WATU wanne wakazi wa Jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia zenye thamani ya shilingi milioni 1.5.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoani humo ACP Pius Lutumo alisema kuwa watuhumiwa hao pia walikutwa na mtambo wa kutengeneza fedha hizo.
Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya mchana huko Kijiji cha Msata Wilaya ya Kipolisi Chalinze
Alisema kuwa chanzo cha fedha hizo kukamatwa ni taarifa iliyotolewa na raia mwema ambaye alitilia mashaka noti ya shilingi 10,000 aliyoipokea kwa ajili ya malipo kwa huduma ya kulala nyumba ya wageni.
"Katika upelelezi baada ya tukio hilo Polisi walifanikiwa kukamata mtambo wa kutengenezea fedha hizo bandia na zana nyingine kama kompyuta, kemikali mbalimbali za kutengenezea fedha bandia,"alisema Lutumo.
Aidha alisema kuwa mtambo huo ulikamatwa kwa moja ya watuhumiwa huko Goba Jijini Dar es Salaam na watuhumiwa walikutwa na noti za shilingi elfu 10,000 noti 155.
"Baada ya mtuhumiwa wa kwanza kukamatwa na noti hiyo bandia ya shilingi 10,000 aliwataja watuhumiwa wengine watatu wakiwa na bandia milioni 1.2 zikiwa noti za shilingi elfu tano na elfu mbili,"alisema Lutumo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mbaraka Miraji (48), Zena Naringa (42) wakazi wa Buza, Masumbuko Kiyogoma mkazi wa Goba na Elias Wandiba (50) mkazi wa Kimara Suka Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment