Saturday, September 7, 2024


VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kutoa nafasi watu wenye mahitaji maalum kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwani nao wana haki ya kushiriki.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Umoja wa Amani Kwanza Mkoani Pwani Halima Yusuph wakati wa mkutano kwa vyama vya siasa na jamii ambapo katiba inaonyesha kuwa binadamu wote ni sawa.

Yusuph alisema kuwa vyama vya siasa kutoa nafasi kwa kundi maalum la watu wenye ulemavu ili wapate nafasi kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024 mwaka huu bila ya kuwatenga kwani wana haki ya kushiriki uchaguzi.

"Kwa mujibu wa Katiba binadamu wote ni sawa hivyo kuna kila sababu ya watu wenye ulemavu kupata nafasi za kushiriki uchaguzi kwa kuchagua na kuchaguliwa na tunakemea ramli chonganishi ambazo husababisha wenye ulemavu wa ngozi kuuwawa,"alisema Yusuph.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Africa Talent Forum (ATF) MaryRose Bujash aliomba watu wenye ulemavu wasitengwe wala kunyanyapaliwa.

Bujash alisema kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa jamii isiwatenge na pia na wao wanahitaji elimu zaidi ya masuala ya uchaguzi na uongozi ili kuweza kushiriki uchaguzi.

Naye Katibu wa siasa na uenezi Mkoani Pwani David Mramba alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajali na kutoa nafasi mbalimbali za ushiriki wa masuala mbalimbali kwa wenye ulemavu mbalimbali.

Mramba alosema kuwa katiba inaeleza kuwa binadamu wote ni sawa kama katiba inavyoelekeza na CCM inasimamia hilo.

No comments:

Post a Comment