Na John Gagarini, Chalinze
HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo imeshauriwa kuisitisha
mikata ya umiliki wa ardhi iliyochukuliwa na wawawkezaji ambao hawajaiendeleza
ardhi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 wairejeshe kwenye serikali za
vijiji kwa ajili ya matumizi ya umma.
Hayo yalisemwa na mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kwa tiketi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete wakati wa mikutano ya hadhara ya
kampeni kwenye Vijiji vya Makombe na Kinzagu kwenye kata ya Lugoba na kusema
kuwa wamiliki hao kama wameshindwa kuiendeleza ardhi hiyo ni vema wakairudisha
kwa wananchi.
Ridhiwani alisema kuwa inashangaza kuona kuwa wananchi kwenye
vijiji hivyo wamekuwa wakihangaika kutafuta ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na
matumizi mengine lakini wanakosa maeneo ambayo yamehodhiwa na watu wachache.
“Kwa sasa ni vema halmashauri zikasitisha mikata ya umiliki
wa ardhi hiyo kutokana na kushindwa kuiendeleza kwa kipindi cha miaka zaidi yha
10 ambapo sheria inataka mwekezaji kuiendeleza ardhi ndani ya kipindi cha miezi
32 na endapo atashindwa kuiendeleza anaweza kufutiwa umiliki,” alisema
Ridhiwani.
Alisema kuwa haipendezi kuona wananchi wanahangaika kutafuta
maeneo huku baadhi ya watu wakiwa wamehodhi maeneo bila ya kuyaendeleza na
kuacha yakiwa mapori ambayo yanahatarisha usalama wao.
“Ni vema maeneo hayo yakarejeshwa kwenye serikali za vijiji
ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo kwani itakuwa ni sehemu ya
kutoa ajira kwa wananchi hususani vijana,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ya Lugoba ambaye amepita
bila ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa ni kweli maeneo hayo yalichukuliwa
na wawekezaji muda mrefu lakini hayajaendelezwa.
Mwene alisema wananchi wa maeneo hayo hususani vijana hawana
ajira lakini endapo ardhi hiyo itarejeshwa itasadia kujiajiri kupitia kilimo
ambacho ni ajira ya uhakika lakini wanashindwa kujiajiri kupitia kilimo
kutokana na kukosa maeneo kwa ajili ya kulima.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Kijiji cha Makombe wameomba uwekwe utaratibu wa
malori yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo ya kokoto yapimwe uzito ili
yabebe uzito kutokana na uwezo wa barabara.
Sambamba na hilo wameomba kuwe na utaratibu wa magari hayo kutoa
fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibika vibaya kutokana
na kupitishwa malori hayo ambayo yana uzito mkubwa.
Ombi hilo lilitolewa na Rehema John alipozungumza na
waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
John alisema kuwa barabara hizo zimeharibika vibaya kutokana
na magari ya kubebea kokoto ambayo ni mazito na hakuna utaratibu wa kuyapima
uzito hali inayosababisha barabara kuharibika.
“Tunaiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa malori hayo
yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo na kusababisha uharibifu wa barabara
inayoelekea kwenye machimbo hayo na kutoka huko kwenda barabara kubwa ya lami,”
alisema John.
Alisema kuwa kwa sasa barabara hizo zinazoelekea kwenye
machimbo hayo ya kokoto zimeharibika vbaya kutokana na uzito kuwa mkubwa hivyo
kushindwa kuhimili uzito.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Lugoba ambaye amepita bila
ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa atahakikisha maombi hayo anayapeleka
sehemu husika ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani uharibifu ni mkubwa sana.
Mwene alisema kuwa barabara zinazoelekea kwenye machimbo hayo
zote ni mbaya kutokana na kutofanyiwa ukarabati ambapo licha ya halmashauri
kuzifanyia matengenezo lakini zinaharibika haraka kutokana na uzito mkubwa wa
malori hayo.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chalinze
Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kuna haja ya wanaotumia barabara hizo hasa wale
wenye magari yanayobeba kukoto pamoja na wawekezaji kwenye machimbo hayo
kufanya ukarabati wa barabara hizo.
Ridhiwani alisema kuwa wawekezaji wanapaswa kuboresha huduma
mbalimbali ndani ya kijiji ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wao na
hivyo ni vema wakazikarabati barabara hizo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wakiwemo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wilayani Bagamoyo hususani wanawake
wametakiwa wasikubali kurubuniwa na baadhi ya watu na kuuza shahada zao kwa
matapeli kwa madai ya kuipunguzia kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka
huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM
Ridhiwani Kikwete kwenye kijiji cha Lunga kata ya Lugoba wilayani humo katibu
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mwatabu Husein alisema kuwa wapinzani wao
wameanza kununua kadi za wapiga kura ili kukipunguzia kura.
Hussein alisema kuwa kuna watu wanapita na kuwarubuni wananchi
na wanachama wa CCM ili wawauzie kadi za mpiga kura ili kupunguza idadi ya
wapiga kura kwani endapo mtu atakuwa hana kadi ya mpiga kura hatakuwa na haki
ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo.
“Nawashauri wananchi na wana CCM kuwa makini na watu hao
kwani wamekuwa wakitumia njia hiyo ya kuzinunua kadi hizo ili kutuathiri kupata
ushindi wa kishindo hivyo mnapaswa kuwa macho hasa wakinamama msikubali
kuyumbishwa,” alisema Hussein.
Alisema kuwa tayari wamewashika pabaya wapinzani wao ambao
sasa wamenza kuweweseka na kufanya vitendo vinavyoashiria kushindwa na kuanza
kutapatapa.
“Wapinzani wetu hawatuwezi wamenza kununua kadi za wapiga
kura ili kutupunguzia ushindi wa kishindo lakini tayari wameshachelewa tutawashinda
kwa kishindo kikubwa na mwisho wao utakuwa Oktoba 25 mwaka huu,”a lisema
Hussein.
Aidha alisema kuwa wapinzani hali yao imekuwa mbaya kwani
hawana uwezo wa kuishinda CCM ambayo imejipanga vizuri kwa mikakati yake ya
ushindi na washindani wao tayari wameshakubali kushindwa sasa wanatafuta sababu
ya kushindwa hata kabla uchaguzi haujafanyika.
Mwisho.