Na
John Gagarini, Kibaha
MGOMBEA
Ubunge anayewania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Jimbo la Kibaha
Mjini Abdulaziz Jad Maarufu kama Mwarabu amesema kuwa wana CCM wasichague mbunge
ambaye ni sawa na mfadhili kwani atakwamisha shughuli za maendeleo katika Jimbo
hilo.
Jad
aliyasema hayo juzi mjini Kibaha kwenye mkutano wa wagombea wa ubunge wa CCM
kuomba kura kwenye kata ya Maili Moja na kusema kuwa baadhi ya wabunge ni sawa
na wafadhili ambao hutoa misaada kwa msimu.
Alisema
kuwa wabunge wa namna hiyo hujitokeza wakati wa vipindi vya uchaguzi lakini wakishachaguliwa
na uchaguzi ukipita hawaonekani tena kwani maendeleo yake yatakuwa ya msimu na
si endelevu.
“Sisi
wakazi wa Jimbo la Kibaha tunahitaji Mbunge wa kutuletea maendeleo na si
mfadhili ambaye anatoa misaada kwa msimu hasa ule wa uchaguzi na mkishamchagua
hamuoni tena hadi baada ya miaka mitano,” alisema Jad.
Aidha
alisema kuwa wabunge wa namna hiyo wanaleta maendeleo ya msimu lakini endapo
watamchagua yeye atawaletea maendeleo endelevu na si ya msimu kama wanavyofanya
baadhi ya wafadhili.
“Baadhi
yao ni wafadhili lakini wanavaa kofia ya uongozi hawa hawatufai lakini
mkinichagua mimi nitawaletea maendeleo enedelevu na si yale ya msimu ambayo
yametudumaza,” alisema Jad.
Alibainisha
kuwa endapo ilani ya chama itatekelezwa kwa ufanisi basi maendeleo yatapatikana
kwani inajibu changamoto zilizopo kwenye sekta zote za maendeleo pia aliahidi
kuondoa makundi yaliyojitokeza katika kipindi hichi cha uchaguzi.
Mwisho.
Na
John Gagarini, Bagamoyo
SERIKALI
imeombwa kuajiri watu wenye taaluma ya sheria kwenye mabaraza ya ardhi ili
kupunguza migogoro ya ardhi iliyopo kwenye maeneo mengi ya miji na vijiji.
Hayo
yalisemwa Bagamoyo na Raya Fereji makamu mwenyekiti wa asasi isiyo ya
kiserikali ya Mkombozi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa mafunzo ya
sheria ya ardhi kwa waandishi wa habari na wadau wa ardhi wilayani humo.
Fereji
alisema kuwa mabaraza ya ardhi yanaendeshwa na watu wasiokuwa na taaluma ya
sheria wakati masuala yenyewe ni ya kisheria hali ambayo inasababisha migogoro
ishindwe kwisha.
“Mabaraza
haya yanaundwa na watu maarufu kwenye maeneo yao lakini hawana taaluma ya
kisheria licha ya kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi unakwenda kisheria,”
alisema Fereji.
Alisema
kuwa ili migogoro hiyo ipungue hakuna budi kuwatumia watu wenye taaluma ya
sheria ili kukabiliana na migogoro hiyo am,bayo imekithiri.
“Hata
kama itashindwa kuwatumia watu wenye taaluma hiyo basi iyapatie mafunzo ya
sheria mabaraza hayo kwani uzoefu unaonyesha kuwa maamuzi mengi yanayotolewa ya
utatuzi wa migogoro ya ardhi inakuwa na kasoro nyingi,” alisema Fereji.
Kwa
upande wake mwanasheria wa Kujitegemea Boka Lyamuya alisema kuwa migogoro mingi
ya ardhi inashindwa kutatuliwa kutokana na baadhi ya watendaji kwenye maeneo hayo kupindisha sheria.
Mwisho.
Na
John Gagarini, Kibaha
WAGOMBEA
wa nafasi za Ubunge na Udiwani mkoani Pwani wametakiwa kuweka ajenda ya
kuhifadhi misitu kama sehemu ya kampeni zao za kuomba nafasi za uongozi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa Mradi wa Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG)
Yahaya Mtonda alisema kuwa misitu hiyo endapo itaundiwa sera nzuri itasaidia
kurejesha uoto wa asili ambao umetoweka kutokana na uharibifu wa mazingira.
Mtonda
alisema kuwa misitu hiyo imekuwa ni chanzo kikuu cha upatikanaji wa mvua pamoja
na hali ya hewa nzuri pia kukabiliana na mmomonyoko wa ardhi hivyo wawania
nafasi za uongozi lazima watoe kipaumbele cha jinsi gani ya kukabiliana na hali
hiyo ya uharibifu wa mazingira.
“Mabadiliko
ya tabianchi yanatokana na uharibifu wa
misitu hivyo wawania nafasi za uongozi lazima wabebe suala hilo kama ajenda
muhimu wanaponadi sera zao ili kuokoa misitu ya asili na ile isiyo ya asili,”
alisema Mtonda.
Aidha
alisema kuwa moja ya misitu ya asili hasa ile iliyojirani na Jiji la Dar es
Salaam ambayo ni Kazimzumbwi na msitu wa Pugu iliyopo wilayani Kisarawe ni
muhimu kwani ndiyo inayochuja hali ya hewa na kuifanya iwe nzuri.
“Kama
mnavyofahamu Jiji la Dar es Salaam lina zalisha hewa mbaya kutokana na magari,
viwanda na shughuli mbalimbali za kimaendeleo hivyo misitu hii ni kama mapafu
ya kupumulia hivyo kutufanya tupate hewa nzuri lakini endapo isingekuwepo basi
athari za kiafya zingekuwa kubwa sana,” alisema Mtonda.
Aliwataka
wananchi kuwauliza wagombea kuwa wameweka mikakati gani ya kuhifadhi misitu na
utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na uvunaji holela wa misitu kwenye mkoa
huo.
Mwisho.
Na John
Gagarini, Kibaha
WAKAZI
wa Kijiji cha Minazimikinda kata ya Ruvu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha
mkoani Pwani wamemwomba Waziri wa Ardhi na Makazi Wliam Lukuvi kutembelea
Kijiji chao ili kukabiliana na mgogoro wa muda mrefu baina yao na Kijiji cha
Kwala.
Moja
ya wakazi wa Kijiji hicho Mohamed Palu alisema kuwa mgogoro huo ni wa muda
mrefu na umekuwa ukiwachukulia muda mrefu kuutatua bila ya mafanikio hivyo
kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.
Palu
alisema kuwa mgogoro huo umesababisha shughuli za kimaendeleo katika eneo hilo
kukwama kutokana na kila upande kudai eneo hilo ni la upande mwingine.
“Tumetumia
njia nyingi za kusuluhisha mgogoro huu lakini hadi sasa hakuna hatua zozote
zilizofikiwa kuumaliza mgogoro huo hivyo tunaona endapo waziri atakuja anaweza
kuutatua,” alisema Palu.
Alisema
kuwa kamati ya Bunge inayoshughulikia migogoro ya ardhi ilifika Kijijini hapo
mwezi Machi mwaka huu lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote juu ya suluhu ya
mgogoro huo.
“Mgogoro
huu na mingine iliyopo Kijijini ni moja ya changamoto kubwa zinazotukabili
hivyo endapo waziri atakuja atatusaidia kuitatua na hivyo itasaidia wananchi
kuendelea na shughuli za maendeleo,” alisema Palu.
Aidha
alisema kuwa baadhi ya viongozi wa Vijiji wamekuwa wakichangia migogoro hiyo
kutokana na kutozingatia ramani za vijiji hivyo hali inayosababisha kuwa na
migogoro hiyo.
Baadhi ya wanachama wa CCM kata ya Maili Moja wakiwasikiliza watia nia wa CCM walipokuwa wakimwaga sera jana mjini Maili Moja |