Friday, April 19, 2024

KUNDI LA KIBAHA HURU FIKRA HURU LATOA MADAWATI 30

KUNDI la Whatsapp la Kibaha Huru Fikra Huru limetoa msaada wa madawati 30yenye thamani ya shilingi milioni tatu ili kusaidia wanafunzi ambao wanakabilia na upungufu wa madawati kwenye Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mwenyekiti wa Kundi hilo la Kijamii Mchungaji Paschal Mnemwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mara baada ya kukabidhi madawati hayo amesema wameguswa na changamoto ya wanafunzi hao kukaa chini.

Mch Mnemwa amesema kuwa wameamua kuchangia madawati hayo ili kuisaidia serikali ili kukabiliana na changamoto hiyo ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.

"Nawashukuru wana kikundi na watu mbalimbali kwa kutoa fedha na huu siyo mwisho kwani huo ni mwanzo wa kusaidia kumfuta vumbi mtoto wa Kibaha ili kumfanya mtoto awe na moyo wa kusoma na wadau mbalimbali wajitoe kusaidia tujenge tabia kusaidia maendeleo,"amesema Mnemwa. 

Amesema jamii isitegemee misaada toka nje bali ianze kuchanga yenyewe ili kusaidiana wenyewe kwa wenyewe badala ya kusubiri kusaidia kutoka nje ya nchi wafadhili wa kwanza iwe jamii yenyewe ili kuleta maendeleo.

"Mifumo ya mitandao ya kijamii ilitengenezwa ili kuiweka jamii pamoja kusaidiana na wasiitumie vibaya kwani endapo itatumika vibaya itaharibu maadili ya jamii ikitumika vizuri inaweza kuleta maendeleo,"amesema Mnemwa.

Akipokea madawati hayo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anawashukuru na kuwapongeza kundi hilo kwa kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitolea madawati hayo.

Ndomba amesema kuwa madawati hayo yatasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati kwenye shule mbalimbali za Mji wa Kibaha na kuwataka wadau wengine kuchangia kama walivyofanya kundi hilo.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Taaluma wa Halmashauri ya Mji Kibaha Adinani Livamba amesema kuwa wana upungufu wa madawati zaidi ya 3,000 ambapo madawati ni hitaji kubwa kwani wanafunzi wanafunzi wanaongezeka pia yanaharibika hivyo changamoto hiyo haiwezi kwisha kabisa.

Livamba amesema kuwa wanachukua hatua mbalimbali kukabili changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa madawati 1,321 na wanafanya na matengenezo na madawati hayo yatasaidia wanafunzi 90 wa darasa la kwanza, la pili na la tatu ambao ndiyo watanufaika.

Naye msemaji wa kundi hilo Hamis Mponji amesema kuwa fedha zimechangwa na watu wa Kibaha na nje ya Kibaha ambapo kulikuwa hakuna kiwango maalum cha kuchanga ni kile ambacho mtu kaguswa kukitoa.

Moja ya viongozi wa kundi hilo Hamad Kibwelele amesema kuwa wakati wanaanzisha kundi wakaona lisiwe na maongezi tu bali wafanye kitu cha maendeleo kwenye jamii na kukubaliana kuchangia madawati huku wakiangalia nini cha kufanya kwa baadaye ili kuleta maendeleo Kibaha.

Tuesday, April 16, 2024

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAONGEZA MELI ZA UVUVI BAHARI KUU

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu  (Deep Sea Fishing Authority-DSFA) imefanya maboresho katika kanuni za Sheria Uvuvi wa Bahari Kuu  na kupandisha utoaji wa vibali vya uvuvi katika Bahari Kuu kutoka  meli tisa mwaka 1988 hadi meli 61 mwaka 2023/24 kwa ajili ya kufanya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) upande wa Tanzania.

Hayo yamesemwa Leo Tarehe 16 Aprili 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Muungano kuelekea maadhimisho ya miaka 60.

Ameeleza kuwa DSFA imeingia mkataba na Kampuni ya Albacora ya nchini Hispania kwa ajili ya ujenzi wa  kiwanda cha kuchakata samaki katika Mkoa wa Tanga na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku, kuhifadhi tani 2,400 za samaki na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100.

Pia amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukitumia Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Machui – Tanga kupata vifaranga vya samaki na viumbe maji wengine wakiwemo jongoo bahari kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu.

Aidha, zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanakadiriwa kupata kipato chao cha kila siku kutokana na shughuli za Uvuvi, zikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao yake pamoja na Baba na Mama lishe. 

Ikumbukwe kuwa sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta tatu za Kilimo ambazo zinaajiri wananchi wengi na imeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji wapatao 35,986.

SERIKALI YATOA BILIONI 696.7 KUPUNGUZA UMASKINI

SERIKALI imetoa shilingi bilioni 696.7 kwa ajili ya kupunguza na kuondoa umaskini kwa kaya milioni 1.3 kwenye vijiji  na mitaa.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano.

Simbachawene amesema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato.

Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na serikali  mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.

"Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF awamu ya I awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya,”amesema Simbachawene.

Simbachawene amesema awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar.

Amefafanua kuwa  jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).

Amesema katika miaka 60 ya Muungano, serikali inayoongozwa na Rais,  Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Aidha amesema kuwa TAKUKURU kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa.

Pia amesema Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni “Jeshi kubwa” ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa.

WANAOTUKANA VIONGOZI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa  wanaotumia mitandao kuwatukana viongozi wa nchi  watakumbana na mkono wa sheria popote walipo.

Masauni ametoa kauli hiyo Aprili 15/2024  katika kumbi wa habari Maelezo Jijini  Dodoma alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua watu wanaomtukana Rais Samia katika mitandao.

Amesema kuwa hawatakuwa na msamaha  kwa mtu yoyote atakayevunja sheria ya kutukana viongozi na atatafutwa popote mpaka apatikane.

‘’Mimi niseme tu Serikali haina msalie mtume kwa mtu yeyote anayevunja sheria kwa kutukana viongozi katika mitandao na ina mkono mrefu wanaofanya hivyo watatafutwa popote walipo mkono wa sheria utawakamata,’’amesema Masauni.

Aidha Masauni ambaye alikuwa akielezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano amesema tangu enzi za waasisi wa Muungano Mwalimu Nyerere na Amani Karume walijenga Taifa lenye maadili hivyo ni budi kuendeleza yale waliyoacha waasisi wetu.

Sambamba na hayo ametoa wito kwa wananchi kuwa Serikali haitamfumbia macho mtu au kikundi cha watu wanaotukana viongozi kupitia mitandao  kwa kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

‘’Msifikirie haya mambo yanayoenendelea mitandaoni na kutukana watu hawachukuliwi hatua utajikuta na wewe unafuata mkumbo usiige kwani hakuna atakayeachwa salama,"amesema Masauni.

Waziri huyo amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwani Serikali ya Rais Samia haipendi kusumbua watu inataka watu waishi kwa amani na kila mmoja atii sheria bila shuruti.

‘’Dhamira ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapendi kuona watoto wake wanapata shida hivyo vyombo vya usalama vipo kazini’’, amesema Masauni.

Pia amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano sekta ya usalama wa nchi  iko vizuri na mafanikio ni mengi ikiwemo kuwa na majeshi ya polisi imara.

Sunday, April 14, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI YATOA SHUKRANI KWA CHUO CHA VETA MKOA WA PWANI KUWAPATIA USAFIRI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA 102 KUZALIWA KWA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA DODOMA




Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ndugu Omary Abdul Punzi kwa niaba ya uongozi ameshukuru chuo cha Veta Pwani kupitia Mkuu wa chuo hicho Madam Crala Kibodya kuwezesha safari hiyo kwa kutoa usafiri wa Coaster.

Ndugu Omary Punzi amesema huo ni uzalendo mkubwa kawa wadau nchini wasisite kusaidia katika shughuli nyingine.

Maadhimisho hayo yaliyofana yaliyohudhiliwa na Wananchi wengi wanafunzi na makundi mengine Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Dkt Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MWAKILISHI WA BALOZI WA UGANDA YAPONGEZA UBUNIFU WA TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI







Mwakilishi wa Balozi wa Uganda Bregedia Ronald Bigirwa apongeza ubunifu wa Uongozi Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani kwa Tshirt yenye maneno mazuri.

Akipokeaa Tshirt hizo  yeye na mke wake katika maadhimisho hayo ya miaka 102 ya kuzaliwa kwa Mwl Julius Kambarage Nyerere lililofanyika katika Ukumbi wa Mji wa  Mtumba Mkoani Dodoma tarehe 13.4.2024

MEJA JENERALI BALOZI ANSELM BAHATI SHIGONGO ATUMA SALAMU ZA MKOA WA PWANI KONGAMANO LA MIAKA 102 YA KUZALIWA KWA MWALIMU NYERERE DODOMA

 



MWENYEKITI wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani Mh Meja Jenerali Balozi Anselm Bahati Shigongo amesema kuwa Mkoa wa Pwani ni mkoa bora katika uwekezaji wa viwanda.

Mh Meja Jenerali Balozi Bahati ameyasema hayo katika maadhimisho ya kitaifa ya miaka 102 ya kuzaliwa kwa Mwl Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mtumba Mjini Dodoma tarehe 13.4.2024 maadhimisho hayo yalihudhuliwa na Mh Daktari Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Amewaomba wadau wa maendeleo nchini waende Mkoani Pwani kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.