Wednesday, April 30, 2014

SIMBA YANGA ZAPEWA SOMO

Na John Gagarini, Kibaha
TIMU za soka za Simba na Yanga zimetakiwa kujipanga ili ziweze kupata mafanikio kama ilivyo klabu ya Azam ambayo imepongezwa na Shirikisho la Soka la Miguu la Dunia (FIFA) kwa kuweza kuwa klabu ambayo imepata mafanikio kwa kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.
Wito huo umetolewa na mdau wa soka wilayani Kibaha mkoani Pwani, Fahim Lardhi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi na kusema kuwa Azam imeweza kuzipiku Simba na Yanga kwa mafanikio licha ya timu hizo kuanzishwa miaka zaidi ya 50 iliyopita.
Lardhi alisema kuwa Azam imeanzishwa miaka 9 iliyopita lakini imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na uwanja wa kisasa ambao una kidhi haja ya kuwa uwanja ambao unaweza kutumia na timu kubwa kama ilivyo kwa timu za Ulaya.
“Timu za Simba na Yanga zimebaki kuwa timu za malumbano tu badala ya kufikiria masuala ya kimaendeleo kama ilivyo kwa timu ya Azam ambayo ni timu changa katika ramani ya soka hapa nchini na hata barani Afrika,” alisema Lardhi.
Aidha alisema kuwa ili kuleta mafanikio kwenye timu lazima timu hizo zibadili mifumo ya wanachama ili wazichangie timu zao badala ya wao kutaka timu hizo ziwanufaishe hali ambayo inasababisha zishindwe kupata mafanikio.
“Inashangaza kuona timu hizo zinakosa viwanja jambo ambalo linatia aibu ambapo zimebaki kusema tu kuwa zitajenga viwanja matokeo yake yamebaki maneno tu ya kujenga viwanja vyao vya kisasa,” alisema Lardhi.
Alivitaka vilabu hivyo kuwa na mifumo kama ya ulaya ili viweze kupata maendeleo na kuachana na mifumo ambayo haina tija zaidi ya kuleta malumbano na kuzitaka zijifunze kupitia timu ya Azam ambayo inaendeshwa kitaalamu.
Na John Gagarini, Kibaha
MASHINDANO ya kutafuta timu ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kwa Umoja wa Shule za Sekondari na Sanaa Tanzania (UMISSETA) yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 3 mwaka huu.
Timu hiyo ambayo itaundwa na wachezaji 125 wa michezo mbalimbali inatarajiwa kuchuana kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha Tumbi ambapo kwa sasa timu hizo zinacheza ngazi ya Kanda ili kupata timu moja ya wilaya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha mratibu wa mashindano hayo Rajab Kauta alisema kuwa kwa sasa mashindano hayo ya kanda ndogo yanaendelea kwenye vituo vinne ambavyo ni Kibaha Sekondari, Kongowe, Tanita na Kilangalanga.
“Mashindano haya ya kanda ndogo yanshirikisha jumla ya 43 kutoka halmashauri ya Mji wa Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambapo kila kituo kina wachezaji 125 na baada ya hapo watakutana kupata timu moja ya wilaya,” alisema Kauta
Kauta alisema kuwa michezo hiyo inachezwa kila Jumamosi ili kutoathiri masomo na mara bada ya kumalizika mashindano ya kanda ndogo ndipo wataunda timu moja ili kupata timu ya wilaya hiyo.
“Mashindano ya mkoa yatafanyika Bagamoyo kuanzia Mei 27 na tunaamini tutapata timu nzuri licha ya changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na shule nyingi kutokuwa na viwanja vya michezo, viwanja vingi kujaa maji kutokana na mvua kubwa kunyesha, upungufu wa vifaa vya michezo ,” alisema Kauta.
Aliwaomba wadau kushirikiana na shule ili kusaidia kuboresha viwanja kwenye mashule pmaoja na upatikanaji wa vifaa ili kuweza kupata vijana wenye uwezo.
Mwisho.    

No comments:

Post a Comment