WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamemwahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kulinda rasilimali na kujenga uchumi imara wa nchi ili ipate maendeleo.
Walitoa ahadi hiyo wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria Operesheni miaka 60 ya Muungano kwenye kambi ya Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Akisoma risala ya wahitimu hao Hilda Edward alisema kuwa watayatumia mafunzo hayo kwa kuifanyia nchi yao uzalendo ambao wamefundishwa kwenye mafunzo hayo ya miezi mitatu yaliyoanza Juni mwaka huu.
Edward alisema kuwa mbali ya kujifunza mafunzo ya kijeshi pia wamejifunza stadi mbalimbali za maisha ambazo wataziendeleza kule watakakokwenda.
"Tunaishukuru serikali kwa kurejesha mafunzo haya kwa mujibu wa sheria ambayo yatatuwezesha kuitumikia nchi na kulinda rasilimali kwani hapa tuko tayari kulitumikia Taifa tutadumisha nidhamu na uzalendo,"alisema Edward.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa Taifa linawategemea vijana kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na wanapaswa kuwa wabunifu.
Kunenge alisema kuwa wanapaswa kuitumikia jamii na kutatua changamoto kwa kutumia mafunzo hayo pasipo vurugu na anaiona Tanzania yenye Neema na kuilisha dunia na kuwa juu kiuchumi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujitunza na kuacha kutumia vilevi ambavyo vitasababisha kupata matatizo ya afya ya akili na miili.
Nshushi alisema kuwa mafunzo hayo yamezingatia kuanzishwa kwa jeshi hilo bila ya kujali dini, kabila wala hali ya mtu kwani wote wamekuwa kitu kimoja.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali George Kazaula alisema kuwa vijana hao wanapaswa kutumia nidhamu kama silaha kwa kila jambo wanalolifanya.
Kazaula alisema kuwa wao ni nguzo ya Taifa wakizingatia kiapo chao cha utii ikiwa ni pamoja na uzalendo mshikamano ukakamavu na kujiamini na kulitetea Taifa.
Awali Mkuu wa kikosi hicho cha Ruvu Kanali Peter Mnyani alisema kuwa kambi hiyo pia inachukua vijana wenye mahitaji maalumu ambao nao wamehitimu mafunzo hayo.
Mnyani alisema kuwa baadhi yao walishindwa kumaliza mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro na utovu wa nidhamu.
No comments:
Post a Comment