Monday, August 12, 2024

VIJANA WAJA NA SERA MPYA

SERIKALI imezindua Sera mpya ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 toleo la 2024, ambayo inakwenda kujibu changamoto mbalimbali za vijana na kutoa mwongozo wa kuanzishwa rasmi kwa Baraza la Taifa la Vijana.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 12,2024 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu,Mhe. Ridiwani Kikwete, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya vijana kimataifa.

“Serikali imekwisha kamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 na marekebisho yake imefanyiwa mwaka 2024 na leo hii tunakwenda kuizindua muda mfupi ujao.

“Ndugu washiriki changamoto nyingi zinazoelezwa kwa vijana zinatokana na ukweli kwamba yako baadhi ya maeneo hayana miongozo yake kupitia sera hii ya vijana ambayo tutaizundua leo nina hakika kabisa vilio vya vijana wengi vinakwenda kupataiwa ufumbuzi baada ya kupitishwa kwa sera hii”ameeleza.

Aidha, amesema kuwa sera hiyo inaeleza uelekeo na njia ambazo wanakwenda kuzitumia kwa pamoja ili kufikia malengo ambayo yanatatua matatizo waliyonayo vijana.

“Sera hii inakwenda kuanzisha baraza la taifa la vijana uanzishaji wa baraza hili la vijana unakwenda kuwa muarobani wa kutambua na kutatua changamoto nyingi za vijana.

“Vijana wamekosa maeneo ya kueleza changamoto zao vijana walikosa watu wa kuwasikiliza, vijana walikosa msukumo wa kufikisha changamoto zao na kuzitafutia majawabu kwa pamoja”amesema Mhe.Ridhiwan.

Amesema, ujio wa sera hiyo ya vijana na uudwaji wa baraza la taifa la vijana unaonesha wazi azma ya Rais Samia kujidhatiti na changamoto zote zinazo wakabili vijana zinapatiwa majibu.

Hata hivyo amesema kuwa sera hiyo pia inakwenda kutambua vijana katika sekta zote wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi ikiwemo ya madini, maeneo ya uzalishaji mali ikiwemo mashambani na kwenye mifugo.

“Wapo vijana wanaofanya kazi za sanaa ikiwemo wabunifu, muziki, michezo, ubunifu na utungaji wa sanaa mbalimbali sera hii inakwenda katika maeneo hayo.

Pia  ametoa  wito kwa maafisa kazi kutambua kuwa nafasi zao siyo za kukaa ofisini wakisubiri vijana waje kulia na kueleza changamoto zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Maganga,amesema katika kuadhimisha siku ya vijana, wameendesha kongamano la siku mbili lililokutanisha vijana zaidi ya 3,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Katika kongamano hilo, vijana wamechangia juu ya mada za Sera ya Maendeleo ya 2050, fursa za kidigitali, vijana na uchumi, afya ya akili na saikolojia ya vijana na kusisitiza kuwa serikali imechukua maoni ya vijana katika eneo la elimu, afya, ajira na uwezeshaji.”amesema Bi.Maganga

Naye Mwakilishi wa Vijana, Charles Ruben amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake kuwainua na kuwasaidia vijana wa kitanzania na kuwa vijana wamepata elimu na ujuzi wa kazi unaofanya vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuwapo ongezeko la vijana kwenye uongozi.

 “Ajira za vijana zimeongezeka ambapo kuanzia mwaka 2023 hadi 2024 ajira 607675 zimezalishwa huku ajira 204,000 zikitokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini huku akitenga Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi ya jenga kesho iliyobora BBT ambayo inawalenga vijana.”amesema Ruben

Friday, August 9, 2024

SELF MICROFINANCE WATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika kuadhimisha kilele cha siku ya wakulima na wafugaji Nane Nane, Mfuko wa Fedha wa (SELF MICROFINANCE) ulio chini ya Wizara ya Fedha umewataka  wananchi wote wanaojishughulisha na shuguli za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kukuza na kuongeza uzalishaji.

Wito huo umetolewa na Bi. Linda Mshana ambaye ni meneja masoko na uhamasishaji kutoka mfuko wa SELF wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la SELF lililopo katika maonesho ya Kitaifa ya Nanenane Jijini Dodoma.

Bi. Linda amesema, Mfuko huo una vifurushi mbalimbali kwaajili ya Wakulima, Wavuvi na wafugaji hivyo amewahimiza kujitokeza kwa wingi na kukopa mikopo hiyo ambayo imewekwa maalumu kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Aidha,  Linda ameongeza kuwa mbali na Mikopo hiyo pia Mfuko wa Self unatoa Mikopo kwa taasisi ndogondogo za kifedha kwaajili ya kuwakopesha wakulima, wafugaji na wavuvi sambamba na mikopo mingine inayolenga kukuza uchumi wa watu mbalimbali.

"Self ina mikopo ya aina mbalimbali, tuna mkopo kwa ajili ya taasisi zinazokopesha, hivyo tunawakaribisha wakope na baadaye wawakopeshe wakulima, wafugaji na wavuvi,"amesema.

Linda amewakaribisha wananchi wote kutembelea banda lao lililopo katika maonesho hayo ili kupata elimu na kujua namna gani wanaweza kunufaika na Mikopo mbalimbali inayotolewa na Mfuko wa SELF.

Thursday, August 8, 2024

OFISI MAKAMU WA RAIS YAPONGEZWA UBUNIFU UTENGANISHAJI TAKA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utoaji wa elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka ambao ni fursa ya ajira.

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo Jumatano Julai 7, 2024) wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa taka zinazozalishwa nchini kwa sasa zimekuwa ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.

“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu kuhusu fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira” amesema Mhe. Jaji Mwaimu.

Aidha Jaji Mwaimu amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais na kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya uhifadhi wa mazingira kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa taka ni fursa iliyojificha na hivyo elimu kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani sio kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.

“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na namna zinavyotakiwa kutenganishwa” amesema Jaji Mwaimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde amesema Ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya habari.

Ameongeza kuwa katika kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa buluu, fursa zitokanazo na taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Kupitia maonesho tuna nyaraka mbalimbali ambazo ni vitabu ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), vipeperushi, majarida ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau nk” amesema Kibonde.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki maonesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2024.

Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.



DIB KULINDA AMANA ZA WATEJA


Na Wellu Mtaki, Dodoma

Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ikiwa na jukumu la kusimamia amana za wateja zinapokuwa kwenye mabenki endapo benki ikifilisika inaweza kumlinda mteja aliyeweka amana zake asiweze kupata hasara.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa bodi ya Amana (DIB) Emmanuel Tutuba wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la maonyesho ya nanenane Zuguni Jijini Dodoma huku akiwataka wananchi waliokuwa wateja wa benki zilizofilisika waweze kufika katika taasisi hiyo ili kuhakikiwa na kupewa stahiki zao.

Amesema DIB mpaka sasa imeongeza zaidi ya shilingi trilioni 1 ambazo wanaendelea kuwekeza sehemu mbalimbali ambazo fedha hizo ni za wateja endapo benki ikifilisika mteja aweze kupata gawio lake kulingana na alivyowekeza.

"Tangu kuanzishwa DIB ilipewa mtaji  mwaka 1994 na benki kuu ya Taifa (BOT)  walipewa kiasi cha  shilingi bilioni1.5 kwa sasa wana atirioni 1.2.3 fedha hizo zinaendele kuongezeka kwa sababu wanaendelea kuwekeza sehemu mbalimbali fedha hizo zipo  kwa ajiri ya kukinga  amana za wateja hata kama bank ikitokea bahati mbaya  ikafilisika kila  aliyekuwa na account kwenye benki atalipwa kulingana na kiwango  ambacho alichokuwa anaweza kulingana na kiwango  cha asilimia atarejeshewa,"amesema Tutuba. 

Pia ametoka wito kwa wateja wa benki FDME  kama kuna mtu ajapewa mgawanyo wa asilimia 30 aweze kufika kwenye  bodi ya bima ya Amana ili aweze kupatiwa utaratibu.

"Wametoa wito kwa wateja  kwenye benki FDME kama kuna mtu ajapewa mgawanyo wa asilimia  30 cha awali aweze kufika taasisi hii ya bima ya amana ili aweze kupitia taratubu zote kujiludhisha Ili  arejeshewa kiwango 30 Cha awali." Amesema Tutuba.

Aidha Tutuba hakusita kueleza mfano wa faida ya mfuko huo unaosimamiwa na DIB kupitia mfano wa zile benki ambazo zilizowahi kufilisika nchini.

Amewapongeza kusimamia shughuli zao za kusimamia amana za wateja na cha msingi DIB  kazi yake ni kuweka  na kuendelea kuwekeza bima ili kukinga viatarishi ambavyo  vitajitokeza endapo benki itafilisika, pia  kuna baadhi ya watu ambao benki zao zilifilisika mwanzano wanatakiwa wafiki DIB" Amesema Tutuba.

Wednesday, August 7, 2024

FILBERT BAYI WATAMBA KUFANYA VEMA FEASSA

WANARIADHA tisa kutoka Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi ambao wataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya shule za sekondari Afrika Mashariki na Kati (FEASSA) yanayotarajiwa kufanyika mwezi huu nchini Uganda wameahidi ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi vikombe walivyoshinda huko Tabora kitaifa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta ofisini kwake Mjini Kibaha mwalimu wa timu hiyo Ally Nyonyi alisema kuwa wanariadha hao ni wa mbio tofauti tofauti.

Nyonyi alisema kuwa wanariadha hao wanaendelea vizuri na mazoezi kwenye uwanja wa shule uliopo Kibaha Mkoani Pwani huku wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

"Wachezaji wetu tisa ambao walichaguliwa kwenye mashindano ya Umisseta yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Tabora wanaendelea vizuri na mazoezi kwenye kambi iliyoko pale shule na wote wako vizuri,"alisema Nyonyi.

Alisema kuwa kambi inaendelea vizuri na hakuna mchezaji ambaye ana tatizo wote wako vizuri wanasubiri tu kuingia kwenye kambi ya mwisho itakayokuwa huko Tabora na mwaka huu wamejiandaa vizuri.

"Tangu mashindano ya Raidha ya Taifa yaliyofanyika mkoani Tabora timu iliingia kambini na hadi sasa inaendelea na mazoezi na hawana muda wa kusubiri kwani sisi ndiyo utaratibu wetu wa kufanya mazoezi kila siku,"alisema Nyonyi.

Aidha alisema kuwa wana mazoezi ya kutosha na wana morali ya hali ya juu na hakuna changamoto yoyote inayowakabili na wako vizuri wakiwa na afya nzuri.

"Sisi ni mabingwa wa Umisseta hapa nchini kwa miaka mitatu mfululizo siri kubwa ya wachezaji wangu kufanya vizuri ni nidhamu na kufuata maelekezo ya mwalimu na vifaa vipo mazingira ni rafiki,"alisema Nyonyi.

Aliomba wadau wa mchezo huo kuwaunga mkono kwa kuwasaidia baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na maji, matunda na motisha ili waweze kufanya vyema.

Kwa upande wa mwanariadha Emanuel Amos alisema kuwa amejipanga vizuri na anategemea kushinda kwani atahakikisha anafanya juhudi ili kufanikisha kushinda.

Amos alisema kuwa amepata uzoefu mkubwa kwani hayo yatakuwa mashindano yake ya pili ambapo mara ya kwanza hakuweza kufanya vizuri sana kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki hivyo hakuwa na uzoefu.

Naye Elizabeth Kelaryo alisema kuwa wamejiandaa vyema na watavitumia vyema vipaji vyao na watahakikisha wanapambana kwani shuleni kwao wamefundishwa kupambana.

Kelaryo alisema kuwa wanajiamini na kikubwa ni ushirikiano walionao ndiyo unaowafanya waweze kufanya vizuri na maandalizi wanayoyafanya na mbinu bora za mwalimu wao watafanya vyema.

Wachezaji wanaounda timu hiyo ni Emanuel Amos anayekimbia mbio mita 100 na 200, Kimana Kibase 100 na 200, Wiliam Makaranga kupokezana vijiti mita 400, Yohana Samwel 400, Sharifa Mawazo kupokezana vijiti mita 400.

Wengine ni Eliza Kelaryo kutupa mkuki, Sara Masalu mita 1,500, Lucia Pius mita 400 kupokezana vijiti, Salma Samwel 800 na kupokezana vijiti mita 400.



 




BRELA YAZUIYA KUTAPELIWA KWA WATEJA

Na Wellu Mtaki,Dodoma.

Wakala wa Usajili wa biashara na leseni (BRELA) imeweka mfumo wa kujisajili katika mtandao ambao utazuia mteja kuacha  kutumia mtu ambaye atasimamia katika usajili ambao utamfanya mteja kulipa kiasi cha ziada tofauti na malipo ambayo yamewekwa na BRELA

Hayo yameelezwa leo tarehe 6 Agost 2024 na Msaidizi wa Usajili Yvonne Massele wakati akizungumza na waandishi wa habari katika  maonesho ya nanenane Zuguni Jijini Dodoma huku akiwataka wananchi kutembelea banda la Brela ili kutambua huduma zinazopatika katika banda hilo.

Massele amesema kuwa mfumo wa usajili wa Brela kwa njia ya Mtandao unamsaidia mteja kurahisisha usajiri kwa mteja ambaye yupo mbali na huduma.

"Sasa hivi tunajisajiri kwa njia ya mfumo na ukiingia kwenye Mfumo unaweza kupata naomba ya malipo ( control number) na kama mteja atapata changamoto Kuna mawasiliano ambayo atawasiliana na mtoa huduma moja kwa moja,"amesema Massele.

Aidha ameelaza kuwa huduma ambazo zinatolewa katika maonesho ya nanenane ni pamoja na usajili wa kampuni,  usajili wa biashara, usajili wa harama za biashara, huduma pamoja na kutoa leseni ya biashara jina la kampuni kwa siku hiyo hiyo uliofika kujisajili.

"Ujio wao ni kwa ajili wa kutoa huduma zetu za Brela ambazo zinafanyika ni usajiri wa kampuni, usajili wa biashara , usajili wa harama za biashara na huduma pamoja na kutoa leseni la biashara la kundi A pamoja na leseni za viwanja,"amesema Massele 

Pia amesema kuwa wanaendelea kutoa Elimu kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa ili waweze kutambua namna ya kusajili biashara zao kwa wale ambao bado hawajasajili 

"Tumekuja kutoa Elimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao awajasajili biashara  waweze kusajili biashara zao na wale ambao biashara zao zishakuwa waweze kusajiri majina ya Kampuni " amesema

Tuesday, August 6, 2024

MSONGO WA MAWAZO HUSABABISHA MAZIWA YA AKINAMAMA WANAONYONYESHA YASITOKE








IMEELEZWA kuwa moja ya sababu zinazosababisha maziwa ya akinamama wanaonyonyesha kushindwa kutoka ni msongo wa mawazo.

Aidha wanaume ambao wake zao wananyonyesha wameshsuriwa wasiwaudhi wake zao ili wasisababishe maziwa yashindwe kutoka na kushindwa kunyonyesha watoto wao.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Afya Amour Mohamed ambaye alimwakilisha mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa Siku ya Unyonyeshaji Duniani kwa Halmashauri hiyo yaliyofanyika kwenye Zahanati ya Mwendapole.

Mohamed alisema kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwasababishia wake zao wanaonyonyesha msongo wa mawazo hivyo maziwa kushindwa kutoka hivyo watoto kukosa maziwa.

"Wanaume tunapaswa tushiriki katika makuzi ua watoto wetu wachanga kwani ndiyo chakula chao kikuu ambapo moja ya changamoto ni maziwa kushindwa kutoka na moja ya chanzo ni wazazi kuwa na mawazo ambayo wakati mwingine husababishwa na waume zao,"alisema Mohamed.

Alisema kuwa wasiwaudhi wake zao katika kipindi hicho cha unyonyeshaji kwani hudababisha maziwa yasitoke na wanapaswa kuhakikisha wazazi wanapata lishe bora ili makuzi ya watoto yawe mazuri.

Naye Diwani wa Kata ya Kibaha Goodluck Manyama ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema kuwa maziwa ya mama ni muhimu tofauti na maziwa mengine.

Manyama alisema kuwa maziwa ya mama yana kinga nyingi kujikinga na maradhi kuliko ya ng'ombe au ya kopo lakini ya mama yana ubora na ukuzaji wa mtoto kwa haraka.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu na Kaimu Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Kibaha Asteria Massawe alisema kuwa ndani ya saa moja mama aanze kumnyonyesha mtoto.

Massawe alisema kuwa yanayoanza kutoka ni maji hivyo lazima mtoto anyonye vya kutosha ili maziwa yaishe kabisa ndipo uhamishie ziwa lingine na amnyonyeshe mara 10 kwa siku au kila baada ya saa moja.

Akitoa maelekezo juu ya unyonyeshaji sahihi Muuguzi wa Zahanati ya Mwendapole Nyasungi Pepya alisema kuwa mtoto anapaswa kupata vipimo mara tano tangu mama akiwa mjamzito lengo ni mtoto azaliwe akiwa salama.

Pepya alisema kuwa vipimo husaidia kujua hali ya mama na kama akigundulika kuwa na maambukizi atapewa dawa ili kumlinda mtoto.