TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Pwani inatarajia kujenga kituo cha kulea watoto waishio kwenye mazingira magumu kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 150.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu wa Taasisi hiyo Omary Punzi alipokutana na wadau wanaoshirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Punzi amesema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu ambao wanasoma shule za msingi na sekondari, watu wenye uhitaji wakiwemo wafungwa na watu mbalimbali.
"Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imekuwa ikitoa misaada kwa makundi kama hayo lakini baada ya kuona kuna changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu mitaani tumeona kuna haja ya kujenga kituo kwa ajili ya watoto hao,"amesema Punzi.
Amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaacha alama kwa Taasisi hiyo na wadau wanaoshirikiana nao katika kuihudumia jamii yenye uhitaji ambapo ni moja ya malengo Taasisi.
"Tunatarajia kujenga kituo hicho hapa Kibaha lengo likiwa ni kuihudumia jamii na kuenzi falsafa za Mwalimu Nyerere za kupambana na adui watatu umaskini, ujinga na maradhi,"amesema Punzi.
Aidha amesema kuwa watoto hao wakiwa hapo Taasisi itahakikisha watoto hao wanapata huduma muhimu za msingi ikiwani pamoja na elimu na matibabu ambazo ni falsafa za Mwalimu Nyerere,"alisema Punzi.
Ameomba wadau kushiriki kikamilifu wakati ujenzi utakapoanza ili malengo ya taasisi yafikiwe ya ujenzi wa kituo hicho ili kuwaondoa watoto hao kuishi mitaani badala yake waishi kwenye makazi maalumu.
No comments:
Post a Comment