Sunday, June 16, 2024

DK BITEKO AZINDUA TAARIFA ZA UTENDAJI SEKTA NDOGO UMEME, GESI ASILIA NA MAFUTA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa za utendaji katika Sekta ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa mwaka 2022/2023 ambapo ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara na Taasisi mbalimbali kufanyia kazi taarifa hizo zinazoonesha mafanikio na changamoto katika Sekta Nishati.

Akizindua taarifa hizo tarehe 14 Juni, 2024 jijini Dodoma, Dkt. Biteko ameagiza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Mipango na Uwekezaji kusoma taarifa hizo na kuzichambua na changamoto zilizoainishwa zipatiwe majibu ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Aidha ameagiza kuwa, kila aina ya fursa iliyoonekana kwenye taarifa hizo ichukuliwe kwa uzito mkubwa na itambuliwe nani ana uwezo wa kuitumia fursa hiyo ndani ya Serikali na katika taasisi binafsi.

“ Vilevile nawaagiza EWURA mhakikishe kuwa, tathmini ya mwaka ujao ihusishe utendaji wa Nishati Safi ya kupikia ili kuweza kujipima kwa usahihi kuhusu utekelezaji wa ajenda hii inayopewa kipaumbele na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Dkt. Biteko.

Agizo jingine ni kuwa, matishio yote ya Sekta ya Nishati yaliyoainishwa katika ripoti kati ya mwaka 2023 hadi 2025 yawekewe mabunio ya suluhisho lake ili katika ripoti ijayo changamoto husika zisiwepo ikiwemo suala la kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila mwaka.

Dkt. Biteko pia ameitaka EWURA kupima uhusiano wa rasilimali zilizopo na mafanikio ya watu ambapo amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta lazima yaendane na mabadiliko ya maisha ya watu.

Pia ametaka mifumo ya uagizaji mafuta iendelee kuboreshwa baada ya kufanyika utafiti wa kina na kueleza kwamba miundombinu ya mafuta bado inahitajika huku akisisitiza kuwa urasimu usiwepo kwenye Sekta ya Nishati.

Ameipongeza  EWURA kwa tathmini ambayo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika, akitolea mfano kutolewa kwa leseni ya kuchimba gesi asilia katika kisima cha Ntorya kilichopo mkoani Mtwara kitakachotoa gesi futi za ujazo milioni 140 kwa siku ambapo leseni ya mwisho ya kuchimba gesi ilitolewa mwaka 2006.

Kuhusu sekta ndogo ya umeme amesema amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuiboresha ambapo leo ametoa taarifa kuwa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) umeingiza mtambo wa pili katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba 8 na hivyo kufanya mradi huo kuingiza megawati 470 katika gridi.

Kuhusu sekta binafsi amesema, “Sekta binafsi imetutoa kimasomaso, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme, wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa, na kwa taasisi zilizo chini ya Wizara msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele.” Amesema Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiimarisha Sekta ya Nishati na kusema kuwa Dodoma imeshuhudia matunda ya uimarishaji huo wa sekta kwani sasa umeme haukatiki.

Pia amepongeza utashi mkubwa wa uongozi wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambao unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuiimarisha Sekta kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa katika tathmini iliyozinduliwa inaonesha Sekta ya Nishati  imepiga hatua kwenye maeneo megi ikiwemo uhakika wa upatikanaji umeme, upatikanaji na usambazaji wa mafuta kuimarika hasa baada ya Mhe. Dkt. Doto Biteko kuanza kuongoza Wizara ya Nishati, aidha upatikanaji na uwekezaji wa gesi unaendelea kuimarika na hii ikijumuisha usambazaji gesi kwenye maeneo mbalimbali kama katika magari, majumbani na viwandani.

Ameongeza kuwa, taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za Dunia ya Tatu zinazofadhiliwa na Benki hiyo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na Bara la Afrika kwa ujumla na hii ni matunda ya usimamizi madhubuti wa Mhe.Dkt. Doto Biteko ambapo  eneo lililofanya vizuri zaidi ni usambazaji umeme vijijini na miradi mingine ya nishati kama JNHPP na mradi wa TAZA.

Ameongeza kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola.za Marekani milioni  300 ili ziendeleze sekta ya umeme kutokana na ufanisi huo wa Tanzania.

Akitoa taarifa za utendaji katika Sekta ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu ya mafuta, uwekezaji wa vituo vya mafuta na maghala umeongezeka, kuna ongezeko la uagizaji wa Gesi ya Mitungi (LPG) kwa asilimia 16 na ongezeko la uagizaji wa mafuta kwa asilimia 8.

 Amesema kuwa katika Sekta ya umeme uwekezaji umeongezeka katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, upotevu wa umeme unazidi kupungua na wateja wa umeme wameongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2021/22 hadi milioni 4.4 mwaka 2022/2023.

Baadhi ya  changamoto zilizoainishwa kwenye taarifa katika sekta ya umeme ni uchakavu wa miundombinu ambao unaendelea kufanyiwa kazi na uwekezaji endelevu kwenye sekta.

Saturday, June 15, 2024

WAZIRI JAFO ATUA KWA DC MAGOTI KUWEKA MIPANGO YA MAENDELEO

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi Makamu wa Rais Muungano na  Mazingira na Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Seleman Jafo amefika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kwenda kumsalimia Mkuu mpya wa Wilaya hiyo Petro Magoti.

Waziri Jafo alikwenda kumtembelea mkuu huyo mpya wa Wilaya ikiwa imepita  siku moja tu baada ya kuapishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge.

Waziri Jafo amesema kwamba ameamua kwenda kumtembelea mkuu huyo kwa lengo la kuweza kumpongeza kwa dhati baada ya kuteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenda kuwaongoza wananchi wa Kisarawe.

 Jafo amesema kwamba ana mfahamu Magoti kwa muda mrefu kutoka na kuwa mchapakazi hodari na anatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.

 "Kitu kikubwa nimekuja katika ofisi za Mkuu wa Wilaya lakini lengo kubwa ni kubadilisha mawazo katika Wilaya yetu ya Kisarawe na mimi nampongeza sana Magoti kwa kuletwa hapa,"amesema Waziri Jafo.

Pia Waziri Jafo alimshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kumteua Magoti nakumleta Kisarawe kwa lengo la kuwatumikia wananchi.

Sambamba na hilo Jaffo hakusita kumpa pongezi mkuu huyo wa Wilaya kwa kuchapa kazi kwa bidii zaidi kwani wanafahamiana tangu alipokuwa Waziri wa TAMISEMI waliweza i kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali na mali.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Wilaya Petro Magoti amemwahidi waziri Jafo kumpa ushirikiano wa karibu zaidi lengo ikiwa ni kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.


  

Friday, June 14, 2024

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI YA MAFUTA KINGA KWA WATU WENYE UALBINO

 

SERIKALI imezitaka Halmashauri nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mafuta kinga ya kujipaka watu wenye ualbino ili kuepukana na mionzi ya jua ambayo inawasababishia kansa ya ngozi.

Hayo yalisemwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi ambapo hotuba yake ilisomwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya kuongeza uelewa juu ya Ualbino Duniani (IAAD) ambapo kitaifa ilifanyika Kibaha.

Ndejembi alisema kuwa serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino wanawekewa mazingira mazuri ili kupata huduma muhimu zikiwemo za kiafya.

"Tunaziagiza Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kununulia mafuta hayo (sun screen lotion) ili ziweze kuwasaidia kukabiliana na mionzi ya jua ambayo imekuwa ikiwasababishia kansa ya ngozi,"alisema Ndejembi.

Alisema kuwa huduma za afya ni sehemu ya jukumu la serikali kama inavyotoa huduma nyingine na hiyo ni huduma mojawapo kwa wananchi.

"Pia ni vema kuwapatia vifaa zaidi kuliko fedha pale wanapokuwa wanahitaji vifaa kama vile vyerehani ili waweze kushonea kofia ambazo zinawasaidia kukabiliana na mwanga mkali na jua,"alisema Ndejembi.

Aidha alisema kuwa serikali iko makini katika kuangalia ustawi wa watu wenye ulemavu ambapo inawndelea na utaratibu wa kuboresha sheria ya watu wenye ulemavu na inalaani matukio ya kuwafanyia vitendo vya ujatili watu wenye ualbino.

"Jamii inapaswa kuthamini utu wa mtu na ni jukumu la kila mwananchi na kamati za usalama za mikoa zihakikishe vitendo hivyo vinakomeshwa na wao kwa wao waache migongano na washiriki uchaguzi kwa kuchagua na kuchaguliwa kwani ni haki yao,"alisema Ndejembi.

Aliwataka maofisa watendaji kuhakikisha wanafanya utambuzi wa watu wenye ualbino na kuhusu asilimia mbili ya mikopo ya Halmashauri kwa watu wenye ukemavu kwa mtu mmoja mmoja badala ya kukopa kwa vikundi serikali inalifanyia kazi suala hilo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, SACP Ralph Meela  alisema kuwa wataendelea kusimamia ulinzi na usalama hivyo watu wenye ualbino wasiwe na wasiwasi.

Meela alisema kuwa wanafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na wakaguzi wa polisi ngazi ya kata zaidi ya 3,000 nchini na kuna makamishna wa polisi jamii kwenye mikoa hivyo kutakuwa na usalama wa kutosha.

Kwa upande waka katibu wa Chama Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) Batha Totei amesema kuwa wanaomba ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu na kuondoa gharama za matibabu ya kansa kwa watu wenye ualbino na kuwa na mpango wa bima ya afya.

Totei alisema kuwa serikali iweke mpango wa kuwa na kliniki kwenye hospitali za wilaya na kliniki tembezi na kuwashirikisha kwenye mikutano ya kampeni ili waweze kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa watu wenye ualbino.



MAGOTI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI KUWATUMIKIA WANAKISARAWE

MKUU mpya wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na viongozi waliopo ili kuleta maendeleo kwa wabanchi wa wilaya hiyo. 

Magoti ameyasema hayo Mjini Kibaha alipokula kiapo cha kuwa Mkuu wa Wilaya ambapo aliapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge 

Amesema kuwa anamshukuru Rais kwa kumpa nafasi hiyo na hilo ni kama deni atalilipa deni hilo alilonalo kwa kuwatumikia wananchi wa Kisarawe katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kunenge amewataka wakuu wa Wilaya zote kuhakikisha wanasimamia mapato kwenye Halmashauri zao ili ziweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

 Amewataka kutatua changamoto za wananchi kwa wakati na usimamizi kwenye utoaji huduma za afya na maji na usimamizi wa miradi ya elimu, barabara ili fedha zinazotolewa na serikali ziwe na tija.

Wednesday, June 12, 2024

WATU WENYE ULEMAVU WATAKA KUTEULIWA NAFASI NGAZI ZA MAAMUZI

CHAMA Cha Watu Wenye UalbinoTanzania (TAS) kimeiomba serikali iwateue kwenye nafasi za ngazi za maamuzi.

Aidha ametaja nafasi hizo za maamuzi kama vile Uwaziri, Ukuu wa Mikoa na Ukuu wa Wilaya kwani nao wanauwezo kama walivyo watu wengine.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Bodi ya chama hicho Thomas Diwani wakati akitoa salama za chama kwenye kongamano la kuongeza uelewa juu ya Ualbino lililofanyika kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwa Mfipa Kibaha.

Naye Mkurugenzi kitengo cha huduma kwa watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Rasheed Maftah amesema kuwa serikali inaanda sera na miongozo mbalumbali kwa watu wenye ulemavu za kuweka usawa na haki.

Awali mwenyekiti wa Tas Godson Mollel amesema kuwa wanampongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Hospitali Rufaa ya KCMC kwa kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 124 kwa ajili ya kuzalisha losheni zinazotumiwa na watu wenye ualbino.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa mkoa wa Pwani Nickson John amesema kuwa watu wenye ualbino wapatao 368 wanapatiwa misaada mbalimbali na zimeundwa kamati za watu wenye ualbino.


MAHAKAMA YATAKIWA KUTOA ADHABU KALI WANAOWAFANYIA VITENDO VYA UKATILI WATU WENYE UALBINO



CHAMA cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimeiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa watu wanaokutwa na hatia ya kuwakata viungo au kuwaua watu wenye Ualbino.

Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Taifa wa TAS Godson Mollel alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku kuongeza uelewa juu ya Ualbino (IAAD) duniani.

Mollel amesema kuwa Mahakama ikotoa hukumu kali kwa wahusika hao itakuwa fundisho kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha kuwadhuru watu wenye Ualbino.

Naye ofisa ustawi mkuu toka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu Joy Maongezi amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2010 inataka kuwa na haki kwa watu wenye ulemavu ambapo watu wenye Ualbino ni sehemu yao.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amesema kuwa wakati wa maadhimisho hayo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwa ni pamoja na upimaji saratani ya ngozi, utoaji miwani, kofia na losheni ya kuzuia ngozi kuathirika, upimaji wa tezi dume na kansa ya kizazi.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka duniani ambapo kilele huwa tarehe 13 Juni kila mwaka na kwa mwaka huu kitaifa yanafanyika Kibaha Mkoani Pwani.


Monday, June 10, 2024

KAMPUNI YA REFUELLING TANZANIA LIMITED YATOA MABATI 72 KWA KIKUNDI CHA KUKAYA MIONO

KAMPUNI ya Refuelling Tanzania Ltd imekipatia mabati 72 kikundi cha KUKAYA-Miono Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Miono.

Akipokea mabati hayo kwa niaba ya kikundi cha KUKAYA MIONO ,Mwenyekiti Omary Mtiga ameishukuru kampuni ya Refuelling kwa msaada huo.

Alieleza ujenzi una miezi sita kwa nguvu zao wananchi ,wameshapokea milioni 13.5 kutoka kwa wadau, lengo lilikuwa kujenga kuongeza darasa moja lakini wamefanikiwa kujenga madarasa mawili.

Mtiga alifafanua, kwasasa bado kuna mahitaji ya mabati 34 ,malori sita ya mchanga ,maroli manne ya kokoto na mifuko ya saruji 60 ili kukamilisha ujenzi huo.

"Tunashukuru uongozi wa kampuni hii, chini ya Mkurugenzi Mohsin Bharwani ambae ameguswa na jambo hili, Mohsin amekuwa akijitoa katika masuala ya kijamii kwenye maeneo mengi ndio na sisi tuliamua kumuomba msaada na tunashukuru kutusaidia "

Aidha Mtiga alitoa wito kwa makampuni na wadau wengine kuendelea kujitolea kwani bado kuna uhitaji.

Aliiomba jamii Miono kuendelea kushirikiana katika masuala ya maendeleo ili kujiinua kimaendeleo ikiwemo kuboresha sekta ya elimu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Refuelling Tanzania limited, Mohsin Bharwani, Meneja wa kampuni hiyo Renatus Kabeyo alisema wamekabidhi mabati 72 na kusafirisha jumla milioni mbili (mil.2).

Alifafanua kuwa, kampuni hiyo inashirikiana na jamii kwa kila jambo kulingana na uwezo wao.

"Nimeona kuna madarasa tunaona mnajenga ,vyoo ,niweze kuahidi tutajenga hoja ,pamoja na misaada inayokuja nikuombe ofisa elimu kata andika andiko ,ili mpate misaada mikubwa kutoka kwa wadau mbalimbali" alieleza Kabeyo.

Kabeyo alisema wanafunzi wanasoma ila wanatakiwa kusoma kwenye mazingira bora.