Thursday, May 5, 2016
johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI
johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI: John Gagarini, Kibaha JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Frowin Peter Mbwale (26) mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma z...
WATAKA VYUO VYA KATI KUUNGANISHWA NA BODI YA MIKOPO
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI na Bodi ya Mikopo Nchini (TCU) imeshauriwa kuviingiza kwenye mpango wa mikopo wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Kati kama ilivyo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu wakati mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu wa (CCM).
Sharifu alisema kuwa wanafunzi hao ni sawa na wale wa vyuo vikuu na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu na wanahitaji mikopo ili waweze kupata elimu ya juu.
“Hali ya sasa ni ngumu na wazazi ni wale wale wanahitaji kupunguziwa mzigo wa kulipa ada ambazo ni kubwa hivyo tunaona kuwa kuna haja ya serikali kuviingiza na vyuo vya kati kwenye mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa kwa kuwa nchi imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora hadi kufikia elimu ya juu ambayo ndiyo inaweza kumsaidia mtoto.
“Kwa sasa elimu ya juu ndiyo inayotakiwa tofauti na elimu ya kawaida ambayo si ya juu ambayo kwa sasa haina nafasi ya muhitimu kupata ajira hivyo kulazimisha watu wapate elimu ya juu,” alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa shirikisho hilo ni mboni ya chama na linafanya kazi kubwa ya kukijenga chama kwani hapo ni tanuru la kuandaa viongozi wa baadaye wa kukiongoza chama pamoja na nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Maulid Bundala ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa Mkoa Mwinshehe Mlao alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alisema kuwa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM linafanya kazi kubwa ya kukitetea chama.
Bundala alisema kuwa CCM imeleta ukombozi ndani ya nchi na ni chama kikongwe hivyo kwa wanavyuo waliojiunga na shirikisho hilo wako sehemu salama kwani mawazo yao yataleta manufaa kwa nchi.
Aidha alisema kuwa nchi kwa sasa ina hitaji kuongozwa na wasomi hivyo wasomi hawa wataleta mabadiliko na chama kiko tayari kubadilika na wao wananafasi ya kumshauri Rais na wao ndiyo watakaoliinua taifa.
Naye naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Siraji Madebe alisema kuwa shirikisho lao linakabilia na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wancahama wake wale wa vyuo vya kati kutotambuliwa na Bodi ya Mikopo hivyo kutopata mikopo.
Madebe alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali lakini watahakikisha wanaendeleza umoja wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa shirikisho hilo ambayo ni kuwaunganisha wasomi walio vyuo kuwa na umoja wao ili kukipigania chama.
Mwisho.
TANESCO KUWAUNGANISHIA UMEME WANA VIJIJI MRADI WA BILIONI 30
Na John Gagarini, Kisarawe
SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) unatarajia kusambaza umeme kwa wananchi 11,000 wenye thamani ya shilingi bilioni 30 kwenye vijiji 109 vya mkoa huo .
Kwa mujibu wa Mhandisi mkuu wa Mradi huo wa REA mkoa wa Pwani Leo Mwakatobe alisema mradi huo wa awamu ya pili utakamilika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.
Mwakatobe alisema kuwa lengo kubwa kwa sasa ni kutekeleza agizo lililotolewa na serikali la kuhakikisha miradi hiyo ya umemem vijijini inawafiki wananchi wengi na kwa wakati uliopangwa.
“Tumeshaanza katika kutekeleza miradi hiyo katika maeneo ya Chalinze, Kisarawe na tutaendelea katika sehemu mbali mbali za Mkoa wetu wa Pwani na tunatarajia kufikia vijiji vipatavyo 109 vilivyopo katika Mkoa wetu,” alisema Madulu.
Alisema kuwa kuwa mbali ya kuendelea kukutekeleza miradi hiyo hata hivyo wanakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa wakati wanapotaka kupitisha miundomibu katika makazi ya watu.
“Baadhi ya watu wamekuwa hawataki kuridhia umeme kupita kwenye maeneo yao au kutaka fidia kubwa hali ambayo inasababisha kuwa na changamoto za hapa na pale lakini hata hivyo tunajitahidi kuwaelewe umuhimu wa miradi hiyo na kupata nishati hiyo ya umeme,” alisema Mwakatobe.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani Martin Madulu alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza agizo lililotolewa na serikali kuhakikisha wanawafikia wateja wao wote hususani wale wa vijijini kwa lengo kuweza kuwaunganishia umeme kwa bei nafuu.
Madulu alisema kuwa watahakikisha wanafanya jitihada ili kuwafikia wateja wao ili waweze kuwa na nishati ya umeme katika maeneo mbai mbali hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Wakati huo huo wakazi zaidi wa 100 katika kijiji cha Nyeburu Wilayani Kisarawe waliokuwa na tatizo la upatikanaji wa nishati ya umeme na kuishi katika giza kwa kipindi cha muda mrefu kwa sasa wamenufaika baada ya kuunganishiwa umeme kutokana na kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu wa pili.
Baadhi ya wakazi hao walisema kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuleta chachu kubwa ya kimaendeleo katika kijiji hicho kwani mwanzoni walikuwa wanashindwa tutimiza malengo yao waliyojiwekea kutokana na kutokuwa na nishati hiyo ya umeme.
Mwisho.
ADAMJEE KUIONGOZA TCCIA PWANI
Na John Gagarini, Kibaha
CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoa wa Pwani imemchagua Zainuddin Adamjee kuwa mwenyekiti wake ambaye ataongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Uchaguzi huo ulifanyika Mjini Kibaha mwishoni mwa wiki ambapo Adamjee ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kawe alichaguliwa bila ya kupingwa kutokana na kutokuwa na mpinzani ambapo uchaguzi huo uliitishwa baada ya uongozi uliopita kumaliza muda wake.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni Ana Maridadi ambaye ni makamu mwenyekiti biashara, Karim Mtambo makamu mwenyekiti Kilimo na Mohamed Kiaratu mwakilishi wa mkutano mkuu Taifa.
Wengine waliochaguliwa ni Frank Mzoo mweka Hazina na Attiki Mohamed ambaye ni mjumbe wa kamati ambapo wagombea hao wote hawakuwa na wapinzani.
Akizungumza na wanachama na viongozi waliochaguliwa Rais wa TCCIA Taifa Injinia Peter Kisawilo alisema kuwa viongozi waliochaguliwa wanapaswa kuhakikisha wanawawekea mazingira mazuri wanachama ili waweze kuingia kwenye soko la ushindani la kimataifa.
Kisawilo alisema kuwa nchi ya Tanzania imeingia kwenye mikataba ya masoko makubwa yakiwemo yale ya Comesa, Sadc na la Afrika Mashariki ambapo wafanyabiashara wanapaswa kutengeneza bidhaa zitakazoingia kwenye ushindani na si kuwa watazamaji.
Kwa upande wake Adamjee alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha mkoa wa Pwani unakuwa moja ya mikoa ambayo inainua uchumi wake kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwa na viwanda ili nchi iwe na uchumi wa kati.
Adamjee alisema kuwa kwa kuwa mkoa huo una uzalishaji mkubwa wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji viwandani na rasilimali za uvuvi hivyo una nafasi kubwa ya kuinua kipato cha wananchi wa mkoa.
Awali mwakilishi wa mgeni rasmi Anatoly Mhango ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kibaha alisema kuwa chemba hiyo ina nafasi kubwa ya kuwainua wanachama wake kupitia masoko ya ndani na nje.
Mhango alisema kuwa njia mojawapo wanayopaswa kuitumia ni kujitangaza ili watu waweze kujua fursa zinazopatikana kupitia chemba hiyo pia kupitia Chama Cha Kuweka na Kukopa SACCOS kilichopo ndani yake wanachama wanapaswa kurejesha mikopo kwa wakati ili watu wengi waweze kukopa.
Mwisho.
MADIWANI WATAKA BODI YA TENDA IVUNJWE
Na John Gagarini, Kibaha
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameridhia kuvunjwa kwa Bodi ya Tenda kwa kushindwa kutekeleza vizuri majukumu yake hivyo kusababisha miradi mingi kukwama.
Wakizungumza kwenye kikao cha Madiwani kilichofanyika mjini Kibaha madiwani hao walisema kuwa kutokana na bodi hiyo kutokuwa makini imesababisha wakandarasi wengi kuidai Halmashauri huku miradi mingi ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Akizungumza kwenye kikao hicho Diwani wa Kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa wazabuni wengi wameingia kwenye mgogoro na Halmashauri kwani wengi wameshindwa kufikia vigezo vya kazi wanazopewa huku mawakala wakishindwa kupeleka fedha za makusanyo kwa wakati.
Chanyika alisema kuwa bodi hiyo imeshindwa kuchagua wazabuni ambao wana uwezo wa kufanya kazi na inafanya kazi kwa mazoea pia ni ya muda mrefu hivyo inapaswa kubadilishwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwa wazabuni kwa lengo la kuleta maendeleo.
“Baadhi ya miradi mingi imekwama kwani wazabuni wengine wameshindwa kukamilisha kazi zao wengine wamekuwa wakiachia kazi bila ya kukamilika na kuondoka matokeo yake ni kuitia hasara Halmashauri na kudumaza maendeleo ya Mji wetu,” alisema Chanyika.
Kwa upande wake Kambi Legeza alisema kuwa miradi mingi iko chini ya kiwango kutokana na kutokuwa na wakandarasi wasiokuwa na uwezo pia mapato ya Halmashauri yameshuka hivyo kuna haja ya kuibadili ili kupata bodi nyingine itakayokuja na mawazo mapya.
Legeza alisema kuwa bodi hiyo ya tenda ndiyo yenye uwezo wa kuwapitisha wazabuni mbalimbali ambao wanapaswa kuwa na uwezo lengo likiwa ni kuleta maendeleo kwa halmashauri ambayo yanaleta manufaa kwa wananchi ambao ndiyo wanaolengwa.
Akijibu hoja hizo kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Leah Lwanji alisema kuwa ofisi yake imelipokea suala hilo na italifanyia kazi kama mapendekezo ya madiwani yalivyotolewa.
Lwanji alisema kuwa kuna taratibu za kisheria za kuvunja bodi hivyo lazima zifuatwe na endapo itabidi kufanya hivyo itafanyika ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa kwa lengo la kuboresha.
Mwisho.
MKUU WA MKOA AWATAKA WAKURUGENZI WATAKIWA KULIPA ZAWADI HEWA
Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametoa muda wa siku tatu hadi Mei 3 kwa wakurugenzi wa Halmashauri tatu za mkoa huo kuwapa zawadi za fedha watumishi bora kwa mwaka huu baada ya Halmashauri hizo kutoa zawadi hewa kwenye Sherehe za siku kuu ya wafanyakazi May Mosi .
Sambamba na wakurugenzi hao wa Halmashauri pia ofisi ya Katibu Tawala mkoa (RAS) pamoja na mkurugenzi wa Shirika la Elimu nao wametakiwa kuwalipa wafanyakazi ambao walifanya vizuri kwenye vitengo vyao ambapo walipewa vyeti tu bila ya fedha kama taratibu zinavyokuwa za kuwapa fedha taslimu au hundi.
Ndikilo alitoa agizo hilo wilayani Mkuranga kwenye sherehe hizo ambazo kimkoa zilifanyika wilayani humo na kusema kuwa hayo ni masihara na yeye hayuko tayari kufanyiwa mzaha katika suala ambalo liliandaliwa kwa muda mrefu na kuwakopa zawadi hizo za fedha kwani nyingine toka mwaka jana hazijalipwa .
“Katika risala ya Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri kama motisha lakini kwa hali hili siwezi kukubaliana nalo nawapa siku tatu muwe mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini kwangu akutane na adhabu niliyoiandaa,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo mazito na kwamba atachukua hatua kali kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kutoa zawadi hizo kwani zingene zimetoa kwanini wengine washindwe.
“Mimi siyo mtani wenu wala si saizi yenu haiwezekani mniite nije kutoa zawadi hewa ndo maana hatoa zikichukuliwa za kinidhamu mnasema mnaonewa ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika huu ni mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa ameshangazwa na kitendo hicho cha wao kumfanya atoe zawadi hewa kwani hiyo ni dharau Ras Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji na Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha.
“Hatutaniani hapa huu ni mzaha uliopitiliza kiwango ujumbe umefika namna hii mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni jambo ambalo halijanifurahisha na nisingependa hali hii isijitokeze tena,” alisema Ndikilo.
Awali akisoma risala ya TUCTA Amini Msambwa alisema kuwa wafanyakazi wana haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima zipatikane kwa shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje waajiri.
Msambwa alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa nje na wandani kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao sehemu za kazi ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za wafanyakazi.
Aidha wameomba Halmashauri kuruhusu kuwa na mabaraza ya wafanyakazi na ambako yako yakutane kwenye vikao vyao vya kisheria lakini yanafanyika kwa ajili ya kupitisha bajeti za halmashauri.
Mwisho.
UGAWAJI VIWANJA WAINGIA MTAFARUKU MADIWANI WATAKA KUJUA UNDANI WA ZOEZI HILO
Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la ugawaji wa viwanja kwenye eneo la Mitamba limeingia dosari baada ya Madiwani wa Halamshauri ya Mji Kibaha kutaka ufafanuzi juu ya utaratibu wa kugawa viwanja vilivyopo kwenye eneo hilo kabla ya kuvigawa kwa wananchi ambao walilivamia.
Madiwani hao walitaka ufafanuzi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Mjini Kibaha na kusema kuwa kabla ya zoezi hilo wataalamu wanapaswa kuwajulisha utaratibu wa jinsi watakavyovigawa viwanja hivyo.
Eneo hilo lilikuwa chini ya Wizara ya Mifugo Kilimo na Umwagiliaji lakini lilivamiwa na wananchi hali ambayo ilibidi Halmashauri igawane na wananchi nusu kwa nusu ambapo kuna jumla ya viwanja 6,500 kwenye hekari 747.
Diwani wa kata ya Sofu Yusufu Mbonde alisema kuwa mradi huo ambao una thamani ya shilingi bilioni 2.7 ulitakiwa uanze kutekelezwa mwezi huu hauko wazi hasa katika suala zima la jinsi fedha zitakavyotumika katika kuutekeleza kwake.
Mbonde alisema kuwa kwa kuwa serikali imeamua kulipima eneo hilo na kugawana na wavamizi hao wapatao 350 ni vema kukawa na uwazi kwa lengo la kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
“Tunachokitaka ni kupewa ufahamu juu ya zoezi hili kabla halijaanza kutekelezwa ili tuweze kujua kitakachofanyika pale kwani mradi huo ni mkubwa na utakuwa na faida kubwa kwa wananchi pamoja na Halmashauri hivyo ni vema kukawa na uwazi,” alisema Mbonde.
Kwa upande wake diwani wa Viti Maalumu Tuaje Ponza alisema kuwa moja ya vitu ambavyo vinashangaza ni kukodisha greda kwa ajili ya kazi hiyo huku Halmashauri nayo ikiwa na greda lake kwanini lisitumike hilo.
“Katika kupunguza gharama ni vema tukatumia greda letu kwani hatuwezi kukodisha wakati tuna la kwetu tulinunua kwa ajili ya kufanyia kazi zetu hivyo ni vema tukatumia la kwetu,” alisema Ponza.
Akijibu hoja mbalimbali mkuu wa Idara ya Mipangomiji Lucy Kimoi alisema kuwa viwanja hivyo vitatolewa kwa vipindi vinne tofauti ambapo awamu ya kwanza itakuwa viwanja 500 awamu ya pili viwanja 1,500 ya tatu 2,000 na ya tatu viwanja 2,500.
Kimoi alisema kuwa kutokana na ukosefu wa fedha zoezi hilo la ugawaji wa viwanja hivyo utafanywa na Halmashauri pamoja na wazabuni ambapo vitapimwa kwa shilingi 334,500 huku wazabuni wakivipima kwa shilingi 150,000 kwa kiwanja kimoja.
“Ni kweli tuna greda letu lakini kutoakana na zoezi hilo kuwa la muda mrefu ndiyo sababu tunahitaji mawili kwa ajili ya kufanikisha ugawaji huo kwani moja itabidi lisitoke eneo la kazi huku lingine likifanya kazi za nje kwani kazi zitakuwa ni nyingi sana ikiwa ni pamoja na sehemu ya huduma za jamii, makazi na huduma nyingine muhimu,” alisema Kimoi.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Leah Lwanji alisema kuwa ombi la madiwani kuwapa uelewa juu ya mradi huo limekubaliwa na watakaa nao kabla ya kuanza ugawaji huo.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)