Thursday, July 4, 2024

UMAUKI WAPANDA MITI KWENYE MAENEO YALIYOCHIMBWA MCHANGA







CHAMA cha Ushirika cha Umoja wa Wanamazingira na Udhibiti wa Uchimbaji Mchanga Kibaha (UMAUKI) kimeanzisha mradi wa upandaji wa miti katika maeneo yaliyoathiriwa na uchimbaji wa mchanga na shughuli ambazo si rafiki wa mazingira. 

Hayo yamesemwa na Meneja wa chama hicho Hay Mshamu wakati wa unzinduzi uliofanyika Mwendapole Kibaha.

Mshamu amesema kuwa chama kimeendelea na shughuli za kudhibiti uharibifu wa Mazingira unaotokana na sababu mbalimbali zikiwemo uchimbaji wa mchanga kiholela, ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji.  

"Tulitekeleza mradi wa upandaji wa miti ya kivuli na matunda kuzunguka katika mipaka na katikati mwa eneo la shule ya Msingi Muungano,"amesema Mshamu.

Amesema kuwa mradi ambao umekamilika kwa 100 na sasa watoto wetu wananufaika na uwepo wa miti hiyo tumeendelea kufanva kazi mbalimbali rafiki wa mazingira hadi kufikia sasa.

Aidha amesema kuwa pia wanajihusisha na uvuvi, ufugaji wa nyuki lengo likiwa ni kulinda mazingira ili yawe salama na kurejesha uoto wa asili ambao umetoweka kutokana na uharibufu wa mazingira.

"Tunahitaji kiasi cha shilingi milioni 6.5 kwa ajili ya mradi wa kilimo cha matunda ya pasheni na papai ambapo tulianzisha kuanzia miche hadi kupanda lakini nguvu imeishia hapo huku tukihitaji kupata uzalishaji mzuri,"amesema Mshamu.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Kilimo Halmashauri ya Mji Kibaha Suzana Mgonja amesema kuwa chama hicho kinapaswa kutumia wataalam wa kilimo ili waweze kuzalisha kwa ubora.

Mgonja amesema kuwa wao wako tayari kushirikiana na wakulima ili kuhakikisha wanainuka na kulima kilimo bora na chenye manufaa siyo kilimo kisicho na tija.

Wednesday, July 3, 2024

MTAA MAILI MOJA A WAJENGA OFISI

 





UONGOZI wa Mtaa wa Maili Moja A umetimiza ahadi yake ya kujenga ofisi ambapo Diwani wa Kata ya Maili Moja aliizindua ofisi hiyo na kuondokana na ofisi waliyokuwa wamepanga.

Akiwaaga wananchi wa Mtaa huo kwente mkutano wa hadhara Mwenyekiti wa Mtaa huo Yassin Mudhihiri amesema wanawashukuru wananchi kwa kufanikisha ujenzi huo.

Mudhihiri amesema kuwa ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 95 lakini imeanza kutumika na wananchi wanapata huduma kwenye ofisi hiyo iliyoko eneo la Minazini.

"Tumemalia muda wetu wa uongozi wa kipindi cha miaka mitano ambapo mafanikio mengine ni kupata mradi wa barabara za lami, kurasimisha ardhi, kudhibiti wizi, kupata mradi wa Tasaf wa ujenzi wa barabara na mambo mengine ya maendeleo,"amesema Mudhihiri. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Ramadhan Lutambi akizindua ofisi hiyo amesema kuwa  uongozi uliomaliza muda wake umefanya kazi kubwa ya kujenga ofisi hiyo.

Lutambi amesema kuwa mtaa utapunguza gharama za kila mwezi za kulipa kodi hivyo fedha walizokuwa wakilipa kodi zitatumika kwenye matumizi mengine.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Maili Moja Methew Mkayala amesema kuwa mafanikio yote hayo yanatokana na utekelezaji wa ilani ya Chama.

Mkayala amesema kwa sasa wanajiandaa na uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za Mitaa utakaofanyika hivi karibuni na kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda kwa kishindo. 


Tuesday, July 2, 2024

KAMATI YA BUNGE YAISHAURI TARURA UBORESHAJI BARABARA ZAKE

 

WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na mkoa huo wametakiwa kuandika ombi maalumu la fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo ya uwekezaji.

Hayo yemesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Denis Londo wakati wa majumuisho ya ziara ya siku moja kutembelea barabara zilizojengwa na Tarura Mkoa huo.

Londo amesema kuwa kutokana na mkoa huo kuwa na uwekezaji mkubwa hasa wa viwanda ambao una manufaa kwa Taifa ni vema wakaomba maombi maalumu ya fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara badala ya kuomba kidogo kidogo.

"Angalieni mahitaji ya barabara zote ambazo zinahitajika kwenye maeneo muhimu ya uwekezaji badala ya kuomba sehemu chache ili muweze kuboresha kwa pamoja,"amesema Londo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kukiwa na miundombinu mizuri ya barabara kwenye maeneo hayo kutakuwa ni kivutio kwa wawakezaji kuendelea kuwekeza.


Kunenge amesema kuwa Tarura imeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilometa 12.5 kwenye eneo la viwanda la Zegereni yenye thamani ya shilingi bilioni 16.4 ambayo imekamilika kwa sasa ikiwa kwenye muda wa matazamio.


Naye Meneja wa Tarura Mkoa wa Pwani Mhandisi Leopold Runji alisema miradi mitatu ambayo imetembelewa na kamati hiyo ni kutoka barabara ya Morogoro kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha yenye urefu wa mita 300 na umekamilika unathamani ya shilingi milioni 500.


Runji alisema kuwa barabara nyingine ni Visiga Zegereni ni eneo la viwanda kiwango cha lami kilometa 12.5 tunamshukuru kutoa fedha bilioni 16.4 na umekamilika sasa kipindi cha matazamio barabara nyingine ni ya Picha ya Ndege Boko Timiza kilometa 7.8 ambapo hadi sasa zimekamilika kilometa 1.2 awamu ya kwanza milioni 950 kwa awamu ya kwanza ujenzi huku ukiwa na awamu tatu.

Mjumbe wa Kamati hiyo Saasisha Mafuwe alisema kuwa katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Tarura kuwe na kiwango maalum cha gharama za ujenzi ijulikane mfano kwa kilometa na kuwe na bei maalumu siyo kila mtu kujenga kwa utashi ambapo gharama zinatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kamati hiyo ilitembelea barabara za Picha ya Ndege-Boko Timiza, barabara kuelekea ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Visiga Zegereni na kuridhishwa na ujenzi wa barabara hizo.

Tuesday, June 25, 2024

FAMILIA ZISIONEA AIBU KUWAWAJIBISHA WANAOFANYA VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO





IMEELEZWA watu kuoneana aibu ndani ya familia kumesababisha vitendo vya ukatili kuendelea ndani ya jamii ambapo hali hiyo imezipeleka familia pabaya.

Aidha serikali ya Mkoa wa Pwani imesema kuwa itachukua hatua kali kwa watu wanaowafanyia ukatili watoto washindwe kufikia ndoto zao na kukosa haki zao.

Hayo yamesemwa na  Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala wakati wa Siku ya Mtoto wa Afrika kimkoa iliyofanyika Mjini Kibaha.

Twamala amesema kuwa baadhi ya taarifa zinaonyesha kuwa wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu.

"Ukatili unafanywa na ndugu wa karibu ambapo familia zinashindwa kuchukua hatua sababu ya kuoneana Muhali (Aibu) hili hatulikubali,"amesema Twamala.

Akisoma risala ya watoto wa mkoa wa Pwani Evelin Mhema amesema kuwa baadhi ya changamoto ni pamoja kufanyiwa vitendo vya ukatili mimba za utotoni, ubakaji, vipigo na vitendo vingine vinavyowanyima haki zao.

Mhema amesema kuwa watashirikiana na viongozi wakiwemo walimu ili waweze kufikia ndoto zao walizojiwekea kwa kusoma kwa bidii na kutii wazazi na walezi wao.

Kwa upande wake Said Mwinjuma amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa changamoto kwa vijana na kusababisha mmomonyoko wa maadadili.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga amesema kuwa watoto pia nao wajilinde kwa kutotembea usiku na kwenda kwenye mabanda ya video ma kulindana wao kwa wao.

Mlenga amesema kuwa pia wasipokee zawadi au kuomba fedha kwa watu wasiowafahamu na wazazi wawalinde watoto kwa kutokuwa wakali na

GRACE JUNGULU ATOA TOFALI 300

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Picha ya Ndege Grace Jungulu ametoa tofali 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini.

Hayo yamesemwa na Katibu wa UWT Kibaha Mjini Cecilia Ndalu wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya hiyo kilichofanyika mjini Kibaha ambapo aliwashukuru wote waliochangia tofali ili kufanikisha ujenzi huo.

Ndalu amesema anawashukuru wanaccm waliojitolea kuchangia tofali ili ujenzi huo usichelewe na kukamilika kwa wakati kama malengo yaliyowekwa.

Ndalu amesema kuwa katika harambee hiyo jumla ya tofali 1,500 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi huo ambapo mlezi wa UWT Selina Koka alitoa tofali 500 huku Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akitoa mifuko ya simenti 100.

"Malengo yetu ni kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu ujenzi huo uwe umekamilika ili kuepusha katibu kuishi kwenye nyumba ya kupanga ambapo pia itapunguza gharama,"amesema Ndalu. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Eline Mgonja amesema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha mipango yote waliyojiwekea ikiwemo ujenzi huo na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mgonja amesema kuwa juu ya uchaguzi wamejipanga kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Naye Mgeni rasmi kwenye Baraza hilo Mbunge Koka amesema kuwa ataendelea kushirikiana na umoja huo katika kuhakikisha chama kinapiga hatua na kuwaletea wananchi maendeleo.

Koka amesema kuwa ili kufanikisha ushindi wa chama wanawake lazima waungane washirikiane na kuacha kugawanyika kwani wasiposhirikiana watakigawanya chama.

Monday, June 24, 2024

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAPATA HATI SAFI

MKUU wa Mkoa Pwani Abubakar Kunenge ameipongeza Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha kilichofanyika Kibaha wakati wa kupitia hoja za CAG.

Kunenge amesema kuwa Halmashauri imefanya vema kwa ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 54 Februari na kufikia asilimia zaidi 100 ambapo ni kazi kubwa imefanyika.

"Nawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya lakini mnapaswa kudhibiti matumizi ya fedha kwani baadhi ya hoja zimetokana matumizi ya fedha na kutekeleza miradi kwa wakati,"amesema Kunenge.

Kwa upande wake katibu wa baraza hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa amesema kuwa kulikuwa na jumla ya hoja 69 zikiwemo za nyuma ambapo hoja 31 zimefungwa.

Shemwelekwa alisema kuwa hoja 38 ambazo hazijatekelezwa ni kutokana na masuala ya kisera lakini wanaendelea kuzifanyia kazi ili zisiwepo kabisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa wanaomba bajeti ya barabara iangaliwe kwani miundombinu imeharibika sana.

Ndomba amesema kuwa Halmashauri hiyo ipewe msukumo wa kuwa Manispaa kwani hapo ni Makao Makuu ya Mkoa huo kwani hata baadhi ya miradi inaweza kupatikana.

Naye Mkaguzi wa Mkuu wa nje wa Mkoa wa Owabi Pastory Massawe amesema kuwa baadhi ya changamoto zimeonekana kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato.

Massawe amesema kuwa kinachokusanywa kitumike vizuri ili kuleta tija kwa wananchi na miradi izingatie sheria kanuni, utaratibu na kuzingatia miongozo.

Wednesday, June 19, 2024

KIBAHA KUKUSANYA CHUPA 800 KWA MWAKA

WILAYA ya Kibaha imejiwekea lengo la kukusanya chupa za damu 700 hadi 800 kwa mwaka ili ziweze kusaidia wahitaji wakiwemo akinamama wanaojifungua watoto na majeruhi wa ajali.

Hayo yamesemwa na mratibu wa damu salama wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Nyaisawa Birore alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye zoezi la uchangiaji damu kwenye Kituo cha Afya Mlandizi.

Birore amesema kuwa wamejiwekea malengo ya kukusanya chupa 85 hadi 200 kwa kipindi cha robo mwaka ili ziweze kutumika kwa wagonjwa wenye mahitaji ya damu.

"Matumuzi ya damu kwa mwezi yalikuwa ni chupa 45 lakini yameongezeka na kufikia ni chupa 80 hadi 100 hivyo mahitaji ni makubwa sana na tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujitolea,"amesema Birore.

Moja ya wachangiaji wa damu ambaye ni  katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kibaha Vijijini Joel Kijuu amesema ameamua kujitolea ili kusaidia kuokoa maisha ya akinamama na wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.

Kwa upande wake mhamasishaji uchangiaji damu Mariam Ngamila amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa na dhana kuwa damu inayochangwa inauzwa kitu ambacho siyo cha kweli.

Naye mhamasishaji uchangiaji damu Maria Ngamila amesema tone moja la damu linaweza kuokoa maisha ya watu wengi hivyo vijana wahamasike kuchangia damu.

Faudhi Kinanga ambaye yuko kwenye kambi ya uchangiaji damu amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana kushiriki zoezi la uchangiaji damu ili kuisaidia jamii.