Na Wellu Mtaki, Dodoma
MSEMAJI Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amefungua Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) na akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.
Msigwa amesisitiza hilo leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya MISA.
Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani hakuna chombo kilichofungiwa na vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa.
Aidha amesema katika kipindi hiki mafunzo au semina kwa waandishi zinahitajika hivyo kuiomba Misa Tanzania na wadau wengine kuwapatia mafunzo mbalimbali waandishi wa habari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Salome Kitomari amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwatumikia Watanzania, lakini zaidi kwa namna amechukua hatua kadhaa zilizowezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuondoa vikwazo vingi.
Kitomari amesema MISA Tanzania imepita kwenye safari ya miaka 30 yenye milima na mabonde na kutokana na mambo yote hayo ameupongeza uongozi, sekretarieti na wanachama wa MISA Tanzania kwa kushikamana mpaka kufikia hatua hiyo.
Sanjari na hayo ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kutoa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa waandishi wa habari, Kuwezesha uanzishwaji wa vyombo vingine vya habari zikiwamo Radio za Kijamii na kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali tangu Sheria ya Magazeti, Sheria ya Huduma za Habari, Sheria ya Haki ya Taarifa na nyinginezo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Elizabeth Riziki amesema Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya kikao cha wanahabari waliokutana Windhoek, Namibia kujadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaukabili Ukanda wa Nchi za Kusini.
MISA ina matawi tisa katika nchi za Zambia, Msumbiji, Malawi, Lesotho, Botswana, Namibia, Angola, Tanzania na Zimbabwe ambako ndiyo makao makuu ya matawi yote.
Amefafanua kuwa katika mkutano huo wa siku mbili wadau watajadiliana kuhusu kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na namna ambavyo umma unahusishwa kwenye uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa lakini pia watajadili changamoto zilizopo kwenye sekta ya habari na kuweka mkakati wa kuzitatua ikiwamo namna ya kuboresha maisha ya waandishi wa habari.
Pia amesema Majadiliano hayo yana lengo la kuongeza ukaribu na ushirikiano baina ya waandishi wa habari na Jamii, pia kuibua hoja zitakazowaleta pamoja Jamii na waandishi wa habari katika kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ili kuhakikisha kila mwanajamii anatumia vizuri nafasi ya uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari kwaajili ya maendeleo endelevu.
Ikumbukwe kuwa Misa Tanzania inaadhimisha miaka 30 huku kauli mbiu ikiwa ni "Uhuru wa Kujieleza Msingi wa Haki Zote kwa Maendeleo Endelevu.