Na John Gagarini,
Bagamoyo
MKOA wa Pwani
umefanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni nane kupitia Wakala
wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kipindi cha mwaka 2013/2014.
Hayo yalisemwa juzi
wilayani Bagamoyo na Ofisa Misitu wa mkoa huo Daniel Isara, wakati wa
maadhimisho ya upandaji miti kimkoa iliyofanyika kwenye eneo la la Gareza la
Kigongoni ambapo ilipandwa zaidi ya miti 3,000.
Isara alisema kuwa
fedha hizo zimetokana na kukabiliana na uharibifu wa rasilimali misitu na
mazingira ambapo doria ziliimarishwa na ukusanyaji wa mapato kufikia kiasi
hicho.
Alisema kuwa hadi kufikia
mwezi Januari 2014/2015 makusanyo yalifikia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni
sita baada ya wakala hao kuongeza watumishi kwenye ngazi za wilaya.
“Mbali ya mafanikio ya
ukusanyaji wa mapato hayo ya Serikali pia mkoa umehamasisha na mwamko umekuwa mkubwa
na kuongeza uanzishwaji wa vitalu vya miche na upandaji wa miti kwe taasisi za
serikali na zisizo za serikali na watu binafsi kutoka miche ya miti milioni
2,253,136 mwaka 2013/2014 na kufikia milioni 2,663,202 mwaka 2014/2015,”
alisema Isara.
Aidha alisema kuwa pia
wakala imeweza kuwaondoa wavamizi kwenye misitu ya Ruvu Kaskazini, Ruvu Kusini,
Kiloka, Kazimzumbwi na wavuvi kwenye Delta ya Rufiji pia kuweka mipaka ya
misitu ya hifadhi kiasi cha kilometa 640 katika hekta 10,704.
“Changamoto
zinazoikabili rasilimali ya misitu ni pamoja na ongezeko kwa wakazi wa mkoa wa
Dar es Salaam ambalo huongeza mahitaji ya mkaa na kuni hivyo kuongezeka kwa
ukataji na ufyekaji wa misitu na mapori,” alisema Isara.
Alibainisha kuwa kuna
wafanyabiashara 320 waliosajiliwa kufanyabiashara ya kuvuna mazao ya misitu
mkoani Pwani kwa mwaka 2013/2014 na 336
mwaka 2014/2015 na zaidi ya asilimia 90 wanatoka nje ya mkoa.
Kwa upande wake mkuu
wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ambaye
aliwakilishwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa taasisi
zinazotumia kuni kwa wingi kwa ajili ya kupikia na shughuli nyingine zinapaswa
kupanda miti kwa wingi.
Ndikilo alisema kuwa
zinapaswa kutumia majiko sanifu yanayotumia kuni au mkaa kidogo ili iwe sehemu
ya ubunifu wa kupunguza matumizi makubwa ya nishati ya miti.
Aliwataka wananchi
kila mtu kupanda miti ili kulinda mazingira pia mamalaka za serikali za mitaa
kuomba vibali vya kuajiri watumishi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa
rasilimali misitu na misitu iliyohifadhiwa inatunzwa na kuzuia wavamizi wanaoingiza
mifugo, uchimbaji wa mchanga, kilimo na makazi kwenye misitu.
Mkoa wa Pwani una
misitu 34 ya hifadhi yenye jumla ya hekta 335,712 iliyohifadhiwa kisheria na
hekta milioni 2.2 ya misitu kwenye ardhi huria ambayo hutegemewa na mikoa ya
Pwani na Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya nishati za magogo, mbao, samani
na matumizi mengine.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment