Maandalizi yanaendelea vizuri ambapo baadhi ya vitu vimekamilika na bado tunaendelea kuomba michango kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ili kufanikisha sherehe hizo zinazofanyika kila mwaka,” alisema Msilu.
Alisema sherehe hizo ni muhimu kwa wafanyakazi ambao siku hiyo hukaa kwa pamoja na kubadilishana mawazo pamoja na kujua changamoto na mafanikio yao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WALIMU na wanafunzi wametakiwa kushirikiana ili kuhakikisha Taifa la Tanzania linakuwa na watafiti na wagunduzi wa teknolojia mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka wakati wa sherehe za kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri kwenye shindano la Insha iliyokuwa inasema utatumiaje rasilimali zlizopo kukiabilina na umaskini lililoandaliwa na mbunge huyo.
Koka alisema kuwa utafiti na ugunduzi ndiyo utakaopelekea nchi kupata mafanikio katika maenedeleo kupitia tafiti na ugunduzi wa masuala mbalimbali.
“Tafiti na ugunduzi ndiyo silaha ya kujiletea maendeleo kwa nchi yoyote ile hivyo lazima tuwajenge wanafunzi wetu kuwa wagunduzi na watafiti wa mambo ya kimaendeleo,” alisema Koka.
Alisema kuwa endapo wanafunzi wataandaliwa katika katika masuala hayo basi watweza kugundua teknolojia ambazo wataziuza kama ilivyo kwa mataifa yaliyoendelea ambayo yananufaika.
“Hayo yote tunaweza kuyafikia kwa kuwa na ushirikiano baina ya pande zote wakiwemo walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe na insha kama hizi huwasaidia wanafunzi kujenga ujasiri wa kujieleza na kama maandalizi ya elimu ya juu,” alisema Koka.
Awali kwa upande wake mwenyekiti wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Youth Under Umbrella Castro David alisema kuwa lengo la insha hiyo ambayo ilishirikisha shule 14 za sekondari ni kuwajengea wanafunzi ustadi wa uandishi wa kazi za fasihi za ubunifu .
David alisema kuwa pia lengo lingine ni  kuziunganisha shule ili ziwe na ushirikiano wa kitaaluma na kufanya utafiti ambapo mshindi alikuwa ni Sara Malambo kutoka shule ya sekondari ya Tumbi ambaye alijinyakulia 100,000, akifuatiwa na Hija Hega wa Visiga 50,000 na Peter Asenga 30,000 ambazo walikabidhiwa na Mbunge huyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment