Monday, January 27, 2014

WAANDISHI WAPIGWA MSASA JUU YA PETS



Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ili nchi iweze kuendelea watendaji na mamalaka zikiwemo halmashauri hapa nchini zimetakiwa kuwa na uwazi na uwajibikaji ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkuu wa shule kuu ya uandishi wa habari ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt Herbert Makoye  wakati akifungua mafunzo ya ufuatiliaji wa rasilimali za Umma (PETS) kwa waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya Business Times na Mlimani.
Dkt Makoye alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa wananchi juu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma zinazotolewa na serikali hivyo kusababisha huduma muhimu za kijamii.
“Tumeona tufanya mafunzo haya kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuweza kuandika taarifa juu ya matumizi ya fedha hizo ambazo madhumuni yake ni kuwapunguzia kero wananchi hivyo watapata taarisa sahihi,” alisema Dkt Makoye.
Alisema bila ya uwazi kutakuwa hakuna uwajibikaji hali ambayo itasababisha kutokuwa na maendeleo ya haraka ya mwananchi kujikwamu na hali ngumu ya kimaisha.
“Kupitia mafunzo haya waandishi wanapaswa kuyatumia kwa lengo la kuwapatia wananchi taarifa sahihi juu ya michakato mbalimbali ya matumizi ya fedha hizo na zitasaidia watendaji kuwajibika kwani watakuwa na hofu ya kufuja fedha kwani kuna vyombo vinavyowafuatilia,” alisema Dkt Makoye.
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa gazeti la Majira Bw Imma Mbuguni alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi katika ufuatiliaji wa rasilimali za umma zikiwemo fedha zinazotolewa na serikali kwa maendeleo ya wananchi.
Bw Mbuguni alisema pia mafunzo hayo yatasaidia kuibua mijadala mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya fedha za Umma ambapo baadhi ya watendaji wanaonekana kutozitumia kwa malengo yaliyowekwa au mahitaji ya wananchi.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa pamoja na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na kampuni ya Business Times kutokana na ufadhili wa Mfuko wa Ufadhili wa Vyombo vya Habari (TMF).
Mwisho.

No comments:

Post a Comment