Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baadhi ya wananchi walisema kuwa kupanda kwa bei hiyo inasababisha washindwe kununua nyama.
Happy Ngilangwa alisema kuwa kama kuna namna ya kufanya ni vema serikali ikakaa na wafanyabiashara wa nyama ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa wanannchi.
"Tunaomba serikali ikae nao chini ili waangalie kama kuna baadhi ya mambo wayaweke sawa sababu sisi tunashangaa tu kuona bei imepanda ghafla,"alisema Ngilangwa.
Alisema kuwa nyama ni kitoweo muhimu ambacho ndicho chakula kikuu kwa wananchi wengi ukilinganisha na mboga zingine ambapo hata samaki nazo bei iko juu.
"Kwa sasa maisha yamekuwa magumu hivyo kupandisha bei ni kuwaongezea mzigo wananchi kutokana na bei kupanda baadhi ya watu wameshindwa kumudu bei,"alisema Ngilangwa.
Kwa upande wake mama lishe Neema Maneno alisema kupanda kwa bei ya nyama kumewaathiri ambapo kwa sasa imebidi wapunguze ukubwa wa vipande vya nyama.
Maneno alisema wana wateja wengi ambao wanakula chakula pamoja na kunywa supu wanalamika lakini hawana jinsi ya kufanya inabidibwaendane na hali halisi.
Naye moja ya wauzaji nyama Albert Koka alisema kuwa yeye kashindwa kufanya biashara na amefunga bucha kwani yeye hununua mabuchani na kuongeza kidogo ili apate chochote.
Koka alisema kuwa wao nao wanaumia kwani nao wanategemea kununua kwa wenye mabucha makubwa na kuuza kwa wananchi mitaani ili nao wapate riziki.
Naye mwenyekiti wa Chama Cha Wauzaji Nyama Kibaha Aidan Mchiwa alisema kuwa nyama imepanda bei kwa sababu ya nyama nyingi inauzwa nje.
Mchiwa alisema kuwa soko la nyama nje limekuwa kubwa sana ambapo ngombe nyingi zinanunuliwa na makampuni ambayo yanasafirisha kwenda nje ya nchi kwenye soko la Uarabuni.
No comments:
Post a Comment