Sunday, April 5, 2015

PIMENI MAENEO YA SHULE NA WAKRISTO WAOMBEENI POLISI

Na John Gagarini, Chalinze
VIONGOZI wa Vijiji na Vitongoji kwenye Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo  mkoani Pwani wametakiwa kupima maeneo yao ya shule ili kupata hati miliki na kuepuka uvamizi wa maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete wakati wa uzinduzi wa shule ya Msingi ya Happy Lukwambe kwenye kijiji cha Visakazi.
Ridhiwani alisema kuwa baadhi ya shule Jimboni humo maeneo yake hayajapimwa hivyo kufanay baadhi ya watu kuvamia maeneo ya shule.
“Kwa kuwa eneo lenu la shule liko kwenye mazingira mazuri na mmefanya uhifadhi wa misitu ni vema mkalipima eneo lenu ili muwe na hati ya umiliki wa ardhi muweze kukabiliana na wavamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shule,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa kwa kuwa shule hiyo imejengwa kisasa ni moja ya shule za msingi ambazo ni za mfano katika wilaya ya Bagamoyo na hata nchi nzima lazima mazingira yake yalindwe.
“Isije ikawa baada ya muda si mrefu mkaja kwangu kulalamika kuwa eneo lenu limevamiwa nawashauri pimeni eneo lenu kupitia uongozi wa shule na Kijiji ili kufanikisha zoezi hilo,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake moja ya wafadhili wa ujenzi wa shule hiyo Happy Frank kutoka nchini Uingereza alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi huo na kusema kuwa kukamilika kwa shule hiyo japo ni madarasa matatu lakini ni mafanikio na ni kumbukumbu nzuri kwa familia yake.
Naye msimamizi wa ujenzi huo Remigius Mshenga alisema kuwa shule hiyo imejengwa kutokana na eneo hilo kutokuwa na shule ambapo wanafunzi walikuwa wakienda kilometa 17 kwenye shule ya Msingi Bwawani.
Mshenga alisema kuwa watoto wengi wa eneo hilo walikuwa wakishindwa kwenda shule kutokana na umbali ambapo wengine waliacha shule na sasa inaanza na wanafunzi 55 ambapo gharama za ujenzi ni shilingi milioni 60 pamoja na madawati na ujenzi wake ulianza mwaka 2013 wa madarasa matatu.
Naye ofisa elimu wa wilaya ya Bagamoyo Abdul Buheti alisema kuwa wataendelea kuisaidia shule hiyo kwa kuhakikisha wanapeleka walimu wenye sifa pamoja na vitabu vya ziada na kiada na kwa kuitambua shule hiyo tayari wameshapeleka walimu wawili wanaofundisha watoto hao wa darasa la kwanza hadi la tatu.
Shule hiyo imekengwa kwa ufadhili wa Happy Bricks Foundation ya nchini Uingereza na kusimamiwa na taasisi ya Ngerengere River Eco Camp.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kibaha
WAKRISTO nchini wametakiwa wakati wakiadhimisha sikukuu ya kufufuka Yesu Kristo  (Pasaka)  waliombee Jeshi la Polisi lisendelee kufanyiwa vitendo vya kinyama na baadhi ya watu wenye nia mbaya na nchi.
Siku za hivi karibuni kuwamekuwa na matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi na kuwaua askari kisha kupora silaha ambazo hazifahamiki huwa zinapelekwa wapi.
Akizungumza kwenye ibaada ya Pasaka kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Jimbo la Magharibi Usharika wa Maili Moja, Mchungaji wa kanisa hilo Isai Ntele alisema kuwa hali hiyo inahatarisha amani ya nchi.
Mch Ntele alisema kuwa hali hiyo ya uvamizi wa vituo vya polisi na kuwaua kisha kuchukua silaha havipaswi kuachwa kuendelea kwani haifahamiki silaha zinazoibiwa zinatumika vipi.
“Hali hii si ya kuifumbia macho hata sisi wakristo wakati tunasherehekea sikukuu hii ya kufufuka Yesu Kristo lazima tuiombee amani ya nchi kwani walinda amani wanashambuliwa sasa na kuuwawa sisi tutakuwa salama,” aliuliza Mch Ntele.
Aidha alisema kuwa watu hao wanaofanya vitendo hivyo wanaweza wakawa wanafanya uhalifu kwa kutumia silaha hizo hivyo wananchi wakawa hawawezi tena kuishi kwa amani na kuwajengea hofu.
“Watu hawa ni wabaya kwani wakiingia mtaani na hizo silaha tutakuwa hatuna amani tena kwani vitendo vya uhalifu vitaongezeka hivyo lazima tufanya maombi ya kuwaombea askari wetu ili wawe salama waweze kutulinda na sisi,” alisema Mch Ntele.
Aliwataka wakristo kuadhimisha sikukuu hiyo kwa upendo na mshakamano na kuacha vitendo ambavyo vitaleta athari ndani ya jamii ili kudumisha amani ya nchi yetu.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment