John Gagarini, Bagamoyo
KITONGOJI cha Biga kata ya Mkange wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambacho kilikumbwa na mafuriko hivi karibuni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini kimeomba serikali kuwapatia mbegu za mahindi tani 2.5 kwa ajili ya kupanda tena zao hilo.
Ombi hilo limekuja baada ya hekari 510 za wakazi wa kitongoji hicho kusombwa na maji ya mvua ambazo zilinyesha kabla ya mvua kubwa za mafuriko kunyesha hivi karibuni ambapo kilizungukwa na maji na kuwafanya wakazi wengine kupewa hifadhi ya muda.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi diwani wa kata hiyo ya Mkange Abdala Mwendadi alisema kuwa mazao ya wakazi hao yote yalisombwa na maji hali ambayo itasababisha kitongoji hicho kuwa hatarini kukumbwa na njaa.
"Kutokana na hali hiyo wakazi wa kitongoji hicho wanaomba serikali iwapatie mbegu kwa ajili ya kupanda mahindi mara mvua hizi zitakapokwisha ambapo msimu huo mahindi yake huitwa "Mahindi ya Kitopeni" ambayo hupandwa baada ya mvua kwisha mwezi Mei kiloa mwaka," alisema Mwindadi.
Mwindadi alisema kuwa jumla ya kaya 63 zimeathiriwa na mvua hizo ambapo zaidi ya watu 200 wameathirika hivyo kuwafanya kuhama kwenye maeneo hayo na kwenda kwa ndugu jamaa kwa ajili ya hifadhi.
"Wakazi wengi waliokumbwa na mafuriko hayo ni wale waliokuwa wakiishi kwenye mkondo wa maji ambapo kutokana na mvua hizo kumechangia kukumbwa na mafuriko hayo ambayo yamesomba mazao yote yaliyopandwa msimu wa kilimo," alisema Mwindadi.
Aidha diwani huyo wa kata ya Mkange alisema kuwa kutokana na maombi hayo atayapeleka halmashauri ili hatua za kuwasaidia zianze kwani endapo hawatapata msaada huo hali ya chakula kwenye kitongoji hicho itakuwa mbaya.
mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
MWENYEKITI wa Kijiji cha Kinzagu William Makumu ameshangzwa na wawekezaji kwenye kijiji hicho kushindwa kuchangia maendeleo hasa kwenye sekta ya barabara kutokana na kuingiza magari makubwa kwa ajili ya kubeba kokoto.
Alisema kuwa kuna wawekezaji wengi ambao wamewekeza kwenye uchimbaji kokoto ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na barabara hasa Jijini Dar es Salaam.
Makumu alisema kuwa uwekezaji mkubwa kijijini hapo ni uchimbaji wa kokoto kutokana na kijiji hicho kuzungukwa na milima ya mawe.
"Wamekuwa wakiingiza mamilioni ya fedha kwa ajili ya uchimbaji wa kokoto ambapo magari makubwa ambayo yanafikia hadi uzito wa tani 30 hutumia barabara za kijiji lakini hawazikarabati licha ya wao kufanya uharibifu mkubwa," alisema Mukamu.
Alisema kuwa kabla ya kupewa maeneo kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao huomba kupitia mkutano wa Kijiji ambapo hutakiwa kutoa asilimia fulani kutokana na mapato yao pia hutakiwa kutoa nguvu zao kwa ajili ya kufanya kazi za maendeleo.
"Tatizo wao wamekuwa wakiangalia upande wao mfano ni eneo la barabara ambazo zimeharibika sana kutokana na wao kuingiza magari yao ya kubebea kokoto lakini hawako tayari kuzitengeneza licha ya kuwa wao ndiyo watumiaji wakubwa kwa ajili ya kupitisha kokoto kwenda maeneo mengine," alisema Mukamu.
Alibainisha kuwa uchangiaji wa wawekezaji hao ni mdogo sana ikilinganishwa na mapato wanayoyapata na athari wanazoziacha baada ya kupasua mawe kwenye kijiji hicho.
Aliwataka wawekezaji hao kujitahidi kuheshimu mikataba waliyoingia ya kuisadia jamii inayowazunguka ambayo ndiyo iliyowapa ardhi wanayoitumia kwa uwekezaji wao.
mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
HUKU Tarafa ya Chalinze ikiwa kwenye maombi ya kupatiwa wilaya kata ya Bwiringu wilayani Bagamoyo inaendelea na mchakato wa kuhakikisha kuwa inapata nafasi ya kuwa makao makuu ya wilaya hiyo yanakuwa hapo.
Moja ya mambo waliyofanya ni pamoja na kugawa viwanja zaidi ya 11,000 kwa ajili ya makazi na huduma za kijamii kwa wakazi wa kata hiyo iliyopo katikati ya mji huo wa Chalinze.
Hivi karibuni kupitia baraza la Madiwani lilipitisha mpango wa tarafa hiyo kuwa wilaya ambapo suala hilo bado liko kwenye mchakato kwa kupeleka maombi hayo kwenye ngazi husika.
Akizungumza mjini Chalinze diwani wa kata hiyo Nasa Karama alisema kuwa wao wako tayari kufanya hivyo na kuwa makao makuu ya wilaya mpya mara maombi hayo yakapopitishwa na wizara husika.
Karama alisema kuwa moja ya mambo waliyoyafanya kuhakikisha wanapata nafasi hiyo ya kuwa makao makuu ya wilaya ni pamoja na kugawa viwanja hivyo.
"Tumegawa viwanja hivyo kwa kushirikiana na halmashauri ili kuupanga mji wetu uwe kwenye mandhari nzuri na kuepukana na ujenzi holela usiozingatia ramani za mipangomiji," alisema Karama.
Alisema kuwa viwanja hivyo vimetolewa kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kwenye vijiji vya Mbala, Kibiki na Koo lengo kubwa ikiwa ni kuondokana na ujenzi holela.
"Baadhi ya wadau waliopewa viwanja hivyo tayari wameanza ujenzi huku wengine wakiendelea na michakato ya kuendeleza maeneo yao baadhi yao ni NSSF, wanaotaka kujenga soko la kisasa wakiwa kwenye hatua ya tathmini, ujenzi wa nyumba za watumishi, tume ya utumishi wa umma, ofisi ya Mbunge, TAKUKURU, benki na kituo cha polisi," alisema Nasa.
Aidha alisema kuwa wametoa fidia ya shilingi milioni 98 kwa wananchi kutokana na kuchukua maeneo yao kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya maendeleo.
mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
HOSPITALI Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi imesisitiza kuwa haiuzi damu kama baadhi ya watu wanavyodai kwani hilo ni kosa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hospitali hiyo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Pwani juu ya hali tete na migogoro iliyoandaliwa na Baraza la habari Tanzania (MCT), mkuu wa kitengo cha maabara Boaz Motto alisema kuwa sera ya afya hairuhusu uuzaji wa damu.
Motto alisema kuwa utaratibu unaonyesha kuwa mgonjwa akipewa damu anapaswa kurejesha ili wagonjwa wengine nao waweze kupata damu wanapokuwa wanahitaji.
"Tatizo huwa linakuwa ni kwa wanafamilia ambapo wanapoambiwa wachangie damu baadhi yao huwa wanashindwa hali ambayo inasababisha kutafuta watu na kuwaomba damu lakini kwa makubaliano ya kuwalipa fedha," alisema Motto.
Alisema kuwa mapatano ya kuuziana damu hayafanyiki hospitalini bali ni makubaliano ya watoa damu na wenye mgonjwa lakini hospitali hutoa damu bure bila ya malipo lakini sharti ni kwamba wenye mgonjwa nao watoe damu ili itumike kwa wengine.
"Hii dhana ya damu kuuzwa imeenea sana lakini sera ya afya hairuhusu hospitali kuuza damu kwa mgonjwa bali ni kwa wanandugu kumtolea damu ambapo watu huwanunua watoa damu na wakifika hospitali hudai kuwa ni ndugu," alisema Motto.
Alisema kuwa kwa sasa hospitali ina damu ya kutosha na haina upungufu ambapo kuna uniti 150 ambazo watu hujitolea kama vile taasisi za jeshi, watu binafsi, wanafunzi na makundi mbalimbali ndani ya jamii.
"Changamoto tuliyonayo ni vipimo vya damu ambapo hutubidi kupeleka kwenye hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kupimwa kujua ubora wake ili iweze kutumika kwa wagonjwa wanaohitaji damu," alisema Motto.
Aidha alisema kuwa magonjwa yanayoongoza ni pamoja na yale ya msimu wa mvua kama vile kichocho, malaria na minyoo ambapo mazalia yake ni kwenye maji huku wakati wa kiangazi magonjwa ni yale ya kifua kikuu, kukohoa na malaria.
mwisho.
No comments:
Post a Comment