Friday, November 29, 2024

DK ALICE AWASHUKURU WANANCHI KWA KUWAPATIA USHINDI CCM UCHAGUZI SERIKALI

MBUNGE wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dr Alice Kaijage amewashukuru wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kuwachagua wenyeviti wote na wajumbe wa Serikali za Mitaa wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)


Dk Kaijage ameyasema hayo wakati wa uapisho wa wenyeviti Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Amesema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo.

"Nawapongeza viongozi wetu wa Serikali za Mitaa kwa ushindi mlioupata nendeni mkafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zenu mnapozifanya mnapaswa kumtanguliza Mungu,"amesema Dk Kaijage.

Monday, November 18, 2024

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VINAVYOSIMAMIA ULINZI NA AMANI KUSINI MWA AFRIKA (SADC) ZIANDAE MITAALA KUZINGATIA MATISHIO YANAYOZIKABILI NCHI WANACHAMA

Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu Meja Jenerali Iddi Said Nkambi amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali na Kiraia zinazohusika na Ulinzi wa Amani chini ya Mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) kuhakikisha zinandaa mitaala ya kuendeshea mafunzo ya Ulinzi wa Amani kwa kuzingatia matishio yanayozikabili nchi wanachama.

Meja Jenerali Nkambi ameyasema hayo leo tarehe 18 Novemba 2024 wakati wa ufunguzi wa Semina fupi ya siku 5 inayohusu  uwasilishaji wa mitaala mipya ya mafunzo itakayotumika kuandaa  Majeshi ya SADC, semina inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (PTC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam.

Semina hiyo inayoendeshwa na Chuo cha Ulinzi wa Amani cha Kikanda chenye Makao Makuu yake nchini Zimbabwe inahudhuriwa na washiriki kutoka nchi wanachama wa SADC ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kukabiliana na matishio pindi wanapokuwa katika majukumu ya Ulinzi wa Amani ndani ya ukanda wa SADC na sehemu zingine watakapopewa jukumu.

Tuesday, November 5, 2024

TAKUKURU PWANI KUTOA ELIMU KUPAMBANA NA RUSHWA



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani itaendelea kutoa elimu ya kupambana na rushwa kwa makundi mbalimbali wakati huu wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Aidha makundi hayo ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, wapiga kura, wagombea, wasimamizi, azaki, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoani humo Christopher Myava alisema walishatoa elimu juu ya kupambana na vitendo vya rushwa tangu mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama vya siasa.

Myava alisema kuwa makundi hayo ni muhimu kipindi hichi cha uchaguzi lengo likiwa ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa hawatokani na rushwa.

"Tunataka wananchi wachague viongozi bora ambao wataendana na dira ya serikali ya maendeleo kwani serikali inatumia gharama kubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo viongozi watakaochaguliwa wawe na sifa na uwezo wa kuongoza,"alisema Myava.

Alisema kuwa wanatoa elimu kwa makundi hayo ili kama yataona kuna viashiria vya rushwa waweze kutoa taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani viongozi bora hawatokani na kutoa rushwa bali ni kwa uwezo wao wa kuongoza.

"Tutaendelea kutoa elimu hadi itakapofikia hatua ya kutangaza matokeo ili tuhakikishe wanapatikana viongozi wenye sifa, waadilifu ili wasimamie rasilimali na fedha zinazotolewa ili wananchi wapate maendeleo,"alisema Myava.

Aliongeza kuwa kiongozi atakayechaguliwa apambane na rushwa kwani serikali inatumia gharama kubwa hivyo tutatoa elimu kupitia mikutano na semina.

"Wananchi nao ni sehemu ya mapambano ambapo viashiria vya rushwa ni kama vile kupewa simu, ajira, fedha, ahadi mbalimbali au vitu vya thamani katika hatua za mwanzo tulipata taarifa za vitendo vya rushwa lakini hakuna ushahidi ambao unaweza kutumika kwani ili kufungua shauri lazima kusiwe na shaka,"alisema Myava.

Aliwataka viongozi wanaowania nafasi za uongozi wazingatie sheria, masharti, kanuni na utaratibu wa uchaguzi ili wasije kujikuta wanaingia kwenye changamoto kwa kukiuka miongozo iliyowekwa.

Friday, November 1, 2024

WAHITIMU MAFUNZO JESHI LA AKIBA WAOMBA AJIRA HALMASHAURI

WAHITIMU wa mafunzo Jeshi la akiba Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani wameomba kufikiriwa katika kupata ajira kwenye Halmashauri walipo badala ya kufanya kazi katika makampuni binafsi ambayo huwalipa mishahara ambayo haiendani na mali wanazolinda.
Aidha wamesema kuwa wanaiomba serikali kukabili changamoto ambazo zingetatuliwa basi vijana wengi wangeshiriki na kumaliza mafunzo hayo kwani baadhi wanashindwa kununua sare kutokana na hali ya kiuchumi.

Walitoa maombi hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga amnaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla fupi ya kufunga mafunzo ya Jeshi la akiba iliyofanyika kwenye uwanja wa Mwanakalenge.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mshauri wa mgambo wa wilaya ya Bagamoyo Luteni Kanali Rahimu Tumbi alisema kuna baadhi ya changamoto wanazopata wahitimu wa mafunzo hayo kipindi wanapokuwa kwenye mafunzo hayo.

Mkuu wa wilaya ambae ndio mgeni rasmi Shaibu Ndemanga ametumia fursa hiyo kuwaasa vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la akiba wakaishi kiapo walicho kiapa kwa kuwa waadilifu na wasiyatumie mafunzo vibaya wanapokuwa kwenye jamii.


Tuesday, October 29, 2024

VIJANA NCHINI KUPEWA ELIMU SERA YA VIJANA

ILI kuwapa ufahamu juu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka (2007) toleo la mwaka 2024 Kamati ya Vijana Wazalendo itafanya makongamano kwenye mikoa 10 hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa Kamati ya Vijana Wazalendo Omary Punzi amesema kuwa Makongamano hayo yatakutanisha makundi ya vijana ambayo yatapatiwa elimu juu ya sera hiyo.

Punzi amesema kuwa sera hiyo ya vijana ni nzuri lakini vijana wengi hawaifahamu hali ambayo inawafanya vijana wengi kutotambua haki zao za msingi na makongamano hayo yatawafikia vijana zaidi ya milioni nane na tisa.

Mwenyekiti wa Kamati ya vijana Wazalendo Farida Kongoi amesema kuundwa kwa sera ya taifa ya maendeleo ya vijana lengo lilikuwa ni vijana wapate mwongozo wa kuendana na masuala ya siasa na kijamii ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa kiteknolojia.

Mwanasheria wa Kamati ya vijana Wazalendo Godfrey Kizito amesema pia vijana watafafanuliwa kuhusu Sheria zinazohusu haki na masuala ya vijana.

Naye Mkurugenzi wa Great leaders organization na Mratibu na Mwandaaji wa kongamano la Wazazi na Walezi nchini Dubai Dk Debora Nyamlundwa amesema katika kongamano hilo kuna kujifinza fursa mbalimbali zilizopo katika taifa hilo kuja kuendeleza hapa nchini



Sunday, October 27, 2024

NISHIBISHE PROJECT YAKUSANYA UNGA KILO 1,115 WANAFUNZI KUNUFAIKA CHAKULA SHULENU

MPANGO wa Nishibishe umefanikisha kupatikana kwa unga wa mahindi kiasi cha kilogramu 1,115 kwa ajili ya kuwapatia lishe wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwenye Kata ya Kwala Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Viti Maalum ambaye pia ndiye mwasisi wa mpango huo Josephine Gunda wakati wakukabidhi unga huo kwa viongozi wa Kata ili wasambaze kwenye shule husika.

Gunda alisema unga huo umetolewa na wadau mbalimbali kupitia mradio huo ambapo utasambazwa kwenye Shule ya Sekondari moja na Shule za Msingi tatu.

"Malengo ya kutoa chakula shuleni ni ili kupunguza utoro kwa baadhi ya wanafunzi kwani wanakumbana na changamoto ya chakula na kusababisha kutohudhuria masomo kutokana na hali ya kiuchumi,"alisema Gunda.

Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakila mmlo mmoja ambapo mtoto anaenda shule bila ya kula chochote hadi jioni anaporudi kutoka shule hali ambayo inawafanya washindwe kuhudhuria masomo na kuwa watoro.

"Shuleni kukiwa na chakula hata kama nyumbani kuna changamoto mtoto atakula shuleni na atavutiwa kwenda shule na mafanikio tumeyaona kwani utoro ymepungua na ufaulu umeongezeka kwani mwanafunzi akila na akili inakuwa na uwezo mzuri,"alisema Gunda.

Aliongeza kuwa ifike wakati suala la chakula shuleni iwe ajenda ya kudumu na Halmashauri itenge sehemu ya fedha ya mapato ya ndani kwa ajili ya kununua chakula kwani hilo ni tatizo kubwa kwa watoto mashuleni.

Diwani wa Kata ya Kwala Mansuri Kisebengo alisema kuwa mbali ya changamoto lakini wazazi bado wana nafasi ya kuhakikisha lishe ya watoto wao inapatikana.

Kisebengo alisema kuwa anawapongeza wadau hao ambao wamejitolea unga huo kwani watawapunguzia wazazi gharama za chakula kwa watoto wao ambao ni wanafunzi.

Kwa upande wake mratibu huduma za lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Coletha Chapile alisema kuwa lishe ni kitu muhimu sana kwa wanafunzi kwani endapo mtoto hatapata chakula uwezo wake wa kuelewa utapungua.

Chapile alisema kuwa suala la lishe kwa wanafunzi ni muhimu na ni jambo ambalo wazazi, walezi na wadau kulipa kipaumbe kwa kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa shuleni ili kuongeza uelewa.



Thursday, October 17, 2024

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAKUSANYA MAPATO ASILIMIA 33 ROBO YA KWANZA


HALMASHAURI ya Mji Kibaha imefanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia 33 ya malengo ya ukusanyaji kwenye robo ya kwanza ya makadirio ya makusanyo ya Halmashauri ya shilingi bilioni 8.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Halmashauri Dk Rogers Shemwelekwa  wakati wa kikao cha baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya Julai-Septemba 2024.

Shemwelekwa alisema kuwa kipindi kama hichi mwaka jana walikuwa wamekusanya kwa asilimia 25 hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 8 ya makadirio ya shilingi bilioni 7.

"Tunawashukuru madiwani na wataalamu wa Halmashauri kwa kufikia makusanyo hayo ambayo ni mwanzo mzuri na tunategemea kufikia asilimia 100 tunaomba ushirikiano huu uendelee ili kufikia malengo tuliyoweka,"alisema Shemwelekwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema huo ni mwanzo mzuri wa makusanyo hayo ni mazuri na ushirikiano huo uendelee ili kufikia malengo yaliyowekwa.

John alisema kuwa kwa upande wa uyoaji mikopo asilimia 10 ya Halmashauri dirisha limeshafunguliwa pia zoezi uchongaji barabara kwenye mitaa unaendelea ambapo Halmashauri imetoa milioni 10 kwa kila kata kwa ajili hiyo.