Wednesday, September 11, 2024

NYAMA YAPANDA BEI KIBAHA

KUFUATIA bei ya nyama kupanda kutoka shilingi 7,000 hadi 9,000 Kibaha Mkoani Pwani imesababisha wananchi kulalamika na kuiomba serikali kuwasaidia ili bei irudi kama ilivyokuwa awali.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baadhi ya wananchi walisema kuwa kupanda kwa bei hiyo inasababisha washindwe kununua nyama.

Happy Ngilangwa alisema kuwa kama kuna namna ya kufanya ni vema serikali ikakaa na wafanyabiashara wa nyama ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa wanannchi.

"Tunaomba serikali ikae nao chini ili waangalie kama kuna baadhi ya mambo wayaweke sawa sababu sisi tunashangaa tu kuona bei imepanda ghafla,"alisema Ngilangwa.

Alisema kuwa nyama ni kitoweo muhimu ambacho ndicho chakula kikuu kwa wananchi wengi ukilinganisha na mboga zingine ambapo hata samaki nazo bei iko juu.

"Kwa sasa maisha yamekuwa magumu hivyo kupandisha bei ni kuwaongezea mzigo wananchi kutokana na bei kupanda baadhi ya watu wameshindwa kumudu bei,"alisema Ngilangwa.

Kwa upande wake mama lishe Neema Maneno alisema kupanda kwa bei ya nyama kumewaathiri ambapo kwa sasa imebidi wapunguze ukubwa wa vipande vya nyama.

Maneno alisema wana wateja wengi ambao wanakula chakula pamoja na kunywa supu wanalamika lakini hawana jinsi ya kufanya inabidibwaendane na hali halisi.

Naye moja ya wauzaji nyama Albert Koka alisema kuwa yeye kashindwa kufanya biashara na amefunga bucha kwani yeye hununua mabuchani na kuongeza kidogo ili apate chochote.

Koka alisema kuwa wao nao wanaumia kwani nao wanategemea kununua kwa wenye mabucha makubwa na kuuza kwa wananchi mitaani ili nao wapate riziki.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Wauzaji Nyama Kibaha Aidan Mchiwa alisema kuwa nyama imepanda bei kwa sababu ya nyama nyingi inauzwa nje.

Mchiwa alisema kuwa soko la nyama nje limekuwa kubwa sana ambapo ngombe nyingi zinanunuliwa na makampuni ambayo yanasafirisha kwenda nje ya nchi kwenye soko la Uarabuni.

Saturday, September 7, 2024


VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kutoa nafasi watu wenye mahitaji maalum kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwani nao wana haki ya kushiriki.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Umoja wa Amani Kwanza Mkoani Pwani Halima Yusuph wakati wa mkutano kwa vyama vya siasa na jamii ambapo katiba inaonyesha kuwa binadamu wote ni sawa.

Yusuph alisema kuwa vyama vya siasa kutoa nafasi kwa kundi maalum la watu wenye ulemavu ili wapate nafasi kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024 mwaka huu bila ya kuwatenga kwani wana haki ya kushiriki uchaguzi.

"Kwa mujibu wa Katiba binadamu wote ni sawa hivyo kuna kila sababu ya watu wenye ulemavu kupata nafasi za kushiriki uchaguzi kwa kuchagua na kuchaguliwa na tunakemea ramli chonganishi ambazo husababisha wenye ulemavu wa ngozi kuuwawa,"alisema Yusuph.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Africa Talent Forum (ATF) MaryRose Bujash aliomba watu wenye ulemavu wasitengwe wala kunyanyapaliwa.

Bujash alisema kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa jamii isiwatenge na pia na wao wanahitaji elimu zaidi ya masuala ya uchaguzi na uongozi ili kuweza kushiriki uchaguzi.

Naye Katibu wa siasa na uenezi Mkoani Pwani David Mramba alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajali na kutoa nafasi mbalimbali za ushiriki wa masuala mbalimbali kwa wenye ulemavu mbalimbali.

Mramba alosema kuwa katiba inaeleza kuwa binadamu wote ni sawa kama katiba inavyoelekeza na CCM inasimamia hilo.

Thursday, September 5, 2024

WAHITIMU JKT WAAHIDI KUWA WAZALENDO


WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamemwahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kulinda rasilimali na kujenga uchumi imara wa nchi ili ipate maendeleo.

Walitoa ahadi hiyo wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya JKT Operesheni miaka 60 ya Muungano kwenye kambi ya Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akisoma risala ya wahitimu hao Hilda Edward amesema kuwa watayatumia mafunzo hayo kwa kuifanyia nchi yao uzalendo ambao wamefundishwa kwenye mafunzo hayo ya miezi mitatu yaliyoanza Juni mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa Taifa linawategemea vijana kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na wanapaswa kuwa wabunifu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi amesema kuwa vijana hao wanapaswa kujitunza na kuacha kutumia vilevi ambavyo vitasababisha kupata matatizo ya afya ya akili na miili.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali George Kazaula amesema kuwa vijana hao wanapaswa kutumia nidhamu kama silaha kwa kila jambo wanalolifanya.

Awali Mkuu wa kikosi hicho cha Ruvu Kanali Peter Mnyani amesema kuwa kambi hiyo pia inachukua vijana wenye mahitaji maalumu ambao nao wamehitimu mafunzo hayo.


Wednesday, September 4, 2024

WAHITIMU JKT KULINDA RASILIAMALI ZA NCHI

WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamemwahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kulinda rasilimali na kujenga uchumi imara wa nchi ili ipate maendeleo.

Walitoa ahadi hiyo wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria Operesheni miaka 60 ya Muungano kwenye kambi ya Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akisoma risala ya wahitimu hao Hilda Edward alisema kuwa watayatumia mafunzo hayo kwa kuifanyia nchi yao uzalendo ambao wamefundishwa kwenye mafunzo hayo ya miezi mitatu yaliyoanza Juni mwaka huu.

Edward alisema kuwa mbali ya kujifunza mafunzo ya kijeshi pia wamejifunza stadi mbalimbali za maisha ambazo wataziendeleza kule watakakokwenda.

"Tunaishukuru serikali kwa kurejesha mafunzo haya kwa mujibu wa sheria ambayo yatatuwezesha kuitumikia nchi na kulinda rasilimali kwani hapa tuko tayari kulitumikia Taifa tutadumisha nidhamu na uzalendo,"alisema Edward.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa Taifa linawategemea vijana kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na wanapaswa kuwa wabunifu.

Kunenge alisema kuwa wanapaswa kuitumikia jamii na kutatua changamoto kwa kutumia mafunzo hayo pasipo vurugu na anaiona Tanzania yenye Neema na kuilisha dunia na kuwa juu kiuchumi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujitunza na kuacha kutumia vilevi ambavyo vitasababisha kupata matatizo ya afya ya akili na miili.

Nshushi alisema kuwa mafunzo hayo yamezingatia kuanzishwa kwa jeshi hilo bila ya kujali dini, kabila wala hali ya mtu kwani wote wamekuwa kitu kimoja.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali George Kazaula alisema kuwa vijana hao wanapaswa kutumia nidhamu kama silaha kwa kila jambo wanalolifanya.

Kazaula alisema kuwa wao ni nguzo ya Taifa wakizingatia kiapo chao cha utii ikiwa ni pamoja na uzalendo mshikamano ukakamavu na kujiamini na kulitetea Taifa.

Awali Mkuu wa kikosi hicho cha Ruvu Kanali Peter Mnyani alisema kuwa kambi hiyo pia inachukua vijana wenye mahitaji maalumu ambao nao wamehitimu mafunzo hayo.

Mnyani alisema kuwa baadhi yao walishindwa kumaliza mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro na utovu wa nidhamu.


Tuesday, August 27, 2024

HALMASHAURI KIBAHA YATAKA MBWA WACHANJWE


HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imeagiza kuuwawa mbwa wote wanaozurura ambao wamekuwa wakingata watu na kuwaletea madhara.

Aidha imetaka kufanyika sensa ya wanyama hao ili idadi yake iweze kutambulika kwa wale wanaowafuga kwa utaratibu unaotambulika rasmi na kisheria.

Akitoa azimio hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kwa kipindi cha robo ya Aprili hadi Juni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erasto Makala alisema kuwa mbwa hao wamekuwa kero kwa watu.

Makala alisema kuwa mbwa hao wanaozurura hawana chanjo na wamekuwa wakingata watu hivyo kuhatarisha afya zao.

"Madhara ya mtu kungatwa na mbwa ni makubwa hivyo lazima kuwamaliza mbwa wanaozurura ambao hawana mwenyewe kwani hawana chanjo ya kuwakinga na magonjwa,"alisema Makala.

Alisema kuwa sensa ni muhimu kwa wanayama hao na Halmashauri ikiona kuna changamoto kuna haja ya kumpa mzabuni kwa ajili ya kuchanja mbwa ili kuwafikia mbwa wengi.

Akiibua hoja kuhusiana na mbwa wengi kutochanjwa Diwani wa Viti Maalum ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Halima Jongo alisema mbwa hawajachanjwa ni wengi ukilinganisha na mbwa waliopo.

Jongo alitoa mfano wa Kata ya Ruvu kuna mbwa 361 lakini waliochanjwa ni 35 na Mtambani kuna mbwa 53 lakini hawajachanjwa ambapo Kata za Kwala na Magindu hakuna taarifa ya kuchanjwa mbwa.

Naye Diwani wa Kata ya Kilangalanga Mwajuma Denge alisema kuwa mbwa wasio na wamiliki ambao huzurura ndiyo wanaoleta madhara.

Mwajuma alisema kuwa ikifanyika sensa itakuwa vizuri kwani itakuwa rahisi kujua idadi na kutoa chanjo kwa mbwa na kwa wale wanaozurura wauliwe ili kuepusha madhara kwa wananchi.

Sunday, August 25, 2024

WAHITIMU WAASWA KUEPUKA VISHAWISHI

WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne na darasa la saba nchini watakiwa kuepukana na tamaa na vishawishi ili visikatishe ndoto zao za kuendelea na masomo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chuo cha Diplomasia Jacob Nduye wakati wa mahafali ya Darasa la saba na Kidato cha nne Shule za Filbert Bayi.

Nduye alisema kuwa ili wanafunzi hao waweze kufikia ndoto zao wanapaswa kujiepusha na tamaa na vishawishi ambavyo vimekuwa kikwazo kufikia kule walikopanga kufika.

"Epukeni tamaa na vishawishi na vitu ambavyo havina maadili kwani ili ufikie malengo yako unapaswa kukaa mbali navyo ili ufikie ndoto zako ambazo umejiwekea,"alisema Nduye.

Alisema kuwa wazazi wanawasomesha wanatumia gharama kubwa wanajinyima ili wasome lakini baadhi wamekuwa wakikatisha masomo kutokana na kujiingiza kwenye vishawishi.

"Nyie ni tegemeo la Taifa kwa siku za baadaye lakini ili muwe tegemeo lazima msome na kuachana na matendo yasiyofaa ndani ya jamii hivyo lazima mjilinde,"alisema Nduye.

Aidha alisema kuwa wazazi nao wanapaswa kuwalea watoto wao kwenye maadili mema na washirikiane na walimu katika kuwalea watoto ili wawe na maadili mema kwani ni viongozi wa baadaye.

Naye Mwenyekiti wa bodi Taasisi ya Filbert Bayi alisema kuwa mbali ya shule hizo kufanya vizuri lakini inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara.

Bayi alisema barabara inayotoka Picha ya Ndege kwenda Jamaica na kutoka Jamaica kwenda Picha ya Ndege barabara hiyo ambayo inapita kwenye shule hizo ni mbaya na haijachongwa muda mrefu hivyo jamii inayozunguka shule inapata changamoto kubwa kwenda kupata huduma ya afya kwenye zahanati ya Bayi.

Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Mariam Msabaha alisema kuwa mbali ya masomo ya kawaida pia walisoma masomo ya ujasiriamali ambayo yatawasaidia mara wamalizapo shule.

Msabaha alisema kuwa masomo hayo ni pamoja na ususi, mapishi, upambaji na utunzaji wa mazingira na masuala ya michezo ambapo shule imekuwa ikifanya vizuri kitaifa na kimataifa.



Thursday, August 22, 2024

HALIMA JONGO ACHAGULIWA MAKAMU MWENYEKITI BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha limemchaguaHalima Jongo kuwa makamu mwenyekiti baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Shomari Mwinshehe kumaliza muda wake.

Sambamba na uchaguzi huo wa makamu mwenyekiti ambaye alipata kura zote 17 pia kamati mbalimbali nazo zilichaguwa wenye viti wake.

Jongo ameshukuru madiwani wenzake kwa kumchagua kwa kura nyingi na kusema atashirikiana nao pamoja na watumishi wa Halmashauri ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amesema kuwa ataendeleza yale ambayo aliyoyafanya mtangulizi wake ili Halmashauri iweze kupata mafanikio ambayo itakuwa ni sehemu ya wananchi kujiletea maendeleo.

"Katika ukusanyaji mapato tumefanya vizuri kwenye awamu hii iliyopita kwa kushirikiana na wenzangu, wataalamu na wananchi kuhakikisha tunakuwa na makusanyo makubwa,"amesema Jongo.

Amesema kuwa jambo kubwa ni kupambana kuleta maendeleo kwa wananchi ambao wanawategemea kuwaonyesha njia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Regina Bieda amesema kuwa anampongeza Makamu mwentekiti aliyepita na anamkaribisha Makamu mpya katika kuendeleza jitihada za maendeleo.

Bieda amesema watashirikiana wote kwa pamoja ili kuwapambania wananchi lengo waweze kupata maendeleo.