Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amesema kuwa sheria za
Ushirika zimepitwa na wakati hali ambayo
inasababisha baadhi ya watu kutumia mwanya kuwadhulumu wakulima wa zao hilo
hapa nchini.
Kutokana na fedha nyingi kutumiwa kwa matumizi binafsi na
baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kumesababisha chama kikuu cha ushirika
cha mkoa CORECU kuwa na madeni makubwa ambapo mabenki yamekataa kukikopesha
fedha kwa ajili ya ununuzi wa zao la korosho.
Aliyasema hayo wilayani Mkuranga wakati wa mkutano wa mfuko
wa wakfu wa kuendeleza zao la korosho (CIDTF) kwa wakulima na wataalamu wa mkoa wa Pwani na bodi ya zao
la korosho nchini juu ya msimu mpya wa uuuzaji na ununuzi wa zao hilo.
Mahiza alisema kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika
vya zao la korosho mkoani humo wamewadhulumu wakulima malipo ya korosho walizo
wauzia wanunuzi hali iliyosababisha hasara kubwa kwa mkoa.
“Mfano mkoa wa Pwani ulikidhamini chama kikukuu cha ushirika
cha mkoa (CORECU) kupata mikopo toka kwenye mabenki ambapo CRDB ilitoa bilioni
6 na NMB ilitoa biloni 3 lakini fedha hizo zimeshindwa kurejeshwa hali
ilioyosababisha chama hicho kishindwe kukopeshwa tena,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa kila wanapojaribu kuwachukulia hatua viongozi
hao inashindikana kutokana na sheria zilizopo za ushirika ambazo zinaonekana
zinawalinda viongozi hao hivyo kushindwa kuadhibiwa huku wakulima wakiendelea
kudai fedha zao.
“Ukiwashitaki kwa makosa ya jinai ushirika unasema huwezi
kuwashitaki kwa kosa la jinai lakini baada ya kufuata taratibu za kisheria
tayari tunaweza kuchukua hatua ambazo ni stahiki kwa viongozi hao ambao baadhi
yao wamezitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kuwa sheria hizo si nzuri kwani zinawaumiza
wakulima lakini kwa sasa mkoa umefikia hatua nzuri za kuweza kuwashtaki
waliohusika na kula fedha za wakulima kwani ushirika sio kudhulumu watu bali ni
kuboresha maslahi ya wakulima.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la
korosho Athuman Nkinde alisema kuwa maandalizi ya msimu wa kilimo kwa zao hilo
tayari zimeanza na mkoa wa Pwani utapatiwa pembejeo za dawa za kupulizia pamoja
na miche bora ya zao hilo ipatayo 70,000.
Nkinde alisema kuwa matarajio ni mkoa huo kuzalisha zao hilo
kwa wingi ili kuboresha kipato cha wakulima kwani zao hilo ni utajiri endapo
wakulima na wataalamu watawaelekeza kilimo bora cha zao hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Sadifa Juma
ameomba suala la umri wa kugombea Uspika na Urais liangaliwe ili kuwapa nafasi
vijana kuweza kugombea nafasi hizo kwa kupunguza umri wa sasa wa miaka 40 na
kuwa 30.
Aliyasema hayo wakati wa akiwahutubia vijana wa umoja huo
kutoka Jimbo la Kibaha Mjini, alipokuwa akifunga kambi ya mafunzo ya vijana ya
siku 10 ambayo yalifunguliwa na katibu mkuu wa Abdulrahman Kinana Septemba 19.
Sadifa alisema kuwa kwenye Ubunge unaruhusu umri wa kuanzia
miaka 21 lakini kwenye nafasi hizo umri ni kuanzia miaka 40 jambo ambalo ameona
kuwa vijana hawatendewi haki.
“Kama ubunge ni miaka 21 na Uspika pamoja na Urais angalau
iwe kuanzia miaka 30 na kuendelea kwani kwa umri huo bado kijana ana nguvu na
anaweza kutekeleza vema majukumu yake tofuati na kumchagua Rais mwenye umri
mkubwa,” alisema Sadifa.
Alisema kuwa mambo yanabadilika ifike wakati sasa vijana nao
wapate nafasi kutokana na uwezo wake kwani vijana ndiyo wenye nguvu na
wanauwezo mkubwa wa kutekeleza majuku yao ikiwa ni pamoja na kuongoza.
“Nchi kama Kongo na Korea Marais wao ni vijana lakini
wanaongoza vizuri hivyo hakuna sababu ya kuwawekea mazingira magumu ya kugombea
nafasi hizo za juu wapewe nafasi kama watafanikiwa kuchaguliwa basi wachaguliwe
kwani kiongozi siyo umri bali ni uwezo wa kuongoza,” alisema Sadifa.
Kw upande wake kamanda wa Vijana wa Kibaha Mjini Silvestry
Koka alitoa sare 50 kwa makamanda wa umoja huo Green (Guard) zenye thamani ya
shilingi milioni 2.5 na kuwataka vijana hao kuyatumia mafunzo hayo kukiimarisha
chama.
Awali akisoma risala
ya kambi hiyo ya vijana katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kibaha Mjini Khalid King
alisema kuwa kambi hiyo iliwafundisha vijana 101 juu ya masuala mbalimbali
yakiwemo ya itikadi za chama, ujasiriamali, uongozi na masuala mbalimbali ya
kisiasa.
Mwisho.