Saturday, January 13, 2024

KATA YA MISUGUSUGU YAOMBA WADAU UKAMILISHWAJI JENGO LA WAZAZI

KATA ya Misugusugu Wilayani Kibaha Mkoani Pwani imeomba wadau mbalimbali kuwachangia kiasi cha shilingi milioni 39 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto ili kuwaepusha wajawazito kujifungulia majumbani.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Diwani wa Kata hiyo Upendo Ngonyani kuwa wajawazito wengi wanajifungulia majumbani jambo ambalo ni la hatari kiafya.

Alisema kuwa Zahanati iliyopo haina huduma ya kujifungua licha ya kuwa na huduma nyingine za kitabibu isipokuwa za uzazi kutokana na kutokuwa na jengo la wazazi.

"Baada ya kuona changamoto ni kubwa ya akinamama kunifungua tulianzisha ujenzi kwa nguvu za wananchi kupitia wadau mbalimbali tumeweza kujenga jengo hilo la wazazi limeishia kwenye boma,"alisema Ngonyani.

Alisema kwa sasa wanaomba wadau ikiwemo Halmashauri kuwasaidia hatua iliyobaki ili jengo likamilike na kutoa huduma ambapo litanufaisha wananchi wa mitaa minne ya Vitendo, Karabaka, Misugusugu na Miomboni.

"Baadhi ya wajawazito hujifungulia nyumbani kutokana na kutokuwa na kipato wakihofia kwenda Hospitali kuwa gharama ni kubwa hivyo hujifungua kienyeji na wengine hukaa hadi siku ya mwisho ya kujifungua ndipo wanakwenda Hospitali,"alisema Ngonyani.

Aidha alisema wanapopata ujauzito huwa wanakwenda kliniki kwenye Zahanati ya Kata lakini inapofika muda wa kujifungua kwa wale wasio na uwezo hujifungulia nyumbani na kupeleka watoto kliniki kwa ajili ya chanjo mbalimbali.

"Kwa wale wenye uwezo inapofika muda wa kujifungua kwenye vituo vya afya Mkoani, Lulanzi au Mlandizi ambako ni mbali sana na hutumia gharama kubwa kwa usafiri ndiyo tukaona tujenge jengo hilo ili kuondoa changamoto hiyo,"alisema Ngonyani.

Alibainisha kuwa kuna madhara makubwa kwa wajawazito kujifungulia nyumbani kwani ni hatari ambapo mazazi au mtoto au wote wanaweza kupoteza maisha kwa kukosa huduma bora wakati wa kunifungua.

"Tunawapa elimu juu ya umuhimu wa kujifungulia Hospitali lakini wakati mwingine inakuwa vigumu kutokana na baadhi kuwa na kipato kidogo hivyo kushindwa kumudu gharama,"alisema Ngonyani.

Alizishukuru taasisi, wadau mbalimbali na wananchi kwa kujitolea hadi jengo hilo kufikia hapo na kuendelea kuwaomba waendelee kujitolea hadi litakapokamilika ili kunusuru maisha ya akinamama na watoto.

Mitaa hiyo minne ina jumla ya wakazi 8,000 na gharama za mwanzo za ujenzi wa jengi hilo la mama na mtoto limetumia zaidi ya shilingi milioni 20.

No comments:

Post a Comment