Saturday, August 19, 2023
JUKWAA LA WAZALENDO HURU TANZANIA KUUNGA MKONO ROYAL TOUR
Friday, August 18, 2023
SERIKALI YATOA BILIONI 12 UJENZI VITUO VIDOGO KUSAMBAZA BIDHAA ZA PETROLI NA DIZELI VIJIJINI
Serikali imetoa billion 12 kwa ajili ya mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za Petroli na Diseli vijijini Tanzania bara kwa lengo la kulinda Mazingira na Afya ya watumiaji na kuboresha upatikanaji na Usambazaji wa Mafuta vijijini.
Mkurugenzi Mkuu Wa Wakala wa Nishati Vijiini REA Mhandisi Hassan Said amesema hayo leo Jijini Dodoma katika Mkutano na waandishi wa habari akisema usambazaji wa mradi huo unahusu kuwekeza ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo mbalimbali Vijiini.
Said amesema kuwa moja ya changamoto inayosababisha wananchi wasitumie nishati safi na kuendelea kutumia nishati ya asili yaani mkaa na kuni ni pamoja na upatikanaji wake kwani nishati asilia zimekua zikipatikana kwa urahisi.
Aidha amesema Wakala umeanza kutekeleza Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000 (laki mbili) katika maeneo ya vijijini huku kwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya fedha takribani bilioni 10 zimetengwa kwaajili ya kufanikisha mradi huo.
Pia ametoa rai kwa Watanzania kutumia mafundi wanaotambulika na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kuondoa lawama zinazotolewa na wananchi dhidi ya Serikali zinazosababishwa vishoka wanaofanya uunganishaji wa umeme kinyume cha sheria.
Serikali imetoa jumla ya shilingi trillioni 1.7 kwa Wakala wa Nishati Vijiini (REA) kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.
Kadhalika Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) imetenga Dola za Kimarekani milioni 6 kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia.
DKT KIJAJI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUJENGA MIUNDOMBINU YA UWEKEZAJI
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujenga miundombinu wezeshi kwa wawekezaji na wageni kwani baada ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko la wageni kutoka sehemu mbalimbali Duniani.
Kijaji ameyasema hayo leo Agosti 17, 2023 wakati wa Kikao kazi na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa ambapo kikao hicho kimewahusisha wajasiriamali na wafanyabiashara pamoja na majukwaa yanayojihusisha na ujasiriamali.
Waziri Kijaji amesema uchumi imara wa Taifa upo mikononi wa sekta binafsi hivyo amewahimiza wafanyabiashara hao kutumia fursa zote zinazojitokeza iwe ni sekta binafsi au kutoka serikalini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Kijaji amewahimiza wajasiriamali kuwa waaminifu na Fedha zinazotolewa na Serikali kama sehemu ya mtaji ili kuwawezesha na wengine kupata hiyo fursa.
"Lazima tukubaliane na utaratibu uliowekwa uadilifu wetu, uaminifu wetu ni muhimu hakuna fedha za bure sehemu yeyote lazima uwe na uhakika wa fedha kurudi na mtu unae mpatia fedha hivyo tunatakiwa kumthibitishia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo mtetezi wetu namba moja "ameeleza Kijaji
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitoa salamu za Mkoa amempongeza Waziri huyo kwa kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kutatua changamoto na kero zilizokuwa kikwazo katika utekelezaji wa biashara zao.
Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea wawekezaji na kuongeza idadi ya viwanda ili kuongeza na kukuza mapato ya Serikali na uchumi wa nchi ya Tanzania.
Thursday, August 17, 2023
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TFS
Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema rasilimali za misitu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini Dodoma.
Mhe. Mnzava amewapongeza wahifadhi kwa kujitolea kufanya kazi kwa bidii.
"Tuwatie moyo hawa wapiganaji wetu kwani wameendelea kutekeleza majukumu yao vyema na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, waendelee kuitumikia nchi kwa kuwa wanajitolea na sisi kama Bunge tunawaunga mkono" Mhe. Mnzava amesisitiza.
Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kufanyia kazi mapendekezo ya wajumbe wa Kamati hiyo na kuangalia namna bora ya kuzuia ukataji wa miti kwa kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wanaishi kwa kutegemea miti hiyo .
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa mapendekezo na kuahidi Serikali itafanyia kazi.
Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kuacha kukata miti hovyo pamoja na kuacha matumizi ya nishati chafu na badala yake kutumia nishati safi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Wednesday, August 16, 2023
WAGONJWA ZAIDI YA 500 WA MTOTO WA JICHO MBARALI KUFANYIWA UPASUAJI BILA MALIPO
Na. Majid Abdulkarim, Mbarali
Wagonjwa zaidi ya 500 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanatarajiwa kupatiwa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kutoka kwa madaktari bingwa wa macho ambao wameweka kambi ya wiki moja katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.
Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Kanali Dennis Mwila wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho itakayodumu kwa muda wa siku saba Wilayani hapo.
Kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu, ambapo wakazi wa Wilaya hiyo wanaendelea kupata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Kanali Mwila amesema kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia Moja ya watu wanapata matatizo ya macho.
Aidha, Kanali Mwila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Helen Killer kwa kuanza kampeni ya kutokomeza magonjwa ya macho Juni 2022 ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya Sh: Mil. 140 kwa Mkoa wa Mbeya na walitoa mafunzo kwa watumishi wa Afya ngazi ya jamii wapatao 570.
“Juni, 2022 Shirika la Helen Killer liliweza kugundua wagonjwa 1,750 ambao walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho kwa awamu tatu tofauti”, ameeleza Kanali Mwila.
Amesema, katika kambi hiyo inayoendelea jumla ya watu 500 wanatarajiwa kupatiwa huduma ambapo zaidi ya kiasi cha Sh: Mil. 110 kitatumika katika kuwapatia huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho.
Amesema, kwa mwaka jana (2022) wagonjwa 29,000 waliyo onwa katika Mkoa Mbeya, wagonjwa 3,406 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho na magonjwa mengine.
Vile vile, Kanali Mwila ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa imara katika kuwasogezea huduma za Afya karibu.
Naye, Meneja Mpango wa Taifa wa Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Bernadetha Shilio amesema kuwa mbinu inayotumika kuwapata wagonjwa ni kupitia wahudumu ngazi ya jamii ambao wanaambatana na wataalamu wa Afya nyumba kwa nyumba na kuwabaini wagonjwa.
Dkt. Shilio amesisitiza kuwa Huduma za upasuaji katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali zinatolewa bila malipo chini ya ufadhili wa Shilika la Kimataifa la Helen Killer.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mratibu wa Macho kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ernest Paul amesema Serikali itahakikisha inawezesha upatikanaji wa huduma za macho karibu na wananchi hususani ngazi ya msingi.
BODI YA MKONGE NCHINI IMESAMBAZA MICHE MILIONI 6.9 BURE KWA WAKULIMA WADOGO
Mageuzi hayo yamefanya Tanzania kuwa Nchi ya pili Duniani kwa kuzalisha mkonge ikitanguliwa na Brazili.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona wakati akizugumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa bodi hiyo na mwelekeo katika mwaka huu wa fedha 2023/24.
Kambona ametaja Wilaya zilizopatiwa mbegu hizo ni Korogwe, Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Manyoni, Singida Vijijini na Mkalama.
Amesema Rais Dk.Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata mkonge ya mashamba ya Kibaranga Wilayani Muheza, Tanga na shamba la serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani Wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.
Aidha,Kambona amesema Serikali iliongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026.
WATAKIWA KUTUNZA MISITU KWA VIZAZI VIJAVYO
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS ) imesema kuwa uhifadhi wa rasilimali za Misitu ni manufaa ya kizazi cha Sasa na vizazi vya baadae hivyo jamii inapaswa kujiepusha kuchoma moto Misitu pamoja na uvunaji haramu.
Hayo yamesemwa Leo Agosti 16,2023 na Kamishna wa uhifadhi wakala wa huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Silayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hifadhi hiyo ndani ya Miaka ya miwili ya serikali ya awamu ya sita .
Amesema kuwa sekta ya Misitu na nyiki nchini ni muhimu kutokana na mchango wake Katika ukuaji wa sekta ya Utalii, Maji , kilimo, mifugo, nishati pamoja na viwanda hivyo kutokana na umuhimu huo Wadau wote wanapaswa kulinda rasilimali za Misitu.
Aidha amesema kuwa wakala umeendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi za Misitu na jamii inayoizunguka ambapo jumla ya hekta 296,881 za maeneo zimetolewa kwa wananchi kwa ajili ya makazi , kilimo na ufugaji.
Pia wakala unaendea kutoa Elimu ya uhifadhi na usimamizi wa Misitu kwa jamii sambamba na kuimarisha mipaka kwa kuisafisha , kuweka vigingi na mabango Ili kuzuia uvamizi Katika maeneo ya hifadhi.