Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Kuweka na Kukopa cha KIWAO SACCOS cha wilayani
Kibaha mkoani Pwani kimewapa muda wa miezi mitatu kulipa madeni ya mikopo yao baadhi
ya wanachama wake wenye madeni sugu na endapo watashindwa kurejesha ndani ya
muda huo watawachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani.
Akiongea na wanachama kwenye mkutano mkuu uliofanyika Shirika
la Elimu Kibaha, mwenyekiti wa chama hicho Bi. Magdalena Kabukire alisema kuwa
wanachama hao wapatao tisa wana madeni ya mikopo ya muda mrefu.
Bi. Kabukire alisema kuwa tayari wamewaandikia barua
wanachama hao kuwakumbushia madeni yao ili waweze kurejesha kufanikisha
wanachama wengine waweze kukopa.
“Chama chetu kinakabiliwa na changamoto hiyo ya baadhi yao
kuchelewesha kurejesha mikopo hali inayosababisha wengine washindwe kukopa
kutokana na fedha nyingi kuwa mikononi mwa watu,” alisema Bi Kabukire.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mwanalugali kilipo chama hicho
Deodatus Rwekaza alisema kuwa watashirikiana na chama hicho kuhakikisha
wanarejesha mikopo hiyo.
“Wakiona wanachama hao wanashindwa kulipa kwa kipindi hicho
walete majina kwenye ofisi yangu ili waangalie sheria iweze kuchukua mkoando
wake, kwani mabenki na asasi za kifedha zimefanya hivyo na wadeni wamelipa,”
alisema Bw Rwekaza.
Kwa upande wake ofisa ushirika wa Halmashauri ya Mji wa
Kibaha Bw Kulwa Masambu alisema kuwa ili vyama hivyo viweze kupiga hatua lazima
wanachama warejeshe mikopo kwa wakati.
Bw Masambu alisema kuwa vyama hivyo vimekuwa mkombozi kwa
wananchi hususani wanawake ambao ndiyo wenye changamoto kubwa ya kuziletea
maendeleo familia zao na jamii inayowazunguka.
Kwa mwaka jana chama hicho kiliweza kukopesha wanachama wake
19 kiasi cha shilingi milioni 16.4 na kupata mapato ya shilingi milioni 1.9
hisa zikiwa shilingi 638,000 akiba zikiwa ni m 4.2 na kina jumla ya wanachama
76.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment