Friday, January 12, 2024

KATA PICHA YA NDEGE YAISHUKURU SERIKALI KUWAPATIA MILIONI 340 UJENZI MADARASA PICHA YA NDEGE SEKONDARI



KATA ya Picha ya Ndege imefanikiwa kuongeza madarasa 17 kwenye Shule ya Sekondari Picha ya Ndege ambayo awali ilikuwa na madarasa sita lakini kwa sasa ni madarasa 23 ambapo zimetumika kiasi cha shilingi milioni 340 kwa madarasa hayo yaliyoongezeka.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata hiyo Karim Mtambo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya kuboreka kwa sekta ya elimu kulikofanywa na Serikali ya awamu ya sita.

Mtambo alisema kuwa ongezeko la madarasa hayo kumeondoa changamoto iliyokuwepo ya upungufu wa madarasa ambapo madarasa hayo pia yana viti vyake hivyo wanafunzi watasoma kwa raha bila ya usumbufu.

"Wakati tunaingia kwenye uongozi kulikuwa na boma la maabara mbili za Baiolojia na Kemia Serikali ilitoa milioni 60 kwa awamu ya kwanza na awamu ya ya pili ilitoa milioni 80 ambazo zimekamilisha maabara hizo ambapo bado ya Fizikia,"alisema Mtambo.

Alisema kuwa kuna baadhi ya changamoto zilizopo kwa sasa ni ukosefu wa jengo la Utawala kwaniwalimu imebidi watumie darasa moja kama ofisi kwa ajili ya shughuli zao ambapo walipeleka ombi Halmashauri ili kujengewa jengo la Utawala.

"Changamoto nyingine ni vyoo vya walimu ambapo imebidi watumie matundu ya vyoo vya wanafunzi moja kwa walimu wanawake na walimu wanaume na tumeongea na wazazi watoe tofali tano ili kuwajengea choo walimu kwani jambo ambalo siyo sawa,"alisema Mtambo.

Aidha alisema kulikuwa na changamoto ya maji ambapo walipewa milioni 10 na Halmashauri na kuvuta maji lakini bomba wanalotumia majo yanatoka kwa mgao lakini mradi wa Pangani ukikamilika maji yatapatikana muda wote.

Thursday, January 11, 2024

WATANZANIA WATAKIWA WAPANDE MITI KULINGANA NA UMRI WAO

WATANZANIA wametakiwa kuadhimisha siku za kumbukumbu zao za kuzaliwa kwa kupanda miti kutokana na umri wao ili kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yalisemwa na Brigadia Jenerali Mstaatu Martin Kemwaga mwasisi wa kampeni ya Miti kwa Umri alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuwa malengo yake ni kuifanya nchi kuwa ya kijani.

Kemwaga alisema kuwa kampeni hiyo ambayo alianza miaka mitano iliyopita ambapo ilizinduliwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete eneo la Msata Wilayani Bagamnoyo mkoani Pwani kwenye Hoteli ya Makmar ambayo yeye ni Mtendaji Mkuu.

"Namshukuru Rais Mstaafu Dk Kikwete kwa kutuzindulia kampeni yetu ambayo mimi na familia yangu, marafiki na vikundi mbalimbali huwa tunapanda miti kutokana na umri wetu na ningependa kila Mtanzania apande miti kutokana na umri wake,"alisema Kemwaga.

Alisema kuwa Watanzania waadhimishe siku zao za kuzaliwa kwa kupanda miti badala ya kutumia
gharama kubwa za kukumbuku za kukumbuka siku siku zao za kuzaliwa ambapo idadi ya Watanzania.

"Watu watumie maeneo ya taasisi za Umma kama vile kwenye Mashule, Hospitali, Zahanati, Polisi na vyuo na maeneo mbalimbali ya wazi ambapo miti ikipandwa kutasaidia hali ya hewa kuwa nzuri na kuondokoana na arhari za mabadiliko tabianchi,"alisema Kemwaga.

Aidha alisema kuwa Utamaduni huo warithishwe watoto ili wawe wanafanya hivyo ambapo ndani ya muda mnfupi nchi itakuwa na miti mingi na kukabili changamoto mbalimbali za hali ya hewa inayojitokeza
kutokana na ukosefu wa miti.

Aidha alisema kuwa katika eneo ambalo wamepanda miti wanaifuatilia ili kuhakikisha inakuwa na kama
mtu kapanda atakuwa anafuatilia mti alioupanda tofauti na baadhi ya taasisi zimekuwa zikipanda miti lakini hawaifuatili na kufa.

Monday, January 8, 2024

HALMASHAURI YAWATAKA WAVAMIZI SHAMBA LA MITAMBA KUONDOKA.

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imewataka wavamizi waliovamia Shamba la Mitamba namba 34 kuondoa maendelezo waliyoyafanya kabla ya zoezi la kuwaondoa kufanyika ili wasipate hasara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Munde amesema kuwa watu waliovamia walipewa ilani ya tarehe 22/11/2022 ya kuondoka kwenye eneo hilo lililopo Kata ya Pangani baada ya kamati maalumu kuundwa na waziri wa ardhi na kutoa majibu kuwa watu hao ni wavamizi kwani eneo hilo lina hati.

"Eneo hilo linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na lina hati miliki ni sehemu ya eneo lenye ukubwa wa hekta 4,000 lilitwaliwa kisheria na wizara hiyo kwa kulipa fidia kwa wananchi 1,556 waliokuwa wakimiliki kiasili na kulipwa kwa awamu nne kati ya mwaka 1988 na 1991,"amesema Munde.

Amesema kuwa baada ya kulipa fidia na kumilikishwa kiwanja hicho chenye ukubwa wa hekta 1,037 wananchi walivamia na kuuza sehemu ya kiwanja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kufanya ujenzi kinyume cha sheria.

"Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati huo William Lukuvi alifanya mkutano Julai 15 mwaka 2021 na kuwataka wananchi waache kuvamia eneo hilo na kuuza na kuunda kamati ya wataalamu mbalimbali ikiongozwa na kamishna wa Polisi makao makuu Dodoma,"amesema Munde.

Aidha amesema kuwa baada ya maagizo ya mawaziri Halmashauri ya Mji Kibaha ilitoa ilani ya kwanza ya siku saba iliyotolewa 22/11/2022 kuwataka wavamizi hao kuondoka ili kuruhusu mpango wa uendelezaji wa kiwanja hicho.

"Pia Halmashauri ilipokea barua ya katibu mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye kumbukumbu namba GA.16/200/01/75 ya Septemba 20 mwaka 2023 kwa ajili ya kupanga upya, kusimamia, kuwaondoa wavamizi wote na kupima kiwanja hicho.

Aliongeza kuwa kwa kuwa wananchi walishapewa ilani ya kuondoka mara mbili hivyo waondoe maendelezo yao kwani zoezi la kuwaondoa likianza hawatapata nafasi ya kuondoa mali zao.

Saturday, January 6, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI INATARAJIA KUJENGA KITUO WATOTO WANAOISHI KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Pwani inatarajia kujenga kituo cha kulea watoto waishio kwenye mazingira magumu kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 150.

Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu wa Taasisi hiyo Omary Punzi alipokutana na wadau wanaoshirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Punzi amesema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu ambao wanasoma shule za msingi na sekondari, watu wenye uhitaji wakiwemo wafungwa na watu mbalimbali.

"Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imekuwa ikitoa misaada kwa makundi kama hayo lakini baada ya kuona kuna changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu mitaani tumeona kuna haja ya kujenga kituo kwa ajili ya watoto hao,"amesema Punzi.

Amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaacha alama kwa Taasisi hiyo na wadau wanaoshirikiana nao katika kuihudumia jamii yenye uhitaji ambapo ni moja ya malengo Taasisi.

"Tunatarajia kujenga kituo hicho hapa Kibaha lengo likiwa ni kuihudumia jamii na kuenzi falsafa za Mwalimu Nyerere za kupambana na adui watatu umaskini, ujinga na maradhi,"amesema Punzi.

Aidha amesema kuwa watoto hao wakiwa hapo Taasisi itahakikisha watoto hao wanapata huduma muhimu za msingi ikiwani pamoja na elimu na matibabu ambazo ni falsafa za Mwalimu Nyerere,"alisema Punzi.

Ameomba wadau kushiriki kikamilifu wakati ujenzi utakapoanza ili malengo ya taasisi yafikiwe ya ujenzi wa kituo hicho ili kuwaondoa watoto hao kuishi mitaani badala yake waishi kwenye makazi maalumu.

Monday, January 1, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE PWANI YATOA VYETI VYA PONGEZI KWA WADAU








TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imetoa vyeti vya shukrani kwa vyombo vya habari na wadau mbalimbali ambao ilishirikiana nao katika shughuli zake za maendeleo.

Akikabidhi vyeti hivyo hakimu mkazi mstaafu mkoa wa Pwani Stephen Mbungu amewataka waandishi wa habari na wadau kudumisha amani kwa kuzingatia maadili ya nchi.

Naye naibu katibu mkuu wa taasisi hiyo Neema Mkwachu alisema kuwa moja ya kazi zao ni kufundisha maadili kwa Watanzania ili nchi iendelee kuwa na amani.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dk Abdulsalaam Omar alisema kuwa wanashirikiana na taasisi na mashirika katika utoaji huduma ikiwa ni sehemu ya kuleta maendeleo.

Mwakilishi wa kamishna wa uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Mathew Ntilicha aliwataka wananchi kulinda mazingira kwa kupanda miti na ufugaji wa nyuki.

Meneja wa Shirika la Ugavi la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani Mhandisi Mahawa Mkaka alisema kuwa wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili iendelee kuihudumia jamii.

Mwenyekiti wa (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao alisema kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa viongozi wakiwemo madiwani na viongozi wa umma kwani baadhi hawana maadili mazuri.

Mhamasishaji wa taasisi hiyo kitaifa Jirabi alisema kuwa lengo kuu ni kuwaunganisha Watanzania ili kujua falsafa za Nyerere ambaye alikuwa akipambana na adui watatu wa Taifa ambao ni Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Kwa upande wake katibu wa taasisi hiyo Mkoani Pwani Omary Punzi alisema kuwa wamefanya hafla hiyo ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali ambao imeshirikiana nayo katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Sunday, December 31, 2023

ALIYEESHINDA TUZO YA MALKIA WA UINGEREZA ATAKA DIASPORA WAPEWE HADHI MAALUM WAWEZE KULETA MAENDELEO NCHINI.





MTANZANIA ambaye alipata Tuzo ya Malkia Elizabeth || wa Uingereza, Prudence Kimiti amesema kuwapa hadhi maalum Diaspora itasaidia waweze kuwekeza nchini.

Kimiti aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipotua nchini akitokea Uingereza anapoishi ambapo  hadhi hiyo ikitolewa itasaidia sana kwa Diaspora kufanya uwekezaji ili kuleta maendeleo.

Prudence ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa baadhi ya Mikoa hapa nchini alisema kuwa yeye anaipenda Tanzania hivyo anatamani kutoa mchango wake wa maendeleo kwa nchi. 

"Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopambana kuwaletea Watanzania maendeleo hivyo watoe hadhi hiyo maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi na ikiwa hivyo itasaidia kuwekeza ndani ya nchi yao,"alisema Kimiti.

Alisema kuwa suala kupewa hadhi maalumu kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni zuri kwani litasaidia kuleta maendeleo kwenye nchi yao.

Akizungumzia kuhusu tuzo aliyoipata ya Malkia wa Uingereza ya (MBE) aliipata kutokana na kutetea haki za watu weusi hasa wafanyakazi ambapo kuna baadhi ya changamoto wanazipata kutokana na rangi zao.

"Tuzo hii inafaida kubwa kwani inanipa moyo kuendelea kupigania haki za watu dunia nzima siyo Uingereza hata sehemu nyingine kwani napenda kila mtu apate haki yake,"alisema Kimiti.

Aidha alisema kuwa anatarajia kuanzisha shirika kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto na wale waishio kwenye mazingira magumu.

"Tunaendeleza falsafa za mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere ambaye Waingereza wanampenda hivyo najivunia kuwa Mtanzania na tutaendeleza mazuri aliyoyaacha Nyerere,"alisema Kimiti.

Kwa upande wake Mzee Paul Kimiti alisema kuwa wanajivunia tuzo aliyoipata mtoto wao kwani imeiheshimisha familia na nchi kwa ujumla.

Kimiti alisema kuwa tangu mwanae akiwa mdogo alikuwa hapendi kuona mtu anaonewa na hilo amekwenda nalo hadi kufikia kupata tuzo hiyo na si bahati bali ni kitu kiko kwenye damu yake.

Alisema kuwa hata babu yake aliwahi kupata tuzo  mwaka 1950 na sasa mwanae naye anapata tuzo hiyo hivyo ni jambo la kujivunia sana kwa nchi kutokana na tuzo hiyo.

Prudencia Kimiti alipata tuzo hiyo ya malkia hiyo wakati wa malkia kutimiza miaka 70 ya uongozi wa Malkia ambapo hutolewa kila mwaka.

Saturday, December 30, 2023

SIKU YA LISHE YA KIJIJI GAIRO DC


GAIRO DC

SIKU YA AFYA NA LISHE YA KIJIJI

NIMEPATA FURSA YA KUZUNGUMZA NA WAKINA MAMA. 

NIMESISITIZA KUHUSU LISHE, NIMEWAKUMBUSHA MALEZI YA WATOTO KWA KUWALINDA DHIDI YA UKATILI. UZOEFU UNAONESHA KUWA MATUKIO MENGI YA UKATILI YANAANZIA KWENYE NYUMBA ZETU KWA KUWAAMINI NDUGU TUNAOWAKARIBISHA HADI KUWALAZA KITANDA KIMOJA NA WATOTO WETU.

GAIRO DC - KAZI INAENDELEA

@ortamisemi 

@wizara_afyatz 

@rs_morogoro 

@jabiri_makame