Thursday, January 23, 2014

MWINJILISTI AU AJINYONGA

Na John Gagarini, Kibaha
MWINJILISTI wa Kanisa Anglikana Eliakia Daniel (35) amekufa kwa kujinyonga baada ya kumuua mkewe Bi Mboni Patrick (28) kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani Pwani kamishna Msaidizi Mwandamizi Ulrich Matei alisema kuwa marehemu walikuwa ni wakulima wa Kijiji cha Gama - Makaani wilayani Bagamoyo.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20 mwaka huu majira ya saa 10 jioni kijijini hapo ambako walikuwa wakifanya shughuli ya kuchoma mkaa.
“Mwinjilisti huyo alimwua mkewe baada ya kutokea wivu wa kimapenzi ndipo alipochukua panga na kumkata kichwani upande wa kulia na kumsababishia majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake,” alisema Kamanda Matei.
Alisema baada ya kumwua mkewe alimfunika kwa magogo sehemu waliyokuwa wakifanyia shughuli zao hizo za kuchoma mkaa kwa ajili ya biashara.
“Baada ya kumwua mkewe alijinyonga umbali wa mita 300 kutoka eneo la tukio,” alisema Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kutokana na wivu wa kimapenzi na kupelekea tukio hilo kutokea ambalo limewasikitisha wananchi wa kijiji hicho.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment