HALMASHAURI ya Mji Kibaha imewataka wavamizi waliovamia Shamba la Mitamba namba 34 kuondoa maendelezo waliyoyafanya kabla ya zoezi la kuwaondoa kufanyika ili wasipate hasara.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Munde amesema kuwa watu waliovamia walipewa ilani ya tarehe 22/11/2022 ya kuondoka kwenye eneo hilo lililopo Kata ya Pangani baada ya kamati maalumu kuundwa na waziri wa ardhi na kutoa majibu kuwa watu hao ni wavamizi kwani eneo hilo lina hati.
"Eneo hilo linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na lina hati miliki ni sehemu ya eneo lenye ukubwa wa hekta 4,000 lilitwaliwa kisheria na wizara hiyo kwa kulipa fidia kwa wananchi 1,556 waliokuwa wakimiliki kiasili na kulipwa kwa awamu nne kati ya mwaka 1988 na 1991,"amesema Munde.
Amesema kuwa baada ya kulipa fidia na kumilikishwa kiwanja hicho chenye ukubwa wa hekta 1,037 wananchi walivamia na kuuza sehemu ya kiwanja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kufanya ujenzi kinyume cha sheria.
"Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati huo William Lukuvi alifanya mkutano Julai 15 mwaka 2021 na kuwataka wananchi waache kuvamia eneo hilo na kuuza na kuunda kamati ya wataalamu mbalimbali ikiongozwa na kamishna wa Polisi makao makuu Dodoma,"amesema Munde.
Aidha amesema kuwa baada ya maagizo ya mawaziri Halmashauri ya Mji Kibaha ilitoa ilani ya kwanza ya siku saba iliyotolewa 22/11/2022 kuwataka wavamizi hao kuondoka ili kuruhusu mpango wa uendelezaji wa kiwanja hicho.
"Pia Halmashauri ilipokea barua ya katibu mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye kumbukumbu namba GA.16/200/01/75 ya Septemba 20 mwaka 2023 kwa ajili ya kupanga upya, kusimamia, kuwaondoa wavamizi wote na kupima kiwanja hicho.
Aliongeza kuwa kwa kuwa wananchi walishapewa ilani ya kuondoka mara mbili hivyo waondoe maendelezo yao kwani zoezi la kuwaondoa likianza hawatapata nafasi ya kuondoa mali zao.
No comments:
Post a Comment