Sunday, April 26, 2015

KILUVY UNITED YALILIA UDHAMINI TFF

Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF) limeshauriwa kutafuta wadhamini kwa ajili ya ligi mbalimbali na si ligi kuu pekee ili kuzipunguzia gharama timu za madaraja ya chini.
Ushauri huo ulitolewa na mlezi wa timu ya soka ya Kiluvya United ya mkoa wa Pwani Edward Mgogo wakati wa sherehe za kutambulisha kombe walilochukua la ligi ya mabingwa wa mikoa kwa mkuu wa mkoa huo Evarist Ndikilo na kufanikiwa kupanda daraja la kwanza.
Mgogo alisema kuwa timu za madaraja ya chini zina mzigo mkubwa katika kuziendesha timu zao hivyo ni vema zikasaidiwa kupata ufadhili ili ziweze kushiriki ligi zao vizuri.
“Umefika wakati sasa ligi za chini nazo zikawa na udhamini ndiyo kazi ya TFF kuziwekea mazingira mazuri timu ziweze kushiriki vema kwenye ligi ambapo ligi kuu imekuwa na wadhamini tofauti tofauti,” alisema Mgogo.
Alisema kuwa msingi wa wachezaji wa ligi kuu ni ligi ndogo za chini hivyo ni vema TFF ikatafuta wadhamini ili wadhamini ligi hizo ambazo zinatoa wachezaji ambao wanatamba kwenye ligi ya Voda Com.
“Bila ya udhamini timu zinacheza kwenye mazingira magumu sana ambapo sisi tunatarajia kucheza ligi daraja la kwanza hivyo tunaomba TFF iliangalie hili pamoja na wadau wengine wajitokeze kutusaidia ili tufikie lengo letu la kupanda ligi kuu,” alisema Mgogo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkuu wa mkoa ambaye ni ofisa elimu Yusuph Kipengele alisema kuwa mkoa hauna fungu maalumu kwa ajili ya michezo.
 Kipengele alisema kuwa wao kama mkoa wanachoweza ni kutoa barua kwa ajili ya timu kwenda kuomba misaada sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusaidiwa ili kuendeleza michezo.
Mwisho.             

    

No comments:

Post a Comment